Read the Gospels in 40 Days
Yesu Afundisha Kuhusu Talaka
(Mk 10:1-12)
19 Yesu alipomaliza kuzungumza haya yote, aliondoka Galilaya. Alikwenda maeneo ya Yuda ng'ambo ya Mto Yordani. 2 Watu wengi walimfuata na akaponya wagonjwa wengi huko.
3 Baadhi ya Mafarisayo wakamjia Yesu. Walitaka aseme jambo fulani lisilo sahihi. Wakamwuliza, “Je, ni sahihi kwa mume kumtaliki mke wake kutokana na sababu yoyote ile kama anavyotaka?”
4 Yesu akajibu, “Hakika mmesoma hili katika Maandiko: Mungu alipoumba ulimwengu, ‘aliumba watu wa jinsi ya kiume na wa jinsi ya kike.’(A) 5 Na Mungu alisema, ‘Hii ndiyo sababu mwanaume atawaacha baba na mama yake na kuungana na mke wake. Na hao watu wawili watakuwa mmoja.’(B) 6 Hivyo wao si wawili tena, bali mmoja. Ni Mungu aliowaunganisha pamoja, hivyo mtu yeyote asiwatenganishe.”
7 Mafarisayo wakauliza, “Sasa kwa nini Musa alitoa amri ya kumruhusu mwanaume kumtaliki mke wake kwa kuandika hati ya talaka?”[a]
8 Yesu akajibu, “Musa aliwaruhusu kuwataliki wake zenu kwa sababu mlikataa kupokea mafundisho ya Mungu. Lakini talaka haikuruhusiwa hapo mwanzo. 9 Ninawaambia kuwa, kila anayemtaliki mke wake, isipokuwa kutokana na uzinzi, na akamwoa mwanamke mwingine, anazini.”
10 Wafuasi wakamwambia Yesu, “Ikiwa hiyo ndiyo sababu pekee ambayo mtu anaruhusiwa kumtaliki mke wake, ni bora kutooa.”
11 Akajibu, “Tamko hili ni la kweli kwa baadhi ya watu, lakini si kwa kila mtu. Bali ni kwa wale tu waliopewa karama hii. 12 Kuna sababu tofauti kwa nini baadhi ya wanaume hawaoi.[b] Wengine wamezaliwa wakiwa hawana uwezo wa kuzaa watoto, wengine walifanywa hivyo katika maisha yao ya baadaye. Na wengine walichagua kutokuoa kwa ajili ya ufalme wa Mungu. Hili liko hivyo kwa kila anayeweza kulikubali.”
Yesu Awakaribisha Watoto
(Mk 10:13-16; Lk 18:15-17)
13 Ndipo watu wakawaleta watoto wao wadogo kwa Yesu ili awabariki na kuwaombea. Wafuasi wake walipoliona hili, waliwakataza watu wasiwalete watoto kwa Yesu. 14 Lakini Yesu akasema, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie, kwa sababu ufalme wa Mungu ni wa watu walio kama watoto hawa wadogo.” 15 Baada ya Yesu kuwabariki watoto, aliondoka huko.
Mtu Tajiri Akataa Kumfuata Yesu
(Mk 10:17-31; Lk 18:18-30)
16 Mtu mmoja alimwendea Yesu na kumwuliza, “Mwalimu, nifanye jambo gani lililo jema ili niweze kuupata uzima wa milele?”
17 Yesu akajibu, “Kwa nini unaniuliza kuhusu jambo gani lililo jema? Mungu pekee yake ndiye mwema. Lakini ikiwa unataka kuupata uzima wa milele, zitii amri.”
18 Yule mtu akauliza, “Amri zipi?”
Yesu akajibu, “‘Usiue, usizini, usiibe, usiseme uongo, 19 mheshimu baba na mama yako,’(C) na ‘mpende jirani yako[c] kama unavyojipenda wewe mwenyewe.’”(D)
20 Yule kijana akasema, “Ninazitii amri hizi zote. Nifanye nini zaidi?”
21 Yesu akajibu, “Ikiwa unataka kuwa mkamilifu, nenda ukauze kila kitu unachomiliki. Uwape pesa maskini na utakuwa na utajiri mbinguni. Kisha njoo unifuate!”
22 Lakini kijana aliposikia Yesu anamwambia kuhusu kugawa pesa yake, alihuzunika. Hakutaka kufanya hivi kwa kuwa alikuwa tajiri sana. Hivyo aliondoka.
23 Ndipo Yesu aliwaambia wafuasi wake, “Ukweli ni huu, itakuwa vigumu sana kwa tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu. 24 Ndiyo, ninawaambia, ni rahisi kwa ngamia kupita katika tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.”
25 Wafuasi waliposikia hili walishangaa. Wakauliza, “Sasa ni nani ataweza kuokolewa?”
26 Yesu akawatazama na kuwaambia, “Hili haliwezekani kwa wanadamu, Lakini yote yanawezekana kwa Mungu.”
27 Petro akamwambia, “Tuliacha kila kitu tulichonacho na kukufuata wewe. Tutapata nini?”
28 Yesu akawaambia, “Wakati wa ulimwengu mpya utakapofika, Mwana wa Adamu ataketi kwenye kiti chake cha enzi, kikuu na chenye utukufu mwingi. Na ninaweza kuwaahidi kuwa ninyi mnaonifuata mtaketi kwenye viti kumi na viwili vya enzi, na mtayahukumu makabila kumi na mawili ya Israeli. 29 Kila aliyeacha nyumba, ndugu, dada, baba, mama, watoto au shamba na akanifuata atapata zaidi ya yale aliyoacha. Na atapata uzima wa milele. 30 Watu wengi walio wa kwanza sasa watakuwa wa mwisho siku zijazo. Na walio wa mwisho sasa watakuwa wa kwanza siku zijazo.
Yesu Atumia Mfano wa Wakulima Katika Shamba la Mizabibu
20 Ufalme wa Mungu umefanana na mtu aliyemiliki shamba la mizabibu. Asubuhi mmoja akatoka kwenda kuajiri watu ili walime katika shamba lake la mizabibu. 2 Alikubaliana nao kuwa atawalipa sarafu moja ya fedha ikiwa watafanya kazi siku ile. Kisha akawapeleka kwenye shamba la mizabibu kulima.
3 Ilipofika saa tatu asubuhi mtu huyo alitoka na kwenda sokoni ambako aliwaona baadhi ya watu wamesimama na hawafanyi kazi yo yote. 4 Akawaambia, ‘Ikiwa mtakwenda kufanya kazi shambani kwangu, nitawalipa kutokana na kazi yenu.’ 5 Hivyo walikwenda kufanya kazi kwenye shamba lake la mizabibu.
Ilipofika saa sita mchana na saa tisa alasiri alitoka tena. Na nyakati zote mbili aliwaajiri watu wengine waende kufanya kazi shambani mwake. 6 Ilipofika saa kumi na moja alikwenda sokoni tena. Akawaona watu wengine wamesimama pale. Akawauliza, ‘Kwa nini mmesimama hapa siku nzima na hamfanyi kazi?’
7 Wakasema, ‘Hakuna aliyetupa kazi.’
Mwenye shamba akawaambia, ‘Basi mnaweza kwenda kufanya kazi katika shamba langu la mizabibu.’
8 Mwishoni mwa siku, mwenye shamba akamwambia msimamizi wa wafanyakazi wote, ‘Waite wafanyakazi na uwalipe wote. Anza kwa kulipa watu niliowaajiri mwishoni, na malizia kwa wale niliowaajiri mwanzoni.’
9 Wafanyakazi walioajiriwa saa kumi na moja jioni walipata malipo yao. Kila mfanyakazi alipata sarafu moja ya fedha. 10 Ndipo wafanyakazi walioajiriwa kwanza wakaja kupokea malipo yao. Walidhani wangelipwa zaidi ya wengine. Lakini kila mmoja wao alipokea sarafu moja ya fedha. 11 Walipopata sarafu ya fedha, walimlalamikia mmiliki wa shamba. 12 Walisema, ‘Watu hao walioajiriwa mwishoni wamefanya kazi saa moja tu. Lakini umewalipa sawa na sisi. Na tumefanya kazi siku nzima kwenye jua kali.’
13 Lakini mmiliki wa shamba akamwambia mmoja wao, ‘Rafiki, nimekulipa kama tulivyopatana, ulikubali kufanya kazi kwa malipo ya sarafu moja ya fedha. Sawa? 14 Hivyo chukua malipo yako na uende. Ninataka kumlipa mtu niliyemwajiri mwishoni sawa na kiasi nilichokulipa. 15 Ninaweza kufanya chochote ninachotaka na pesa yangu. Wewe unao wivu[d] na unataka kuwadhuru wengine kwa kuwa mimi ni mkarimu?’
16 Hivyo walio wa mwisho sasa watakuwa wa kwanza siku zijazo. Na walio wa kwanza sasa watakuwa wa mwisho siku zijazo.”
Yesu Azungumza Tena Kuhusu Kifo Chake
(Mk 10:32-34; Lk 18:31-34)
17 Yesu alikuwa anakwenda Yerusalemu akiwa na wafuasi wake kumi na wawili. Walipokuwa wakitembea, aliwakusanya pamoja wafuasi hao na kuzungumza nao kwa faragha. Akawaambia, 18 “Tunakwenda Yerusalemu. Mwana wa Adamu atatolewa kwa viongozi wa makuhani na walimu wa sheria, nao watasema ni lazima auawe. 19 Watamkabidhi wa wageni, watakaomcheka na kumpiga kwa mijeledi, kisha watamwua kwenye msalaba. Lakini siku ya tatu baada ya kifo chake, atafufuliwa kutoka kwa wafu.”
Mama Ataka Upendeleo Maalum kwa Wanaye
(Mk 10:35-45)
20 Ndipo mke wa Zebedayo akamjia Yesu akiwa na wanaye. Akainama mbele ya Yesu na akamwomba amtendee kitu.
21 Yesu akasema, “Unataka nini?”
Akasema, “Niahidi kuwa mmoja wa wanangu atakaa upande wa kuume na mwingine wa kushoto katika ufalme wako.”
22 Hivyo Yesu akawaambia wana wa Zebedayo, “Hamwelewi mnachokiomba. Mnaweza kukinywea kikombe[e] ambacho ni lazima nikinywee?”
Wana wa Zebedayo wakajibu, “Ndiyo tunaweza!”
23 Yesu akawaambia, “Ni kweli kuwa mtakinywea kikombe nitakachokinywea. Lakini si mimi wa kuwaambia ni nani ataketi mkono wangu wa kuume au wa kushoto. Baba yangu amekwisha amua ni nani ataketi kuume au kushoto kwangu. Amekwisha andaa nafasi hizo kwa ajili yao.”
24 Wafuasi wengine kumi waliposikia hili walikasirika kwa ajili ya wale ndugu wawili. 25 Hivyo Yesu akawaita pamoja, akawaambia, “Mnajua kuwa watawala wa watu wasio Wayahudi[f] wanapenda kuonesha nguvu yao kwa watu. Na viongozi wao muhimu wanapenda kutumia mamlaka yao yote juu ya watu. 26 Lakini isiwe hivyo miongoni mwenu. Kila anayetaka kuwa kiongozi wenu lazima awe mtumishi wenu. 27 Kila anayetaka kuwa wa kwanza ni lazima awatumikie ninyi nyote kama mtumwa. 28 Fanyeni kama nilivyofanya: Mwana wa Adamu hakuja ili atumikiwe na watu. Alikuja ili awatumikie wengine na kutoa maisha yake ili kuwaokoa watu wengi.”
Yesu Awaponya Watu Wawili Wasiyeona
(Mk 10:46-52; Lk 18:35-43)
29 Yesu na wanafunzi wake walipokuwa wanaondoka Yeriko, umati mkubwa wa watu ulimfuata. 30 Walikuwepo wasiyeona wawili wamekaa kando ya njia. Waliposikia kuwa Yesu anapita pale walipaza sauti wakasema, “Bwana, Mwana wa Daudi, tafadhali tusaidie!”
31 Watu waliwakemea wale wasiyeona, wakawaambia wanyamaze. Lakini waliendelea kupaza sauti zao zaidi na zaidi, “Bwana, Mwana wa Daudi, tafadhali tusaidie!”
32 Yesu alisimama na kuwaambia, “Mnataka niwafanyie nini?”
33 Wakajibu, “Bwana, tunataka tuweze kuona.”
34 Yesu aliwahurumia wale wasiyeona. Akayagusa macho yao, na mara hiyo hiyo wakaanza kuona. Wakawa wafuasi wa Yesu.
© 2017 Bible League International