Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

New Testament in a Year

Read the New Testament from start to finish, from Matthew to Revelation.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
1 Wakorintho 15:29-58

29 Ikiwa hakuna atakayefufuliwa kutoka kwa wafu, sasa watu wanafikiri wanafanya nini kwa kubatizwa kwa ajili ya wale waliokufa? Ikiwa wafu hawafufuliwi kamwe, kwa nini watu wanabatizwa kwa ajili yao?

30 Na vipi kuhusu sisi? Kwa nini tunajiweka katika hatari wakati wote? 31 Ninakumbana na kifo kila siku. Ni kweli, ndugu zangu kwamba ninajivuna kwa sababu ninyi ni wa Kristo Yesu Bwana wetu. 32 Niliwapiga wanyama wa porini kule Efeso. Ikiwa nilifanya hivyo kwa sababu za kibinadamu tu, sijapata kitu. Ikiwa hatufufuliwi kutoka kwa wafu, “basi tule na tunywe, kwa sababu tutakufa kesho.”(A)

33 Msidanganywe: “Marafiki wabaya huharibu tabia njema.” 34 Rudieni kuwaza kwenu kwa usahihi na acheni kutenda dhambi. Baadhi yenu hamumjui Mungu. Ninasema hivi ili niwafedheheshe.

Tutakuwa na Mwili wa Namna Gani?

35 Lakini mtu mmoja anaweza kuuliza, “Waliokufa wanafufuliwaje? Watakuwa na mwili wa namna gani?” 36 Haya ni maswali ya kijinga. Unapopanda kitu fulani, ni lazima kife udongoni kabla hakijawa hai na kuota. 37 Na unapopanda kitu fulani, unachopanda hakina “mwili” sawa na ule kitakachokuwa nao baadaye. Unapanda mbegu, pengine ngano au kitu kingine. 38 Na yeye Mungu hutoa mwili kwa kila aina ya mbegu. 39 Vitu vyote vilivyoumbwa kwa mwili haviko sawa: Wanadamu wana aina moja ya mwili, wanyama wana aina nyingine, ndege wana nyingine na samaki nao wana aina yao. 40 Pia kuna miili ya kimbingu na miili ya kidunia. Lakini uzuri wa miili ya kimbingu ni wa aina yake na uzuri wa miili ya kidunia ni kitu kingine. 41 Jua lina uzuri wa aina yake, mwezi una aina yake na nyota zina aina nyingine ya uzuri. Na kila nyota iko tofauti kwa uzuri wake.

42 Ndivyo itakavyokuwa waliokufa watakapofufuliwa na kuwa hai. Mwili “uliopandwa” kaburini utaharibika na kuoza, lakini utafufuliwa katika uhai usioharibika. 43 Mwili hauna heshima “unapopandwa”. Lakini utakapofufuliwa, utakuwa na utukufu. Mwili unakuwa dhaifu “unapopandwa”. Lakini unapofufuliwa, unakuwa na nguvu nyingi. 44 Mwili unaopandwa ni mwili wa kawaida, wa asili. Utakapofufuliwa utakuwa mwili wa ajabu uliopewa uwezo na Roho.

Kuna mwili wa asili unaoonekana kwa macho. Na hivyo kuna mwili wa Kiroho wa ajabu. 45 Kama Maandiko yanavyosema, “Mtu[a] wa kwanza, Adamu, alikuwa kiumbe asili kilichokuwa hai.”(B) Lakini Adamu[b] wa mwisho akafanyika roho. 46 Mtu wa kiroho hakuja kwanza. Mtu wa asili anayeonekana kwa macho ndiye alikuja kwanza; kisha akaja wa kiroho. 47 Mtu wa kwanza alitokana na mavumbi ya dunia. Mtu wa pili alitoka mbinguni. 48 Watu wote ni wa dunia. Wako sawa na yule mtu wa kwanza wa dunia. Lakini wale walio wa mbinguni wako kama mtu wa mbinguni. 49 Tumeivaa sura ya mtu aliyetoka mavumbini, pia tutaivaa sura ya mtu aliyetoka mbinguni.

50 Ninawaambia hili ndugu zangu: Miili yetu na nyama na damu haiwezi kuwa na nafasi katika ufalme wa Mungu. Kitu kitakachoharibika hakiwezi kuwa na sehemu katika kitu kisichoharibika kamwe. 51 Lakini sikilizeni, ninawaambia siri hii: Sote hatutakufa, lakini sote tutabadilishwa. 52 Itachukuwa sekunde moja. Tutabadilishwa kufumba na kufumbua. Hili litatokea parapanda ya mwisho itakapopulizwa. Parapanda itakapolia wale waliokufa watafufuliwa ili waishi milele. Na tutabadilishwa sote. 53 Mungu ataibadilisha miili yetu ili isiharibike kamwe. Mwili huu unaokufa utabadilishwa na kuwa mwili usiokufa. 54 Hivyo mwili huu unaokufa utajivika kutokufa. Hili litakapotokea, ndipo Maandiko yatatimilizwa:

“Mauti imemezwa katika ushindi.(C)
55 Ewe kifo, ushindi wako uko wapi?
    Nguvu yako ya kudhuru iko wapi?”(D)

56 Dhambi ni nguvu ya mauti inayodhuru, na nguvu ya dhambi ni sheria. 57 Lakini tunamshukuru Mungu anayetupa ushindi kupitia Yesu Kristo Bwana wetu!

58 Hivyo, kaka na dada zangu, simameni imara. Msiruhusu kitu chohote kiwabadilishe. Jitoeni nafsi zenu kikamilifu kwa kazi yenu katika Bwana. Mnajua ya kuwa chochote mnachofanya kwa ajili ya Bwana hakitapotea bure bila manufaa.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International