Book of Common Prayer
Mnyama Kutoka Nchi Kavu
11 Pia nikaona mnyama mwingine akija kutoka katika nchi. Alikuwa na pembe mbili kama kondoo, lakini anaongea kama joka. 12 Mnyama huyu alisimama mbele ya mnyama wa kwanza na kutumia nguvu ile ile ya mnyama wa kwanza. Alitumia nguvu hii kumfanya kila mtu aishiye duniani amwabudu mnyama wa kwanza. Mnyama wa kwanza ndiye mwenye jeraha la mauti lililopona. 13 Mnyama wa pili alifanya miujiza[a] mikuu. Alitengeneza hata moto ushuke kutoka mbinguni kuja duniani watu wakiangalia.
14 Mnyama huyu wa pili aliwadanganya watu wanaoishi duniani kwa kutumia miujiza ambayo amepewa uwezo wa kuifanya kwa ajili ya mnyama wa kwanza. Aliwaamuru watu kutengeneza sanamu ili kumheshimu mnyama wa kwanza, aliyejeruhiwa kwa upanga lakini hakufa bali akawa hai tena. 15 Mnyama wa pili alipewa uwezo wa kuipa uzima sanamu ya mnyama wa kwanza. Kisha kinyago kiliweza kuongea na kuamuru watu wote ambao hawakukiabudu wauawe. 16 Pia mnyama wa pili aliwaamuru watu wote, wakubwa na wadogo, matajiri na maskini, walio huru au watumwa, wawekewe alama kwenye mikono yao ya kulia au kwenye vipaji vya nyuso zao. 17 Hakuna ambaye angeweza kununua au kuuza bila ya kuwa na alama hii. (Alama hii ni jina la mnyama au namba ya jina lake.)
18 Kila mwenye uelewa anaweza kujua maana ya namba ya mnyama. Hili linahitaji hekima. Namba hii ni namba ya mtu. Nayo ni 666.
Msitumainie Fedha
32 Msiogope, enyi kundi dogo. Kwa kuwa imempendeza Baba yenu kuwapa ninyi ufalme wake. 33 Uzeni vitu mlivyo navyo, wapeni fedha wale wanaohitaji. Hii ni njia pekee mnayoweza kufanya utajiri wenu usipotee. Mtakuwa mnaweka hazina isiyoisha mbinguni, mahali ambapo wezi hawawezi kuiba na hakuna wadudu wa kuharibu. 34 Kwa kuwa mahali ilipo hazina yako, ndipo roho yako itakapokuwa.
Iweni Tayari Daima
(Mt 24:42-44)
35 Iweni tayari! Vaeni kikamilifu na taa zenu zikiwaka. 36 Iweni tayari kama watumishi wanaomngojea bwana wao anayerudi kutoka kwenye sherehe ya harusi. Bwana wao anaporudi na kubisha mlangoni, watumishi huweza kumfungulia mlango haraka. 37 Bwana wao atakapoona kuwa wako tayari na wanamsubiri, itakuwa siku ya furaha kwa watumishi hao. Ninawaambia bila mashaka, bwana wao atavaa nguo, atawakaribisha kwenye chakula kisha atawahudumia. 38 Watumishi hao wanaweza kumsubiri bwana wao mpaka usiku wa manane. Lakini watafurahi sana kwa sababu aliporudi aliwakuta bado wanamsubiri.
39 Mwenye nyumba angefanya nini ikiwa angejua ni lini mwizi atakuja? Mnajua kuwa asingeruhusu mwizi akavunja na kuingia ndani. 40 Hivyo, iweni tayari ninyi nanyi, kwa kuwa Mwana wa Adamu atakuja wakati msiotarajia!”
Mtumwa Mwaminifu ni Yupi?
(Mt 24:45-51)
41 Petro akasema, “Bwana, mfano ule ulikuwa kwa ajili yetu au kwa ajili ya watu wote?”
42 Bwana akamjibu, “Fikiria kuhusu mtumishi mwenye hekima na mwaminifu, ambaye bwana wake anamwamini na kumweka kuwa msimamizi wa kuwapa watumishi wengine chakula kwa wakati uliokubalika? Mtumishi huyo ataoneshaje kuwa yeye ni msimamizi makini na anayeweza kujisimamia? 43 Mkuu[a] wake atakaporudi na kumkuta akifanya kazi aliyompa, siku hiyo itakuwa siku ya furaha sana kwa mtumishi huyo. 44 Ninawaambia ukweli bila mashaka yo yote, mkuu wake atamweka kuwa msimamizi wa vitu vyake vyote anavyomiliki.
45 Lakini itakuwaje ikiwa mtumishi huyo ni mwovu na akadhani bwana wake hatarudi mapema? Ataanza kuwapiga watumishi wengine, wanaume na wanawake. Atakula na kunywa mpaka atalewa. 46 Ndipo bwana wa mtumishi huyo atakuja wakati usiotarajiwa, wakati ambapo mtumishi hajajiandaa. Ataadhibiwa bila huruma[b] na bwana wake na kumpeleka anakostahili, mahali waliko watumishi wengine wasiotii.
47 Mtumishi huyo alijua kitu ambacho bwana wake alimtaka afanye. Lakini hakuwa tayari kufanya au kujaribu kufanya kile bwana wake alichotaka. Hivyo mtumishi huyo ataadhibiwa sana! 48 Lakini vipi kuhusu mtumishi asiyejua kile ambacho bwana wake anataka? Yeye pia anafanya mambo yanayostahili adhabu, lakini ataadhibiwa kidogo kuliko mtumishi aliyejua alichotakiwa kufanya. Yeyote aliyepewa vingi atawajibika kwa vingi. Hivyo vingi vitategemewa kutoka kwa yule aliyepewa vingi zaidi.”
© 2017 Bible League International