New Testament in a Year
21 Kama Maandiko[a] yanavyosema,
“Kwa kutumia wanaozungumza lugha tofauti
na kutumia midomo ya wageni,
nitazungumza na watu hawa,
hata hivyo, hawatanitii.”(A)
Hivi ndivyo Bwana anasema.
22 Na kutokana na hili tunaona kwamba matumizi ya lugha zingine ni ishara kuonesha namna ambavyo Mungu anawashughulikia wasioamini, na si walioamini. Na unabii unaonesha namna ambavyo Mungu hutenda kazi kupitia wanaoamini, na si wasioamini. 23 Chukulieni kuwa kanisa lote limekusanyika nanyi nyote mkaanza kusema kwa lugha zingine. Ikiwa baadhi ya watu wasio sehemu ya kundi lenu au wasio waamini wataingia katika kusanyiko lenu, watasema ninyi ni wendawazimu. 24 Lakini chukulieni kuwa ninyi nyote mnatabiri na mtu asiyeamini ama asiyekuwa sehemu ya kundi lenu akaingia. Dhambi zao zitawekwa wazi kwao, na watahukumiwa kwa kila kitu mtakachosema. 25 Mambo ya siri katika mioyo yao yatajulikana. Na watapiga magoti na kumwabudu Mungu. Watakiri na kusema, “Pasipo shaka, Mungu yuko hapa pamoja nanyi.”[b]
Mikutano Yenu Inapaswa Kuwasaidia Wote
26 Basi ndugu, mnapaswa kufanya nini? Mnapokusanyika, mtu mmoja ana wimbo, mwingine ana mafundisho na mwingine ana kweli mpya kutoka kwa Mungu. Mmoja anasema kwa lugha nyingine na mwingine anafasiri lugha hiyo. Cho chote mnachofanya lazima kiwe na lengo la kumfanya kila mmoja wenu akue katika imani. 27 Mnapokusanyika, ikiwa kuna yeyote atasema na kanisa katika lugha, iwe watu wawili tu au isiwe zaidi ya watu watatu. Na wanapaswa wanene kwa zamu, mmoja baada ya mwingine. Na mwingine afasiri kile wanachosema. 28 Lakini ikiwa hakuna mfasiri, basi mtu yeyote anayesema kwa lugha nyingine anapaswa kunyamaza kimya. Wanapaswa kuzungumza katika nafsi zao wenyewe ama na Mungu.
29 Na manabii wawili au watatu tu ndiyo wanapaswa kuzungumza. Wengine watathmini kile wanachosema. 30 Na ujumbe kutoka kwa Mungu ukimjia mtu aliyekaa, mzungumzaji wa kwanza anapaswa kunyamaza. 31 Nyote mnaweza kutabiri mmoja baada ya mwingine. Kwa njia hii kila mmoja anaweza kufundishwa na kutiwa moyo. 32 Roho za manabii ziko chini ya udhibiti wa manabii[c] wenyewe. 33 Mungu si Mungu wa machafuko lakini ni Mungu wa amani. Hii ni kanuni kwa ajili ya mikutano yote ya watu wa Mungu.
34 Wanawake wanapaswa kunyamaza katika mikutano hii ya kanisa. Kama Sheria ya Musa inavyosema, hawaruhusiwi kuzungumza pasipo utaratibu bali wawe chini ya mamlaka. 35 Wakiwa na jambo wanalotaka kujua, wawaulize waume zao nyumbani. Ni aibu kwa mwanamke kuzungumza pasipo utaratibu katika mikutano ya kanisa.
36 Je, ni kutoka kwenu neno la Mungu lilikuja ama lilikuja kwa ajili yenu pekee? 37 Ikiwa yeyote kati yenu anafikiri kuwa yeye ni nabii au kwamba ana karama ya kiroho, anapaswa kuelewa kuwa ninachowaandikia ninyi nyote ni amri ya Bwana. 38 Ikiwa yeyote miongoni mwenu hatalikubali hili, basi hatakubaliwa.
39 Hivyo ndugu zangu, mzingatie sana kutabiri. Na msimzuie mtu yeyote kutumia karama ya kusema katika lugha zingine. 40 Lakini kila kitu kifanywe kwa usahihi na kwa utaratibu.
© 2017 Bible League International