Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

New Testament in a Year

Read the New Testament from start to finish, from Matthew to Revelation.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Yohana 18:1-18

Yesu Akamatwa

(Mt 26:47-56; Mk 14:43-50; Lk 22:47-53)

18 Yesu alipomaliza kuomba, akaondoka pamoja na wafuasi wake kwenda ng'ambo kuvuka bonde la Kidroni. Akaenda katika bustani mahali hapo, akiwa bado pamoja na wafuasi wake.

Yuda, yule aliyehusika kumsaliti Yesu, alipafahamu mahali pale. Alipajua kwa sababu Yesu mara nyingi alikutana na wafuasi wake pale. Kwa hiyo Yuda akaongoza kundi la askari hadi katika bustani hiyo pamoja na walinzi wengine kutoka kwa viongozi wa makuhani na Mafarisayo. Hawa walikuwa wamebeba mienge, taa, na silaha.

Yesu alikwisha kujua yote ambayo yangempata. Hivyo aliwaendea na kuwauliza, “Je, ni nani mnayemtafuta?”

Wakamjibu, “Yesu kutoka Nazareti.”

Akawaambia, “Mimi ni Yesu.”[a] (Yuda yule aliyehusika kumsaliti Yesu alikuwa amesimama hapo pamoja nao.) Yesu aliposema, “Mimi ni Yesu,” wale watu walirudi nyuma na kuanguka chini.

Akawauliza tena, “Je, ni nani mnayemtafuta?”

Wakasema, “Yesu kutoka Nazareti.”

Yesu akasema, “Nimewaambia kwamba mimi ndiye Yesu. Hivyo kama mnanitafuta mimi, basi waacheni huru watu hawa waende zao.” Hii ilikuwa kuonesha ukweli wa yale aliyosema Yesu mapema: “Sikumpoteza hata mmoja wa wale ulionipa.”

10 Simoni Petro akauchomoa upanga aliokuwa ameufunga kiunoni. Akampiga nao mtumishi wa Kuhani Mkuu, na kulikata sikio lake la kulia. (Jina la mtumishi huyo lilikuwa ni Maliko.) 11 Yesu akamwambia Petro, “Rudisha jambia lako mahali pake! Ninapaswa kunywa toka kikombe[b] ambacho Baba amenipa nikinywee.”

Yesu Aletwa Mbele ya Anasi

(Mt 26:57-58; Mk 14:53-54; Lk 22:54)

12 Kisha askari hao pamoja na mkuu wao na walinzi wa Kiyahudi wakamkamata Yesu. Wakamfunga, 13 nao wakampeleka kwanza kwa Anasi, baba mkwe wa Kayafa. Kayafa alikuwa Kuhani Mkuu kwa mwaka huo. 14 Naye ndiye aliyewashauri viongozi wengine wa Kiyahudi kwamba ingemfaa mtu mmoja afe[c] kwa ajili ya watu wote.

Petro Amkana Yesu

(Mt 26:69-70; Mk 14:66-68; Lk 22:55-57)

15 Simoni Petro na mmoja wa wafuasi wengine wa Yesu walienda pamoja na Yesu. Mfuasi huyu alimfahamu kuhani mkuu. Hivyo akaingia pamoja na Yesu ndani ya uwanja wa nyumba ya kuhani mkuu. 16 Lakini Petro alisubiri nje karibu na mlango. Yule mfuasi aliyemjua kuhani mkuu alirudi nje na kuongea na mlinda mlango. Kisha alimleta Petro ndani. 17 Msichana aliyekuwepo langoni alimwambia Petro, “Je! Wewe pia ni mmoja wa wafuasi wa mtu yule?”

Petro akajibu, “Hapana, mimi siye!”

18 Ilikuwa baridi, hivyo watumishi na walinzi waliwasha moto wa kuni. Walikuwa wameuzunguka, wakipasha joto miili yao naye Petro alikuwa amesimama pamoja nao.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International