Read the Gospels in 40 Days
Yesu Aomba Kwa ajili Yake na Wafuasi Wake
17 Baada ya Yesu kusema maneno hayo, alitazama mbinguni na kuomba, “Baba, wakati umefika. Mpe utukufu Mwanao ili Mwanao naye akupe wewe utukufu. 2 Ulimpa Mwana mamlaka juu ya watu wote ili awape uzima wa milele wale wote uliompa. 3 Na uzima wa milele ndiyo huu: kwamba watu watakujua wewe, Mungu pekee wa kweli, na kwamba watamjua Yesu Kristo, Yeye uliyemtuma. 4 Mimi nimeimaliza kazi uliyonipa niifanye. Nami nimekupa utukufu duniani. 5 Sasa, Bwana, unipe utukufu wako niwe nao pamoja nawe, utukufu ule niliokuwa nao pamoja nawe kabla ya kuumbwa ulimwengu.
6 Wewe ulinipa baadhi ya wafuasi kutoka watu wa ulimwengu huu. Hao nimewaonesha jinsi wewe ulivyo. Walikuwa watu wako, lakini ukawakabidhi kwangu. Wao wameyashika mafundisho yako. 7 Sasa wanajua kuwa kila kitu nilichonacho kimetoka kwako. 8 Mimi niliwaeleza maneno uliyonipa, nao wakayapokea. Walitambua ukweli kuwa mimi nilitoka kwako na wakaamini kuwa wewe ndiye uliyenituma. 9 Mimi ninawaombea hao sasa. Siwaombei watu walioko ulimwenguni. Bali nawaombea wale watu ulionipa, kwa sababu hao ni wako. 10 Vyote nilivyo navyo ni vyako, na vyote ulivyo navyo ni vyangu. Kisha utukufu wangu umeonekana ndani yao.
11 Sasa nakuja kwako. Mimi sitakaa ulimwenguni, lakini hawa wafuasi wangu bado wamo ulimwenguni. Baba Mtakatifu, uwaweke hao salama kwa nguvu ya jina lako ulilonipa. Ndipo watapokuwa na umoja, kama vile mimi na wewe tulivyo. 12 Nilipokuwa pamoja nao niliwaweka salama kwa nguvu ya jina lako ulilonipa. Niliwalinda. Ni mmoja wao tu aliyepotea; yule ambaye kwa hakika angelikuja kupotea. Hii ilikuwa hivyo ili kuonesha ukweli wa yale yaliyosemwa na Maandiko kuwa yangetokea.
13 Nami nakuja kwako sasa. Lakini maneno haya nayasema ningali nimo ulimwenguni ili wafuasi hawa wawe na furaha kamili ndani yao. 14 Nimewapa mafundisho yako. Nao ulimwengu umewachukia, kwa sababu wao sio wa ulimwengu, kama mimi nisivyokuwa wa ulimwengu.
15 Siombi kwamba uwaondoe katika ulimwengu. Bali ninaomba uwalinde salama kutoka kwa Yule Mwovu.[a] 16 Wao si wa ulimwengu huu, kama mimi nisivyokuwa wa ulimwengu huu. 17 Kupitia kweli yako uwatayarishe kwa utumishi wako. Mafundisho yako ndiyo kweli. 18 Mimi nimewatuma ulimwenguni, kama wewe ulivyonituma mimi ulimwenguni. 19 Nami najiweka tayari kabisa kukutumikia wewe. Ninafanya hivi kwa ajili yao ili wao nao wawe wamekamilika kukutumikia.
20 Siwaombei tu hao wafuasi wangu lakini nawaombea pia wale watakaoniamini kutokana na mafundisho yao. 21 Baba, naomba kwamba wote wanaoniamini waungane pamoja na kuwa na umoja. Wawe na umoja kama vile wewe na mimi tulivyoungana; wewe umo ndani yangu nami nimo ndani yako. Nami naomba nao pia waungane na kuwa na umoja ndani yetu. Ndipo ulimwengu nao utaamini kuwa ndiwe uliyenituma. 22 Mimi nimewapa utukufu ule ulionipa. Nimewapa utukufu huo ili wawe na umoja, kama mimi na wewe tulivyo na umoja. 23 Nitakuwa ndani yao, nawe utakuwa ndani yangu. Hivyo watakuwa na umoja kamili. Kisha ulimwengu utajua kwamba wewe ndiwe uliyenituma na ya kuwa uliwapenda jinsi ulivyonipenda mimi.
24 Baba, ninataka hawa watu ulionipa wawe nami mahali pale nitakapokuwa. Nataka wauone utukufu wangu, utukufu ule ulionipa kwa sababu ulinipenda kabla ulimwengu haujaumbwa. 25 Baba wewe ndiye unayetenda yaliyo haki. Ulimwengu haukujui, bali mimi nakujua, na hawa wafuasi wangu wanajua kuwa wewe ndiye uliyenituma. 26 Nimewaonesha jinsi ulivyo, na nitawaonesha tena. Kisha watakuwa na upendo ule ule ulio nao wewe kwangu, nami nitaishi ndani yao.”
Yesu Akamatwa
(Mt 26:47-56; Mk 14:43-50; Lk 22:47-53)
18 Yesu alipomaliza kuomba, akaondoka pamoja na wafuasi wake kwenda ng'ambo kuvuka bonde la Kidroni. Akaenda katika bustani mahali hapo, akiwa bado pamoja na wafuasi wake.
2 Yuda, yule aliyehusika kumsaliti Yesu, alipafahamu mahali pale. Alipajua kwa sababu Yesu mara nyingi alikutana na wafuasi wake pale. 3 Kwa hiyo Yuda akaongoza kundi la askari hadi katika bustani hiyo pamoja na walinzi wengine kutoka kwa viongozi wa makuhani na Mafarisayo. Hawa walikuwa wamebeba mienge, taa, na silaha.
4 Yesu alikwisha kujua yote ambayo yangempata. Hivyo aliwaendea na kuwauliza, “Je, ni nani mnayemtafuta?”
5 Wakamjibu, “Yesu kutoka Nazareti.”
Akawaambia, “Mimi ni Yesu.”[b] (Yuda yule aliyehusika kumsaliti Yesu alikuwa amesimama hapo pamoja nao.) 6 Yesu aliposema, “Mimi ni Yesu,” wale watu walirudi nyuma na kuanguka chini.
7 Akawauliza tena, “Je, ni nani mnayemtafuta?”
Wakasema, “Yesu kutoka Nazareti.”
8 Yesu akasema, “Nimewaambia kwamba mimi ndiye Yesu. Hivyo kama mnanitafuta mimi, basi waacheni huru watu hawa waende zao.” 9 Hii ilikuwa kuonesha ukweli wa yale aliyosema Yesu mapema: “Sikumpoteza hata mmoja wa wale ulionipa.”
10 Simoni Petro akauchomoa upanga aliokuwa ameufunga kiunoni. Akampiga nao mtumishi wa Kuhani Mkuu, na kulikata sikio lake la kulia. (Jina la mtumishi huyo lilikuwa ni Maliko.) 11 Yesu akamwambia Petro, “Rudisha jambia lako mahali pake! Ninapaswa kunywa toka kikombe[c] ambacho Baba amenipa nikinywee.”
Yesu Aletwa Mbele ya Anasi
(Mt 26:57-58; Mk 14:53-54; Lk 22:54)
12 Kisha askari hao pamoja na mkuu wao na walinzi wa Kiyahudi wakamkamata Yesu. Wakamfunga, 13 nao wakampeleka kwanza kwa Anasi, baba mkwe wa Kayafa. Kayafa alikuwa Kuhani Mkuu kwa mwaka huo. 14 Naye ndiye aliyewashauri viongozi wengine wa Kiyahudi kwamba ingemfaa mtu mmoja afe[d] kwa ajili ya watu wote.
Petro Amkana Yesu
(Mt 26:69-70; Mk 14:66-68; Lk 22:55-57)
15 Simoni Petro na mmoja wa wafuasi wengine wa Yesu walienda pamoja na Yesu. Mfuasi huyu alimfahamu kuhani mkuu. Hivyo akaingia pamoja na Yesu ndani ya uwanja wa nyumba ya kuhani mkuu. 16 Lakini Petro alisubiri nje karibu na mlango. Yule mfuasi aliyemjua kuhani mkuu alirudi nje na kuongea na mlinda mlango. Kisha alimleta Petro ndani. 17 Msichana aliyekuwepo langoni alimwambia Petro, “Je! Wewe pia ni mmoja wa wafuasi wa mtu yule?”
Petro akajibu, “Hapana, mimi siye!”
18 Ilikuwa baridi, hivyo watumishi na walinzi waliwasha moto wa kuni. Walikuwa wameuzunguka, wakipasha joto miili yao naye Petro alikuwa amesimama pamoja nao.
Kuhani Mkuu Amhoji Yesu
(Mt 26:59-66; Mk 14:55-64; Lk 22:66-71)
19 Kuhani Mkuu akamwuliza Yesu maswali kuhusu wafuasi wake pamoja na mafundisho aliyowapa. 20 Yesu akamjibu, “Daima nimesema wazi kwa watu wote. Siku zote nimefundisha kwenye masinagogi na kwenye eneo la Hekalu. Wayahudi wote hukusanyika pale. Sijawahi kusema jambo lo lote kwa siri. 21 Sasa kwa nini unaniuliza? Waulize watu waliosikia mafundisho yangu. Wao wanajua niliyosema!”
22 Yesu aliposema hivyo, mmoja wa walinzi aliyekuwa amesimama hapo akampiga. Mlinzi huyo akasema, “Hupaswi kusema hivyo kwa kuhani mkuu!”
23 Yesu akajibu, “Kama nimesema vibaya jambo lo lote, mwambie kila mtu hapa kosa lenyewe. Lakini kama niliyosema ni sahihi, kwa nini basi unanipiga?”
24 Hivyo Anasi akampeleka Yesu kwa Kayafa kuhani mkuu. Naye alikuwa bado amefungwa.
Petro Amkana Yesu tena
(Mt 26:71-75; Mk 14:69-72; Lk 22:58-62)
25 Simoni Petro alikuwa amesimama karibu na moto, akijipasha joto. Watu wengine wakamwambia Petro, “Je, wewe si mmoja wa wafuasi wa mtu yule?”
Petro alikataa hilo. Akasema, “Hapana, mimi siye.”
26 Mmoja wa watumishi wa kuhani mkuu alikuwapo pale. Naye alikuwa ni jamaa wa mtu yule aliyekatwa sikio na Petro. Mtumishi akamwambia Petro, “Nadhani nilikuona pamoja naye pale kwenye bustani!”
27 Lakini kwa mara nyingine Petro akasema, “Hapana, sikuwa pamoja naye!” Mara tu alipomaliza kusema hayo, jogoo akawika.
Yesu Apelekwa kwa Gavana Pilato
(Mt 27:1-2,11-31; Mk 15:1-20; Lk 23:1-25)
28 Kisha walinzi wakamchukua Yesu kutoka katika nyumba ya Kayafa kwenda kwenye jumba la mtawala wa Kirumi. Nayo ilikuwa ni mapema asubuhi. Wayahudi waliokuwa pale wasingeweza kuingia ndani ya jumba hilo. Wao hawakutaka kujinajisi wenyewe kwa sababu walitaka kuila karamu ya Pasaka. 29 Kwa hiyo Pilato akatoka nje kuwafuata na akawauliza, “Mnasema mtu huyu amefanya makosa gani?”
30 Wakajibu, “Yeye ni mtu mbaya. Ndiyo maana tumemleta kwako.”
31 Pilato akawaambia, “Mchukueni wenyewe na kumhukumu kufuatana na sheria yenu.” Viongozi wa Wayahudi wakamwambia, “Lakini sheria yako haituruhusu sisi kumwadhibu mtu yeyote kwa kumwua.” 32 (Hii ilikuwa ni kuonesha ukweli wa yale aliyosema Yesu juu ya jinsi ambavyo angekufa.)
33 Kisha Pilato alirudi ndani ya jumba lile. Aliagiza Yesu aje na akamuuliza, “Je, wewe ni Mfalme wa Wayahudi?”
34 Yesu akajibu, “Je, hilo ni swali lako mwenyewe au watu wengine wamekuambia juu yangu?”
35 Pilato akajibu, “Mimi sio Myahudi! Ni watu wako mwenyewe na viongozi wa makuhani waliokuleta kwangu. Je, umefanya kosa gani?”
36 Yesu akajibu, “Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu. Kama ungekuwa hivyo, watumishi wangu wangenipigania ili nisikabidhiwe kwa viongozi wa Wayahudi. Hapana, ufalme wangu sio wa kidunia.”
37 Pilato akasema, “Kwa hiyo wewe ni mfalme?”
Yesu akamjibu, “Uko sahihi unaposema kuwa mimi ni mfalme. Nami nilizaliwa kwa ajili ya hili: kuwaeleza watu juu ya kweli. Ni kwa sababu hii nalikuja ulimwenguni. Kila mmoja aliye wa upande wa kweli hunisikiliza.”
38 Pilato akasema, “Kweli ndiyo nini?” Kisha alitoka nje tena kwenda kwa viongozi wa Wayahudi na kuwaimbia, “Mimi sipati kitu chochote kibaya cha kumpinga mtu huyu. 39 Lakini ni moja ya desturi zenu kwangu mimi kuwafungulia mfungwa mmoja wakati wa Pasaka. Je, mnataka niwafungulie huyu ‘Mfalme wa Wayahudi’?”
40 Wakajibu kwa kupiga kelele wakisema, “Hapana, siyo yeye! Mwache huru Baraba!” (Baraba alikuwa jambazi.)
© 2017 Bible League International