M’Cheyne Bible Reading Plan
Joka na Mwanamke Anayezaa
12 Jambo la ajabu lilionekana mbinguni: Mwanamke aliyevalishwa jua, na mwezi ulikuwa chini ya miguu yake alionekana. Alikuwa na taji yenye nyota kumi na mbili kichwani pake. 2 Alikuwa na mimba na alilia kwa uchungu kwa sababu alikuwa karibu ya kuzaa.
3 Kisha ajabu nyingine ikaonekana mbinguni: Alikuweko huko joka mkubwa mwekundu. Joka huyo alikuwa na vichwa saba na alikuwa na taji juu ya kila kichwa. Na alikuwa na pembe kumi. 4 Mkia wake ulizoa theluthi ya nyota na kuziangusha duniani. Joka hili lilisimama mbele ya mwanamke aliyekuwa karibu ya kuzaa mtoto. Lilitaka kumla mtoto mara atakapozaliwa.
5 Mwanamke alimzaa mtoto wa kiume, atakayewatawala mataifa yote kwa fimbo yake ya chuma. Na mwana wa mwanamke huyu alichukuliwa juu mbinguni kwa Mungu, kwenye kiti chake cha enzii. 6 Mwanamke alikimbilia jangwani mpaka mahali ambako Mungu amemwandalia. Huko angetunzwa kwa siku 1,260.
7 Kisha kulikuwa vita mbinguni. Mikaeli[a] na malaika zake walipigana na joka. Nalo joka na malaika zake wakapigana na Mikaeli pamoja na malaika zake, 8 lakini joka na malaika zake hawakuwa na nguvu za kutosha kushinda, na hivyo wakapoteza nafasi zao mbinguni. 9 Likatupwa chini kutoka mbinguni. (Joka hili kubwa ni nyoka yule wa zamani, aitwaye Ibilisi au Shetani, anayeudanganya ulimwengu wote.) Joka na malaika zake walitupwa duniani.
10 Kisha nilisikia sauti kubwa mbinguni ikisema:
“Ushindi na uweza na ufalme wa Mungu wetu
na mamlaka ya Masihi wake umekuja sasa,
kwa sababu mshitaki wa kaka na dada zetu
ametupwa chini.
Ndiye aliyewashitaki kwa Mungu,
mchana na usiku.
11 Walimshinda kwa sadaka ya damu ya Mwanakondoo
na kwa ujumbe wa Mungu waliowaambia watu.
Hawakuyapenda maisha yao sana.
Hawakuogopa kifo.
12 Hivyo furahi, ewe mbingu
na wote waishio humo!
Lakini ole kwa nchi na bahari,
kwa sababu Ibilisi ameshuka kwako.
Amejaa ghadhabu.
Anajua ana muda mchache.”
13 Joka alipoona amekwisha tupwa chini duniani, alimkimbiza mwanamke aliyemzaa mtoto wa kiume. 14 Lakini mwanamke alipewa mabawa mawili ya tai mkuu. Aliweza kuruka mpaka mahali palipoandaliwa kwa ajili yake jangwani. Huko atatunzwa kwa muda wa miaka mitatu na nusu akiwa mbali na joka. 15 Kisha joka lilitoa maji kama mto kutoka katika kinywa chake kuelekea kwa mwanamke ili mafuriko yamchukue. 16 Lakini nchi ilimsaidia mwanamke. Nchi ilifungua kichwa chake na kumeza mto uliotoka kwenye kinywa cha joka. 17 Kisha joka lilimkasirikia sana mwanamke. Likaenda kufanya vita na watoto wake wengine. Watoto wa mwanamke ni wale wanaozitii amri za Mungu na wanayo kweli ambayo Yesu aliifundisha.
18 Joka lilisimama ufukweni mwa bahari.
Kifo cha Lazaro
11 Alikuwepo mtu aliyekuwa mgonjwa aliyeitwa Lazaro. Huyo aliishi katika mji wa Bethania, mahali ambapo Mariamu na dada yake Martha waliishi. 2 (Mariamu ni mwanamke yule aliyempaka Bwana manukato na kumpangusa miguu kwa nywele zake.) Ndugu wa Mariamu alikuwa Lazaro, ambaye sasa alikuwa mgonjwa. 3 Kwa hiyo Mariamu na Martha walimtuma mtu kwa Yesu kumwambia, “Bwana, rafiki yako mpendwa Lazaro ni mgonjwa.”
4 Yesu aliposikia hayo alisema, “ugonjwa huu sio wa kifo. Isipokuwa, ugonjwa huu ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu. Hili limetokea ili kuleta utukufu kwa Mwana wa Mungu.” 5 Yesu aliwapenda Martha, na dada yake na Lazaro. 6 Hivyo aliposikia kwamba Lazaro ni mgonjwa, akabaki alipokuwa kwa siku mbili zaidi, 7 kisha akawaambia wafuasi wake, “Inatupasa kurudi tena Uyahudi.”
8 Wakamjibu, “Lakini Mwalimu, ni muda mfupi tu uliopita viongozi wa Wayahudi pale walijitahidi kukuua kwa mawe. Sasa unataka kwenda huko tena?”
9 Yesu akajibu, “Yako masaa kumi na mawili ya mchana katika siku. Yeyote anayetembea mchana hatajikwaa na kuanguka kwani anamulikiwa na nuru ya ulimwengu huu. 10 Lakini yeyote anayetembea usiku atajikwaa kwa sababu hana nuru[a] inayomwongoza.”
11 Kisha Yesu akasema, “Rafiki yetu Lazaro sasa amelala, lakini nitakwenda ili nimwamshe.”
12 Wafuasi wake wakajibu, “Lakini, Bwana, kama amelala ataweza kupona.” 13 Walifikiri kwamba Yesu alikuwa na maana kwamba Lazaro alikuwa amelala usingizi, lakini Yeye alikuwa na maana kuwa amefariki.
14 Kisha hapo Yesu akasema wazi wazi, “Lazaro amekufa. 15 Na ninafurahi sikuwepo hapo. Ninafurahi kwa ajili yenu kwa sababu sasa mtaniamini mimi. Twendeni kwake sasa.”
16 Ndipo Tomaso, pia aliyeitwa “Pacha”, akawaambia wafuasi wengine, “Nasi pia tutaenda kule kufa pamoja na Yesu.”
Yesu Akiwa Bethania
17 Yesu akaenda Bethania na huko akakuta Lazaro amekufa na kuwa kaburini kwa siku nne. 18 Mji wa Bethania ulikuwa kama kilomita tatu[b] kutoka Yerusalemu. 19 Wayahudi wengi wakaja ili kuwaona Martha na Mariamu. Walikuja ili kuwafariji kwa ajili ya msiba wa kaka yao, Lazaro.
20 Martha aliposikia kuwa Yesu alikuwa anakuja, alikwenda kumpokea. Lakini Mariamu alibaki nyumbani. 21 Martha akamwambia Yesu, “Bwana, kama ungalikuwepo hapa, ndugu yangu asingelikufa. 22 Lakini najua kwamba hata sasa Mungu atakupa chochote utakachomwomba.”
23 Yesu akasema, “Kaka yako atafufuka na kuwa hai tena.”
24 Martha akajibu, “Ninajua kuwa atafufuka tena wakati wa ufufuo siku ya mwisho.”
25 Yesu akamwambia, “Mimi ndiye huo ufufuo. Mimi ndiye uzima. Kila anayeniamini atakuwa na uzima, hata kama atakufa. 26 Kila atakayeniamini hatakufa kiroho hata kama atakufa kimwili. Je, Martha, unaliamini jambo hili?”
27 Martha akajibu, “Ndiyo Bwana naliamini. Nakuamini kwamba wewe ni Masihi, Mwana wa Mungu. Ndiwe unayekuja ulimwenguni.”
Yesu Alia
28 Baada ya Martha kusema maneno haya, alirejea kwa Mariamu dada yake. Aliongea naye peke yake na kusema, “Mwalimu yupo hapa. Anakutafuta.” 29 Mariamu aliposikia hivyo, aliinuka na kwenda haraka kwa Yesu. 30 Yesu hakuwa amefika kijijini. Alikuwa bado yupo pale pale Martha alipomkuta. 31 Wayahudi waliokuwepo nyumbani hapo wakimfariji Mariamu walimwona akiinuka na kuondoka ghafla. Walifikiri alikuwa anaenda kaburini kuomboleza. Hivyo wakamfuata. 32 Mariamu alienda pale Yesu alipokuwa. Naye baada ya kumwona, aliinama miguuni pake Yesu na kusema, “Bwana, kama ungekuwa hapa, kaka yangu asingekufa.”
33 Ndipo Yesu alipomwona Mariamu na watu waliokuwa pamoja naye wakilia, akahuzunika na kusikitika sana. 34 Akawauliza, “Mmemweka wapi?”
Wakasema, “Bwana, njoo uone.”
35 Yesu akalia na kutoa machozi.
36 Na Wayahudi wakasema, “Angalia! Alikuwa anampenda sana Lazaro!”
37 Lakini wengine wao wakasema, “Yesu aliyeyaponya macho ya yule mtu asiyeona kwa nini hakumsaidia Lazaro na kumzuia asife?”
Yesu Amfufua Lazaro Kutoka Mautini
38 Akiwa bado ana uchungu na kusikitika sana, Yesu akaenda kaburini. Kaburi lenyewe lilikuwa ni pango lenye jiwe kubwa lililofunika pa kuingilia. 39 Yesu akasema, “Lisogezeni pembeni hilo jiwe.”
Martha akasema, “Lakini, Bwana, ni siku nne[c] sasa tangu Lazaro alipofariki. Kutakuwa na harufu mbaya.” Martha alikuwa ni dada wa marehemu.
40 Kisha Yesu akamwambia Martha, “Unakumbuka jinsi nilivyokuambia? Je, sikukuambia kwamba kama ukiamini, ungeuona utukufu wa Mungu?”
41 Kwa hiyo wakalisogeza lile jiwe kutoka kwenye sehemu ya kuingilia. Kisha Yesu akatazama juu na kusema, “Baba, Nakushukuru kwa kuwa ulinisikia. 42 Najua kuwa siku zote unanisikia. Lakini nimeyasema mambo haya kwa ajili ya watu walioko hapa. Nataka kwamba waweze kuamini kuwa ni wewe uliyenituma.” 43 Baada ya Yesu kusema hivi akaita kwa sauti kubwa, “Lazaro, toka nje!” 44 Yule mtu aliyekuwa amekufa akatoka nje, mikono na miguu yake ilikuwa imefungwa sanda. Uso wake ulikuwa umefunikwa kwa kitambaa.
Yesu akawaambia watu, “Mfungueni hizo sanda na kumwacha aende.”
Mpango wa Kumwua Yesu
(Mt 26:1-5; Mk 14:1-2; Lk 22:1-2)
45 Walikuwepo Wayahudi wengi waliokuja kumtembelea Mariamu. Hawa walipoona aliyotenda Yesu, wengi wao wakamwamini. 46 Lakini baadhi yao wakaenda kwa Mafarisayo na kuwapa habari ya mambo aliyofanya Yesu. 47 Kisha viongozi wa makuhani na Mafarisayo wakaitisha kikao cha baraza kuu. Wakasema, “Tutafanyaje? Mtu huyu anafanya ishara nyingi sana. 48 Tukimwacha aendelee kufanya hivi, kila mtu atamwamini. Ndipo Warumi watakuja na kulichukua Hekalu na Taifa letu pia.”
49 Mmoja wa watu wale alikuwa ni Kayafa. Yeye alikuwa kuhani mkuu kwa mwaka ule. Akasema, “Ninyi hamjui lo lote! 50 Ni bora mtu mmoja akafa kwa ajili ya watu wengine badala ya taifa zima kuangamia. Ninyi bado hamjalitambua hili.”
51 Kayafa hakufikiri hivi peke yake. Hakika kama kuhani mkuu kwa mwaka ule, alikuwa akitabiri kwamba Yesu angekufa kwa ajili ya Wayahudi. 52 Kweli, angekufa kwa ajili ya Wayahudi. Lakini pia angekufa kwa ajili ya watoto wa Mungu waliotawanyika ulimwenguni pote. Angekufa ili awakusanye na kuwaweka katika kundi moja.
53 Siku ile viongozi wa Wayahudi wakaanza kupanga jinsi ya kumuua Yesu. 54 Hivyo Yesu akaacha kusafiri wazi wazi katikati ya Wayahudi. Akaelekea katika mji ulioitwa Efraimu uliokuwa kwenye eneo karibu na jangwa. Akakaa huko pamoja na wafuasi wake.
55 Wakati huo Sikukuu ya Pasaka ya Wayahudi ilikaribia. Watu wengi kutoka katika nchi yote ya Uyahudi wakaenda Yerusalemu siku chache kabla. Walienda kujitakasa tayari kwa ajili ya sikukuu hiyo. 56 Watu wakamtafuta Yesu. Nao walisimama katika maeneo ya Hekalu na kuulizana, “Je, naye atakuja kwenye sikukuu? Unafikirije wewe?” 57 Lakini viongozi wa makuhani na Mafarisayo walitoa agizo maalumu kuhusu Yesu. Walisema kuwa mtu yeyote anayejua mahali alipo Yesu awaambie ili waweze kumkamata.
© 2017 Bible League International