Beginning
Gavana Pilato Amhoji Yesu
(Mt 27:1-2,11-14; Mk 15:1-5; Yh 18:28-38)
23 Kisha kundi lote likasimama, wakampeleka Yesu kwa Pilato. 2 Wakaanza kumshitaki Yesu na kumwambia Pilato, “Tumemkamata mtu huyu akijaribu kuwapotosha watu wetu. Anasema tusilipe kodi kwa Kaisari. Anajiita Masihi, mfalme.”
3 Pilato akamwuliza Yesu, “Wewe ni mfalme wa Wayahudi?”
Yesu akajibu, “Ndiyo, unaweza kusema hivyo.”
4 Pilato akawaambia wakuu wa makuhani na watu, “Sioni kosa lolote kwa mtu huyu.”
5 Lakini waliendelea kusema, “Mafundisho yake yanasababisha matatizo katika Uyahudi yote. Alianzia Galilaya na sasa yupo hapa!”
Pilato Ampeleka Yesu Kwa Herode
6 Pilato aliposikia hili, akauliza, “Mtu huyu anatoka Galilaya?” 7 Akatambua kuwa Yesu yuko chini ya mamlaka ya Herode. Siku hizo Herode alikuwa Yerusalemu, hivyo Pilato alimpeleka Yesu kwake.
8 Herode alipomwona Yesu alifurahi sana. Alikuwa akisikia habari zake na kwa muda mrefu alikuwa anataka kukutana na Yesu. Herode alitaka kuona muujiza, hivyo alitegemea kwamba Yesu angefanya muujiza mmoja. 9 Akamwuliza Yesu maswali mengi, lakini Yesu hakusema chochote. 10 Viongozi wa makuhani na walimu wa sheria walikuwa wamesimama pale wakipaza sauti zao wakimshitaki kwa Herode. 11 Ndipo Herode na askari wake wakamcheka. Wakamfanyia mzaha kwa kumvalisha mavazi kama ambayo wafalme huvaa. Kisha Herode akamrudisha Yesu kwa Pilato. 12 Nyakati za nyuma Pilato na Herode walikuwa maadui daima. Kuanzia siku ile wakawa marafiki.
Pilato Ajaribu Kumwachia Huru Yesu
(Mt 27:15-26; Mk 15:6-15; Yh 18:39-19:16)
13 Pilato aliwaita viongozi wa makuhani, viongozi wa Kiyahudi na watu wote pamoja. 14 Akawaambia, “Mlimleta mtu huyu kwangu. Mlisema alikuwa anawapotosha watu. Lakini nimemchunguza mbele yenu nyote na sijaona hatia juu ya kitu chochote mnachomshitakia. 15 Hata Herode hakumwona kuwa ana hatia yo yote. Akamrudisha kwetu. Tazameni, hajafanya jambo lolote baya linalostahili adhabu ya kifo. 16 Kwa hiyo, baada ya kumwadhibu kidogo nitamwacha aende zake.” 17 [a]
18 Lakini wote walipaza sauti zao pamoja, “Mwue! Mwachie huru Baraba!” 19 (Baraba alifungwa gerezani kwa sababu ya kuanzisha fujo mjini na kwa mauaji.)
20 Pilato alitaka amwachie huru Yesu. Hivyo Pilato akawaambia atamwachilia. 21 Lakini walipaza sauti tena wakisema, “Mwue, Mwue msalabani!”
22 Mara ya tatu Pilato akawaambia watu, “Kwa nini? Amefanya kosa gani? Hana hatia. Sioni sababu ya kumwua. Hivyo nitamwachia huru baada ya kumwadhibu kidogo.”
23 Lakini watu waliendelea kupaza sauti. Walidai Yesu auawe msalabani. Kelele zao zikawa kubwa kiasi kwamba 24 Pilato aliamua kuwapa kile walichotaka. 25 Walitaka Baraba aliyekuwa gerezani kwa sababu ya kuanzisha fujo na mauaji aachiwe huru. Pilato akamwachia Baraba. Na kumtoa Yesu ili auawe. Hili ndilo watu walitaka.
Yesu Awambwa Msalabani
(Mt 27:32-44; Mk 15:21-32; Yh 19:17-27)
26 Askari wakamwongoza Yesu kumtoa nje ya mji. Wakati huo huo mtu mmoja kutoka Kirene alikuwa anaingia mjini kutoka maeneo nje ya Yerusalemu. Askari wakamlazimisha kuubeba msalaba wa Yesu na kumfuata Yesu kwa nyuma.
27 Kundi kubwa wakamfuata Yesu. Baadhi ya wanawake waliokuwemo kwenye kundi walilia na kuomboleza. Walimwonea huruma. 28 Lakini Yesu aligeuka na kuwaambia, “Wanawake wa Yerusalemu, msinililie. Jililieni ninyi wenyewe na watoto wenu. 29 Wakati unakuja ambapo watu watasema, ‘Wanawake wasioweza kuwa na watoto ndio ambao Mungu amewabariki. Hakika ni baraka kwamba hawana watoto wa kutunza.’ 30 Watu wataiambia milima, ‘Tuangukieni!’ Wataviambia vilima, ‘Tufunikeni!’(A) 31 Kama hili linaweza kutokea kwa mtu aliye mwema, nini kitatokea kwa wenye hatia?”
32 Walikuwepo pia wahalifu wawili waliotolewa nje ya mji pamoja na Yesu ili wauawe. 33 Walipelekwa mahali palipoitwa “Fuvu la Kichwa.” Askari walimpigilia Yesu msalabani pale. Waliwapigilia misalabani wahalifu pia, mmoja aliwekwa upande wa kulia na mwingine kushoto kwa Yesu.
34 Na Yesu alikuwa anasema, “Baba uwasamehe watu hawa, kwa sababu hawajui wanalofanya.”
Askari waligawana nguo zake kwa kutumia kamari. 35 Watu walisimama pale wakiangalia kila kitu kilichokuwa kinatokea. Viongozi wa Kiyahudi walimcheka Yesu. Walisema, “Kama kweli yeye ni Masihi, Mfalme Mteule wa Mungu, basi ajiokoe. Je, hakuwaokoa wengine?”
36 Hata askari walimcheka Yesu na kumfanyia mizaha. Walikuja na kumpa siki ya mvinyo. 37 Wakasema, “Ikiwa wewe ni mfalme wa Wayahudi, jiokoe mwenyewe!” 38 Waliandika maneno haya kwenye kibao msalabani juu ya kichwa chake: “Huyu ni Mfalme wa Wayahudi”.
39 Mmoja wa wahalifu aliyekuwa ananing'inia pale akaanza kumtukana Yesu: “Wewe siye Masihi? Basi jiokoe na utuokoe sisi pia!”
40 Lakini mhalifu mwingine alimnyamazisha asiendelee kumtukana Yesu. Akasema, “Unapaswa kumwogopa Mungu. Sisi sote tutakufa muda si mrefu. 41 Wewe na mimi tuna hatia, tunastahili kufa kwa sababu tulitenda mabaya. Lakini mtu huyu hajafanya chochote kibaya.” 42 Kisha akamwambia Yesu, “Unikumbuke utakapoanza kutawala kama mfalme!”
43 Yesu akamwambia, “Ninakwambia kwa uhakika, leo utakuwa pamoja nami Paradiso.”
Yesu Afariki
(Mt 27:45-56; Mk 15:33-41; Yh 19:28-30)
44 Ilikuwa yapata saa sita mchana, lakini kulibadilika kukawa giza mpaka saa tisa alasiri, 45 kwa sababu jua liliacha kung'aa. Pazia ndani ya Hekalu lilichanika vipande viwili. 46 Yesu alipaza sauti akasema, “Baba, ninaiweka roho yangu mikononi mwako!”(B) Baada ya Yesu kusema haya, akafa.
47 Mkuu wa askari wa Kirumi aliyekuwa pale alipoona yaliyotokea, alimsifu Mungu, akisema, “Ninajua mtu huyu alikuwa mtu mwema!”
48 Watu wengi walikuwa wametoka mjini kuja kuona tukio hili. Walipoona, wakahuzunika, wakaondoka wakiwa wanapiga vifua vyao. 49 Watu waliokuwa marafiki wa karibu wa Yesu walikuwepo pale. Pia, walikuwepo baadhi ya wanawake waliomfuata Yesu kutoka Galilaya. Walisimama mbali kutoka msalabani, waliyaona mambo haya.
Yesu Azikwa
(Mt 27:57-61; Mk 15:42-47; Yh 19:38-42)
50-51 Mtu mmoja aliyeitwa Yusufu kutoka mji wa Uyahudi ulioitwa Arimathaya alikuwapo pale. Alikuwa mtu mwema, aliyeishi namna Mungu alivyotaka. Alikuwa anausubiri ufalme wa Mungu uje. Yusufu alikuwa mjumbe wa baraza la Kiyahudi. Lakini hakukubali pale viongozi wengine wa Kiyahudi walipoamua kumwua Yesu. 52 Alikwenda kwa Pilato na kumwomba mwili wa Yesu. 53 Aliushusha mwili kutoka msalabani na kuufunga kwenye nguo. Kisha akauweka ndani ya kaburi lililochimbwa katika ukuta wa mwamba. Kaburi hili lilikuwa halijatumika bado. 54 Ilikuwa jioni Siku ya Maandalizi ya Sabato. Sabato ilikuwa ianze baada ya jua kuzama.
55 Wanawake waliotoka Galilaya pamoja na Yesu walimfuata Yusufu. Wakaliona kaburi. Ndani yake wakaona mahali alipouweka mwili wa Yesu. 56 Kisha wakaenda kuandaa manukato yanayonukia vizuri ili kuupaka mwili wa Yesu.
Siku ya Sabato walipumzika, kama ilivyoamriwa katika Sheria ya Musa.
Yesu Amefufuka Kutoka Mauti
(Mt 28:1-10; Mk 16:1-8; Yh 20:1-10)
24 Asubuhi mapema sana siku ya Jumapili, wanawake walikwenda kaburini ulikolazwa mwili wa Yesu. Walibeba manukato yanayonukia vizuri waliyoyaandaa. 2 Walikuta jiwe kubwa lililokuwa limeziba mlango wa kaburi limevingirishwa kutoka kwenye mlango wa kaburi. 3 Waliingia kaburini, lakini hawakuuona mwili wa Bwana Yesu. 4 Hawakulielewa hili. Walipokuwa wangali wanashangaa, watu wawili waliovaa mavazi yaliyong'aa walisimama pembeni mwao. 5 Wanawake waliogopa sana. Waliinama nyuso zao zikaelekea chini. Wale watu wakawaambia, “Kwa nini mnamtafuta aliye hai hapa? Hapa ni mahali pa waliokufa. 6 Yesu hayuko hapa. Amefufuka kutoka kwa wafu. Mnakumbuka alivyosema alipokuwa Galilaya? 7 Alisema kwamba, ‘Mwana wa Adamu lazima atatolewa kwa mamlaka ya watu wenye dhambi, lazima atauawa msalabani na kufufuka kutoka kwa wafu siku ya tatu.’” 8 Ndipo wanawake wakakumbuka Yesu alivyosema.
9 Wanawake wakaondoka kaburini na kurudi kwa mitume kumi na mmoja na wafuasi wengine. Waliwaeleza kila kitu kilichotokea kaburini. 10 Wanawake hawa walikuwa Mariamu Magdalena, Yoana, na Mariamu, mama yake Yakobo na wanawake wengine. Waliwaambia mitume kila kitu kilichotokea. 11 Lakini mitume hawakuamini yale waliyosema. Ilionekana kama upuuzi. 12 Lakini Petro alinyanyuka na kukimbia kwenda kaburini kuona. Alitazama ndani, lakini aliona nguo tu iliyotumika kuufunga mwili wa Yesu. Petro aliondoka kwenye kaburi akarudi nyumbani alikokuwa anakaa, akijiuliza nini kilichotokea.[b]
Njiani Kwenda Emausi
(Mk 16:12-13)
13 Siku hiyo hiyo, wafuasi wawili[c] wa Yesu walikuwa wanakwenda kwenye mji mdogo uitwao Emausi, uliokuwa yapata kilomita kumi na mbili[d] kutoka Yerusalemu. 14 Walikuwa wanazungumza kuhusu mambo yote yaliyotokea. 15 Walipokuwa wakizungumza, wakijadiliana juu ya mambo haya, Yesu mwenyewe aliwasogelea na akawa anatembea nao. 16 Lakini hawakuruhusiwa kumtambua. 17 Yesu akawauliza, “Ni mambo gani ninayosikia mnajadiliana mnapotembea?”
Wale wafuasi wawili wakasimama, sura zao zilionekana zenye huzuni. 18 Mmoja wao, aliyeitwa Kleopa akasema, “Lazima wewe ni mtu pekee katika Yerusalemu ambaye hujui yaliyotokea huko.”
19 Yesu akasema, “Unasema kuhusu nini?”
Wakasema, “Ni kuhusu Yesu, kutoka Nazareti, alikuwa nabii mkuu mbele za Mungu na watu wote. Alisema na kutenda mambo makuu mengi. 20 Lakini viongozi wetu na viongozi wa makuhani walimtoa ili ahukumiwe na kuuawa. Wakampigilia msalabani. 21 Tulitegemea kuwa ndiye atakayeiweka huru Israeli. Lakini sasa haya yote yametokea.
Na sasa kitu kingine: Imekuwa ni siku tatu tangu alipouawa, 22 lakini leo baadhi ya wanawake kutoka kwenye kundi letu walituambia jambo la kushangaza. Mapema asubuhi hii walikwenda kaburini ambako mwili wa Yesu ulilazwa. 23 Lakini hawakuuona mwili wake pale. Walikuja na kutuambia kuwa wamewaona malaika. Malaika waliwaambia Yesu yu hai! 24 Hivyo baadhi ya watu walio katika kundi letu walikwenda kaburini pia. Ilikuwa kama wanawake walivyosema. Waliliona kaburi, lakini hawakumwona Yesu.”
25 Ndipo Yesu akawaambia, “Ninyi ni wajinga na wazito wa kuyakubali yale waliyoandika manabii. 26 Manabii waliandika kwamba Masihi lazima ateseke kwa mambo haya kabla hajaingia katika utukufu wa ufalme wake.” 27 Kisha akaanza kufafanua kila kitu walichosema manabii kuhusu yeye. Alianzia katika vitabu vya Musa na kusema yale waliyosema manabii kuhusu yeye.
28 Wakakaribia mji wa Emausi, na Yesu akafanya kama vile alikuwa anaendelea mbele. 29 Lakini walimtaka akae, wakamsihi: “Kaa nasi. Tayari ni usiku. Mchana unakaribia kwisha.” Hivyo aliingia ndani kukaa nao.
30 Alipokuwa mezani pamoja nao ili kula chakula cha usiku, Yesu akachukua mkate na kushukuru. Kisha akaumega na kuwapa. 31 Baada ya kufanya hivyo, wafuasi wale wawili wakaruhusiwa kumtambua. Lakini walipojua yeye ni nani, alitoweka. 32 Wakasemezana, “Alivyokuwa anazungumza nasi tulipokuwa barabarani, tulijisikia kama moto unawaka ndani yetu. Ilitusisimua sana alipotufafanulia maana halisi ya Maandiko!”
33 Hivyo wafuasi wale wawili wa Bwana Yesu wakasimama na kurudi Yerusalemu haraka. Walipofika Yerusalemu waliwakuta mitume kumi na mmoja wamekusanyika pamoja na wafuasi wengine wa Bwana Yesu. 34 Kundi likawaambia wale wafuasi wawili, “Hakika Bwana amefufuka kutoka kwa wafu! Alimtokea Simoni.”
35 Ndipo wafuasi wawili wakaeleza kilichotokea barabarani. Wakaeleza jinsi walivyomtambua Yesu aliposhiriki mkate pamoja nao.
Yesu Awatokea Wafuasi Wake
(Mt 28:16-20; Mk 16:14-18; Yh 20:19-23; Mdo 1:6-8)
36 Wakati wafuasi wawili wakiwa bado wanawaeleza mambo haya wafuasi wengine, Yesu mwenyewe akaja na kusimama katikati yao. Akawaambia, “Amani iwe kwenu.”
37 Wafuasi walishituka na wakaogopa. Walidhani wanaona mzimu. 38 Lakini Yesu akasema, “Kwa nini mnaogopa? Na kwa nini mnakitilia mashaka kile mnachokiona? 39 Angalieni mikono na miguu yangu. Hakika ni mimi. Niguseni. Mtaweza kuona kuwa nina mwili wenye nyama na mifupa; mzimu hauna mwili kama huu.”
40 Mara baada ya Yesu kusema haya, aliwaonesha mikono na miguu yake. 41 Wafuasi walishangaa na kufurahi sana walipoona kuwa Yesu alikuwa hai. Kwa kuwa bado walikuwa hawaamini wanachokiona, akawaambia, “Mna chakula chochote hapa?” 42 Wakampa kipande cha samaki aliyepikwa. 43 Wafuasi wake wakiwa wanaangalia akakichukua na kukila.
44 Yesu akawaambia, “Mnakumbuka nilipokuwa pamoja nanyi? Nilisema kila kitu kilichoandikwa kuhusu mimi katika Sheria ya Musa, vitabu vya manabii na Zaburi lazima kitimilike.”
45 Kisha Yesu akawafafanulia Maandiko ili waelewe maana yake halisi. 46 Yesu akawaambia, “Imeandikwa kuwa Masihi atauawa na atafufuka kutoka kwa wafu siku ya tatu. 47-48 Mliona mambo haya yakitokea, ninyi ni mashahidi. Na maandiko yanasema inawapasa mwende na kuwahubiri watu kuwa ni lazima wabadilike na kumgeukia Mungu, ili awasamehe. Ni lazima mwanzie Yerusalemu na mhubiri ujumbe huu kwa jina langu kwa watu wa mataifa yote. 49 Kumbukeni kwamba nitamtuma kwenu yule ambaye Baba yangu aliahidi. Kaeni jijini mpaka mtakapopewa nguvu hiyo kutoka mbinguni.”
Yesu Arudi Mbinguni
(Mk 16:19-20; Mdo 1:9-11)
50 Yesu akawaongoza wafuasi wake kutoka nje ya Yerusalemu hadi karibu na Bethania. Akanyenyua mikono yake na kuwabariki wafuasi wake. 51 Alipokuwa anawabariki, alitenganishwa nao na kuchukuliwa mbinguni. 52 Wafuasi wake walimwabudu, kisha wakarudi Yerusalemu wakiwa na furaha sana. 53 Walikuwa katika Hekalu wakati wote, wakimsifu Mungu.
© 2017 Bible League International