Old/New Testament
27 Usiku wa kumi na nne tulikuwa bado tunasukumwa na upepo katika bahari ya Adriatiki. Mabaharia wakadhani tulikuwa karibu na nchi kavu. 28 Wakatupa kamba iliyofungwa kitu kizito kwenye ncha yake. Wakakuta kwamba kina cha maji ni futi mia moja na ishirini.[a] Wakaendelea mbele kidogo na kutupa kamba tena. Kina kilikuwa futi tisini.[b] 29 Mabaharia waliogopa kwa kudhani kwamba tungegonga miamba, hivyo wakatupa nanga nne kwenye maji. Kisha wakaomba mchana ufike. 30 Baadhi ya mabaharia walitaka kuiacha meli, waliishusha majini mtumbwi wa kuokolea. Walitaka watu wengine wadhani kuwa walikuwa wanatupa nanga upande wa mbele wa meli. 31 Lakini Paulo alimwambia ofisa wa jeshi na askari wengine, “Iwapo watu hawa hawatakaa ndani ya meli, mtapoteza matumaini yote ya kupona.” 32 Hivyo askari wakakata kamba na kuuacha mtumbwi uanguke majini.
33 Kabla ya kupambazuka Paulo alianza kuwashawishi watu wote kula. Alisema, “Kwa wiki mbili mmekuwa mnasubiri na kuangalia, hamjala kwa siku kumi na nne. 34 Sasa ninawasihi mle chakula, mnakihitaji ili kuishi. Hakuna hata mmoja wenu atakayepoteza hata unywele mmoja kutoka kwenye kichwa chake.” 35 Baada ya kusema hili, Paulo alichukua baadhi ya mikate akamshukuru Mungu kwa ajili ya mikate hiyo mbele yao wote. Akakata kipande na kuanza kula. 36 Watu wote wakafarijika na kuanza kula pia. 37 (Walikuwemo watu mia mbili sabini na sita ndani ya meli.) 38 Tulikula kila tulichohitaji. Kisha tukaanza kumwaga nafaka baharini ili meli iwe nyepesi.
Meli Yaharibiwa
39 Mchana ulipofika, mabaharia waliiona nchi kavu, lakini hawakupafahamu mahali pale. Waliona ghuba yenye ufukwe na walitaka kuipeleka meli ufukweni ikiwa wangeweza. 40 Hivyo walikata kamba kwenye nanga na kuziacha nanga ndani ya bahari. Wakati huo huo walifungua kamba zilizokuwa zinaushikilia usukani. Kisha wakanyanyua tanga la mbele na kutweka tanga kuelekea ufukweni. 41 Lakini meli uligonga mwamba wa michanga. Sehemu ya mbele ya meli ilikwama pale na haikuweza kutoka. Kisha mawimbi makubwa yakaanza kuvunja sehemu ya nyuma ya meli vipande vipande.
42 Askari waliamua kuwaua wafungwa ili asiwepo mfungwa hata mmoja atakayeogelea na kutoroka. 43 Lakini Yulio, ofisa wa jeshi alitaka Paulo asiuawe. Hivyo hakuwaruhusu askari kuwaua wafunga. Aliwaambia watu wanaoweza kuogelea, waruke majini kwenda nchi kavu. 44 Wengine walitumia mbao au vipande vya meli. Hivi ndivyo ambavyo watu wote walifika nchi kavu wakiwa salama.
© 2017 Bible League International