Book of Common Prayer
21 Ninaona aibu kusema haya, lakini tulikuwa “dhaifu sana” kuyafanya mambo kama hayo kwenu.
Lakini kama kuna mtu aliye jasiri vya kutosha kujivuna, nami nitajivuna pia. (Ninaongea hivi kama mjinga.) 22 Je, watu hao ni Wayahudi? Mimi pia. Je, ni Waebrania? Mimi pia. Je, wanatoka katika familia ya Ibrahimu? Mimi pia. 23 Je, wanamtumikia Kristo? Mimi ninamtumikia zaidi sana. (Je, mimi ni mwendawazimu kuongea kwa jinsi hii?) Nimefanya kazi kwa juhudi kuliko wao. Nimekuwa gerezani mara nyingi. Nimepigwa vibaya sana. Nimekuwa katika hali za hatari ya kufa mara nyingi.
24 Mara tano Wayahudi wamenipa adhabu ya viboko 39. 25 Mara tatu katika nyakati tofauti nimepigwa kwa fimbo. Mara moja nilikuwa karibu kuuawa kwa kupigwa kwa mawe. Mara tatu nimevunjikiwa na merikebu, na mara moja katika hizo nilikesha usiku na kushinda kutwa nzima tukielea baharini. 26 Katika safari zangu za mara kwa mara nimekuwa katika hatari za kwenye mito, majambazi, watu wangu wenyewe, na toka kwa watu wasio Wayahudi. Nimekuwa katika hatari mijini, katika maeneo wasioishi watu, na katika bahari. Na nimekuwa katika hatari za watu wanaojifanya kuwa waamini lakini siyo waamini.
27 Nimefanya kazi ngumu na za kuchosha, na mara nyingi sikuweza kulala usingizi. Nimekuwa mwenye njaa na kiu. Mara nyingi nimekosa kula chakula. Nimekuwa katika hali ya baridi na kutokuwa na nguo za kujifunika. 28 Na kuna matatizo mengine mengi zaidi. Mojawapo ya hayo ni mzigo nilio nao kila siku wa majukumu yangu: Ninawaza juu ya makanisa yote. 29 Ninajisikia kuwa mdhaifu kila mara mtu mwingine anapokuwa dhaifu. Ninapata hasira sana pale mtu yeyote anapoingizwa dhambini.
30 Ikiwa ni lazima nisifu, nitajisifu katika vitu vinavyonidhihirisha kuwa mimi ni dhaifu. 31 Mungu ajua kuwa sisemi uongo. Yeye ni Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, na anapaswa kutukuzwa milele.
Yesu Atuliza Dhoruba
(Mt 8:23-27; Lk 8:22-25)
35 Siku ile ilipofika jioni aliwaambia, “Hebu tuvuke kwenda ng'ambo ya pili ya ziwa.” 36 Kwa hiyo wakaliacha lile kundi. Wakamchukua pamoja nao alipokuwa amerudi katika mtumbwi. Wakati ule ule palikuwepo na mitumbwi mingi mingine ziwani. 37 Dhoruba kubwa ikatokea na mawimbi yalikuwa yanakuja katika pembe zote za mtumbwi. Mtumbwi nao ulikaribia kujaa maji kabisa 38 lakini Yesu alikuwa amelala nyuma ya mtumbwi akiegemea mto. Wakamwaamsha na kumwambia, “Mwalimu je wewe hujali kwamba tunazama?”
39 Kisha akainuka, akaukemea upepo, na akaliamuru ziwa, “Nyamaza Kimya! Tulia!” Upepo ule ukatulia na ziwa nalo likatulia kabisa.
40 Kisha akawaambia, “Kwa nini mnaogopa? Je! Bado hamna imani yoyote?”
41 Lakini walikuwa na woga sana, na wakasemezana wao kwa wao, “Ni nani basi huyu ambaye hata upepo na ziwa vinamtii?”
© 2017 Bible League International