Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
6 Hivyo tuna ujasiri daima. Tunafahamu kuwa tunapoendelea kuishi katika mwili huu, tunakuwa mbali na makao yetu pamoja na Bwana. 7 Tunaishi kwa msingi wa yale tunayoamini kuwa yatatokea na siyo kwa msingi wa yale tunayoyaona. 8 Hivyo ninasema tuna ujasiri. Na tungependa kuondoka na kutokuwa katika mwili huu na kuwa nyumbani pamoja na Bwana. 9 Lengo letu pekee ni kumpendeza Bwana, kwamba tupo nyumbani au mbali. 10 Tutasimama sote mbele za Kristo ili tuhukumiwe. Kila mtu atalipwa anachostahili. Kila mtu atalipwa kutokana na matendo yake, mazuri au mabaya, alipoishi katika mwili huu wa kidunia.
Kuwasaidia Watu Ili Wawe Rafiki wa Mungu
11 Tunafahamu maana ya kuwa na hofu na Bwana, hivyo tunajitahidi kuwashawishi watu waipokee. Mungu anafahamu tulivyo, na ni matarajio yangu kuwa nanyi mioyoni mwenu mnatufahamu sisi pia. 12 Hatujaribu tena kujithibitisha kwenu sasa. Lakini tunawapa sababu za ninyi kujivuna kwa ajili yetu. Kisha mtaweza kuwa na majibu kwa ajili wanaojivuna kwa ajili ya yale yanayoonekana. Hawajali kuhusu kilicho katika moyo wa mtu. 13 Ikiwa tuna wazimu, ni kwa ajili ya Mungu na ikiwa tuna akili timamu, ni kwa ajili yenu.
14 Upendo wa Kristo unatutawala, kwa sababu tunafahamu kuwa mmoja alikufa kwa ajili ya wote. Hivyo wote wamekufa. 15 Alikufa kwa ajili ya wote ili wanaoishi wasiendelee kuishi kwa ajili yao wenyewe. Alikufa kwa ajili yao na alifufuka toka kwa wafu ili waishi kwa ajili yake.
16 Kuanzia sasa hatumfikirii mtu yeyote kama ulimwengu unavyowafikiria watu. Ni kweli kuwa zamani kale tulimfikiria Kristo kwa mtazamo wa kidunia. Lakini hatufikirii hivyo sasa. 17 Mtu anapokuwa ndani ya Kristo, anakuwa kiumbe[a] kipya kabisa. Mambo ya zamani yanakoma; na ghafla kila kitu kinakuwa kipya!
Yesu Atumia Simulizi Kuhusu Mbegu Inayokua
26 Yesu akasema, “Hivi ndivyo Ufalme wa Mungu unavyofanana: Mtu mmoja alitoka kwenda kupanda mbegu zake katika udongo shambani. 27 Usiku alienda kulala na asubuhi aliamka na zile mbegu zikiota na kukua; na hakujua jinsi gani hiyo ilifanyika. 28 Ardhi yenyewe inatoa nafaka; kwanza hutoka shina, kisha kinafuata kichwa na mwishoni hutokea nafaka kamili katika kichwa. 29 Nafaka ile inapokuwa imekomaa, basi mkulima huikata kwa fyekeo kwani wakati wa mavuno umekwishafika.”
Simulizi Nyingine ya Ufalme
(Mt 13:31-32,34-35; Lk 13:18-19)
30 Yesu akasema, “Niufanananishe na kitu gani ufalme wa mbinguni? Au tutumie mfano gani kuuelezea? 31 Ni kama mbegu ya haradali, ambayo ni mbegu ndogo sana kuliko zote inapopandwa ardhini. 32 Lakini inapokuwa imepandwa, inakua na kuwa kubwa sana kuliko mimea yote ya bustanini, na pia hubeba matawi makubwa, kiasi kwamba ndege wa angani wanaweza kupumzika katika kivuli chake.”
33 Kwa mifano mingi kama hii aliendelea kuwafundisha kila kitu kwa kuzingatia uwezo wao wa kuelewa. 34 Yesu hakusema kitu kwao bila kutumia mfano. Lakini alipokuwa peke yake pamoja na wanafunzi wake, alifafanua kila kitu kwao.
© 2017 Bible League International