Revised Common Lectionary (Complementary)
Petro Azungumza na Watu
11 Huku wakishangaa, watu wale waliwakimbilia Petro na Yohana pale walikokuwa katika Ukumbi wa Sulemani. Mtu yule aliyeponywa alikuwa akingali amewang'anga'nia Petro na Yohana.
12 Petro alipoona hili, aliwaambia watu: “Ndugu zangu Wayahudi, kwa nini mnashangaa hili? Mnatutazama kama vile ni kwa nguvu zetu tumemfanya mtu huyu atembee. Mnadhani hili limetendeka kwa sababu sisi ni wema? 13 Hapana, Mungu ndiye aliyetenda hili! Ni Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo. Ni Mungu aliyeabudiwa na baba zetu wote. Kwa kufanya hili, alimtukuza Yesu mtumishi wake, yule ambaye ninyi mlimtoa ili auawe. Pilato alipotaka kumwachia huru, mlimwambia Pilato kuwa hamumtaki Yesu. 14 Yesu alikuwa Mtakatifu na mwema, lakini mlimkataa na badala yake mlimwambia Pilato amwache huru mwuaji[a] na awape ninyi. 15 Na hivyo mlimwua yule awapaye uzima! Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu. Sisi ni mashahidi wa jambo hili kwani tuliliona kwa macho yetu wenyewe.
16 Huyu mlemavu wa miguu ameponywa kwa sababu tunalo tumaini katika Yesu. Nguvu ya Yesu ndiyo iliyomponya. Mnamwona na mnamfahamu mtu huyu. Ameponywa kabisa kwa sababu ya imani inayotokana na Yesu. Ninyi nyote mmeona hili likitokea!
© 2017 Bible League International