Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

New Testament in a Year

Read the New Testament from start to finish, from Matthew to Revelation.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Yohana 19:1-22

19 Kisha Pilato akaamuru Yesu aondolewe akachapwe viboko. Askari wakatengeneza taji kutokana na matawi yenye miiba na kuiweka kichwani kwake. Kisha wakamzungushia vazi la rangi ya zambarau mwilini mwake. Wakaendelea kumkaribia wakisema, “Salamu kwako mfalme wa Wayahudi!” Kisha wakampiga Yesu usoni.

Kwa mara nyingine Pilato alienda nje na kuwaambia viongozi wa Wayahudi, “Tazameni! Ninamtoa nje Yesu na kumleta kwenu. Ninataka mfahamu kuwa sijapata kwake jambo lolote ambalo kwa hilo naweza kumshitaki.” Kisha Yesu akatoka nje akiwa amevishwa taji ya miiba na vazi la rangi ya zambarau. Pilato akawaambia Wayahudi, “Huyu ndiye mtu mwenyewe!”

Viongozi wa makuhani na walinzi wa Kiyahudi walipomwona Yesu wakapiga kelele, “Mpigilieni misumari msalabani! Mpigilieni misumari msalabani!”

Lakini Pilato akajibu, “Mchukueni na mpigilieni msalabani ninyi wenyewe. Mimi sioni kosa lolote la kumshitaki.”

Viongozi wa Wayahudi wakasema, “Tunayo sheria inayosema kuwa ni lazima afe, kwa sababu alisema kuwa yeye ni Mwana wa Mungu.”

Pilato aliposikia haya, aliogopa zaidi. Hivyo akarudi ndani ya jumba lake na kumwuliza Yesu, “Wewe unatoka wapi?” Lakini Yesu hakumjibu kitu. 10 Pilato akasema, “Unakataa kusema nami? Kumbuka, ninao uwezo wa kukuweka huru au kukuua msalabani.”

11 Yesu akajibu, “Uwezo pekee ulio nao juu yangu ni ule uwezo uliopewa na Mungu. Kwa hiyo yule aliyenitoa mimi kwenu anayo hatia ya dhambi kubwa zaidi.”

12 Baada ya hayo, Pilato alijaribu kumwacha huru Yesu. Lakini viongozi wa Wayahudi wakapiga kelele, “Yeyote anayejiweka mwenyewe kuwa mfalme yuko kinyume cha Kaisari. Hivyo kama utamwacha huru mtu huyu, hiyo itakuwa na maana kuwa wewe si rafiki wa Kaisari.”

13 Pilato aliposikia maneno hayo, akamtoa nje Yesu na kumweka mahali palipoitwa “Sakafu ya Mawe.” (Kwa Kiaramu jina lake ni Gabatha.) Pale Pilato akaketi katika kiti cha hakimu. 14 Wakati huu, ilikuwa imekaribia kuwa saa sita adhuhuri katika Siku ya Matayarisho ya juma la Pasaka. Pilato akawaambia Wayahudi, “Huyu hapa mfalme wenu!”

15 Wakapiga kelele, “Mwondoe! Mwondoe! Mwue msalabani!”

Pilato akawauliza, “Mnanitaka nimwue mfalme wenu msalabani?”

Viongozi wa makuhani wakajibu, “Kaisari ndiye Mfalme pekee tuliye naye!”

16 Hivyo Pilato akamkabidhi Yesu kwao ili auawe juu ya msalaba. Askari wakamchukua Yesu.

Yesu Awambwa Msalabani

(Mt 27:32-44; Mk 15:21-32; Lk 23:26-43)

17 Naye Yesu akaubeba msalaba wake hadi mahali panapoitwa “Fuvu la Kichwa”. (Kwa Kiaramu mahali hapo paliitwa “Golgotha”.) 18 Hapo wakampigilia Yesu kwa misumari katika msalaba. Pia wakawapigilia kwa misumari watu wengine wawili kwenye misalaba miwili tofauti. Kila mmoja akawekwa pembeni upande wa kushoto na kuume wa msalaba wa Yesu naye akawa katikati yao.

19 Pilato akawaambia waandike kibao na kisha kukiweka juu ya msalaba. Kibao hicho kiliandikwa na kilisema, “Yesu wa Nazareti, Mfalme wa Wayahudi.” 20 Kibao hicho kiliandikwa kwa Kiaramu, Kirumi na Kiyunani. Wayahudi walio wengi walikisoma kibao hicho, kwa sababu mahali ambapo Yesu alipigiliwa kwa misumari msalabani palikuwa karibu na mji.

21 Viongozi wa makuhani wa Kiyahudi wakamwambia Pilato, “Usiandike, ‘Mfalme wa Wayahudi.’ Bali andika, ‘Mtu huyu alisema, Mimi ni Mfalme wa Wayahudi.’”

22 Pilato akawajibu, “Sitayabadili yale niliyokwisha kuyaandika.”

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International