Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Ushirika wa Waamini
42 Waamini walitumia muda wao kusikiliza mafundisho ya mitume. Walishirikiana kila kitu kwa pamoja. Walikula[a] na kuomba pamoja. 43 Maajabu mengi na ishara nyingi zilikuwa zinatokea kupitia mitume, na hivyo kila mtu aliingiwa na hofu na akamtukuza Mungu. 44 Waamini wote walikaa pamoja, na kushirikiana kila kitu. 45 Waliuza mashamba yao na vitu walivyomiliki, kisha wakatoa fedha na kuwapa wenye kuhitaji. 46 Waamini waliendelea kukutana pamoja katika eneo la Hekalu. Pia walikula pamoja katika nyumba zao. Walikuwa na furaha kushirikiana chakula chao na walikula kwa mioyo mikunjufu. 47 Waamini walimsifu Mungu na waliheshimiwa na watu wote. Watu wengi zaidi waliokolewa kila siku, na Bwana alikuwa akiwaongeza kwenye kundi lao.
19 Baadhi yenu mtapata mateso wakati ambapo hamjafanya kosa lolote. Ikiwa utaweza kuvumilia maumivu na kuweka fikra zako kwa Mungu, hilo linampendeza sana Mungu. 20 Kwani kuna sifa gani iliyopo kwako kama utapigwa kwa kutenda mabaya na kuvumilia? Lakini kama utateseka kwa kutenda mema na kustahimili, hili lampendeza Mungu. 21 Ni kwa kusudi hili mliitwa na Mungu, kwa sababu Kristo pia aliteseka kwa ajili yenu na kwa kufanya hivyo aliacha kielelezo kwenu, ili tuweze kuzifuata nyayo zake.
22 “Hakutenda dhambi yo yote,
wala hakukuwa na udanganyifu uliopatikana kinywani mwake.”(A)
23 Alipotukanwa hakurudishia matusi. Alipoteseka, hakuwatishia, bali wakati wote alijitoa mwenyewe kwa Mungu ahukumuye kwa haki. 24 Yeye mwenyewe alizibeba dhambi zetu kwenye mwili wake hadi pale msalabani, ili tuweze kuacha kuishi kwa ajili ya dhambi na kuishi kwa ajili ya haki. Ilikuwa ni kwa njia ya majeraha yake kwamba mliponywa. 25 Kwani mlikuwa kama kondoo wanaotangatanga huko na huko, lakini sasa mmerudi kwa Mchungaji na Mwangalizi wa maisha yenu.
Mchungaji na Kondoo Wake
10 Yesu akawaambia, “Hakika ninawaambia, mtu anapoingia katika zizi la kondoo, hutumia mlango. Kama akiingia kwa kutumia njia nyingine yoyote, huyo ni mwizi. Anajaribu kuwaiba kondoo. 2 Lakini mtu anayewachunga kondoo hupitia mlangoni. Yeye ndiye mchungaji. 3 Mtu anayelinda mlangoni humfungulia mlango mchungaji. Na kondoo huisikiliza sauti ya mchungaji wao. Naye huwaita kondoo wake mwenyewe kwa majina yao, na huwaongoza kwenda nje. 4 Mchungaji huwatoa nje kondoo wake wote. Kisha huwatangulia mbele na kuwaongoza. Kondoo nao humfuata, kwa sababu wanaifahamu sauti yake. 5 Lakini kamwe kondoo hawatamfuata wasiyemfahamu. Bali watamkimbia, kwa sababu hawaifahamu sauti yake.”
6 Yesu aliwaambia watu habari hii, lakini hawakuelewa ilikuwa ina maana gani.
Yesu Mchungaji Mwema
7 Hivyo Yesu akasema tena, “Hakika ninawaambia, Mimi ni mlango wa kondoo. 8 Wote walionitangulia walikuwa wezi na wanyang'anyi. Kondoo hawakuwasikiliza hao. 9 Mimi ni mlango. Yeyote anayeingia kupitia kwangu ataokoka. Ataweza kuingia na kutoka nje. Atapata kila anachohitaji. 10 Mwizi anakuja kuiba, kuua, na kuangamiza. Lakini mimi nilikuja kuwaletea uzima, na muwe nao kwa ukamilifu.
© 2017 Bible League International