Old/New Testament
Barua kwa Waamini Wasio Wayahudi
22 Mitume, wazee na kanisa lote wakataka kuwatuma baadhi ya watu wafuatane na Paulo na Barnaba kwenda Antiokia. Wakawachagua baadhi ya watu kutoka miongoni mwao wenyewe. Waliwachagua Yuda (ambaye pia aliitwa Barsaba) na Sila, watu walioheshimiwa na waamini. 23 Kundi la waamini likaandika barua na kuwatuma watu hawa. Barua ilisema:
Kutoka kwa mitume na wazee, ndugu zenu.
Kwa ndugu wote wasio Wayahudi katika mji wa Antiokia na katika majimbo ya Shamu na Kilikia.
Ndugu Wapendwa:
24 Tumesikia kuwa baadhi ya watu kutoka kwetu walikuja kwenu. Walichosema kiliwasumbua na kuwaudhi. Lakini hatukuwaambia kufanya hili. 25 Sisi sote tumekubaliana kuwachagua baadhi ya watu na kuwatuma kwenu. Watakuwa na rafiki zetu wapendwa, Barnaba na Paulo. 26 Barnaba na Paulo wameyatoa maisha yao kumtumikia Bwana wetu Yesu Kristo. 27 Hivyo tumewatuma Yuda na Sila pamoja nao. Watawaambia mambo yanayofanana. 28 Imempendeza Roho Mtakatifu na sisi kwamba tusiwatwishe mizigo ya ziada, isipokuwa kwa mambo haya ya muhimu:
29 Msile chakula kilichotolewa kwa sanamu.
Msile nyama inayotokana na wanyama walionyongwa au nyama ambayo bado ina damu ndani yake.
Msijihusishe na uzinzi.
Mkijitenga na mambo haya, mtakuwa mnaenenda vyema.
Wasalamu.
30 Hivyo Paulo, Barnaba, Yuda, na Sila waliondoka Yerusalemu na kwenda Antiokia. Walipofika huko walilikusanya kundi la waamini pamoja na wakawapa barua. 31 Waamini walipoisoma, wakafurahi na kufarijika. 32 Yuda na Sila ambao pia walikuwa manabii, waliwatia moyo waamini kwa maneno mengi na kuwafanya waimarike katika imani yao. 33 Baada ya Yuda na Sila kukaa pale kwa muda, waliondoka. Waamini waliwaruhusu waende kwa amani kisha wakarudi Yerusalemu kwa wale waliowatuma. 34 [a]
35 Lakini Paulo na Barnaba walikaa Antiokia. Wao na wengine wengi waliwafundisha waamini na kuwahubiri watu wengine Habari Njema kuhusu Bwana.
Paulo na Barnaba Watengana
36 Wakati fulani baadaye, Paulo akamwambia Barnaba, “Turudi katika miji yote tulikowahubiri watu ujumbe wa Bwana. Tuwatembelee waamini tuone wanaendeleaje.”
37 Barnaba alitaka Yohana Marko afuatane nao pia. 38 Lakini Yohana Marko hakukaa nao mpaka mwisho katika safari ya kwanza. Aliwaacha Pamfilia. Hivyo Paulo alisisitiza kuwa wasiende pamoja naye wakati huu. 39 Paulo na Barnaba walikuwa na mjadala mkali kuhusu hili. Ulikuwa mbaya sana ikabidi watengane na kwenda njia tofauti. Barnaba akatweka tanga kwenda Kipro, akamchukua Marko pamoja naye.
40 Paulo alimchagua Sila kwenda naye. Waamini Antiokia walimweka Paulo katika uangalizi wa Bwana na kumtuma. 41 Paulo na Sila walikwenda kwa kupitia katika majimbo ya Shamu na Kilikia, wakiyasaidia makanisa kuimarika.
© 2017 Bible League International