Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

New Testament in a Year

Read the New Testament from start to finish, from Matthew to Revelation.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Mathayo 20:17-34

Yesu Azungumza Tena Kuhusu Kifo Chake

(Mk 10:32-34; Lk 18:31-34)

17 Yesu alikuwa anakwenda Yerusalemu akiwa na wafuasi wake kumi na wawili. Walipokuwa wakitembea, aliwakusanya pamoja wafuasi hao na kuzungumza nao kwa faragha. Akawaambia, 18 “Tunakwenda Yerusalemu. Mwana wa Adamu atatolewa kwa viongozi wa makuhani na walimu wa sheria, nao watasema ni lazima auawe. 19 Watamkabidhi wa wageni, watakaomcheka na kumpiga kwa mijeledi, kisha watamwua kwenye msalaba. Lakini siku ya tatu baada ya kifo chake, atafufuliwa kutoka kwa wafu.”

Mama Ataka Upendeleo Maalum kwa Wanaye

(Mk 10:35-45)

20 Ndipo mke wa Zebedayo akamjia Yesu akiwa na wanaye. Akainama mbele ya Yesu na akamwomba amtendee kitu.

21 Yesu akasema, “Unataka nini?”

Akasema, “Niahidi kuwa mmoja wa wanangu atakaa upande wa kuume na mwingine wa kushoto katika ufalme wako.”

22 Hivyo Yesu akawaambia wana wa Zebedayo, “Hamwelewi mnachokiomba. Mnaweza kukinywea kikombe[a] ambacho ni lazima nikinywee?”

Wana wa Zebedayo wakajibu, “Ndiyo tunaweza!”

23 Yesu akawaambia, “Ni kweli kuwa mtakinywea kikombe nitakachokinywea. Lakini si mimi wa kuwaambia ni nani ataketi mkono wangu wa kuume au wa kushoto. Baba yangu amekwisha amua ni nani ataketi kuume au kushoto kwangu. Amekwisha andaa nafasi hizo kwa ajili yao.”

24 Wafuasi wengine kumi waliposikia hili walikasirika kwa ajili ya wale ndugu wawili. 25 Hivyo Yesu akawaita pamoja, akawaambia, “Mnajua kuwa watawala wa watu wasio Wayahudi[b] wanapenda kuonesha nguvu yao kwa watu. Na viongozi wao muhimu wanapenda kutumia mamlaka yao yote juu ya watu. 26 Lakini isiwe hivyo miongoni mwenu. Kila anayetaka kuwa kiongozi wenu lazima awe mtumishi wenu. 27 Kila anayetaka kuwa wa kwanza ni lazima awatumikie ninyi nyote kama mtumwa. 28 Fanyeni kama nilivyofanya: Mwana wa Adamu hakuja ili atumikiwe na watu. Alikuja ili awatumikie wengine na kutoa maisha yake ili kuwaokoa watu wengi.”

Yesu Awaponya Watu Wawili Wasiyeona

(Mk 10:46-52; Lk 18:35-43)

29 Yesu na wanafunzi wake walipokuwa wanaondoka Yeriko, umati mkubwa wa watu ulimfuata. 30 Walikuwepo wasiyeona wawili wamekaa kando ya njia. Waliposikia kuwa Yesu anapita pale walipaza sauti wakasema, “Bwana, Mwana wa Daudi, tafadhali tusaidie!”

31 Watu waliwakemea wale wasiyeona, wakawaambia wanyamaze. Lakini waliendelea kupaza sauti zao zaidi na zaidi, “Bwana, Mwana wa Daudi, tafadhali tusaidie!”

32 Yesu alisimama na kuwaambia, “Mnataka niwafanyie nini?”

33 Wakajibu, “Bwana, tunataka tuweze kuona.”

34 Yesu aliwahurumia wale wasiyeona. Akayagusa macho yao, na mara hiyo hiyo wakaanza kuona. Wakawa wafuasi wa Yesu.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International