Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Beginning

Read the Bible from start to finish, from Genesis to Revelation.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Marko 12-13

Yesu Atoa Simulizi Kuhusu Shamba la Mzabibu

(Mt 21:33-46; Lk 20:9-19)

12 Yesu alianza kuongea nao kwa simulizi zenye mafumbo: “Mtu mmoja alipanda mizabibu shambani. Akajenga ukuta kuizunguka, akachimba shimo kwa ajili ya kukamulia mizabibu na kisha alijenga mnara. Baadaye alilikodisha kwa baadhi ya wakulima na akaenda safari nchi ya mbali.

Yalipotimia majira ya kuvuna, alimtuma mtumishi wake kwa wakulima wale, ili kukusanya sehemu yake ya matunda ya mzabibu. Lakini wakulima wale walimkamata mtumishi yule, wakampiga, na kumfukuza pasipo kumpa chochote. Kisha akamtuma mtumishi mwingine kwao. Huyu naye wakampiga kichwani na kumtendea mambo ya aibu. Yule mmiliki wa shamba la mzabibu akamtuma mtumishi mwingine, na wakulima wale wakamuua na yule pia. Baada ya hapo alituma wengi wengine. Wakulima wale waliwapiga baadhi yao na kuua wengine.

Hata hivyo mwenye shamba yule bado alikuwa na mmoja wa kumtuma, mwanaye mpendwa. Alimtuma akiwa mtu wa mwisho. Akasema, ‘nina hakika watamheshimu mwanangu!’

Lakini wakulima wale walisemezana wao kwa wao, ‘Huyu ndiye yule mrithi. Njooni tukamuue, na urithi utakuwa wetu!’ Kwa hiyo wakamchukua na kumuua, kisha wakautupa mwili wake nje ya shamba la mizabibu.

Je! Mnadhani mwenye kumiliki lile shamba la mizabibu atafanya nini? Atakuja na kuwaua wakulima wale, na kukodisha shamba lile kwa watu wengine. 10 Je! Hamjayasoma maandiko haya:

‘Jiwe ambalo wajenzi wamelikataa
    limekuwa jiwe kuu la msingi.
11 Hii imefanywa na Bwana
    na ni ajabu kubwa kwetu kuona!’”(A)

12 Na viongozi wa kidini wakatafuta njia ya kumkamata Yesu, lakini waliogopa lile kundi la watu. Kwani walijua ya kwamba Yesu alikuwa ameisema simulizi ile yenye mafumbo ili kuwapinga. Kwa hiyo viongozi wa kidini wakamwacha na kuondoka.

Yesu Ajibu Swali Lenye Mtego

(Mt 22:15-22; Lk 20:20-26)

13 Viongozi wa Kidini wakamtumia baadhi ya Mafarisayo na Maherode ili kumkamata kama akisema chochote kimakosa. 14 Wale waliotumwa walifika na kumwambia, “Mwalimu tunajua, kwamba wewe ni mkweli, na tena hujali yale watu wanayoyafikiri kuhusu wewe, kwa sababu wewe hubabaishwi na wadhifa wa mtu. Lakini unafundisha ukweli wa njia ya Mungu. Tuambie ni haki kulipa kodi kwa Kaisari ama la? Je, tulipe au tusilipe?”

15 Lakini Yesu aliutambua unafiki wao na akawaambia, “Kwa nini mnanijaribu hivi? Mniletee moja ya sarafu ya fedha mnazotumia ili niweze kuiangalia.” 16 Hivyo wakamletea sarafu, naye akawauliza, “Je, sura hii na jina hili ni la nani?” Nao wakamwambia, “Ya Kaisari.”

17 Ndipo Yesu alipowaambia, “Mpeni Kaisari vilivyo vyake, na Mungu mpeni vilivyo vyake.” Wakastaajabu sana kwa hayo.

Baadhi ya Masadukayo Wajaribu Kumtega Yesu

(Mt 22:23-33; Lk 20:27-40)

18 Kisha Masadukayo wakamjia. (Hawa ni wale wanaosema hakuna ufufuo wa wafu.) Wakamwuliza, 19 “Mwalimu, Musa alituandikia kwamba ikiwa kaka wa mtu atafariki na kumwacha mke asiye na watoto, Basi yule kaka lazima aoe mke yule wa nduguye na kuzaa naye watoto kwa ajili ya kaka yake aliyefariki. 20 Palikuwepo na ndugu wa kiume saba. Wa kwanza alioa mke, naye alikufa bila kuacha mtoto yeyote. 21 Wa pili naye akamwoa yule mke wa nduguye wa kwanza aliyeachwa naye akafa bila kuacha watoto wowote. Ndugu wa tatu pia alifanya vivyo hivyo. 22 Ndugu wote wale saba walimwoa yule mwanamke na wote hawakupata watoto. Mwisho wa yote, yule mwanamke pia akafariki, 23 Katika ufufuo, pale wafu watakapofufuka toka katika kifo, Je, yeye atakuwa mke wa nani? Kwani wote saba walikuwa naye kama mke wao.”

24 Yesu akawaambia, “Hakika hii ndiyo sababu mmekosa sana: Hamyajui Maandiko wala uwezo wa Mungu. 25 Kwa kuwa wafu wanapofufuka toka katika wafu, hawaoi wala kuolewa. Badala yake wanakuwa kama malaika walioko Mbinguni. 26 Lakini kuhusu kufufuka kwa wafu, Je, hamjasoma katika kitabu cha Musa katika sura ile ya kichaka kinachoungua? Pale ndipo Mungu alipomwambia Musa, ‘Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo.’(B) 27 Yeye si Mungu wa waliokufa, bali wa wale wanaoishi. Hivyo ninyi mmekosa sana.”

Amri ipi ni ya Muhimu Zaidi?

(Mt 22:34-40; Lk 10:25-28)

28 Mwalimu wa Sheria alifika naye aliwasikia wakijadiliana. Alipoona jinsi Yesu alivyowajibu vizuri sana, alimwuliza, “Je, amri ipi ni muhimu sana kuliko zote?”

29 Yesu akajibu, “Muhimu sana ni hii: ‘Sikiliza, Israeli, Bwana Mungu wetu ni mmoja. 30 Nawe unapaswa kumpenda Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa nafsi yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote.’(C) 31 Amri ya pili ni hii: ‘mpende jirani yako[a] kama unavyojipenda mwenyewe.’(D) Hakuna amri nyingine kubwa kuliko hizi.”

32 Na mwalimu wa Sheria akamwambia, “Umejibu vema kabisa mwalimu. Upo sahihi kusema kuwa Mungu ni mmoja, na hakuna mwingine ila yeye. 33 Ni muhimu zaidi kumpenda Mungu kwa moyo wako wote, kwa ufahamu wako wote, na kwa nguvu zako zote, na kumpenda jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe kuliko sadaka zote za kuteketezwa na matoleo tunayompa Mungu.”

34 Yesu alipoona kwamba yule mtu amejibu kwa busara, alimwambia, “Wewe hauko mbali na Ufalme wa Mungu.” Baada ya hapo hakuwepo mtu mwingine aliyediriki kumwuliza maswali mengine zaidi.

Je, Masihi ni Mwana wa Daudi?

(Mt 22:41-46; Lk 20:41-44)

35 Yesu alipokuwa akifundisha katika mabaraza ya Hekalu, alisema, “Inawezekana vipi walimu wa Sheria kusema kwamba Kristo ni mwana wa Daudi? 36 Daudi mwenyewe kwa kupitia Roho Mtakatifu alisema,

‘Bwana Mungu alimwambia Bwana Mfalme wangu:
Keti karibu nami upande wangu wa kuume,
    nami nitawaweka adui zako chini ya udhibiti wako.’[b](E)

37 Daudi anamwita Masihi ‘Bwana’. Itakuwaje tena Kristo awe yote Bwana na pia mwana wa Daudi?”

Hapo lilikuwepo kundi kubwa la watu liliokuwa likimsikiliza kwa furaha.

Yesu Anawakosoa Walimu wa Sheria

(Mt 23:6-7; Lk 11:43; 20:45-47)

38 Katika mafundisho yake alisema, “Jihadharini na walimu wa Sheria.” Wao wanapenda kutembea huko na huko katika mavazi yanayopendeza huku wakipenda kusalimiwa masokoni, 39 Hao wanapenda kukaa viti vya mbele katika masinagogi na kupewa sehemu muhimu zaidi za kukaa katika karamu za chakula. 40 Hawa huwadanganya wajane ili wazichukue nyumba zao na wanasali sala ndefu ili kujionesha kwa watu. Watu hawa watapata hukumu iliyo kubwa zaidi.

Mjane Aonesha Jinsi Ulivyo Utoaji wa Kweli

(Lk 21:1-4)

41 Yesu aliketi mahali kuvuka pale palipokuwepo na sanduku la matoleo, alitazama jinsi ambavyo watu walikuwa wakiweka sadaka zao sandukuni. Matajiri wengi waliweka fedha nyingi. 42 Kisha mjane maskini alikuja na kuweka sarafu mbili ndogo za shaba, ambazo zilikuwa na thamani ndogo sana.

43 Yesu aliwaita wanafunzi wake pamoja na kuwaambia, “Nawaambieni ukweli mjane huyu maskini ameweka sarafu mbili tu. Lakini ukweli ni kwamba ametoa zaidi ya matajiri wote wale.” 44 Kwa kuwa wote walitoa kile cha ziada walichokuwa nacho. Lakini yeye katika umasikini wake, aliweka yote aliyokuwa nayo. Na hiyo ilikuwa fedha yote aliyokuwa nayo kutumia wa maisha yake.

Yesu Aonya Kuhusu Wakati Ujao

(Mt 24:1-25; Lk 21:5-24)

13 Yesu alikuwa akiondoka katika eneo la Hekalu na moja ya wanafunzi wake akamwambia, “Mwalimu, tazama mawe haya yanavyopendeza na jinsi majengo haya yanavyopendeza!”

Yesu akamjibu, “Je, mnayaona majengo haya makubwa? Yote yatabomolewa. Kila jiwe litaporomoshwa hata chini. Hakuna jiwe lolote kati ya haya litakaloachwa mahali pake.”

Naye alipokuwa ameketi juu ya Mlima wa Mizeituni upande wa pili kuvuka Hekalu, Petro, Yakobo, Yohana na Andrea walimwuliza wakiwa faragha, “Haya tuambie, ni lini mambo haya yatakapotokea? Ni ishara gani itakayoonesha ya kwamba yote yanakaribia kutimizwa?”

Yesu akaanza kuwaeleza, “Muwe waangalifu mtu asije akawadanganya. Wengi watakuja huku wakilitumia Jina langu na kusema, ‘Mimi ndiye Masihi,’[c] nao watawadanganya wengi. Mtasikia juu ya vita vinavyopiganiwa na mtasikia habari juu ya vita vingine vinavyoanza. Hata hivyo msishtushwe. Mambo hayo lazima yatokee, kabla ule mwisho wenyewe kufika. Kwani taifa moja litapigana dhidi ya taifa lingine na ufalme mmoja utapigana dhidi ya ufalme mwingine. Yatatokea matetemeko mengi mahali pengi na kutakuwepo na njaa kali sehemu nyingi. Mambo haya yatakuwa ni mwanzo tu wa uchungu wa mama mzazi kabla ya mtoto kuzaliwa.

Hivyo mjihadhari! Wapo watu watakaowakamata na kuwapeleka mkahukumiwe kwa kuwa ninyi ni wanafunzi wangu. Watawapiga katika masinagogi yao. Mtalazimishwa kusimama mbele ya wafalme na watawala. Nanyi mtawaeleza habari zangu. 10 Kabla ya mwisho kufika, ni lazima kwanza habari Njema itangazwe kwa mataifa yote. 11 Wakati wowote watakapowakamata na kuwashitaki, msiwe na wasiwasi kujiandaa kwa yale mtakayoyasema, lakini myaseme yale mtakayopewa saa ile ile, kwa kuwa si ninyi mnaozungumza; bali, ni Roho Mtakatifu anayezungumza.

12 Na ndugu atamsaliti nduguye hata kuuawa, na baba atamsaliti mwanawe. Watoto nao watawaasi wazazi wao na hata kuwatoa wauawe. 13 Nanyi mtachukiwa na wote kwa sababu yangu. Lakini yeyote atakayevumilia hadi mwisho ataokoka.

14 Wakati mtakapoliona chukizo la uharibifu[d] likisimama mahali pasipotakiwa lisimame.” (Msomaji aelewe hii ina maana gani?[e]) “Kisha wale waliopo katika Uyahudi wakimbilie milimani. 15 Ikiwa mtu yupo katika paa la nyumba yake, asishuke chini na kuingia nyumbani mwake kuchukua kitu chochote. 16 Ikiwa mtu yupo shambani asirudi kuchukua vazi lake.

17 Wakati huo itakuwa hatari kwa wanawake walio waja wazito na wale wenye watoto wachanga. 18 Ombeni kwamba haya yasitokee wakati wa majira ya baridi. 19 Kwa kuwa taabu itakayotokea katika siku hizo itakuwa ile ambayo haijawahi kutokea tangu mwanzo pale Mungu alipoumba dunia hadi sasa. Na hakitatokea tena kitu kama hicho. 20 Kama Bwana asingelifupisha muda huo, hakuna ambaye angenusurika. Lakini yeye amefupisha siku hizo kwa ajili ya watu wale aliowateuwa.

21 Ikiwa mtu atawaambia, ‘Tazama, Kristo ni huyu hapa!’ ama ‘Ni yule pale!’ Usiliamini hilo. 22 Kwani Makristo wa uongo na manabii wa uongo watatokea, nao watafanya ishara na miujiza kuwadanganya watu ikiwezekana hata wale ambao Mungu amewachagua. 23 Kwa hiyo mjihadhari nimewaonya juu ya mambo haya kabla hayajatokea.

Yesu Atakaporudi Tena

(Mt 24:29-51; Lk 21:25-36; 19:12-13,40)

24 Lakini katika siku hizo, baada ya kipindi cha dhiki,

‘Jua litatiwa giza,
    mwezi hautatoa mwanga,
25 nyota zitaanguka kutoka angani,
    na mbingu yote itatikisika.’[f]

26 Ndipo watu watakapomwona Mwana wa Adamu akija mawinguni pamoja na nguvu kubwa na utukufu. 27 Baada ya hapo Mwana wa Adamu atawatuma malaika, na atawakusanya wateule wake kutoka kila upande wa dunia.

28 Jifunzeni somo hili kutoka katika mti wa mtini: Matawi yake yanaponyauka na kubeba majani, unajua kwamba kiangazi kimekaribia. 29 Vivyo hivyo, unapoona mambo haya yanaanza kutokea unajua kwamba muda umekaribia na umeshafika mlangoni. 30 Ninawaambieni ukweli: Kizazi hiki hakitapita kabla ya mambo haya yote hayajatokea. 31 Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.

32 Hakuna anayejua wakiwemo malaika wa mbinguni ama Mwana bali baba peke yake lini siku au saa ile itakapowadia. 33 Mjihadhari; Kesheni! Kwani hamjui lini muda huo utafika.

34 Ni kama mtu anayeenda safarini na kabla ya kuondoka huiacha nyumba yake mikononi mwa watumishi wake. Kabla ya kuiacha nyumba yake anawaweka watumishi wake kusimamia kila mmoja akiwa na kazi yake maalumu. Kisha atamwamuru mlinzi mlangoni awe macho. 35 Vivyo hivyo ni lazima mjihadhari, kwa sababu hamjui ni muda gani mkuu wa nyumba atakuja; hamjui kama atakuja jioni, usiku wa manane, wakati jogoo anawika, au alfajiri. 36 Ikiwa atakuja ghafula, basi asiwakute mmelala. 37 Ninachowaambia, namwambia kila mmoja: ‘muwe tayari.’”

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International