New Testament in a Year
Tahadhari Kutokana na Yaliyotokea Zamani
10 Ndugu zangu, sitaki mshindwe kutambua umuhimu wa kile kilichowatokea baba zetu waliokuwa na Musa. Walifunikwa na wingu,[a] na walipita katika bahari. 2 Walibatizwa[b] wote katika Musa katika wingu na katika bahari. 3 Wote walikula chakula kilichotolewa na Roho wa Mungu, 4 na wote walikunywa kinywaji kinachotolewa na Roho wa Mungu. Kinywaji walichokunywa kilitoka katika mwamba wa roho uliokuwa pamoja nao, na mwamba huo ni Kristo. 5 Lakini Mungu hakupendezwa na wengi wao, na hivyo waliangamizwa jangwani.
6 Mambo haya yaliyotokea ni tahadhali kwa ajili yetu. Mifano hii itufanye tuache kutamani maovu kama baadhi yao walivyofanya. 7 Msiabudu sanamu kama ambavyo baadhi yao walifanya. Na kama Maandiko yanavyosema, “Waliketi chini kula na kunywa kisha wakasimama kucheza.”(A) 8 Tusifanye dhambi ya uzinzi kama baadhi yao walivyofanya na watu ishirini na tatu elfu miongoni mwao wakafa. 9 Tusimjaribu Kristo[c] kama vile baadhi yao walivyofanya. Kwa sababu hiyo, waliuawa na nyoka. 10 Na msinung'unike kama baadhi yao walivyofanya na wakauawa na malaika anayeangamiza.
11 Mambo yaliyowapata wale watu ni mifano na yaliandikwa ili kututahadharisha sisi tunaoishi nyakati hizi za mwisho. 12 Hivyo kila anayedhani kuwa yuko imara katika imani yake, basi awe mwangalifu asianguke. 13 Majaribu mliyonayo ni yale yale waliyonayo watu wote. Lakini Mungu ni mwaminifu maana hataacha mjaribiwe kwa kiwango msichoweza kustahimili. Mnapojaribiwa, Mungu atawapa mlango wa kutoka katika jaribu hilo. Ndipo mtaweza kustahimili.
14 Hivyo rafiki zangu wapenzi, zikimbieni ibada za sanamu. 15 Ninyi ni watu wenye akili. Upimeni ukweli wa haya ninayosema sasa. 16 Kikombe cha baraka[d] tunachokitolea shukrani ni ushirika wa sadaka ya damu ya Kristo, sawa? Na mkate ule tunaomega, ni ushirika wa mwili wa Kristo, sawa? 17 Kuna mkate mmoja, nasi tulio wengi tu mwili mmoja, kwa kuwa tunashiriki katika mkate huo mmoja.
18 Na fikirini kuhusu Waisraeli wanavyofanya. Wanapokula sadaka, wanaunganishwa pamoja kwa kugawana kile kilichotolewa kwenye madhabahu.
© 2017 Bible League International