Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Read the Gospels in 40 Days

Read through the four Gospels--Matthew, Mark, Luke, and John--in 40 days.
Duration: 40 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Luka 1

Luka Aandika Kuhusu Maisha ya Yesu

Mheshimiwa Theofilo:[a]

Watu wengine wengi wamejaribu kuandika juu ya mambo yaliyotokea katikati yetu ili kuukamilisha mpango wa Mungu. Mambo hayo waliyoyaandika yanalingana na yale tuliyosikia kutoka kwa watu walioyaona tangu mwanzo. Na walimtumikia Mungu kwa kuwaambia wengine ujumbe wake. Nimechunguza kila kitu kwa makini tangu mwanzo. Na nimeona kuwa ni vyema nikuandikie kwa mpangilio mzuri. Nimefanya hivi ili uwe na uhakika kuwa yale uliyofundishwa ni ya kweli.

Malaika Amjulisha Zakaria Kuhusu Kuzaliwa kwa Yohana Mbatizaji

Herode alipokuwa mfalme wa Uyahudi, alikuwepo kuhani mmoja aliyeitwa Zakaria, aliyekuwa mmoja wa makuhani wa kikundi[b] cha Abiya. Mkewe alikuwa mzaliwa wa ukoo wa Haruni, na jina lake alikuwa Elizabeti. Wote wawili Zakaria na Elizabeti walikuwa wema waliompendeza Mungu na daima walifanya yote yaliyoamriwa na Bwana na kila mara walifuata maagizo yake kwa ukamilifu. Lakini hawakuwa na watoto kwa sababu Elizabeti alikuwa tasa, na wote wawili walikuwa wazee sana.

Ilipofika zamu ya kundi la Zakaria kuhudumu Hekaluni, yeye mwenyewe alikuwepo ili kuhudumu kama kuhani mbele za Mungu kwa ajili kundi. Makuhani walikuwa wanapiga kura kumchagua mmoja wao atakayeingia katika Hekalu la Bwana ili kufukiza uvumba. Na Zakaria alichaguliwa wakati huu. 10 Wakati wa kufukiza uvumba ulipofika watu wote walikusanyika nje ya Hekalu wakiomba.

11 Zakaria akiwa ndani ya Hekalu alitokewa na malaika wa Bwana akiwa amesimama mbele yake upande wa kulia wa madhabahu ya uvumba. 12 Zakaria alipomwona malaika aliogopa, na akaingiwa na hofu. 13 Lakini Malaika akamwambia, “Usiogope, Zakaria. Mungu amelisikia ombi lako. Mkeo Elizabeti atakuzalia mtoto wa kiume, nawe utamwita jina lake Yohana. 14 Utafurahi sana, na watu wengine wengi watamfurahia pamoja nawe. 15 Atakuwa mkuu kwa ajili ya Bwana. Kamwe asinywe mvinyo wala kitu chochote kile kitakachomlewesha. Atajazwa Roho Mtakatifu tangu akiwa tumboni mwa mama yake.

16 Naye atawafanya Waisraeli wengi wamrudie Bwana Mungu wao. 17 Atamtangulia Bwana ili kuwaandaa watu kuupokea ujio wake. Atakuwa na nguvu na roho kama Eliya. Atawapatanisha wazazi na watoto wao na kuwafanya wale wasiomtii Mungu kubadilika na kuanza kumtii Mungu.”

18 Zakaria akamwambia malaika, “Nitajuaje kuwa haya unayosema ni ya kweli? Maana mimi ni mzee na mke wangu ana umri mkubwa pia.”

19 Malaika akamjibu, “Mimi ni Gabrieli, ambaye daima husimama mbele za Mungu nikiwa tayari. Amenituma kuzungumza nawe na kukujulisha habari hizi njema. 20 Sasa sikiliza! Hautaweza kuzungumza mpaka siku ambayo mambo haya yatatokea kwa sababu hukuyaamini yale niliyokwambia. Lakini nilichosema hakika kitatokea.”

21 Watu waliokuwa nje ya Hekalu wakimngojea Zakaria walishangaa kwa sababu alikaa kwa muda mrefu ndani ya Hekalu. 22 Zakaria alipotoka nje hakuweza kuzungumza nao. Aliwafanyia watu ishara kwa mikono yake. Hivyo watu walitambua kuwa alikuwa ameona maono alipokuwa Hekaluni. 23 Zamu ya utumishi wake ilipokwisha alirudi nyumbani.

24 Wakati fulani baadaye, Elizabeti, mke wa Zakaria akawa mjamzito. Alikaa katika nyumba yake na hakutoka nje kwa miezi mitano. Alisema, 25 “Na sasa, hatimaye Bwana amenisaidia kwa kuniondolea aibu yangu.”

Malaika Atangaza Kuzaliwa kwa Yesu

26-27 Mwezi wa sita wa ujauzito wa Elizabeti, Mungu alimtuma malaika Gabrieli kwa msichana mmoja bikira aliyeishi Nazareti, mji wa Galilaya. Msichana huyo alikuwa amechumbiwa na Yusufu mzaliwa katika ukoo wa Daudi. Jina la bikira huyo lilikuwa Mariamu. 28 Malaika alimwendea na kusema “Salamu! Bwana yu pamoja nawe; Kwa kuwa neema yake iko juu yako.”

29 Lakini, Mariamu alichanganyikiwa kutokana na yale aliyosema malaika. Akajiuliza, “Salamu hii ina maana gani?”

30 Malaika akamwambia, “Usiogope Mariamu, kwa kuwa neema ya Mungu iko juu yako. 31 Sikiliza! Utapata mimba na kuzaa mtoto mwanamume, nawe utamwita jina lake Yesu. 32 Mtoto huyo atakuwa Mkuu na watu watamwita Mwana wa Mungu Aliye Mkuu Sana na Bwana Mungu atamfanya kuwa mfalme kama Daudi baba yake. 33 Naye ataitawala nyumba ya Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho.”

34 Mariamu akamwambia malaika, “Jambo hili litatokeaje? Kwa maana mimi bado ni bikira.”

35 Malaika akamwambia Mariamu, “Roho Mtakatifu atakujia, na nguvu zake Mungu Mkuu zitakufunika. Na hivyo mtoto atakayezaliwa atakuwa mtakatifu na ataitwa Mwana wa Mungu. 36 Pia sikiliza hili: Jamaa yako Elizabeti ni mjamzito. Ijapokuwa ni mzee sana, atazaa mtoto wa kiume. Kila mtu alidhani hataweza kuzaa, lakini sasa huu ni mwezi wa sita wa ujauzito wake. 37 Mungu anaweza kufanya jambo lolote!”

38 Mariamu akasema, “Mimi ni mtumishi wa Bwana, basi jambo hili litokee kwangu kama ulivyosema.” Kisha malaika akaondoka.

Mariamu Amtembelea Elizabeti

39 Mariamu akajiandaa na kwenda haraka katika mji mmoja ulio vilimani katika jimbo la Yuda. 40 Alikwenda nyumbani kwa Zakaria, alipofika akamsalimu Elizabeti. 41 Elizabeti aliposikia salamu ya Mariamu, mtoto aliyekuwa tumboni mwake akirukaruka, na Elizabeti akajazwa Roho Mtakatifu.

42 Kisha akapaza sauti na kumwambia Mariamu, “Umebarikiwa kuliko wanawake wote, na mtoto utakayemzaa amebarikiwa. 43 Lakini jambo hili kuu limetokeaje kwangu, hata mama wa Bwana wangu aje kwangu? 44 Kwa maana sauti ya salamu yako ilipofika masikioni mwangu, mtoto aliye ndani yangu amerukaruka kwa furaha. 45 Umebarikiwa wewe uliyeamini kuwa mambo aliyokuambia Bwana yatatokea.”

Mariamu Amsifu Mungu

46 Mariamu akasema,

“Moyo wangu unamwadhimisha Bwana,
47     kwa maana, Yeye, Mungu na Mwokozi
    wangu amenipa furaha kuu!
48 Kwa maana ameonesha kunijali,
    mimi mtumishi wake, nisiye kitu.
Na kuanzia sasa watu wote
    wataniita mbarikiwa.
49 Kwa kuwa Mwenye Nguvu amenitendea mambo makuu.
    Jina lake ni takatifu.
50 Na huwapa rehema zake wale wamchao,
    kutoka kizazi hadi kizazi.
51 Ameonesha nguvu ya mkono wake;
    Amewatawanya wanaojikweza.
52 Amewaangusha watawala kutoka katika viti vyao vya enzi,
    na kuwakweza wanyenyekevu.
53 Amewashibisha wenye njaa kwa mambo mema,
    na amewatawanya matajiri bila ya kuwapa kitu.
54 Amemsaidia Israeli, watu aliowachagua ili wamtumikie.
    Amekumbuka kuonesha rehema;
55 Maana ndivyo alivyowaahidi baba zetu,
    Ibrahimu na wazaliwa wake.”

56 Mariamu alikaa na Elizabeti kwa muda wa kama miezi mitatu, kisha alirudi nyumbani kwake.

Kuzaliwa kwa Yohana Mbatizaji

57 Wakati ulipotimia kwa Elizabeti kujifungua, alizaa mtoto wa kiume. 58 Majirani na jamaa zake waliposikia jinsi Bwana alivyokuwa mwema kwake, walifurahi pamoja naye.

59 Mtoto alipofikisha umri wa siku nane, walikuja kumtahiri.[c] Walipotaka kumwita mtoto Zakaria kutokana na jina la baba yake. 60 Mama yake akasema, “Hapana, mtoto ataitwa Yohana.”

61 Lakini wao wakamwambia, “Hakuna jamaa yako hata mmoja mwenye jina hilo.” 62 Ndipo wakamfanyia ishara baba yake wakimwuliza jina alilotaka kumpa mtoto.

63 Zakaria akataka ubao wa kuandikia,[d] Kisha akaandika, “Jina lake ni Yohana.” Wote wakashangaa. 64 Mara hiyo hiyo mdomo wake ulifunguliwa na ulimi wake ukaachia, akaanza kuzungumza na kumsifu Mungu. 65 Majirani zao wakajawa hofu na watu katika sehemu zote za vilima katika jimbo la Yuda wakawa wanazungumza kuhusu jambo hili. 66 Watu wote waliosikia kuhusu mambo haya walijiuliza, wakisema, “Mtoto huyu atakuwa wa namna gani?” Kwa kuwa nguvu ya Bwana ilikuwa pamoja naye.

Zakaria Amsifu Mungu

67 Kisha Zakaria, baba yake Yohana, akajaa Roho Mtakatifu, akatabiri, akisema:

68 “Asifiwe Bwana, Mungu wa Israeli,
    kwa kuwa amekuja kuwasaidia
    watu wake na kuwaweka huru.
69 Na ametuletea sisi Mwokozi Mwenye Nguvu,
    kutoka katika ukoo wa mtumishi wake Daudi.
70 Hivi ndivyo alivyoahidi
    kupitia manabii wake watakatifu tangu zamani.
71 Aliahidi kwa Agano kuwa atatuokoa na adui zetu
    na milki za wote wanaotuchukia.
72 Ili kuonesha rehema kwa baba zetu,
    na kulikumbuka agano lake takatifu aliloagana nao.
73 Agano hili ni kiapo alichomwapia
    baba yetu Ibrahimu.
74 Alipoahidi kutuokoa kutoka katika nguvu za adui zetu,
    ili tuweze kumwabudu Yeye bila hofu.
75 Katika namna iliyo takatifu na yenye haki
    mbele zake siku zote za maisha yetu.

76 Sasa wewe, mtoto mdogo,
    utaitwa nabii wa Mungu Aliye Juu Sana,
kwa sababu utamtangulia Bwana
    kuandaa njia yake.
77 Utawaambia watu wake kwamba wataokolewa
    kwa kusamehewa dhambi zao.

78 Kwa rehema ya upendo wa Mungu wetu,
    siku mpya[e] itachomoza juu yetu kutoka mbinguni.
79 Kuwaangazia wale wanaoishi katika giza,
    kwa hofu ya mauti,
na kuongoza hatua zetu
    katika njia ya amani.”

80 Na hivyo mtoto Yohana akakua na kuwa na nguvu katika roho. Kisha akaishi maeneo yasiyo na watu mpaka wakati alipotokea hadharani akihubiri ujumbe wa Mungu kwa watu wa Israeli.

Kuzaliwa kwa Yesu

(Mt 1:18-25)

Ulikuwa wakati ambapo amri ilitolewa na Kaisari Augusto kwamba watu wote wanaoishi katika utawala wote wa Rumi[f] wahesabiwe na kuorodheshwa[g] katika kumbukumbu za serikali. Orodha hii ilikuwa ya kwanza tangu Kirenio alipokuwa gavana wa Shamu. Kila mtu alikwenda katika mji aliozaliwa ili akahesabiwe na kuingizwa katika orodha hiyo.

Hivyo Yusufu alitoka Nazareti, mji uliokuwa katika jimbo la Galilaya na kwenda katika mji wa Bethlehemu uliokuwa katika jimbo la Uyahudi. Pia, mji huu ulijulikana kama mji wa Daudi. Yusufu alikwenda Bethlehemu kwa sababu alikuwa mzaliwa wa ukoo wa Daudi. Yusufu alijiandikisha akiwa pamoja na Mariamu kwani alikuwa tayari amemchumbia ili amwoe. Na Mariamu alikuwa mjamzito. Yusufu na Mariamu walipokuwa Bethlehemu, wakati wa Mariamu kujifungua ulifika. Akamzaa mwanawe wa kwanza. Akamvingirishia nguo vizuri, kisha akamlaza katika hori la kulishia mifugo.[h] Walimweka humo kwa sababu chumba cha wageni kilikuwa kimejaa.

Wachungaji wa Mifugo Wajulishwa Kuhusu Yesu

Usiku ule, baadhi ya wachungaji walikuwa mashambani nje ya mji wa Bethlehemu wakilinda kondoo zao. Malaika wa Bwana akawatokea ghafla, na utukufu wa Bwana ukaangaza kuwazunguka, wakaogopa sana. 10 Malaika akawaambia, “Msiogope, kwa kuwa nimewaletea habari njema zitakazowafurahisha watu wa Mungu wote. 11 Kwa sababu leo katika mji wa Daudi amezaliwa Mwokozi, ndiye Kristo,[i] Bwana. 12 Na hivi ndivyo mtakavyomtambua: Mtamkuta mtoto mchanga amevingirishiwa nguo na amelala katika hori la kulishia mifugo.”

13 Kisha malaika pamoja na jeshi kubwa la mbinguni wakaanza kumsifu Mungu, wakisema:

14 “Atukuzwe Mungu juu mbinguni,
    na amani iwepo duniani
    kwa watu wote wanaompendeza.”

15 Malaika walipoondoka kurudi mbinguni, wale wachungaji wakaambiana wakisema, “Twendeni Bethlehemu, tukalione jambo hili lililotokea, ambalo Bwana ametujulisha.”

16 Wakaenda haraka, wakamkuta Mariamu na Yusufu, na yule mtoto mchanga amelala katika hori la kulishia mifugo. 17 Wachungaji walipomwona huyo mtoto, walisimulia kile walichoambiwa na malaika kuhusu mtoto. 18 Kila aliyesikia maelezo ya wachungaji, alishangaa. 19 Mariamu aliendelea kuyatafakari mambo haya, na kuyaweka moyoni. 20 Wachungaji waliirudia mifugo yao, wakawa wanamsifu na kumshukuru Mungu kwa mambo yote waliyosikia na kuyaona. Ilikuwa kama walivyoambiwa na malaika.

21 Ilipofika siku ya nane mtoto alitahiriwa, akaitwa Yesu. Hili ndilo jina alilopewa na malaika kabla mama yake hajaibeba mimba yake.

Yesu Atambulishwa Hekaluni

22 Muda wa kutakaswa ulimalizika, kama ilivyotakiwa na Sheria ya Musa baada ya mtoto kuzaliwa.[j] Baada ya hapo walimpeleka Yesu Yerusalemu na kumweka mbele za Bwana. 23 Kama ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana: Mzaliwa wa kwanza akiwa mtoto wa kiume, atolewe wakfu kwa ajili ya Bwana.[k] 24 Pia Mariamu na Yusufu walikwenda Yerusalemu kutoa dhabihu kama Sheria ya Bwana inavyosema kuwa, “Ni lazima utoe dhabihu ya jozi moja ya hua[l] au makinda mawili wa njiwa.”

Simeoni Amwona Yesu

25 Alikuwepo mtu mmoja aliyeishi katika mji wa Yerusalemu, mtu huyu aliitwa Simeoni. Alikuwa mtu mwema na mcha Mungu na Roho Mtakatifu alikuwa pamoja naye. Alikuwa akiusubiri wakati ambao Mungu angeisaidia Israeli. 26 Roho Mtakatifu alimwambia kwamba asingekufa kabla ya kumwona Masihi kutoka kwa Bwana. 27 Roho Mtakatifu alimwongoza mpaka Hekaluni. Hivyo, alikuwemo Hekaluni wakati Mariamu na Yusufu walipomleta mtoto Yesu ili wamfanyie kama ilivyotakiwa katika Sheria ya Kiyahudi. 28 Simeoni alimbeba mtoto Yesu mikononi mwake, akamshukuru Mungu na kusema,

29 “Sasa, Bwana, niruhusu mimi mtumishi wako nife kwa amani
    kwa kuwa umeitimiza ahadi yako kwangu.
30 Nimeona kwa macho yangu namna utakavyowaokoa watu wako.
31     Sasa watu wote wanaweza kuuona mpango wako.
32 Yeye ni mwanga wa kuionesha njia yako kwa mataifa mengine,
    na atawaletea heshima watu wako Israeli.”

33 Mariamu na Yusufu walishangazwa sana na maneno aliyosema Simeoni kuhusu Yesu. 34 Kisha Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu; “Wayahudi wengi wataanguka na wengi watainuka kwa sababu ya mtoto huyu. Atakuwa ishara kutoka kwa Mungu, lakini baadhi ya watu watamkataa. 35 Mawazo ya siri ya watu wengi yatajulikana. Na mambo yatakayotokea yatakuumiza, kama upanga unaokuchoma moyoni.”

Ana Amwona Yesu

36 Alikuwapo nabii aliyeitwa Ana binti Fanueli, kutoka katika kabila la Asheri. Alikuwa mwanamke mzee sana. Aliishi na mume wake kwa miaka saba, 37 kabla ya mume wake kufa na kumwacha peke yake. Na sasa alikuwa na umri wa miaka themanini na nne. Ana alikuwa Hekaluni daima, hakutoka. Alimwabudu Mungu kwa kufunga na kuomba usiku na mchana.

38 Simeoni alipokuwa anazungumza na Yusufu na Mariamu, Ana alikwenda walipokuwa na akaanza kumsifu Mungu na kuwaambia kuhusu Yesu watu wote waliokuwa wanasubiri Mungu kuikomboa Yerusalemu.

Yusufu, Mariamu na Yesu Warudi Nyumbani

39 Yusufu na Mariamu walipotimiza mambo yote yanayotakiwa katika sheria ya Bwana, walirudi Galilaya, katika mji wao wa Nazareti. 40 Mtoto Yesu aliendelea kukua na kuwa kijana mwenye nguvu na aliyejaa hekima nyingi. Na Mungu alikuwa anambariki.

Yesu Akiwa Mvulana

41 Kila mwaka wazazi wa Yesu walikwenda Yerusalemu kwa ajili ya sikukuu ya Pasaka. 42 Yesu alipokuwa na umri wa miaka kumi na miwili, walikwenda kwenye sikukuu kama ilivyokuwa desturi ya Kiyahudi. 43 Sikukuu ilipokwisha, walirudi nyumbani, lakini Yesu alibaki Yerusalemu bila wazazi wake kutambua. 44 Walianza kumtafuta kwa jamaa na rafiki zao baada ya kusafiri kutwa nzima, wakidhani kuwa alikuwa pamoja nao katika msafara. 45 Walipomkosa, walirudi Yerusalemu kumtafuta.

46 Ikawa baada ya siku tatu wakamkuta Hekaluni, amekaa katikati ya walimu wa dini, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. 47 Na wote waliomsikiliza walishangazwa sana kwa ufahamu wake na majibu yake ya busara. 48 Wazazi wake walipomwona walishangaa pia, ndipo mama yake akamwambia, “Mwanangu, kwa nini umefanya hivi? Mimi na baba yako tulikuwa na wasiwasi sana, na tumekuwa tukikutafuta.”

49 Yesu akawaambia, “Kwa nini mlikuwa mnanitafuta? Mnapaswa kujua kuwa inanilazimu kuwemo nyumbani mwa Baba yangu?” 50 Lakini wao hawakuelewa alichowaambia.

51 Yesu alirudi pamoja nao mpaka Nazareti, naye alikuwa akiwatii. Mama yake aliendelea kuyaweka mambo haya yote moyoni mwake. 52 Naye Yesu akakua katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu.

Yohana Atayarisha Njia kwa Ajili ya Yesu

(Mt 3:1-12; Mk 1:1-8; Yh 1:19-28)

Katika mwaka wa kumi na tano wa utawala wa Kaisari Tiberio, ambapo:

Pontio Pilato alikuwa gavana wa Uyahudi;

Herode alikuwa mtawala wa Galilaya;

Filipo ndugu yake Herode alikuwa mtawala wa Iturea na Trakoniti;

na Lisania, alikuwa mtawala wa Abilene.

Anasi na Kayafa walikuwa makuhani wakuu. Katika kipindi hiki, Yohana, mwana wa Zakaria, alikuwa akiishi jangwani na alipata ujumbe kutoka kwa Mungu. Alipita katika maeneo yote yaliyo karibu na Mto Yordani akiwahubiri watu ujumbe kutoka kwa Mungu. Aliwaambia wabatizwe kuonesha kuwa wamekubali kubadili maisha yao ndipo dhambi zao zitasamehewa. Hii ni kama maneno yaliyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya, yanayosema,

“Kuna mtu anayeipaza sauti yake kutokea nyikani:
‘Tayarisheni njia kwa ajili ya Bwana;
    nyoosheni njia kwa ajili yake.
Kila bonde litajazwa,
    na kila mlima na kilima vitasawazishwa.
Barabara zilizopinda zitanyooshwa,
    na barabara zenye mashimo zitasawazishwa.
Na kila mtu ataona
    jinsi Mungu atakavyowaokoa watu wake.’”(A)

Makundi ya watu walimwendea Yohana ili awabatize. Lakini aliwaambia, “Enyi nyoka! Ni nani aliyewaonya kuikimbia hukumu ya Mungu inayokuja? Badilisheni mioyo yenu! Kisha onesheni ya kuwa mmebadilika kwa namna mnavyoishi. Ninajua mtasema kuwa, ‘Ibrahimu ni baba yetu.’ Hilo halijalishi chochote. Ninawaambia Mungu anaweza kumwumbia Ibrahimu watoto kutokana na mawe haya! Na sasa shoka liko tayari kukata miti,[m] kila mti usiozaa matunda mazuri utakatwa na kutupwa motoni.”

10 Watu wakamwuliza Yohana, “Tufanye nini?”

11 Akajibu, “Ukiwa na mashati mawili mpe moja asiyekuwa na shati. Kama una chakula, kigawe pia.”

12 Hata watoza ushuru walikuja kwa Yohana. Walitaka wabatizwe. Walimwambia, “Mwalimu, tufanye nini sisi?”

13 Akawaambia, “Msitoze ushuru zaidi kuliko kiwango kilichoamriwa.”

14 Askari wakamwuliza, “Vipi kuhusu sisi? Tufanye nini?”

Akawaambia, “Msitumie nguvu au kutengeneza mashtaka ya uongo ili watu wawape pesa. Mtosheke na mishahara mnayopata.”

15 Kila mtu alitarajia kuja kwa Masihi,[n] na walijiuliza wakisema, “Labda Yohana ndiye Masihi.”

16 Yohana aliwajibu watu wote, akasema, “Ninawabatiza ninyi katika maji, lakini yupo mwingine ajaye baada yangu, mwenye nguvu zaidi kuliko mimi, huyo atafanya mengi zaidi yangu. Nami niliye mtumwa wa chini kabisa sistahili hata kuinama na kufungua kamba za viatu vyake. Yeye huyo atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto. 17 Yuko tayari sasa kuja kusafisha nafaka. Atatenganisha nafaka nzuri na makapi, na kuiweka katika ghala yake kisha ataichoma ile isiyofaa katika moto usiozimika.” 18 Hivi ndivyo ambavyo Yohana aliwahubiri watu Habari Njema. Aliwaonya sana kuwa wanatakiwa kubadili njia zao.

Kazi ya Yohana Ilivyomalizika Baadaye

19 Yohana alimkosoa Herode kwa sababu ya mambo mabaya aliyokuwa ameyafanya na Herodia, mkewe kaka yake Herode, na pia kwa mambo mengine mabaya aliyokuwa ameyafanya. 20 Hivyo Herode aliongeza jambo jingine baya katika matendo yake maovu. Alimfunga Yohana gerezani.

Yohana Ambatiza Yesu

(Mt 3:13-17; Mk 1:9-11)

21 Watu wote walipokuwa wakibatizwa, Yesu alikuja naye akabatizwa. Na alipokuwa akiomba, mbingu zilifunguka, 22 na Roho Mtakatifu aliyekuwa katika umbo la njiwa akashuka juu yake. Sauti ikasikika toka mbinguni, “Wewe ni mwanangu, ninayekupenda, napendezwa nawe sana.”

Ukoo wa Yesu

(Mt 1:1-17)

23 Yesu alipoanza kufundisha, alikuwa na umri kama wa miaka thelathini. Watu walidhani kuwa Yesu alikuwa Mwana wa Yusufu.

Yusufu alikuwa mwana wa Eli.

24 Eli alikuwa mwana wa Mathati.

Mathati alikuwa mwana wa Lawi.

Lawi alikuwa mwana wa Melki.

Melki alikuwa mwana wa Yana.

Yana alikuwa mwana wa Yusufu.

25 Yusufu alikuwa mwana wa Matathia.

Matathia alikuwa mwana wa Amosi.

Amosi alikuwa mwana wa Nahumu.

Nahumu alikuwa mwana wa Esli.

Esli alikuwa mwana wa Nagai.

26 Nagai alikuwa mwana wa Maathi.

Maathi alikuwa mwana wa Matathia.

Matathia alikuwa mwana wa Semei.

Semei alikuwa mwana wa Yusufu.

Yusufu alikuwa mwana wa Yoda.

27 Yoda alikuwa mwana wa Yoana.

Yoana alikuwa mwana wa Resa.

Resa alikuwa mwana wa Zerubabeli.

Zerubabeli alikuwa mwana wa Shealtieli.

Shealtieli alikuwa mwana wa Neri.

28 Neri alikuwa mwana wa Melki.

Melki alikuwa mwana wa Adi.

Adi alikuwa mwana wa Kosamu.

Kosamu alikuwa mwana wa Elmadamu,

Elmadamu alikuwa mwana wa Eri.

29 Eri alikuwa mwana wa Yoshua.

Yoshua alikuwa mwana wa Eliezeri.

Eliezeri alikuwa mwana wa Yorimu.

Yorimu alikuwa mwana wa Mathati.

Mathati alikuwa mwana wa Lawi.

30 Lawi alikuwa mwana wa Simeoni.

Simeoni alikuwa mwana wa Yuda.

Yuda alikuwa mwana wa Yusufu.

Yusufu alikuwa mwana wa Yonamu.

Yonamu alikuwa mwana wa Eliakimu.

31 Eliakimu alikuwa mwana wa Melea.

Melea alikuwa mwana wa Mena.

Mena alikuwa mwana wa Matatha.

Matatha alikuwa mwana wa Nathani.

Nathani alikuwa mwana wa Daudi.

32 Daudi alikuwa mwana wa Yese.

Yese alikuwa mwana wa Obedi.

Obedi alikuwa mwana wa Boazi.

Boazi alikuwa mwana wa Salmoni.[o]

Salmoni alikuwa mwana wa Nashoni.

33 Nashoni alikuwa mwana wa Aminadabu.

Aminadabu alikuwa mwana wa Admini,

Admini alikuwa mwana wa Aramu.[p]

Aramu alikuwa mwana wa Hesroni.

Hesroni alikuwa mwana wa Peresi.

Peresi alikuwa mwana wa Yuda.

34 Yuda alikuwa mwana wa Yakobo.

Yakobo alikuwa mwana wa Isaka.

Isaka alikuwa mwana wa Ibrahimu.

Ibrahimu alikuwa mwana wa Tera.

Tera alikuwa mwana wa Nahori.

35 Nahori alikuwa mwana wa Serugi,

Serugi alikuwa mwana wa Ragau.

Ragau alikuwa mwana wa Pelegi.

Pelegi alikuwa mwana wa Eberi,

Eberi alikuwa mwana wa Sala.

36 Sala alikuwa mwana wa Kenani.

Kenani alikuwa mwana wa Arfaksadi.

Arfaksadi alikuwa mwana wa Shemu.

Shemu alikuwa mwana wa Nuhu.

Nuhu alikuwa mwana wa Lameki.

37 Lameki alikuwa mwana wa Methusela.

Methusela alikuwa mwana wa Henoko.

Henoko alikuwa mwana wa Yaredi.

Yaredi alikuwa mwana wa Mahalaleli.

Mahalaleli alikuwa mwana wa Kenani.

38 Kenani alikuwa mwana wa Enoshi.

Enoshi alikuwa mwana wa Sethi.

Sethi alikuwa mwana wa Adamu.

Adamu alikuwa mwana wa Mungu.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International