Revised Common Lectionary (Complementary)
4 Hata kama ninaweza kujitumainisha mimi mwenyewe, bado sifanyi hivyo. Ikiwa kuna watu wanadhani wana sababu za kutumaini sifa za kibinadamu, wanapaswa kujua kuwa nina sababu zaidi za kufanya hivyo. 5 Nilitahiriwa siku ya nane baada ya kuzaliwa. Mimi ni Myahudi wa kabila la Benjamini. Mimi ni Mwebrania halisi, hata wazazi wangu pia. Nikawa Farisayo na nilitii torati kwa uangalifu sana. 6 Nilikuwa na hamu sana ya kumridhisha Mungu[a] hata nikalitesa kanisa. Kwa usahihi niliitii sheria ya Musa.
7 Wakati fulani mambo haya yote yalikuwa muhimu kwangu. Lakini kwa sababu ya Kristo, sasa ninayachukulia mambo haya yote kuwa yasiyo na thamani. 8 Na si haya tu, lakini sasa ninaelewa kuwa kila kitu ni hasara tu ukilinganisha na thamani kuu zaidi ya kumjua Kristo Yesu, ambaye sasa ni Bwana wangu. Kwa ajili yake nilipoteza kila kitu. Na ninayachukulia yote kama kinyesi, ili nimpate Kristo. 9 Ninataka niwe wake. Katika Kristo ninayo haki mbele za Mungu, lakini kuwa na haki mbele za Mungu hakuji kwa kuitii sheria, Bali inakuja toka kwa Mungu kupitia imani kwa[b] Kristo. Mungu anatumia imani yangu kwa Kristo kunihesabia haki. 10 Ninachotaka ni kumjua Kristo na nguvu iliyomfufua kutoka kwa wafu. Ninataka kushiriki katika mateso yake na kuwa kama yeye hata katika kifo chake. 11 Kisha mimi mwenyewe naweza kuwa na matumaini kwamba nitafufuliwa kutoka kwa wafu.
Kuyafikia Malengo
12 Sisemi kuwa nimekwisha kupata ujuzi huo au kuifikia shabaha ya mwisho. Lakini bado ninajitahidi kuifikia shabaha kwa kuwa ndivyo ambavyo Kristo Yesu anataka nifanye. Ndiyo sababu alinifanya kuwa wake. 13 Kaka na dada zangu, ninajua ya kuwa bado nina safari ndefu. Lakini kuna kitu kimoja ninachofanya, nacho ni kusahau yaliyopita na kujitahidi kwa kadri ninavyoweza kuyafikia malengo yaliyo mbele yangu. 14 Ninaendelea kupiga mbio kuelekea mwisho wa mashindano ili niweze kushinda tuzo ambayo Mungu ameniitia kutoka mbinguni kwa njia ya Kristo Yesu.
Mwanamke Ampa Yesu Heshima
(Mt 26:6-13; Mk 14:3-9)
12 Siku sita kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu alienda Bethania. Huko ndiko alikoishi Lazaro, yule mtu aliyefufuliwa na Yesu kutoka wafu. 2 Hapo walimwandalia Yesu karamu ya chakula. Naye Martha alihudumu na Lazaro alikuwa mmoja wa watu waliokuwa wakila chakula pamoja na Yesu. 3 Mariamu akaleta manukato ya thamani sana yaliyotengenezwa kwa nardo asilia kwenye chombo chenye ujazo wa nusu lita[a] hivi. Akayamwaga manukato hayo miguuni mwa Yesu. Kisha akaanza kuifuta miguu ya Yesu kwa nywele zake. Harufu nzuri ya manukato hayo ikajaa nyumba nzima.
4 Yuda Iskariote, mmoja wa wafuasi wa Yesu, naye alikuwepo hapo. 5 Yuda ambaye baadaye angemkabidhi Yesu kwa maadui zake akasema, “Manukato hayo yana thamani ya mshahara wa mwaka[b] wa mtu. Bora yangeuzwa, na fedha hizo wangepewa maskini.” 6 Lakini Yuda hakusema hivyo kwa vile alikuwa anawajali sana maskini. Alisema hivyo kwa sababu alikuwa mwizi. Naye ndiye aliyetunza mfuko wa fedha za wafuasi wa Yesu. Naye mara kadhaa aliiba fedha kutoka katika mfuko huo.
7 Yesu akajibu, “Msimzuie. Ilikuwa sahihi kwake kutunza manukato haya kwa ajili ya siku ya leo; siku ambayo maziko yangu yanaandaliwa. 8 Nyakati zote mtaendelea kuwa pamoja na hao maskini.[c] Lakini si kila siku mtakuwa pamoja nami.”
© 2017 Bible League International