Revised Common Lectionary (Complementary)
1 Kutoka kwa Yakobo mtumishi wa Mungu na wa Bwana Yesu Kristo.
Kwa makabila Kumi na Mawili[a] ya watu wa Mungu yaliyotawanyika kote ulimwenguni: Salamu!
Imani na Hekima
2 Kaka na dada zangu, jueni kuwa mtakutana na adha za kila aina. Lakini hilo liwape ninyi sababu ya kuwa na furaha zaidi. 3 Kwa sababu mnajua kuwa imani yenu inapojaribiwa ndipo mnapojifunza kuwa wavumilivu. 4 Na uvumilivu unapaswa kukamilisha kazi yake, ili kwamba muwe watu waliokomaa na wakamilifu msiopungukiwa na kitu cho chote.
5 Hivyo kama mmoja wenu atapungukiwa na hekima, anapaswa kumwomba Mungu anayewapa watu wote kwa ukarimu, naye atampa hekima. 6 Lakini anapaswa kuwa na imani anapoomba pasipo mashaka yo yote, kwani yule aliye na mashaka ni kama wimbi la baharini, linalosukumwa na upepo na kusukwa sukwa. 7 Mtu wa jinsi hiyo asidhani kuwa anaweza kupokea cho chote kutoka kwa Bwana; 8 yeye ni mwenye mashaka na hufikiria mambo mawili tofauti kwa wakati mmoja.
© 2017 Bible League International