Book of Common Prayer
12 Petro alipoona hili, aliwaambia watu: “Ndugu zangu Wayahudi, kwa nini mnashangaa hili? Mnatutazama kama vile ni kwa nguvu zetu tumemfanya mtu huyu atembee. Mnadhani hili limetendeka kwa sababu sisi ni wema? 13 Hapana, Mungu ndiye aliyetenda hili! Ni Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo. Ni Mungu aliyeabudiwa na baba zetu wote. Kwa kufanya hili, alimtukuza Yesu mtumishi wake, yule ambaye ninyi mlimtoa ili auawe. Pilato alipotaka kumwachia huru, mlimwambia Pilato kuwa hamumtaki Yesu. 14 Yesu alikuwa Mtakatifu na mwema, lakini mlimkataa na badala yake mlimwambia Pilato amwache huru mwuaji[a] na awape ninyi. 15 Na hivyo mlimwua yule awapaye uzima! Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu. Sisi ni mashahidi wa jambo hili kwani tuliliona kwa macho yetu wenyewe.
16 Huyu mlemavu wa miguu ameponywa kwa sababu tunalo tumaini katika Yesu. Nguvu ya Yesu ndiyo iliyomponya. Mnamwona na mnamfahamu mtu huyu. Ameponywa kabisa kwa sababu ya imani inayotokana na Yesu. Ninyi nyote mmeona hili likitokea!
17 Kaka zangu, ninajua kwamba hamkujua mlilomtendea Yesu wakati ule. Hata viongozi wenu hawakujua walilokuwa wanatenda. 18 Lakini Mungu alikwishasema kupitia manabii kuwa mambo haya yangetokea. Masihi wake angeteseka na kufa. Nimewaambia jinsi ambavyo Mungu alifanya jambo hili likatokea. 19 Hivyo lazima mbadili mioyo na maisha yenu. Mrudieni Mungu, naye atawasamehe dhambi zenu. 20 Kisha Bwana atawapa muda wa faraja kutokana na masumbufu yenu. Atamtuma Yesu kwenu, aliyemchagua kuwa Masihi wenu.
21 Lakini Yesu lazima akae mbinguni mpaka wakati ambapo kila kitu kitafanywa upya tena. Mungu alikwisha sema kuhusu wakati huu tangu zamani kupitia manabii wake watakatifu. 22 Musa alisema, ‘Bwana Mungu wako atakupa nabii. Nabii huyo atatoka miongoni mwa watu wako. Atakuwa kama mimi. Ni lazima mtii kila kitu atakachowaambia. 23 Na yeyote atakayekataa kumtii nabii huyo atakufa na kutengwa na watu wa Mungu.’(A)
24 Samweli, na manabii wengine wote walisema kwa niaba ya Mungu. Baada ya Samweli, walisema kuwa wakati huu ungekuja. 25 Na kile ambacho manabii walikisema ni kwa ajili yenu ninyi wazaliwa wao. Mmepokea Agano ambalo Mungu alilifanya na baba zenu. Mungu alimwambia baba yenu Ibrahimu kuwa, ‘Kila taifa duniani litabarikiwa kupitia wazaliwa wako.’(B) 26 Mungu amemtuma Yesu, mtumishi wake maalumu. Alimtuma kwenu kwanza, ili awabariki kwa kuwageuza kila mmoja wenu aache njia zake za uovu.”
Yesu, Mwanakondoo wa Mungu
29 Siku iliyofuata Yohana akamwona Yesu akija kwake na kusema, “Tazama, Mwanakondoo wa Mungu mwenye kuondoa dhambi za ulimwengu.” 30 Huyu ndiye niliyezungumza habari zake niliposema, “Kuna mtu anayekuja baada yangu aliye mkuu zaidi yangu, kwa sababu yeye aliishi muda mrefu kabla ya kuzaliwa kwangu.” 31 Nami sikumjua yeye ni nani. Lakini nilikuja kuwabatiza watu kwa maji ili watu wa Israeli waelewe kuwa huyo ndiye Masihi.
32-34 Kisha Yohana akasema maneno yafuatayo ili kila mtu asikie, “Mimi pia sikujua nani hasa alikuwa Masihi. Lakini yule aliyenituma kubatiza aliniambia, ‘Utamwona Roho akishuka na kutua kwa mtu. Huyo ndiye atakayewabatiza watu kwa Roho Mtakatifu.’ Nami nimeyaona haya yakitokea. Nilimwona Roho akishuka kutoka mbinguni kama njiwa na kutulia juu ya mtu huyu. Hivyo haya ndiyo ninayowaambia watu: ‘Yeye huyo ndiye Mwana wa Mungu.’”[a]
Wafuasi wa Kwanza wa Yesu
35 Siku iliyofuata Yohana alirejea tena mahali hapo pamoja na wafuasi wake wawili. 36 Naye akamwona Yesu akitembea, hivyo akasema, “Angalieni, Mwanakondoo wa Mungu!”
37 Wale wafuasi wake wawili walimsikia Yohana akisema haya, basi wakaondoka na kumfuata Yesu. 38 Yesu aligeuka na kuwaona watu wawili wakimfuata. Akawauliza, “Mnataka nini?” Nao wakajibu wakimwuliza, “Rabi, unakaa wapi?” (Rabi tafsiri yake ni Mwalimu.)
39 Yesu akajibu, “Njooni tufuatane pamoja nanyi mtapaona ninapokaa.” Hivyo wale watu wawili wakaenda pamoja naye. Wakaona mahali alipokuwa anakaa, nao wakashinda huko pamoja naye mchana wote. Hiyo ilikuwa ni saa kumi ya jioni.
40 Watu hawa wakamfuata Yesu baada ya kusikia habari zake kutoka kwa Yohana. Mmoja wao alikuwa Andrea, nduguye Simoni Petro.
41 Kitu cha kwanza alichokifanya Andrea kilikuwa ni kwenda kumtafuta ndugu yake Simoni. Andrea alipompata nduguye akamwambia, “Tumemwona Masihi.” (Masihi tafsiri yake ni Kristo.) 42 Kisha Andrea akamleta Simoni nduguye kwa Yesu. Yesu akamtazama, na kumwambia, “Wewe ndiwe Simoni, mwana wa Yohana. Basi utaitwa Kefa.” (“Kefa” tafsiri yake ni “Petro”.[b])
© 2017 Bible League International