Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Msiwakosoe Wengine
14 Iweni tayari kuwakubali wenye mashaka kuhusu yale ambayo waamini wanaweza kufanya. Tena msibishane nao kuhusu mawazo yao tofauti. 2 Baadhi ya watu wanaamini kuwa wanaweza kula aina yoyote ya chakula,[a] lakini wale walio na mashaka wanakula mboga za majani tu. 3 Wale wanaojua kuwa wanaweza kula chakula cha aina yoyote hawapaswi kujisikia kuwa ni bora kuliko wale wanaokula mboga za majani tu. Na wale wanaokula mboga za majani tu hawapaswi kuamua kuwa wale wanaokula vyakula vyote wanakosea. Mungu amewakubali. 4 Huwezi kuwahukumu watumishi wa mtu mwingine. Hilo linamhusu bwana wao mwenyewe ikiwa watafaulu au watashindwa. Na watakubaliwa, kwa sababu Bwana yuko tayari kuwafanya wafaulu.
5 Watu wengine wanaweza kuamini kuwa siku moja ni ya muhimu zaidi kuliko nyingine. Na wengine wanaweza kuwa na uhakika kuwa siku zote ziko sawa. Kila mtu anapaswa kujihakikisha juu ya imani yake katika akili zake wenyewe. 6 Wale wanaofikiri kuwa siku moja ni ya muhimu kuliko siku zingine wanafanya hivyo kwa ajili ya Bwana. Na wale wanaokula vyakula vya aina zote wanafanya hivyo kwa ajili ya Bwana. Ndiyo, wanamshukuru Mungu kwa ajili ya chakula. Na wale wanaokataa kula vyakula fulani wanafanya hivyo kwa ajili ya Bwana. Nao pia wanamshukuru Mungu.
7 Hatuishi au kufa kwa ajili yetu sisi wenyewe tu. 8 Kama tukiishi, tunaishi kwa ajili ya Bwana. Na kama tukifa, tunakufa kwa ajili ya Bwana. Hivyo kuishi au kufa, sisi ni mali ya Bwana. 9 Ndiyo sababu Kristo alikufa na kuishi tena ili awe Bwana juu ya wote waliokufa na wanaoishi.
10 Hivyo kwa nini unamhukumu kaka au dada yako katika familia ya Mungu? Au kwa nini unafikiri kuwa wewe ni bora kuliko wao? Sote tutasimama mbele za Mungu, naye atatuhukumu sisi sote. 11 Ndiyo, Maandiko yanasema,
“‘Hakika kama niishivyo’, asema Bwana,
‘kila mtu atapiga magoti mbele zangu,
na kila mtu atasema kuwa mimi ni Mungu.’”(A)
12 Hivyo kila mmoja wetu ataeleza kuhusu matendo yake mbele za Mungu.
Simulizi Kuhusu Msamaha
21 Kisha Petro akamwendea Yesu na kumwuliza, “Bwana, ndugu yangu akiendelea kunikosea, ninapaswa kumsamehe anaponikosea mara ngapi? Mara saba?”
22 Yesu akamjibu, “Ninakwambia, ni lazima umsamehe zaidi ya mara saba. Ni lazima uendelee kumsamehe hata kama atakukosea saba mara sabini.[a]
23 Ninawaambia kwa sababu ufalme wa Mungu unafanana na mfalme aliyetaka kupata taarifa kutoka kwa watumishi wake. 24 Mtumishi aliyekuwa anadaiwa na mfalme tani 300[b] za fedha aliletwa kwake. 25 Hakuwa na fedha za kutosha kulipa deni lake. Hivyo mfalme aliamuru kila kitu anachomiliki mtumishi yule kiuzwe ikiwa ni pamoja na mke na watoto wake.
26 Lakini mtumishi alipiga magoti na kumsihi mfalme akisema, ‘Nivumilie. Nitakulipa kila kitu unachonidai.’ 27 Mfalme alimhurumia. Hivyo akamsamehe yule mtumishi deni lote na akamwacha aende akiwa huru.
28 Lakini mtumishi huyo alipoondoka, alimwona mtumishi mwingine aliyekuwa anamdai sarafu mia za fedha. Akamkaba shingo yake na akasema, ‘Nilipe pesa ninayokudai!’
29 Mtumishi anayedaiwa akapiga magoti na kumsihi akisema, ‘Nivumilie. Nitakulipa kila kitu unachonidai.’
30 Lakini mtumishi wa kwanza alikataa kumvumilia. Alimwambia hakimu kuwa alikuwa anamdai pesa, na mtumishi yule alitupwa gerezani mpaka atakapoweza kulipa deni lake. 31 Watumishi wengine walipoona hili, walimhurumia mtumishi aliyefungwa gerezani. Hivyo walienda na kumwambia mfalme kila kitu kilichotokea.
32 Ndipo mfalme alimwita msimamizi wa kwanza na kumwambia, ‘Wewe ni mbaya sana! Ulinisihi nikusamehe deni lako, na nilikuacha ukaondoka bila kulipa kitu chochote! 33 Hivyo ulipaswa kumpa mtu yule mwingine anayetumika pamoja nawe rehema ile ile niliyokupa mimi.’ 34 Mfalme alikasirika sana. Hivyo alifungwa gerezani mpaka atakapoweza kulipa kila kitu anachodaiwa.
35 Mfalme huyu alifanya kama ambavyo Baba yangu wa mbinguni atawafanyia ninyi. Ni lazima umsamehe ndugu au dada yako kwa moyo wako wote, usipofanya hivyo, Baba yangu wa mbinguni hatakusamehe wewe.”
© 2017 Bible League International