Revised Common Lectionary (Complementary)
16 Ninyi hamkunichagua mimi. Bali ni mimi niliyewachagua ninyi. Nami niliwapa kazi hii: Kwenda na kutoa matunda; matunda ambayo yatadumu. Ndipo Baba atakapowapa chochote mtakachomwomba katika jina langu. 17 Hii ndiyo amri yangu: Mpendane ninyi kwa ninyi.
Yesu Awatahadharisha wafuasi Wake
18 Endapo ulimwengu utawachukia, mkumbuke kwamba umenichukia mimi kwanza. 19 Kama mngekuwa wa ulimwengu huu, ulimwengu ungewapenda kama watu wake. Lakini ulimwengu unawachukia kwa sababu ninyi siyo wa ulimwengu huu. Badala yake, mimi niliwachagua ninyi ili muwe tofauti na ulimwengu.
20 Kumbukeni somo nililowafundisha: Watumwa sio wakubwa kuliko mabwana wao. Kama watu walinitendea mimi vibaya, watawatendea vibaya hata nanyi pia. Na kama waliyatii mafundisho yangu, watayatii hata ya kwenu pia. 21 Watawatendea yale waliyonitendea mimi, kwa sababu ninyi ni wangu. Wao hawamjui yeye aliyenituma. 22 Kama nisingekuwa nimekuja na kusema na watu wa ulimwengu, basi wasingekuwa na hatia ya dhambi. Lakini sasa nimekwisha sema nao. Hivyo hawana cha kisingizio cha dhambi zao.
23 Yeyote anayenichukia mimi anamchukia na Baba pia. 24 Mimi nilifanya mambo miongoni mwa watu wa ulimwengu ambayo hayajawahi kufanywa na mtu yeyote mwingine. Kama nisingefanya mambo hayo, wao nao wasingekuwa na hatia ya dhambi. Ijapokuwa waliyaona niliyofanya, bado wananichukia mimi na Baba yangu. 25 Lakini haya yalitokea ili kuweka wazi yaliyoandikwa katika sheria zao: ‘Walinichukia bila sababu yoyote.’”[a]
© 2017 Bible League International