Read the Gospels in 40 Days
Yesu Aonekana Akiwa na Musa na Eliya
(Mk 9:2-13; Lk 9:28-36)
17 Siku sita baadaye, Yesu aliwachukua Petro, Yakobo na Yohana ndugu yake Yakobo na akapanda nao kwenye mlima mrefu. Walikuwa peke yao huko. 2 Wafuasi wake hawa walipokuwa wakimwangalia, Yesu alibadilika. Uso wake ukawa angavu kama jua na nguo zake zikawa nyeupe kama mwanga. 3 Ndipo wanaume wawili waliozungumza naye wakaonekana wakiwa pamoja naye. Walikuwa Musa na Eliya.
4 Petro akamwambia Yesu, “Bwana, ni vizuri tuko hapa. Ukitaka, nitajenga vibanda vitatu,[a] kimoja kwa ajili ya heshima yako, kingine kwa ajili ya heshima ya Musa na kingine kwa ajili ya heshima ya Eliya.”
5 Petro alipokuwa akizungumza, wingu jeupe liliwafunika. Sauti ikatoka katika wingu na akasema, “Huyu ni Mwanangu, ninayempenda, ninafurahishwa naye. Mtiini yeye!”
6 Wafuasi waliokuwa na Yesu walipoisikia sauti hii waliogopa sana na wakaanguka chini. 7 Lakini Yesu akawaendea na kuwagusa. Akasema, “simameni, msiogope.” 8 Wafuasi wakatazama juu, wakaona kuwa Yesu yuko peke yake.
9 Yesu na wafuasi wake walipokuwa wanateremka kutoka mlimani, akawaamuru akisema: “Msimwambie mtu yeyote yale mliyoyaona mlimani. Subirini mpaka Mwana wa Adamu atakapofufuliwa kutoka kwa wafu. Ndipo mtaweza kuwaambia watu juu ya kile mlichokiona.”
10 Wafuasi wakamwuliza Yesu, “Kwa nini walimu wa sheria wanasema ni lazima Eliya aje[b] kabla ya Masihi kuja?”
11 Yesu akajibu, “Wako sahihi kusema ni lazima Eliya aje, na ni kweli kuwa Eliya ataweka mambo yote kama yanavyopaswa kuwa. 12 Lakini ninawaambia, Eliya amekwisha kuja. Watu hawakumjua yeye ni nani, na walimtendea vibaya, wakafanya kama walivyotaka. Ndivyo itakavyokuwa hata kwa Mwana wa Adamu. Watu hao punde tu watamletea mateso Mwana wa Adamu.” 13 Ndipo wafuasi wakaelewa kuwa Yesu aliposema kuhusu Eliya, alikuwa anazungumza juu ya Yohana Mbatizaji.
Yesu Amweka Huru Mvulana Kutoka Pepo Mchafu
(Mk 9:14-29; Lk 9:37-43a)
14 Yesu na wafuasi walirudi kwa watu. Mtu mmoja akamjia Yesu na kuinama mbele zake. 15 Akasema, “Bwana, umwonee huruma mwanangu. Anateswa sana na kifafa alichonacho. Anaangukia kwenye moto au maji mara kwa mara. 16 Nilimleta kwa wafuasi wako, lakini wameshindwa kumponya.”
17 Yesu akajibu, “Ninyi watu mnaoishi katika nyakati hizi cha kizazi kisicho na imani. Maisha yenu ni mabaya sana! Nitakaa nanyi mpaka lini? Nitawavumilia mpaka lini? Mleteni kijana hapa.” 18 Yesu akamwamuru pepo aliye ndani ya kijana, na pepo akamtoka na yule kijana akapona.
19 Kisha wafuasi wakamjia Yesu wakiwa peke yao. Wakasema, “Tulijaribu kumtoa pepo kwa kijana, lakini tulishindwa. Kwa nini tulishindwa kumtoa pepo?”
20 Yesu akajibu, “Mlishindwa kumtoa pepo kwa sababu imani yenu ni ndogo sana. Niaminini ninapowaambia, imani yenu ikiwa na ukubwa wa mbegu ya haradali mtaweza kuuambia mlima huu, ‘Ondoka hapa na uende kule,’ nao utaondoka. Nanyi mtaweza kufanya jambo lolote.” 21 [c]
Yesu Azungumza Kuhusu Kifo Chake
(Mk 9:30-32; Lk 9:43b-45)
22 Baadaye, wafuasi walipokusanyika pamoja Galilaya, Yesu aliwaambia, “Mwana wa Adamu atakabidhiwa kwenye mamlaka ya watu wengine, 23 watakaomwua. Lakini atafufuliwa kutoka kwa wafu siku ya tatu.” Wafuasi waliposikia kuwa Yesu angeuawa walihuzunika sana.
Yesu Afundisha Kuhusu Kulipa Kodi
24 Yesu na wafuasi wake walikwenda Kapernaumu. Walipofika huko watu waliokuwa wakikusanya ushuru wa Hekalu[d] wakamwendea Petro na kumwuliza, “Je, mwalimu wenu hulipa kodi ya Hekalu?”
25 Petro akajibu, “Ndiyo, hulipa.”
Petro akaingia katika nyumba alimokuwa Yesu. Kabla Petro hajazungumza jambo lolote, Yesu akamwambia, “Wafalme wa dunia huchukua kila aina ya kodi kutoka kwa watu. Lakini ni akina nani ambao hutoa kodi? Je, ni jamaa wa familia ya mfalme? Au watu wengine ndiyo hulipa kodi? Unadhani ni akina nani?”
26 Petro akajibu, “Watu wengine ndiyo hulipa kodi.”
Yesu akasema, “Basi wana wa mfalme hawapaswi kulipa kodi. 27 Lakini kwa kuwa hatutaki kuwaudhi watoza ushuru hawa, basi fanya hivi: Nenda ziwani na uvue samaki. Utakapomkamata samaki wa kwanza, mfungue kinywa chake. Ndani ya kinywa chake utaona sarafu nne za drakma mdomoni mwake. Ichukue sarafu hiyo mpe mtoza ushuru. Hiyo itakuwa kodi kwa ajili yangu mimi na wewe.”
Nani ni Mkuu Zaidi?
(Mk 9:33-37; Lk 9:46-48)
18 Wakati huo huo wanafunzi wake wakamjia Yesu na kuuliza, “Nani ni mkuu zaidi katika ufalme wa Mungu?”
2 Yesu akamwita mtoto mdogo, akamsimamisha mbele yao. 3 Kisha akasema, “Ukweli ni huu, ni lazima mbadilike katika namna mnavyofikiri na muwe kama mtoto mdogo. Msipofanya hivi hamtaingia katika ufalme wa Mungu. 4 Aliye mkuu zaidi katika ufalme wa Mungu ni yule anayejinyenyekeza kama mtoto huyu.
5 Unapomkubali mtoto mdogo kama huyu kama aliye wangu, unanikubali mimi.
Yesu Aonya Kuhusu Chanzo cha Dhambi
(Mk 9:42-48; Lk 17:1-2)
6 Ikiwa mmoja wa watoto hawa wadogo ananiamini, na mtu yeyote akasababisha mtoto huyo kutenda dhambi, ole wake mtu huyo. Ingekuwa bora mtu huyo kufungiwa jiwe la kusagia shingoni mwake na kuzamishwa katika kina kirefu baharini. 7 Nawasikitikia watu wa ulimwengu kwa sababu ya mambo yanayofanya watu watende dhambi. Mambo haya lazima yatokee, lakini ole wake mtu yeyote anayeyafanya yatokee.
8 Mkono au mguu wako ukikufanya utende dhambi, ukate na uutupe. Ni bora ukapoteza kiungo kimoja cha mwili wako na ukaupata uzima wa milele kuliko kuwa na mikono au miguu miwili na ukatupwa katika moto wa milele. 9 Jicho lako likikufanya utende dhambi, ling'oe na ulitupe. Ni bora kwako kuwa na jicho moja tu na ukaupata uzima wa milele kuliko kuwa na macho mawili na ukatupwa katika moto wa Jehanamu.
Yesu Atumia Simulizi ya Kondoo Aliyepotea
(Lk 15:3-7)
10 Iweni waangalifu, msidhani kuwa watoto hawa wadogo si wa muhimu. Ninawaambia kuwa watoto hawa wana malaika mbinguni. Na hao malaika daima wako pamoja na Baba yangu mbinguni. 11 [e]
12 Mtu akiwa na kondoo 100, lakini mmoja wa kondoo akapotea, atafanya nini? Atawaacha kondoo wengine 99 kwenye kilima na kwenda kumtafuta mmoja aliyepotea. Sawa? 13 Na akimpata kondoo aliyepotea, atafurahi kwa sababu ya kondoo huyo mmoja kuliko kondoo wengine 99 ambao hawakupotea. Ninaweza kuwathibitishia, 14 Kwa namna hiyo hiyo, Baba yenu wa mbinguni hapendi mmoja wa watoto hawa wadogo apotee.
Mrekebishe Kila Anayekosea
(Lk 17:3)
15 Ikiwa mmoja wa ndugu au dada yako katika familia ya Mungu akifanya kosa kwako,[f] umwendee na umwambie kile alichokukosea. Ufanye hivi mnapokuwa ninyi wawili tu. Ikiwa mtu huyo atakusikiliza, basi umemsaidia na umfanye kuwa kaka ama dada yako tena. 16 Lakini ikiwa mtu huyo atakataa kukusikiliza, mrudie ukiwa pamoja na ndugu wengine wawili waaminio. Ndipo watakuwepo watu wawili au watatu watakaoweza kueleza kile kilichotokea.[g] 17 Ikiwa mtu aliyetenda dhambi atakataa kuwasikiliza, ndipo uliambie kanisa. Na akikataa kulisikiliza kanisa, mchukulie kama ambavyo ungemchukulia mtu asiyemfahamu Mungu au mtoza ushuru.
18 Ninawahakikishia kuwa mnapotoa hukumu hapa duniani, hukumu hiyo itakuwa hukumu ya Mungu. Na mnapotoa msamaha, nao utakuwa msamaha wa Mungu.[h] 19 Kwa namna nyingine, ikiwa watu wawili waliopo duniani watakubaliana kwa kila wanachokiombea, Baba yangu wa mbinguni atatenda kile wanachokiomba. 20 Ndiyo, ikiwa watu wawili au watatu wanaoniamini watakusanyika pamoja, mimi nitakuwa pamoja nao.”
Simulizi Kuhusu Msamaha
21 Kisha Petro akamwendea Yesu na kumwuliza, “Bwana, ndugu yangu akiendelea kunikosea, ninapaswa kumsamehe anaponikosea mara ngapi? Mara saba?”
22 Yesu akamjibu, “Ninakwambia, ni lazima umsamehe zaidi ya mara saba. Ni lazima uendelee kumsamehe hata kama atakukosea saba mara sabini.[i]
23 Ninawaambia kwa sababu ufalme wa Mungu unafanana na mfalme aliyetaka kupata taarifa kutoka kwa watumishi wake. 24 Mtumishi aliyekuwa anadaiwa na mfalme tani 300[j] za fedha aliletwa kwake. 25 Hakuwa na fedha za kutosha kulipa deni lake. Hivyo mfalme aliamuru kila kitu anachomiliki mtumishi yule kiuzwe ikiwa ni pamoja na mke na watoto wake.
26 Lakini mtumishi alipiga magoti na kumsihi mfalme akisema, ‘Nivumilie. Nitakulipa kila kitu unachonidai.’ 27 Mfalme alimhurumia. Hivyo akamsamehe yule mtumishi deni lote na akamwacha aende akiwa huru.
28 Lakini mtumishi huyo alipoondoka, alimwona mtumishi mwingine aliyekuwa anamdai sarafu mia za fedha. Akamkaba shingo yake na akasema, ‘Nilipe pesa ninayokudai!’
29 Mtumishi anayedaiwa akapiga magoti na kumsihi akisema, ‘Nivumilie. Nitakulipa kila kitu unachonidai.’
30 Lakini mtumishi wa kwanza alikataa kumvumilia. Alimwambia hakimu kuwa alikuwa anamdai pesa, na mtumishi yule alitupwa gerezani mpaka atakapoweza kulipa deni lake. 31 Watumishi wengine walipoona hili, walimhurumia mtumishi aliyefungwa gerezani. Hivyo walienda na kumwambia mfalme kila kitu kilichotokea.
32 Ndipo mfalme alimwita msimamizi wa kwanza na kumwambia, ‘Wewe ni mbaya sana! Ulinisihi nikusamehe deni lako, na nilikuacha ukaondoka bila kulipa kitu chochote! 33 Hivyo ulipaswa kumpa mtu yule mwingine anayetumika pamoja nawe rehema ile ile niliyokupa mimi.’ 34 Mfalme alikasirika sana. Hivyo alifungwa gerezani mpaka atakapoweza kulipa kila kitu anachodaiwa.
35 Mfalme huyu alifanya kama ambavyo Baba yangu wa mbinguni atawafanyia ninyi. Ni lazima umsamehe ndugu au dada yako kwa moyo wako wote, usipofanya hivyo, Baba yangu wa mbinguni hatakusamehe wewe.”
© 2017 Bible League International