Read the Gospels in 40 Days
Yesu Aingia Yerusalemu Kama Mfalme
(Mk 11:1-11; Lk 19:28-38; Yh 12:12-19)
21 Yesu na wafuasi wake walipokaribia Yerusalemu, walisimama Bethfage kwenye kilima kinachoitwa Mlima wa Mizeituni. Wakiwa hapo Yesu aliwatuma wafuasi wake wawili mjini. 2 Aliwaambia, “Nendeni kwenye mji mtakaoweza kuuona huko. Mtakapoingia katika mji huo, mtamwona punda na mwanapunda wake.[a] Wafungueni wote wawili, kisha waleteni kwangu. 3 Mtu yeyote akiwauliza kwa nini mnawachukua punda, mwambieni, ‘Bwana anawahitaji. Atawarudisha mapema.’”
4 Hili lilitimiza maneno yaliyosemwa na nabii:
5 “Waambie watu wa Sayuni,[b]
‘Mfalme wako anakuja sasa.
Ni mnyenyekevu na amempanda punda.
Na amempanda mwana punda dume tena safi.’”(A)
6 Wafuasi walikwenda na kufanya yale walioambiwa na Yesu. 7 Waliwaleta kwake punda jike na mwanapunda. Waliwafunika punda kwa nguo zao na Yesu akaketi juu yao. 8 Akiwa njiani kuelekea Yerusalemu, watu wengi walitandaza mavazi yao barabarani kwa ajili Yake. Wengine walikata matawi ya miti na kuyatandaza barabarani ili kumkaribisha. 9 Wengine walimtangulia Yesu, na wengine walikuwa nyuma yake. Wote walipaza sauti wakisema:
“Msifuni[c] Mwana wa Daudi!
‘Karibu! Mungu ambariki yeye
ajaye katika jina la Bwana!’(B)
Msifuni Mungu wa mbinguni!”
10 Kisha Yesu aliingia Yerusalemu. Watu wote mjini wakataharuki. Wakauliza, “Mtu huyu ni nani?”
11 Kundi la watu waliomfuata Yesu wakajibu, “Huyu ni Yesu. Ni nabii kutoka katika mji wa Nazareti ulio Galilaya.”
Yesu Asafisha Eneo la Hekalu
(Mk 11:15-19; Lk 19:45-48; Yh 2:13-22)
12 Yesu alipoingia katika eneo la Hekalu, aliwatoa nje wote waliokuwa wanauza na kununua vitu humo. Alizipindua meza za watu waliokuwa wanabadilishana pesa. Na alipindua viti vya watu waliokuwa wanauza njiwa. 13 Yesu aliwaambia, “Maandiko yanasema, ‘Hekalu langu litaitwa nyumba ya sala.’(C) Lakini mmelibadilisha na kuwa ‘maficho ya wezi’.(D)”
14 Baadhi ya watu waliokuwa wasiyeona na walemavu wa miguu walimjia Yesu alipokuwa eneo la Hekalu, naye aliwaponya. 15 Viongozi wa makuhani na walimu wa sheria waliona mambo ya ajabu aliyokuwa anatenda. Na waliona watoto walivyokuwa wanamsifu wakisema, “Sifa kwa Mwana wa Daudi.” Mambo haya yote yaliwakasirisha makuhani na walimu wa sheria.
16 Wakamwuliza Yesu, “Unasikia wanayosema watoto hawa?”
Akajibu, “Ndiyo. Maandiko yanasema,
‘Umewafundisha watoto wadogo na watoto
wanyonyao kusifu.’(E)
Hamjasoma Maandiko haya?”
17 Kisha Yesu akawaacha na akaenda katika mji wa Bethania akalala huko.
Yesu Aulaani Mtini
(Mk 11:12-14,20-24)
18 Mapema asubuhi iliyofuata, Yesu alikuwa anarudi mjini Yerusalemu naye alikuwa na njaa. 19 Aliuona mtini karibu na njia na akaenda kuchuma tini kwenye mti huo. Yalikuwepo maua tu. Hivyo Yesu akauambia mti ule, “Hautazaa matunda tena!” Mtini ukakauka na kufa hapo hapo.
20 Wafuasi wake walipoona hili, walishangaa sana. Wakauliza, “Imekuwaje mtini ukakauka na kufa haraka hivyo?”
21 Yesu akajibu, “Ukweli ni kuwa, mkiwa na imani na msiwe na mashaka, mtaweza kufanya kama nilivyofanya kwa mti huu. Na mtaweza kufanya zaidi ya haya. Mtaweza kuuambia mlima huu, ‘Ng'oka na ujitupe baharini.’ Na ikiwa una imani, litafanyika. 22 Mkiamini, mtapokea kila mnachoomba.”
Viongozi Wawa na Mashaka Kuhusu Mamlaka ya Yesu
(Mk 11:27-33; Lk 20:1-8)
23 Yesu aliingia katika eneo la Hekalu na akaanza kufundisha humo. Viongozi wa makuhani na viongozi wa wazee wakamjia. Wakasema, “Tuambie! Una mamlaka gani ya kufanya mambo haya unayofanya? Na nani amekupa mamlaka hii?”
24 Yesu akajibu, “Nitawauliza swali pia. Mkinijibu, ndipo nitawaambia nina mamlaka gani ya kufanya mambo haya. 25 Niambieni: Yohana alipowabatiza watu, mamlaka yake ilitoka kwa Mungu au kwa wanadamu?”
Makuhani na viongozi wa Kiyahudi wakajadiliana kuhusu swali la Yesu, wakasemezana, “Tukisema, ‘Ubatizo wa Yohana ulitoka kwa Mungu,’ atasema, ‘Sasa kwa nini hamkumwamini Yohana?’ 26 Lakini hatuwezi kusema ubatizo wa Yohana ulitoka kwa watu wengine. Tunawaogopa watu, kwa sababu wote wanaamini kuwa Yohana alikuwa nabii.”
27 Hivyo wakamwambia Yesu, “Hatujui jibu.”
Yesu akasema, “Basi hata mimi siwaambii aliyenipa mamlaka ya kufanya mambo haya.”
Yesu Atumia Simulizi Kuhusu Wana Wawili
28 “Niambieni mnafikiri nini kuhusu hili: Alikuwepo mtu mwenye wana wawili. Alimwendea mwanaye wa kwanza na kumwambia, ‘Mwanangu, nenda ukafanye kazi kwenye shamba la mizabibu leo.’
29 Mwanaye akasema, ‘Siendi.’ Lakini baadaye akabadili uamuzi wake na akaenda.
30 Kisha baba akamwendea mwanaye mwingine na kumwambia, ‘Mwanangu, nenda ukafanye kazi kwenye shamba la mizabibu leo.’ Akajibu, ‘Sawa baba, nitakwenda kufanya kazi.’ Lakini hakwenda.
31 Ni yupi kati ya wana hawa wawili alimtii baba yake?”
Viongozi wa Kiyahudi wakajibu, “Ni mwana wa kwanza.”
Yesu akawaambia, “Ukweli ni huu, ninyi ni wabaya kuliko watoza ushuru na makahaba. Ukweli ni kuwa hao wataingia katika ufalme wa Mungu kabla yenu. 32 Yohana alikuja akiwaonesha njia sahihi ya kuishi, na hamkumwamini. Lakini watoza ushuru na makahaba walimwamini Yohana. Mliona yaliyotokea, lakini hamkubadilika na mlikataa kumwamini.
Yesu Atoa Simulizi Kuhusu Shamba la Mzabibu
(Mk 12:1-12; Lk 20:9-19)
33 Sikilizeni simulizi hii: Alikuwepo mtu aliyemiliki shamba la mizabibu. Alijenga uzio kuzunguka shamba lile la mizabibu na akachimba shimo kwa ajili ya kukamulia zabibu.[d] Kisha akajenga mnara wa lindo. Akalikodisha shamba kwa wakulima kisha akasafiri. 34 Wakati wa kuvuna zabibu ulipofika, akawatuma watumishi wake waende kwa wakulima ili apate gawio lake la zabibu.
35 Lakini wakulima waliwakamata wale watumishi na kumpiga mmoja wao. Wakamwua mwingine na wa tatu wakampiga kwa mawe mpaka akafa. 36 Hivyo mwenye shamba akawatuma baadhi ya watumishi wengine wengi zaidi ya aliowatuma hapo kwanza. Lakini wakulima wakawatendea kama walivyowatendea watumishi wa kwanza. 37 Hivyo mwenye shamba akaamua kumtuma mwanaye kwa wakulima. Alisema, ‘Wakulima watamheshimu mwanangu.’
38 Lakini wakulima walipomwona mwanaye, wakaambizana, ‘Huyu ni mwana wa mwenye shamba. Shamba hili litakuwa lake. Tukimwua, shamba la mizabibu litakuwa letu.’ 39 Hivyo wakulima wakamchukua mwana wa mwenye shamba, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu na kumwua.
40 Hivyo mmiliki wa shamba la mizabibu atawafanya nini wakulima hawa atakaporudi?”
41 Makuhani wa Kiyahudi na viongozi wakasema, “Kwa hakika atawaua watu hao waovu. Kisha atawakodishia wakulima wengine shamba hilo, watakaompa gawio la mazao yake wakati wa mavuno.”
42 Yesu akawaambia, “Hakika mmesoma hili katika Maandiko:
‘Jiwe walilolikataa waashi
limekuwa jiwe kuu la pembeni.
Bwana amefanya hivi,
na ni ajabu kubwa kwetu kuliona.’(F)
43 Hivyo ninawaambia kuwa, ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu na watapewa watu wanaofanya mambo anayoyataka Mungu katika ufalme wake. 44 Kila aangukaye kwenye jiwe hili atavunjika na litamsaga kila linayemwangukia.”[e]
45 Viongozi wa makuhani na Mafarisayo waliposikia simulizi hizi, wakajua kuwa Yesu alikuwa anawasema wao. 46 Walitaka kumkamata Yesu. Lakini waliogopa kwani watu waliamini kuwa Yesu ni nabii.
Simulizi Kuhusu Watu Walioalikwa Kwenye Sherehe
(Lk 14:15-24)
22 Yesu aliendelea kuwajibu viongozi wa Kiyahudi kwa mifano zaidi. Akasema, 2 “Ufalme wa Mungu unafanana na jambo lililotokea mfalme alipoandaa sherehe ya harusi kwa ajili ya mwanaye. 3 Aliwaalika baadhi ya watu. Wakati ulipofika mfalme aliwatuma watumwa wake kuwaambia watu waende kwenye sherehe. Lakini walikataa kwenda kwenye sherehe ya mfalme.
4 Ndipo mfalme aliwaita baadhi ya watumishi wengine zaidi na akawaambia namna ya kuwaambia wale aliowaalika: ‘Njooni sasa! Sherehe imeandaliwa. Nimechinja ng'ombe wangu madume na ndama wanono waliolishwa nafaka, na kila kitu kiko tayari kuliwa. Njooni kwenye sherehe ya harusi.’
5 Lakini watu walioalikwa hawakujali yale waliyoambiwa na watumwa wa mfalme. Wengine waliondoka wakaenda kufanya mambo mengine. Mmoja alikwenda shambani na mwingine alikwenda kwenye shughuli zake. 6 Wengine waliwakamata watumwa wa mfalme, wakawapiga na kuwaua. 7 Mfalme alikasirika sana na akatuma jeshi lake kuwaua wale waliowaua watumwa wake. Na jeshi likauchoma moto mji wao.
8 Kisha mfalme akawaambia watumishi wake, ‘Sherehe ya harusi iko tayari. Niliwaalika wale watu lakini hawakustahili. 9 Hivyo nendeni kwenye pembe za mitaa na mwalikeni kila mtu mtakayemwona, waambieni waje kwenye sherehe yangu.’ 10 Hivyo watumwa wake waliingia mitaani, wakawakusanya watu wote waliowaona, wabaya na wema na kuwaleta kwenye sherehe. Na jumba la sherehe likawa na wageni wengi.
11 Mfalme alipoingia ili kuwasalimu wageni, alimwona mtu ambaye hakuwa amevaa vazi rasmi la harusi. 12 Mfalme akamwuliza, ‘Rafiki ilikuwaje ukaruhusiwa kuingia humo? Hujavaa vazi nadhifu kwa arusi!’ Lakini mtu yule hakuwa na neno la kusema. 13 Hivyo mfalme akawaambia baadhi ya wale waliokuwa wanawahudumia watu kwa chakula, ‘Mfungeni mtu huyu mikono na miguu yake na mtupeni gizani, ambako watu wanalia na kusaga meno yao kwa maumivu.’
14 Ndiyo, watu wengi wamealikwa, lakini wachache tu ndiyo waliochaguliwa.”
Yesu Ajibu Swali Lenye Mtego
(Mk 12:13-17; Lk 20:20-26)
15 Kisha Mafarisayo wakaondoka mahali ambapo Yesu alikuwa anafundisha. Wakapanga mpango wa kumfanya aseme kitu ambacho wangekitumia dhidi yake. 16 Wakawatuma kwake baadhi ya wafuasi wao na baadhi ya watu kutoka katika kundi la Maherode. Watu hawa walipofika kwa Yesu wakasema, “Mwalimu, tunajua kuwa wewe ni mtu mwema na kwamba daima unafundisha ukweli kuhusu njia ya Mungu, bila kujali ni nani anakusikiliza. Huna wasiwasi namna ambavyo wengine wanaweza wakasema. 17 Sasa tuambie, unadhani ni sahihi kulipa kodi kwa Kaisari au la?”
18 Lakini Yesu alijua kuwa watu hawa walikuwa wanamtega. Hivyo akasema, “Enyi wanafiki! Kwa nini mnajaribu kunitega ili niseme jambo lililo kinyume? 19 Nionesheni sarafu inayotumika kulipa kodi.” Wakamwonesha Yesu sarafu iliyotengenezwa kwa fedha. 20 Kisha Yesu akauliza, “Picha iliyo kwenye sarafu hii ni ya nani? Na jina lililo kwenye sarafu hii ni la nani?”
21 Wakajibu, “Ni picha ya Kaisari na ni jina la Kaisari.”
Ndipo Yesu akawajibu, “Mpeni Kaisari vilivyo vyake na mpeni Mungu vilivyo vyake.”
22 Waliposikia yale Yesu aliyosema, wakashangaa na kuondoka.
Baadhi ya Masadukayo Wajaribu Kumtega Yesu
(Mk 12:18-27; Lk 20:27-40)
23 Siku hiyo hiyo baadhi ya Masadukayo walimjia Yesu. (Masadukayo hawaamini kuwepo kwa ufufuo wa wafu.) Masadukayo walimwuliza Yesu swali. 24 Wakasema, “Mwalimu, Musa alituambia kuwa ikiwa mwanaume aliyeoa atakufa na hana watoto, ndugu yake lazima amwoe mkewe ili aweze kuzaa watoto kwa ajili ya nduguye aliyekufa.[f] 25 Walikuwepo ndugu saba miongoni mwetu. Ndugu wa kwanza alioa lakini akafa bila ya kupata watoto. Hivyo ndugu yake akamwoa mkewe. 26 Na ndugu wa pili akafa pia, jambo hili hilo likatokea kwa ndugu wa tatu na ndugu wengine wote. 27 Mwanamke akawa wa mwisho kufa. 28 Lakini wanaume wote saba walikuwa wamemwoa. Sasa watu watakapofufuliwa kutoka kwa wafu, mwanamke huyu atakuwa mke wa yupi?”
29 Yesu akajibu, “Mnakosea sana! Hamjui kile ambacho Maandiko yanasema. Na hamjui lolote kuhusu nguvu ya Mungu. 30 Watu watakapofufuliwa kutoka kwa wafu, wanaume hawataoa wake na wanawake hawataozwa kwa wanaume. Kila mtu atakuwa kama malaika walio mbinguni. 31 Someni kile ambacho Mungu alikisema kuhusu watu kufufuliwa kutoka kwa wafu. 32 Mungu alisema, ‘Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo.’(G) Ni Mungu wa walio hai tu, hivyo hakika watu hawa hawakuwa wafu.”
33 Watu waliposikia hili, waliyashangaa mafundisho ya Yesu.
Amri ipi ni ya Muhimu Zaidi?
(Mk 12:28-34; Lk 10:25-28)
34 Mafarisayo waliposikia kuwa Yesu amewafanya Masadukayo waonekane wajinga nao wakaacha kumwuliza maswali. Kwa hiyo Mafarisayo wakafanya mkutano. 35 Ndipo mmoja wao, aliye mtaalamu wa Sheria ya Musa, akamwuliza Yesu swali ili kumjaribu. 36 Akasema, “Mwalimu, amri ipi katika sheria ni ya muhimu zaidi?”
37 Yesu akajibu, “‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote na akili yako yote.’(H) 38 Hii ndiyo amri ya kwanza na ya muhimu zaidi. 39 Na amri ya pili ni kama ya kwanza: ‘Mpende jirani yako[g] kama unavyojipenda wewe mwenyewe.’(I) 40 Sheria yote na maandiko ya manabii yamejengwa katika amri hizi mbili.”
Je, Masihi ni Mwana wa Daudi?
(Mk 12:35-37; Lk 20:41-44)
41 Hivyo Mafarisayo walipokuwa pamoja, Yesu aliwauliza swali. 42 Akasema, “Nini mawazo yenu juu ya Masihi? Je, ni mwana wa nani?” Mafarisayo wakajibu, “Masihi ni Mwana wa Daudi.”
43 Yesu akawaambia, “Sasa ni kwa nini Daudi anamwita ‘Bwana’? Daudi alikuwa anazungumza kwa nguvu ya Roho. Aliposema,
44 ‘Bwana Mungu alimwambia Bwana Mfalme wangu:
Keti karibu nami upande wangu wa kuume,
na nitawaweka adui zako chini ya udhibiti wako.’[h](J)
45 Ikiwa Daudi anamwita Masihi ‘Bwana’. Inakuwaje Masihi ni mwana wa Daudi?”
46 Hakuna Farisayo aliyeweza kumjibu Yesu. Na baada ya siku hiyo, hakuna aliyekuwa jasiri kumwuliza maswali zaidi.
© 2017 Bible League International