New Testament in a Year
Yesu Apelekwa kwa Gavana Pilato
(Mk 15:1; Lk 23:1-2; Yh 18:28-32)
27 Mapema asubuhi, viongozi wote wa makuhani na viongozi wazee walikutana na kuamua kumwua Yesu. 2 Wakamfunga kamba, wakamwondoa na kwenda kumkabidhi kwa Pilato, gavana wa Kirumi.
Yuda Ajiua
(Mdo 1:18-19)
3 Baada ya kumkabidhi Yesu, Yuda aliona kila kitu kilichotokea na kujua kuwa wameamua kumwua Yesu. Naye alihuzunika sana kutokana na kile alichokifanya. Hivyo alirudisha vile vipande thelathini vya sarafu vya fedha kwa wakuu wa makuhani na viongozi wazee. 4 Yuda aliwaambia, “Nimetenda dhambi. Nimemsaliti kwenu mtu asiye na hatia ili auawe.”
Viongozi wa Kiyahudi wakajibu, “Hilo halituhusu. Ni tatizo lako, siyo letu sisi.”
5 Hivyo Yuda akavitupa vipande thelathini vya fedha Hekaluni, kisha akatoka akaenda kujinyonga.
6 Viongozi wa makuhani wakaviokota vile vipande vya fedha Hekaluni. Wakasema, “Sheria yetu haituruhusu kuweka fedha hii katika hazina ya Hekalu, kwa sababu fedha hii imelipwa kwa ajili ya kifo, ni fedha yenye damu.” 7 Hivyo wakaamua kutumia fedha hiyo kwa kununulia shamba linaloitwa Shamba la Mfinyanzi kwa ajili ya kuwazikia wageni wanapokufa wakiwa ziarani katika mji wa Yerusalemu. 8 Ndiyo sababu eneo hilo bado linaitwa Shamba la Damu. 9 Hili lilitimiza maneno ya nabii Yeremia aliposema:
“Walichukua sarafu thelathini za fedha. Hicho ni kiasi ambacho Waisraeli waliamua kulipa kwa ajili ya uhai wake. 10 Walizitumia sarafu hizo thelathini za fedha kununulia shamba la mfinyanzi, kama Bwana alivyoniamuru.”[a]
Gavana Pilato Amhoji Yesu
(Mk 15:2-5; Lk 23:3-5; Yh 18:33-38)
11 Yesu alisimama mbele ya Gavana, Pilato, ambaye alimwuliza Yesu, “Wewe ni mfalme wa Wayahudi?”
Yesu akajibu, “Waweza kusema hivyo.”
12 Lakini viongozi wa makuhani na viongozi wazee wa Kiyahudi walipomshutumu, hakusema kitu.
13 Hivyo Pilato akamwambia, “Husikii mashtaka haya yote wanayokushtaki wewe? Kwa nini hujibu?”
14 Lakini Yesu hakujibu kitu, gavana alishangaa sana.
Pilato Ajaribu Kumwachia Huru Yesu
(Mk 15:6-15; Lk 23:13-25; Yh 18:39-19:16)
15 Kila mwaka wakati wa Pasaka, gavana angemwachia huru mfungwa mmoja yeyote ambaye watu wangetaka aachiwe huru. 16 Wakati huo alikuwepo mtu gerezani aliyejulikana kuwa ni mtu mbaya. Mtu huyu aliitwa Baraba.
17 Kundi la watu lilipokusanyika, Pilato aliwaambia, “Nitamwacha huru mtu mmoja. Mnataka nani nimwache huru: Baraba au Yesu aitwaye Masihi?” 18 Pilato alijua kuwa viongozi wa makuhani na viongozi wazee wa Kiyahudi walimkabidhi Yesu kwake kwa sababu walikuwa wanamwonea wivu.
19 Pilato alipokuwa ameketi kwenye kiti cha hukumu, mkewe akamtumia ujumbe uliosema, “Usifanye jambo lolote juu ya huyo mtu. Hana hatia. Nimeota ndoto juu yake usiku, na ndoto hiyo imenihangaisha sana.”
20 Lakini viongozi wa makuhani na viongozi wazee wa Kiyahudi waliwaambia watu waombe Baraba aachiwe huru na Yesu auawe.
21 Pilato akasema, “Nina Baraba na Yesu. Je, mnataka nimwache huru yupi?”
Watu wakajibu, “Baraba!”
22 Pilato akauliza, “Sasa nimfanye nini Yesu, aitwaye Masihi?”
Watu wote wakasema, “Mwue msalabani!”
23 Pilato akauliza, “Kwa nini mnataka nimwue Yesu? Amefanya kosa gani?”
Lakini walipaza sauti wakisema, “Mwue msalabani!”
24 Pilato akaona hakuna jambo ambalo angefanya ili kubadili nia yao. Kiukweli ilionekana wazi kuwa kungetokea fujo. Hivyo alichukua maji na kunawa mikono yake[b] mbele yao wote. Akasema, “Sina hatia na kifo cha mtu huyu. Ninyi ndio mnaofanya hili!”
25 Watu wakajibu, “Tutawajibika kwa kifo chake sisi wenyewe na hata watoto wetu!”
26 Kisha Pilato akamwachia huru Baraba. Na akawaambia baadhi ya askari wamchape Yesu viboko. Kisha akamkabidhi Yesu kwa askari ili akauawe msalabani.
© 2017 Bible League International