Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Chronological

Read the Bible in the chronological order in which its stories and events occurred.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Matendo 11

Petro Arudi Yerusalemu

11 Mitume na waamini katika Uyahudi walisikia kwamba watu wasio Wayahudi wameyapokea mafundisho ya Mungu pia. Lakini Petro alipokuja Yerusalemu, baadhi ya waamini wa Kiyahudi[a] walimkosoa. Walisema, “Uliingia katika nyumba za watu wasio Wayahudi ambao hawajatahiriwa na ukala pamoja nao!”

Hivyo Petro akawaelezea namna ilivyotokea. Akasema, “Nilikuwa katika mji wa Yafa. Nilipokuwa nikiomba, niliona maono. Niliona kitu kikishuka chini kutoka mbinguni. Kilionekana kama shuka kubwa ikishushwa chini kwa pembe zake nne. Kikaja chini karibu yangu. Nilipotazama ndani yake, niliona aina zote za wanyama, pamoja na wale wa porini, wanyama wanaotambaa na ndege. Nilisikia sauti ikiniambia. Chinja chochote hapa na ule!”

“Lakini nilisema, ‘Siwezi kufanya hivyo Bwana! Sijawahi kula kitu cho chote kisicho safi au kisichostahili kuliwa kama chakula.’

Lakini sauti kutoka mbinguni ikajibu tena, ‘Mungu amevitakasa vitu hivi. Usiseme havistahili kuliwa!’

10 Hili lilitokea mara tatu. Ndipo kitu chote kikachukuliwa kurudi mbinguni. 11 Saa hiyo hiyo baada ya hayo wakawepo watu watatu wamesimama nje ya nyumba nilimokuwa ninakaa. Walikuwa wametumwa kutoka Kaisaria kunichukua. 12 Roho Mtakatifu aliniambia niende nao bila kuwa na mashaka. Ndugu hawa hapa sita walikwenda pamoja nami, na tulikwenda katika nyumba ya Kornelio. 13 Alitwambia kuhusu malaika aliyemwona amesimama katika nyumba yake. Malaika alimwambia, ‘Tuma baadhi ya watu waenda Yafa kumchukua Simoni, ambaye pia anaitwa Petro. 14 Atazungumza na wewe. Ujumbe atakaokwambia utakuokoa wewe na kila mtu anayeishi katika nyumba yako.’

15 Nilipoanza kuzungumza, Roho Mtakatifu alikuja juu yao kama vile alivyokuja juu yetu mwanzo.[b] 16 Ndipo nilikumbuka maneno ya Bwana Yesu, aliyosema: ‘Yohana alibatiza katika maji, lakini ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu.’ 17 Mungu amewapa watu hawa karama ile ile aliyotupa sisi tuliomwamini Bwana Yesu Kristo. Hivyo ningewezaje kupinga yale ambayo Mungu alitaka kufanya?”

18 Waamini wa Kiyahudi waliposikia hili, wakaacha kubisha. Wakamsifu Mungu na kusema, “Kwa hiyo Mungu anawaruhusu watu wasio Wayahudi kubadili mioyo yao na kuwa na maisha anayotoa!”

Habari Njema Zafika Antiokia

19 Waamini walitawanyika kwa sababu ya mateso[c] yaliyoanza baada ya Stefano kuuawa. Baadhi ya waamini walikwenda mbali mpaka Foeniki, Kipro na Antiokia. Walihubiri Habari Njema katika maeneo haya, lakini kwa Wayahudi tu. 20 Baadhi ya waamini hawa walikuwa watu kutoka Kipro na Kirene. Watu hawa walipofika Antiokia, walianza kuwahubiri watu wasio Wayahudi.[d] Waliwahubiri Habari Njema kuhusu Bwana Yesu. 21 Nguvu ya Bwana iliambatana na watu hawa, na idadi kubwa ya watu waliamini na kuamua kumfuata Bwana.

22 Kanisa katika mji wa Yerusalemu liliposikia kuhusu hili, lilimtuma Barnaba kwenda Antiokia. 23-24 Barnaba alikuwa mtu mwema, aliyejaa Roho Mtakatifu na imani. Alipokwenda Antiokia na kuona jinsi Mungu alivyowabariki waamini pale, alifurahi sana. Akawatia moyo wote, akasema, “Iweni waaminifu kwa Bwana daima. Mtumikieni Yeye kwa mioyo yenu yote.” Watu wengi zaidi wakawa wafuasi wa Bwana.

25 Kisha Barnaba alikwenda katika mji wa Tarso kumtafuta Sauli. 26 Alipompata, alimpeleka Antiokia. Walikaa pale mwaka mzima. Kila wakati kanisa lilipokusanyika, Barnaba na Sauli walikutana nao na kuwafundisha watu wengi. Ni katika mji wa Antiokia ambako wafuasi wa Bwana Yesu walianza kuitwa “Wafuasi wa Kristo”.[e]

27 Katika wakati huo huo baadhi ya manabii walitoka Yerusalemu na kwenda Antiokia. 28 Mmoja wao, aliyeitwa Agabo, huku akisaidiwa na Roho Mtakatifu, alisimama na kuzungumza. Alisema, “Wakati mbaya sana unakuja katika dunia yote. Hakutakuwa chakula kwa ajili ya watu kula.” (Kipindi hiki cha njaa kilitokea Klaudio alipokuwa mtawala wa Kirumi) 29 Wafuasi wa Bwana wakaamua kwamba kila mmoja wao atatuma kiasi anachoweza kuwasaidia ndugu wote[f] wanaoishi Uyahudi. 30 Walikusanya pesa na kuwapa Barnaba na Sauli, waliozipeleka kwa wazee, katika Uyahudi.

Matatizo Mengi kwa waamini

12 Katika wakati huu huu, Mfalme Herode akaanza kuwatesa baadhi ya waamini waliokuwa sehemu ya kanisa. Aliamuru Yakobo aliyekuwa kaka yake Yohana, auawe kwa upanga. Herode alipoona kuwa Wayahudi wamelifurahia jambo hili, aliamua kumkamata Petro pia. Hii lilitokea katika kipindi cha Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu. Alimkamata Petro na kumfunga gerezani, ambako alilindwa na kundi la askari kumi na sita.[g] Herode alipanga kumleta Petro mbele ya watu ili ahukumiwe, lakini alisubiri mpaka baada ya sikukuu ya Pasaka. Hivyo Petro aliwekwa gerezani lakini kanisa lilikuwa likiomba kwa Mungu bila kuacha kwa ajili yake.

Petro Atolewa Nje ya Gereza

Wakati wa usiku kabla ya siku ambayo Herode alipanga kumhukumu mbele ya watu, Petro, akiwa amefungwa minyororo miwili, alikuwa amelala katikati ya askari wawili. Na askari waliokuwa nje ya mlango walikuwa wanalinda gereza. Ghafla malaika wa Bwana alikuwa amesimama pale, na chumba kilijaa mwanga. Malaika akamwamsha Petro kwa kumpiga upande, akasema, “Amka haraka!” Minyororo ikaanguka kutoka mikono mwa Petro. Malaika akasema, “Vaa nguo na viatu vyako.” Petro alifanya kama alivyoambiwa. Kisha malaika akasema, “Vaa koti lako na unifuate.”

Hivyo malaika akatoka nje na Petro alimfuata. Hakujua kama kweli malaika alikuwa anafanya hili. Alidhani alikuwa anaona maono. 10 Petro na malaika wakavuka lindo la kwanza na lindo la pili. Kisha walifika kwenye lango la chuma lililowatenganisha na mji. Lango likafunguka. Baada ya kuvuka lango na kutembea umbali wa kama mtaa mmoja, malaika akatoweka ghafla.

11 Ndipo Petro akatambua kuwa haikuwa ndoto. Akawaza moyoni akisema, “Sasa ninajua kwamba Bwana hakika alimtuma malaika wake kwangu. Ameniokoa kutoka kwa Herode na kutoka kwenye mabaya yote ambayo Wayahudi walidhani yatanipata.”

12 Petro alipotambua hili, alikwenda nyumbani kwa Mariamu, mama yake Yohana, aliyeitwa Marko. Watu wengi walikuwa wamekusanyika pale wakiomba. 13 Petro alibisha kwenye mlango wa nje. Mtumishi wa kike aliyeitwa Rhoda alikuja ili afungue mlango. 14 Alipoitambua sauti ya Petro, alifurahi sana hata akasahau kufungua mlango. Akakimbilia ndani na kuliambia kundi, “Petro yuko mlangoni!” 15 Waamini wakamwambia, “Wewe una kichaa!” Lakini alipoendelea kusema kwamba ni kweli Petro yuko mlangoni. Waamini walisema, “Lazima atakuwa malaika wa Petro.”

16 Lakini Petro aliendelea kubisha mlangoni. Waamini walipoufungua mlango na kumwona, wakashangaa. 17 Petro akawafanyia ishara kwa mkono wake kuwaambia wanyamaze. Akawaeleza namna Bwana alivyomtoa nje ya gereza. Akasema, “Mwambieni Yakobo na ndugu wengine kilichotokea.” Kisha akawaacha na kwenda sehemu nyingine.

18 Siku iliyofuata askari walichanganyikiwa. Walijiuliza nini kimempata Petro. 19 Herode alimtafuta kila mahali lakini hakumpata. Hivyo aliwahoji walinzi na kuamuru wauawe.

Kifo cha Herode Agripa

Baadaye, Herode alihama kutoka Uyahudi na kwenda katika mji wa Kaisaria na kukaa huko kwa muda. 20 Herode aliwakasirikia sana watu katika miji ya Tiro na Sidoni. Lakini miji hii ilihitaji chakula kutoka katika nchi yake, hivyo baadhi yao walimjia wakitaka amani naye. Waliweza kumshawishi Blasto mtumishi binafsi wa Mfalme ili awasaidie.

21 Herode alichagua siku maalumu ya kukutana nao. Siku hiyo alivaa vazi zuri la kifalme. Aliketi kwenye kiti chake cha enzi na kuwahutubia watu. 22 Watu wakapaza sauti zao na kusema, “Hii ni sauti ya mungu, siyo mwanadamu!” 23 Herode hakumpa Mungu utukufu. Hivyo malaika wa bwana akampiga kwa ugonjwa. Akaliwa na minyoo ndani na kufa.

24 Ujumbe wa Mungu ulikuwa unasambaa, ukiwafikia watu wengi zaidi.

25 Baada ya Barnaba na Sauli kumaliza kazi yao Yerusalemu, walirudi Antiokia, walimchukua Yohana aliyeitwa Marko pamoja nao.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International