Add parallel Print Page Options

Yesu Aenda Kwenye Mji wa Kwao

(Mt 13:53-58; Lk 4:16-30)

Yesu akaondoka pale, na kwenda katika mji wa kwao; na wanafunzi wake wakamfuata. Sabato ilipofika, alianza kufundisha katika sinagogi. Watu wengi walishangazwa walipomsikiliza. Wakasema, “Mtu huyu alipata wapi mambo haya? Alipata wapi hekima hii? Na anaifanyaje miujiza hii inayofanyika kwa mikono yake? Je, yeye si yule seremala? Je, yeye si mwana wa Maria? Je, yeye si kaka yake Yakobo, Yusufu, Yuda, na Simoni? Je, dada zake hawaishi hapa katika mji wetu?” Kulikuwa na vikwazo vilivyowazuia wasimkubali.

Yesu akawaambia, “kila mtu humheshimu nabii isipokuwa watu wa mji wa kwao mwenyewe, jamaa zake mwenyewe na wale wa nyumbani mwake mwenyewe.” Yesu hakuweza kufanya miujiza ya aina yoyote pale, isipokuwa aliweka mikono juu ya wagonjwa wachache na kuwaponya. Naye akashangazwa na jinsi watu wa mji wa kwao mwenyewe walivyokosa kuwa na imani. Kisha Yesu alizunguka vijijini akiwafundisha watu.

Yesu Awatuma Kazi Mitume Wake

(Mt 10:1,5-15; Lk 9:1-6)

Akawaita kwake wanafunzi wake kumi na wawili, na akaanza kuwatuma wawili wawili. Akawapa uwezo wa kuwaweka huru watu kutoka pepo wachafu. Akawapa amri kuwa wasichukue kitu chochote kwa ajili ya safari yao isipokuwa fimbo; hawakupaswa kuchukua mkate, mfuko, hata kubeba fedha kwenye mikanda yao. Aliwaruhusu kuvaa makobazi lakini wasichukue kanzu ya pili. 10 Naye akawambia, “ikiwa mtu atawapa mahali pa kuishi mkae katika nyumba hiyo kwa muda wote mtakapokuwa katika mji ule msihamehame kutoka nyumba moja hadi nyingine. 11 Ikiwa hamtakaribishwa ama kusikilizwa katika mji wowote au mahali popote, kwa kuwaonya kunguteni mavumbi toka miguuni mwenu.”

12 Kwa hiyo mitume wakatoka na kuhubiri ili watu watubu. 13 Mitume wakafukuza mashetani wengi na kuwapaka mafuta ya mizeituni[a] wagonjwa wengi na kuwaponya.

Herode Adhani Yesu ndiye Yohana Mbatizaji

(Mt 14:1-12; Lk 9:7-9)

14 Mfalme Herode alisikia habari hii kwani umaarufu wa Yesu ulikuwa umeenea mahali pote. Watu wengine walisema, “Yohana Mbatizaji amefufuka kutoka wafu, ndiyo maana ana uwezo wa kufanya miujiza.”

15 Wengine wakasema, “Yeye ni Eliya.”

Wengine walisema, “Yeye ni nabii kama mmoja wa manabii wa zamani.”

16 Lakini Herode aliyasikia haya na kusema, “Yohana, yule mtu niliyemkata kichwa, amefufuka kutoka kifo.”

Yohana Mbatizaji Alivyouawa

17 Kwa kuwa Herode mwenyewe alikuwa ametoa amri ya kumkamata Yohana na kumweka gerezani. Alifanya hivi kwa sababu ya Herodia, mkewe Filipo kaka yake ambaye Herode alikuwa amemwoa. 18 Kwani Yohana alizidi kumwambia Herode, “Si halali kwako kisheria kumwoa mke wa kaka yako.” 19 Herodia alikuwa na kisa na Yohana. Hivyo alitaka auwawe, lakini hakuweza kumshawishi Herode kumuua Yohana. 20 Hii ni kwa sababu Herode alimhofu Yohana. Herode pia alifahamu ya kuwa Yohana alikuwa ni mtu mtakatifu na mwenye haki, hivyo akamlinda. Herode alimpomsikia Yohana, alisumbuka sana; lakini alifurahia kumsikiliza.

21 Lakini muda maalumu ukafika; katika siku ya kuzaliwa kwake. Herode aliandaa sherehe ya chakula cha jioni kwa maafisa mashuhuri wa baraza lake, maafisa wake wa kijeshi, na watu maarufu wa Galilaya. 22 Binti ya Herodia alipowasili ndani ya ukumbi alicheza na kumpendeza Herode na wageni aliowaalika katika sherehe hiyo.

Mfalme Herode akamwambia yule msichana, “Uniombe chochote unachotaka, nami nitakupa.” 23 Akamuahidi: “Nitakupa chochote utakachoniomba, hata nusu ya ufalme wangu!”

24 Naye akatoka na kumwambia mama yake, “Niombe kitu gani?”

Mama yake akasema, “Omba kichwa cha Yohana Mbatizaji.”

25 Yule msichana mara moja aliharakisha kuingia ndani kwa mfalme na kuomba: “Nataka unipe sasa hivi kichwa cha Yohana Mbatizaji katika sinia.”

26 Mfalme alisikitika sana. Lakini kwa sababu ya viapo vyake alivyovifanya mbele ya wageni wake chakulani hakutaka kumkatalia ombi lake. 27 Kwa hiyo mfalme mara moja akamtuma mwenye kutekeleza hukumu za kifo akiwa na amri ya kukileta kichwa cha Yohana. Kisha akaenda kukikata kichwa cha Yohana, 28 na kukileta katika sinia na kumpa yule msichana, na msichana akampa mama yake. 29 Wanafunzi wa Yohana waliposikia haya walikuja na kuchukua mwili na kuuweka ndani ya kaburi.

Yesu Awalisha Watu Zaidi ya 5,000

(Mt 14:13-21; Lk 9:10-17; Yh 6:1-14)

30 Mitume walikusanyika kumzunguka Yesu, na wakamweleza yote waliyofanya na kufundisha. 31 Kisha Yesu akawaambia, “Njooni mnifuate peke yenu hadi mahali patulivu na palipo mbali na watu wengine ili mpumzike kidogo”, kwani pale walikuwepo watu wengi wakija na kutoka, nao hawakuwa na nafasi ya kula.

32 Kwa hiyo wakaondoka na mtumbwi kuelekea mahali patulivu na mbali na watu wakiwa peke yao. 33 Lakini watu wengi waliwaona wakiondoka na waliwafahamu wao ni kina nani; kwa hiyo walikimbilia pale kwa njia ya nchi kavu kutoka vitongoji vyote vilivyolizunguka eneo hilo wakafika kabla ya Yesu na wanafunzi wake. 34 Alipotoka katika mashua, Yesu aliona kundi kubwa, na akawahurumia, kwa sababu walikuwa kama kondoo wasiokuwa na mchungaji, Kwa hiyo akaanza kuwafundisha mambo mengi.

35 Kwa sasa ilikuwa imekwisha kuwa jioni sana. Kwa hiyo wanafunzi wake walimwijia na kusema, “Hapa ni mahali palipojitenga na sasa hivi saa zimeenda. 36 Uruhusu watu waende zao, ili kwamba waende kwenye mashamba na vijiji vinavyozunguka na waweze kujinunulia kitu cha kula.”

37 Lakini kwa kujibu aliwaambia, “Ninyi wenyewe wapeni kitu cha kula.”

Wao Wakamwambia, “Je, twende kununua mikate yenye thamani ya mshahara wa mtu mmoja[b] wa miezi minane na kuwapa wale?”

38 Yesu akawambia, “Ni mikate mingapi mliyonayo? Nendeni mkaone.”

Walienda kuhesabu, wakarudi kwa Yesu na kusema, “Tunayo mikate mitano na samaki wawili.”

39 Kisha akawaagiza wakae chini kila mmoja kwenye majani mabichi kwa vikundi. 40 Nao wakakaa kwa vikundi vya watu mia na mmoja na vya watu hamsini.

41 Akachukua ile mikate mitano na samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akashukuru na akaimega. Akawapa wanafunzi wake ili wawape watu. Pia aligawanya samaki wawili miongoni mwao wote.

42 Wakala na wote wakatosheka. 43 Wakachukua mabaki ya vipande vya mikate na samaki na kujaza vikapu kumi na viwili. 44 Na idadi ya wanaume waliokula ile mikate ilikuwa 5,000.

Yesu Atembea Juu ya Maji

(Mt 14:22-33; Yh 6:16-21)

45 Mara Yesu akawafanya wafuasi wake wapande kwenye mashua na wamtangulie kwenda Bethsaida upande wa pili wa ziwa, wakati yeye akiliacha lile kundi liondoke. 46 Baada ya Yesu kuwaaga wale watu, alienda kwenye vilima kuomba.

47 Ilipotimia jioni, mashua ilikuwa katikati ya ziwa, na Yesu alikuwa peke yake katika nchi kavu. 48 Naye akawaona wanafunzi wake wakihangaika kupiga makasia, kwani upepo uliwapinga. Kati ya saa tisa na saa kumi na mbili asubuhi Yesu aliwaendea akitembea juu ya ziwa. Yeye akiwa karibu kuwapita, 49 wanafunzi wake wakamwona akitembea juu ya ziwa,[c] na wakafikiri kuwa alikuwa ni mzimu, ndipo walipopiga kelele. 50 Kwa kuwa wote walimwona, na wakaogopa. Mara tu alizungumza nao na kuwaambia, “Jipeni moyo! Ni mimi. Usiogope.” 51 Kisha alipanda kwenye mtumbwi pamoja nao, na upepo ukatulia. Wakashangaa kabisa, 52 kwa kuwa walikuwa bado hawajauelewa ule muujiza wa mikate. Kwani fahamu zao zilikuwa zimezibwa.

Yesu Awaponya Watu Wengi Wagonjwa

(Mt 14:34-36)

53 Walipolivuka ziwa, walifika Genesareti na wakaifunga mashua. 54 Walipotoka katika mashua, watu wakamtambua Yesu, 55 Wakakimbia katika lile jimbo lote na kuanza kuwabeba wagonjwa katika machela na kuwapeleka pale waliposikia kuwa Yesu yupo. 56 Na kila alipoenda vijijini, mijini na mashambani, waliwaweka wagonjwa kwenye masoko, na wakamsihi awaache waguse pindo la koti lake. Na wote walioligusa walipona.

Footnotes

  1. 6:13 kuwapaka mafuta ya mizeituni Mafuta ya mizeituni yalitumika kama dawa. Ilikuwa pia ni alama ya uponyaji wa Mungu aliopewa Yesu na baadaye wanafunzi wake na Roho Mtakatifu.
  2. 6:37 thamani ya mshahara wa mtu mmoja Kwa Kiyunani vipande 200 vya fedha vimelinganishwa na TKU kama kiasi cha mshahara wa mtu mmoja kwa miezi minane.
  3. 6:49 akitembea juu ya ziwa Watu zama za Marko waliamini kwamba mizimu isingeweza kutembea juu ya maji, lakini waliamini miungu wangeweza kutembea juu ya maji. Watu hao wangeshangaa kuona mitume wa Yesu wakiwa tayari kuamini kitu potovu kabla ya kuamini kuwa Yesu alisimama mbele yao ni Mungu kwani ametembea majini.