New Testament in a Year
Kuja kwa Roho Mtakatifu
2 Siku ya Pentekoste ilipofika, wote walikuwa pamoja sehemu moja. 2 Ghafla sauti ikaja kutoka mbinguni. Ilikuwa kama sauti ya upepo mkali unaovuma. Sauti hii ikajaa katika nyumba yote walimokuwa. 3 Waliona miali iliyoonekana kama ndimi za moto. Miali ilitengana na kukaa juu ya kila mmoja wao pale. 4 Wote walijaa Roho Mtakatifu na wakaanza kuzungumza kwa lugha tofauti. Roho Mtakatifu aliwapa uwezo wa kuzungumza lugha hizi.
5 Wakati haya yanatokea, walikuwepo Wayahudi waliorudi makwao. Hawa walikuwa wacha Mungu kutoka kila taifa ulimwenguni waliokuja mjini Yerusalemu. 6 Kundi kubwa lilikusanyika kwa sababu walisikia kelele. Walishangaa kwa sababu, mitume walipokuwa wakitamka maneno kila mtu alisikia kwa lugha ya kwao.
7 Watu wote walilishangaa hili. Hawakuelewa ni kwa namna gani mitume waliweza kufanya hili. Wakaulizana, “Tazama! Watu wote hawa tunaowasikia wanatoka Galilaya.[a] 8 Lakini tunawasikia wanatamka maneno kwa lugha zetu za asili. Hili linawezekanaje? Sisi tunatoka sehemu hizo mbalimbali: 9 Parthia, Umedi, Elamu, Mesopotamia, Uyahudi, Kapadokia, Ponto, Asia, 10 Frigia, Pamfilia, Misri na maeneo ya Libya karibu na mji wa Kirene, Rumi, 11 Krete na Uarabuni. Baadhi yetu ni Wayahudi kwa kuzaliwa na wengine si Wayahudi, bali wamechagua kumwabudu Mungu kama Wayahudi. Tunatoka katika nchi hizi mbalimbali, lakini tunawasikia watu hawa wakizungumza kwa lugha zetu tofauti! Sisi sote tunaweza kuelewa yote wanayosema kuhusu matendo makuu ya Mungu.”
12 Watu wote walistaajabu na pia walichanganyikiwa. Wakaulizana, “Hii yote inamaanisha nini?” 13 Lakini wengine waliwacheka mitume, wakisema wamelewa kwa mvinyo mwingi waliokunywa.
Petro Azungumza na Watu
14 Ndipo Petro akasimama akiwa pamoja na mitume wengine kumi na moja. Akapaza sauti ili watu wote waweze kusikia. Alisema, “Ndugu zangu Wayahudi, nanyi nyote mnaoishi Yerusalemu. Nitawaeleza kuhusu jambo lililotokea, nisikilizeni kwa makini. 15 Watu hawa hawajalewa kwa mvinyo kama mnavyodhani; bado ni saa tatu asubuhi. 16 Lakini Nabii Yoeli aliandika kuhusu jambo hili mnaloliona likitokea hapa. Aliandika:
17 ‘Mungu anasema: Katika siku za mwisho,
nitaimimina Roho yangu kwa watu wote.
Wana wenu na binti zenu watatabiri.
Vijana wenu wataona maono,
na wazee wenu wataota ndoto.
18 Katika siku hizo nitaimimina Roho
yangu kwa watumishi wangu,
wanaume na wanawake, nao watatabiri.
19 Nitafanya maajabu juu angani.
Nitasababisha ishara chini duniani.
Kutakuwa damu, moto na moshi mzito.
20 Jua litakuwa giza,
na mwezi utakuwa mwekundu kama damu
kabla ya ile siku kuu yenye utukufu ya Bwana kuja.
21 Na kila amwombaye Bwana’[b] ataokolewa.(A)
© 2017 Bible League International