Chronological
Baadhi ya Watu Wawa na Mashaka Kuhusu Mamlaka ya Yesu
(Mk 8:11-13; Lk 12:54-56)
16 Mafarisayo na Masadukayo walimjia Yesu. Walitaka kumjaribu, kwa hiyo wakamwomba awaoneshe muujiza kama ishara kutoka kwa Mungu.
2 Yesu akawajibu, “Ninyi watu mnapoona jua limezama, mnajua hali ya hewa itakavyokuwa. Anga ikiwa nyekundu, mnasema tutakuwa na hali ya hewa nzuri. 3 Na asubuhi, ikiwa anga ni nyeusi na nyekundu, mnasema mvua itanyesha. Hizi ni ishara za hali ya hewa. Mnaziona ishara hizi angani na mnajua zinamaanisha nini. Kwa namna hiyo hiyo, mnaona mambo yanayotokea sasa. Hizi ni ishara pia, lakini hamwelewi maana yake. 4 Ninyi watu mnaoishi sasa ni waovu na si waaminifu kwa Mungu. Ndiyo sababu kabla ya kuamini mnataka kuona muujiza. Lakini hakuna muujiza utakaofanyika ili kuwathibitishia kitu cho chote. Yona[a] ndiyo ishara pekee mtakayopewa.” Kisha Yesu akaondoka mahali pale.
Wafuasi Washindwa Kumwelewa Yesu
(Mk 8:14-21)
5 Yesu na wafuasi wake wakasafiri kwa kukatisha ziwa. Lakini wafuasi wakasahau kubeba mikate. 6 Yesu akawaambia, “Mwe waangalifu! Jilindeni na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo.”
7 Wafuasi wakajadiliana maana ya hili. Wakasema, “Amesema hivi kwa sababu tumesahau kubeba mikate?”
8 Yesu alipotambua kuwa wanajadiliana hili, akawauliza, “Kwa nini mnajadiliana kuhusu kutokuwa na mikate? Imani yenu ni ndogo. 9 Bado hamwelewi? Mnakumbuka mikate mitano waliyokula watu 5,000 na vikapu vingi mlivyojaza mikate iliyosalia? 10 Na mnakumbuka mikate saba waliyokula watu 4,000 na vikapu vingi mlivyojaza wakati ule? 11 Hivyo inakuwaje mnadhani kuwa mimi ninajali sana kuhusu mikate? Ninawaambia muwe waangalifu na mjilinde dhidi ya chachu ya Mafarisayo na Masadukayo.”
12 Ndipo wafuasi wakaelewa Yesu alimaanisha nini. Hakuwa akiwaambia wajilinde na chachu inayotumika katika mikate bali wajilinde na mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo.
Petro Atambua Yesu ni Nani
(Mk 8:27-30; Lk 9:18-21)
13 Yesu alikwenda eneo la Kaisaria Filipi na akawauliza wafuasi wake, “Watu wanasema mimi ni nani[b]?”
14 Wakajibu, “Baadhi ya watu wanasema wewe ni Yohana Mbatizaji. Wengine wanasema wewe ni Eliya. Na wengine wanasema wewe ni Yeremia au mmoja wa manabii.”
15 Kisha Yesu akawauliza, “Na ninyi mnasema mimi ni nani?”
16 Simoni Petro akajibu, “Wewe ni Masihi, Mwana wa Mungu aliye hai.”
17 Yesu akajibu, “Umebarikiwa, Simoni mwana wa Yona. Hakuna aliyekufundisha hilo ila Baba yangu wa mbinguni ndiye amekuonesha mimi ni nani. 18 Hivyo ninakwambia, Wewe ni Petro. Na nitalijenga kanisa langu kwenye mwamba[c] huu. Nguvu ya mauti[d] haitaweza kulishinda kanisa langu. 19 Nitawapa funguo za Ufalme wa Mungu. Mnapohukumu hapa duniani, hukumu hiyo itakuwa hukumu ya Mungu. Mnapotamka msamaha hapa duniani, msamaha huo utakuwa msamaha wa Mungu.”[e]
20 Kisha Yesu akawaonya wafuasi wake wasimwambie mtu yeyote kuwa yeye ndiye Masihi.
Yesu Asema ni Lazima Afe
(Mk 8:31-9:1; Lk 9:22-27)
21 Kuanzia wakati huo Yesu alianza kuwaambia wafuasi wake kuwa ni lazima aende Yerusalemu. Alifafanua kuwa Viongozi wazee wa Kiyahudi, viongozi wa makuhani na walimu wa sheria watamfanya apate mateso kwa mambo mengi. Na aliwaambia wafuasi wake kuwa lazima auawe. Na siku ya tatu atafufuka kutoka kwa wafu.
22 Petro akamchukua Yesu na kwenda naye faragha mbali na wafuasi wengine. Akaanza kumkosoa Yesu kwa akasema, “Mungu akuepushe mbali na mateso hayo, Bwana! Hilo halitakutokea!”
23 Ndipo Yesu akamwambia Petro, “Ondoka kwangu, Shetani![f] Hunisaidii! Hujali mambo ya Mungu. Unajali mambo ambayo wanadamu wanadhani ni ya muhimu.”
24 Kisha Yesu akawaambia wafuasi wake, “Ikiwa yeyote miongoni mwenu anataka kuwa mfuasi wangu, ni lazima aache kujiwazia yeye mwenyewe na mahitaji yake. Ni lazima awe radhi kuubeba msalaba aliopewa na kunifuata mimi. 25 Yeyote kati yenu anayetaka kuokoa uhai wake, ataupoteza. Lakini ninyi mlioyaacha maisha yenu kwa ajili yangu mtaupata uzima wa kweli. 26 Haina maana kwenu ninyi kuupata ulimwengu wote, ikiwa ninyi wenyewe mtapotea. Mtu atalipa nini ili kuyapata tena maisha yake baada ya kuyapoteza? 27 Mimi, Mwana wa Adamu, nitarudi katika utukufu wa Baba yangu pamoja na Malaika. Na nitamlipa kila mtu kutokana na matendo yake. 28 Niaminini ninaposema wapo watu waliopo hapa watakaoishi mpaka watakaponiona nikija kama Mwana wa Adamu kutawala kama mfalme.”
Yesu Awalisha Watu Zaidi ya 4,000
(Mt 15:32-39)
8 Wakati mwingine katika siku zile kundi kubwa la watu lilikusanyika na halikuwa na chakula. Yesu akawaita wanafunzi wake na kuwaambia, 2 “Nawahurumia watu hawa, kwa sababu hata sasa wamekuwa nami kwa siku tatu, na hawana kitu cha kula.”
3 Nikiwaacha waende majumbani mwao wakiwa na njaa, wataanguka njiani; na baadhi yao wametoka mbali.
4 Wanafunzi wake wakamjibu, “Wapi mtu yeyote atapata chakula cha kutosha mahali hapa jangwani cha kuwalisha watu hawa?”
5 Yesu akawauliza, “Mnayo mikate mingapi?” Wakajibu, “Saba.”
6 Kisha Yesu akaliagiza kundi la watu kuketi chini ardhini Akachukua mikate ile saba, akashukuru, akaimega na kuwapa wanafunzi wake waigawe. Nao wakaigawa kwenye kundi. 7 Kulikuwapo pia samaki wadogo wachache. Yesu akawabariki wale samaki na kuwaambia waigawe nayo pia.
8 Watu walikula na kushiba. Wakakusanya vikapu saba vilivyojaa mabaki. 9 Ilikuwa kama watu 4,000. Kisha Yesu akawaacha waende. 10 Mara Yesu akapanda katika mashua na wanafunzi wake, na akafika katika wilaya ya Dalmanutha.
Baadhi ya Watu Wawa na Mashaka na Mamlaka ya Yesu
(Mt 16:1-4; Lk 11:16,29)
11 Mafarisayo wakamwendea Yesu na kuanza kubishana naye. Ili kumjaribu wakamwomba ishara kutoka mbinguni. 12 Yesu alihema kwa nguvu na kusema, “Kwa nini kizazi kinataka ishara? Ninawaambia ukweli: hakuna ishara itakayooneshwa kwa kizazi hiki.” 13 Kisha Yesu akawaacha, akapanda tena katika mashua, na akaondoka kwenda upande wa pili wa ziwa.
Wafuasi Washindwa Kumwelewa Yesu
(Mt 16:5-12)
14 Wakati huo huo wanafunzi walikuwa wamesahau kuleta mikate yo yote, na hawakuwa na kitu kingine isipokuwa mkate mmoja. 15 Yesu akawaonya, akasema, “Mwe mwangalifu! Jilindeni na chachu ya Mafarisayo na ile ya Herode.”
16 Nao wakaanza kujadiliana haya miongoni mwao: “Labda alisema hivi kwa sababu hatukuwa na mkate wowote.”
17 Akijua walichokuwa wakikisema, akawaambia, “Kwa nini mnajadiliana juu ya kutopata mkate? Je! Bado hamwoni na kuelewa? Je! Mmezifunga akili zenu. 18 Mnayo macho; Je! Hamwoni? Mnayo masikio; Je! Hamwezi kusikia? Mnakumbuka? 19 Nilipomega na kugawa mikate mitano kwa watu 5,000, mlikusanya vikapu vingapi vilivyojaa masalia ya mikate?”
Wakasema “Kumi na viwili”.
20 “Nilipomega na kugawa mikate saba kwa watu 4,000, mlikusanya vikapu vingapi vilivyojaa masalia ya mikate?”
Wakasema “Saba”.
21 Kisha akawaambia, “Bado hamwelewi?”
Yesu Amponya Kipofu katika Kijiji cha Bethsaida
22 Walipofika katika kijiji cha Bethsaida, baadhi ya watu walimleta asiyeona kwa Yesu, na kumsihi Yesu amguse. 23 Yesu alimshika mkono yule asiyeona na kumtoa nje ya kijiji. Kisha Yesu alimtemea mate yule asiyeona kwenye macho yake, akaweka mkono wake juu ya asiyeona, na kumwuliza, “Je! Unaona kitu chochote?”
24 Kipofu akatazama juu na kusema, “Ninaona watu; wanaonekana kama miti inayotembea.”
25 Kisha Yesu akaweka mikono yake tena kwenye macho ya yule asiyeona. Naye akafumbua wazi macho yake yote. Kwani alipona kutokuona kwake na kuona kila kitu kwa uwazi. 26 Kisha Yesu akamwambia arudi nyumbani, na pia akamwambia, “Usiingie kijijini.”
Petro Atambua Yesu ni Nani
(Mt 16:13-20; Lk 9:18-21)
27 Yesu na wanafunzi wake walikwenda kwenye vijiji vinavyozunguka Kaisaria Filipi. Wakiwa njiani aliwauliza wanafunzi wake, “Watu wanasema mimi ni nani?”
28 Nao wakamjibu, “Yohana Mbatizaji. Wengine husema wewe ni Eliya. Na wengine husema wewe ni mmoja wa manabii.”
29 Kisha akawauliza wao, “Na ninyi; Je! Mnasema mimi ni nani?”
Petro akamjibu, “Wewe ni masihi.”
30 Kisha Yesu akawaonya wasimwambie mtu yeyote kuhusu yeye.
Yesu Asema ni Lazima Afe
(Mt 16:21-28; Lk 9:22-27)
31 Ndipo alianza kuwafundisha akisema: “Mwana wa Adamu lazima apate mateso mengi, na kukatataliwa na wazee, wakuu wa makuhani na walimu wa Sheria, na ni lazima atauawa na Kufufufuka baada ya siku ya tatu.” 32 Yesu aliwaambia haya kwa uwazi bila kuwaficha.
Baada ya mafundisho haya Petro alimchukua Yesu pembeni na kuanza kumkemea. 33 Lakini Yesu aligeuka nyuma na kuwaangalia wanafunzi wake, na kumkemea Petro kwa kumwambia, “Shetani,[a] toka mbele yangu! Huyajali yale anayoyajali Mungu bali yale wanayoyaona wanadamu kuwa ni muhimu.”
34 Kisha Yesu akaliita kundi lote pamoja na wanafunzi wake kwake, akawaambia, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, lazima ajikane yeye mwenyewe, na ni lazima auchukue msalaba wake mwenyewe kisha anifuate. 35 Kwa kuwa kila anayetaka kuusalimisha uhai wake, ataupoteza, na yeyote atakayeupoteza uhai wake kwa ajili yangu na kwa ajili ya injili atausalimisha. 36 Itampa mtu manufaa gani akiupata ulimwengu wote kisha akaupoteza uhai wake? 37 Mtu anaweza kuubadilisha uhai wake na kitu gani? 38 Hiki ni kizazi chenye dhambi na kisichokuwa na uaminifu. Hivyo, mtu yeyote atakayenionea haya mimi na mafundisho yangu, Mwana wa Adamu naye atamwonea haya mtu huyo siku ile atakaporudi katika utukufu wa Baba yake akiwa na malaika wake watakatifu.”
Petro Atambua Yesu ni Nani
(Mt 16:13-19; Mk 8:27-29)
18 Wakati mmoja Yesu alikuwa anaomba akiwa peke yake. Wafuasi wake walimwendea na aliwauliza, “Watu wanasema mimi ni nani?”
19 Wakajibu, “Baadhi ya watu wanasema wewe ni Yohana Mbatizaji, wengine wanasema wewe ni Eliya, lakini wengine wanasema wewe ni mmoja wa manabii wa zamani aliyefufuka.”
20 Kisha Yesu akawauliza wafuasi wake, “Na ninyi mnasema mimi ni nani?”
Petro akajibu, “Wewe ni Masihi kutoka kwa Mungu.”
21 Yesu akawatahadharisha wasimwambie mtu yeyote.
Yesu Asema ni Lazima Afe
(Mt 16:21-28; Mk 8:31-9:1)
22 Yesu akasema, “Ni lazima Mwana wa Adamu apate mateso mengi. Nitakataliwa na viongozi wazee wa Kiyahudi, viongozi wa makuhani na walimu wa sheria. Na nitauawa. Lakini siku ya tatu nitafufuliwa kutoka kwa wafu.”
23 Kisha Yesu akamwambia kila mmoja aliyekuwa pale, “Mtu yeyote miongoni mwenu akitaka kuwa mfuasi wangu ni lazima ajikane yeye mwenyewe na mambo anayopenda. Ni lazima uubebe msalaba unaotolewa kwako kila siku kwa sababu ya kunifuata mimi. 24 Yeyote miongoni mwenu anayetaka kuyaponya maisha yake atayaangamiza. Lakini yeyote atakayeyatoa maisha yake kwa ajili yangu atayaokoa. 25 Haina thamani kwenu kuupata ulimwengu wote ikiwa ninyi wenyewe mtateketezwa au kupoteza kila kitu. 26 Msione aibu kwa sababu ya kunifuata na kusikiliza mafundisho yangu. Mkifanya hivyo, Mimi, Mwana wa Adamu, nitawaonea aibu nitakapokuja nikiwa na utukufu wangu, utukufu wa Baba na wa malaika watakatifu. 27 Niaminini ninaposema kwamba baadhi yenu ninyi mliosimama hapa mtauona Ufalme wa Mungu kabla hamjafa.”
© 2017 Bible League International