Beginning
Simulizi Kuhusu Mkulima Aliyepanda Mbegu
(Mt 13:1-9; Lk 8:4-8)
4 Kwa mara nyingine Yesu akaanza kufundisha kando ya ziwa. Umati wa watu ukakusanyika kumzunguka, naye akapanda ndani ya mtumbwi ili akae na kufundisha huku mtumbwi ukielea. 2 Yesu akawafundisha mambo mengi kwa simulizi zenye mafumbo. Katika mafundisho yake alisema:
3 “Sikilizeni! Mkulima mmoja alitoka kwenda kupanda mbegu. 4 Alipokuwa akitupa na kuzisambaza mbegu hizo nyingine ikaanguka katika njia, na ndege wakaja na kuila. 5 Mbegu nyingine ikaanguka juu ya uwanja wenye miamba, mahali ambapo hapakuwa na udongo wa kutosha. Hiyo mbegu ilichanua haraka kwani udongo ule haukuwa na kina cha kutosha. 6 Lakini jua lilipochomoza, ule mmea uliungua na kwa sababu haukuwa na mizizi ya kutosha ulinyauka. 7 Mbegu nyingine ilianguka kwenye magugu yenye miiba, na miiba ile ilikua na hatimaye kuibana sana na hivyo haikuzaa chochote. 8 Mbegu nyingine ilianguka kwenye udongo mzuri, nayo ikaota, ikakua na kuzaa matunda; ikazaa mara thelathini, sitini na hata mia zaidi.”
9 Kisha akasema, “Kila mwenye masikio mazuri ayasikie haya.”
Kwa nini Yesu Alitumia Simulizi Kufundisha
(Mt 13:10-17; Lk 8:9-10)
10 Yesu alipokuwa peke yake, wale waliomzunguka na wale kumi na wawili walimuuliza kuhusu mifano hiyo.
11 Akawaambia, “Ni ninyi tu mliojaliwa kuzifahamu siri juu ya Ufalme wa Mungu. Lakini kwa wale walio nje nanyi mambo yote yatasemwa kwa simulizi zenye mafumbo, 12 Ili kwamba,
‘japo watatazama
sana hawataona,
na kwamba japo watasikia
sana hawataelewa;
vinginevyo,
wangegeuka na kusamehewa!’”(A)
Yesu Afafanua Simulizi Kuhusu Mbegu
(Mt 13:18-23; Lk 8:11-15)
13 Akawaambia, “Hamuelewi mfano huu? Sasa je mtaelewaje mfano wowote nitakaowapa? 14 Mkulima ni badala ya yule anayepanda lile neno la Mungu. 15 Watu wengine ni kama ile mbegu zilizoanguka juu ya njia pale ambapo neno la Mungu limepandwa. Baada ya kulisikia lile neno la Mungu, ndipo Shetani huja haraka na kuyaondoa yale mafundisho ya Mungu yaliyopandwa ndani yao.
16 Watu wengine ni kama mbegu iliyopandwa kwenye eneo lenye mawe mengi. Wanapolisikia neno wanalipokea haraka kwa furaha. 17 Lakini wao wenyewe wanakuwa bado hawajaliruhusu lizame zaidi katika maisha yao. Shida au mateso yanapotokea kwa sababu ya lile neno, kwa haraka sana wanaiacha imani.
18 Watu wengine ni kama mbegu iliyopandwa katika miiba. Hawa ndio wale wanaolisikia neno, 19 lakini mahangaiko ya maisha haya ya sasa, kuvutiwa na mali, na tamaa mbalimbali zingine huja na kulibana sana lile neno, nalo haliwezi kuwa na matokeo mazuri.[a]
20 Wengine ni kama mbegu iliyopandwa katika udongo mzuri. Hawa ni wale wanaolisikia neno, na kulipokea na hivyo kuwa na matokeo mazuri; wengine kutoa thelathini, wengine sitini na wengine mia moja zaidi.”
Zingatieni Nuru
(Lk 8:16-18)
21 Yesu akawaambia, “Unapoileta taa ndani[b] je unaiweka chini ya bakuli ama uvungu wa kitanda? Au unaileta ndani na kuiweka juu ya kitako cha taa? 22 Kwani kila kilichofichika kitafunuliwa, na kila kilicho cha siri kitatokea kweupe kwenye mwanga. 23 Yeyote mwenye masikio mazuri ni bora asikie.” 24 Kisha akawaambia, “Zingatieni kwa makini kile mnachokisikia. Kwani jinsi mnavyosikiliza kwa makini, ndivyo mtakavyoelewa na kuzidi kuelewa. 25 Kwa kuwa kila aliye na uelewa kidogo ataongezewa zaidi. Lakini wale wasiosikiliza kwa makini watapoteza hata ule uelewa mdogo walio nao.”[c]
Yesu Atumia Simulizi Kuhusu Mbegu Inayokua
26 Yesu akasema, “Hivi ndivyo Ufalme wa Mungu unavyofanana: Mtu mmoja alitoka kwenda kupanda mbegu zake katika udongo shambani. 27 Usiku alienda kulala na asubuhi aliamka na zile mbegu zikiota na kukua; na hakujua jinsi gani hiyo ilifanyika. 28 Ardhi yenyewe inatoa nafaka; kwanza hutoka shina, kisha kinafuata kichwa na mwishoni hutokea nafaka kamili katika kichwa. 29 Nafaka ile inapokuwa imekomaa, basi mkulima huikata kwa fyekeo kwani wakati wa mavuno umekwishafika.”
Simulizi Nyingine ya Ufalme
(Mt 13:31-32,34-35; Lk 13:18-19)
30 Yesu akasema, “Niufanananishe na kitu gani ufalme wa mbinguni? Au tutumie mfano gani kuuelezea? 31 Ni kama mbegu ya haradali, ambayo ni mbegu ndogo sana kuliko zote inapopandwa ardhini. 32 Lakini inapokuwa imepandwa, inakua na kuwa kubwa sana kuliko mimea yote ya bustanini, na pia hubeba matawi makubwa, kiasi kwamba ndege wa angani wanaweza kupumzika katika kivuli chake.”
33 Kwa mifano mingi kama hii aliendelea kuwafundisha kila kitu kwa kuzingatia uwezo wao wa kuelewa. 34 Yesu hakusema kitu kwao bila kutumia mfano. Lakini alipokuwa peke yake pamoja na wanafunzi wake, alifafanua kila kitu kwao.
Yesu Atuliza Dhoruba
(Mt 8:23-27; Lk 8:22-25)
35 Siku ile ilipofika jioni aliwaambia, “Hebu tuvuke kwenda ng'ambo ya pili ya ziwa.” 36 Kwa hiyo wakaliacha lile kundi. Wakamchukua pamoja nao alipokuwa amerudi katika mtumbwi. Wakati ule ule palikuwepo na mitumbwi mingi mingine ziwani. 37 Dhoruba kubwa ikatokea na mawimbi yalikuwa yanakuja katika pembe zote za mtumbwi. Mtumbwi nao ulikaribia kujaa maji kabisa 38 lakini Yesu alikuwa amelala nyuma ya mtumbwi akiegemea mto. Wakamwaamsha na kumwambia, “Mwalimu je wewe hujali kwamba tunazama?”
39 Kisha akainuka, akaukemea upepo, na akaliamuru ziwa, “Nyamaza Kimya! Tulia!” Upepo ule ukatulia na ziwa nalo likatulia kabisa.
40 Kisha akawaambia, “Kwa nini mnaogopa? Je! Bado hamna imani yoyote?”
41 Lakini walikuwa na woga sana, na wakasemezana wao kwa wao, “Ni nani basi huyu ambaye hata upepo na ziwa vinamtii?”
Yesu Amweka Huru Mtu Kutoka Pepo Wachafu
(Mt 8:28-34; Lk 8:26-39)
5 Wakafika ng'ambo ya ziwa, katika nchi walimoishi Wagerasi.[d] 2 Yesu alipotoka katika mashua ile ghafla, mtu mmoja aliyekuwa na roho chafu alitoka makaburini kuja kumlaki. 3 Mtu huyu aliishi makaburini, na hakuna mtu yeyote aliyeweza kumfunga hata kwa mnyororo, 4 Watu walijaribu kila mara kumfunga kwa minyororo na vyuma kwenye miguu na mikono. Hata hivyo, aliweza kuivunja minyororo ile na pingu zile za vyuma wala hakuna aliyekuwa na nguvu za kutosha kumdhibiti. 5 Kila mara usiku na mchana akiwa makaburini na kwenye milima alipiga kelele na kujikata kwa mawe.
6 Alipomwona Yesu kutoka mbali, alimkimbilia, na kusujudu mbele yake. 7 Kisha akalia kwa sauti kubwa na kusema, “Unataka nini kwangu, Yesu Mwana wa Mungu Aliye Mkuu zaidi? Nakuomba uape mbele za Mungu kwamba hutanitesa.” 8 Yule pepo alisema haya kwa sababu Yesu alikuwa anamwambia, “Mtoke huyo mtu, ewe pepo mchafu!”
9 Ndipo Yesu akamwuliza yule mtu, “Jina lako nani?”
Naye akamjibu, “Jina langu ni Jeshi,[e] kwa sababu tuko wengi.” 10 Yule pepo akamwomba Yesu tena na tena asiwaamuru kutoka katika eneo lile.
11 Kulikuwepo kundi kubwa la nguruwe likila katika kilima. 12 Wale pepo wakamwomba Yesu awatume waende katika lile kundi la nguruwe na kuliingia, 13 Naye akawaruhusu. Kwa hiyo pepo wachafu walimtoka mtu yule na kuwaingia nguruwe.[f] Kundi lile lilikuwa na idadi karibu ya elfu mbili, lilikimbia kuelekea kwenye kingo zenye mtelemko mkali na kutumbukia ziwani, ambamo walizama.
14 Wale waliowachunga walikimbia. Wakatoa taarifa mjini na katika maeneo jirani ya mashambani. Watu wakaja kuona ni kitu gani kilichotokea. 15 Watu hao wakamwendea Yesu. Nao wakamwona yule aliyekuwa na mashetani ameketi mahali pale, amevaa nguo na akiwa mwenye akili zake nzuri; huyu ni yule aliyekuwa amepagawa na jeshi la mashetani. Wakaogopa. 16 Wale waliokuwa wameona hili waliwasimulia kile kilichomtokea mtu yule aliyekuwa amepagawa na mashetani na kuhusu nguruwe wale. 17 Nao wakamwomba Yesu aondoke katika eneo lile.
18 Wakati Yesu akipanda katika mtumbwi, mtu yule aliyekuwa amepagawa na mashetani alimwomba Yesu afuatane naye. 19 Lakini Yesu hakumruhusu aende naye, isipokuwa alimwambia, “Nenda kwa watu wa kwenu, na uwaambie yote ambayo Bwana amekufanyia, na uwaambie jinsi alivyokuwa na huruma kwako.”
20 Hivyo mtu yule aliondoka, na akaanza kuwaeleza watu katika Dekapoli[g] mambo mengi ambayo Yesu amemtendea, na watu wote walistaajabu.
Yesu Anampa Uhai Msichana Aliyekufa na Kumponya Mwanamke Mgonjwa
(Mt 9:18-26; Lk 8:40-56)
21 Kisha, Yesu alivuka kurudi upande wa magharibi wa ziwa. Pale kundi kubwa la watu lilikusanyika kwake. Yeye alikuwa kando ya ziwa, na 22 mmoja wa viongozi wa sinagogi, aliyeitwa Yairo, alifika pale. Naye alipomwona Yesu, alipiga magoti miguuni pake. 23 Kisha akamwomba kwa msisitizo, akisema, “Binti yangu mdogo yu karibu kufa. Ninakuomba ufike na kumwekea mikono, ili kwamba apone na kuishi.”
24 Hivyo Yesu alienda pamoja naye. Na kundi kubwa la watu lilimfuata; nao walikuwa wakimsonga pande zote kumzunguka.
25 Alikuwepo mwanamke mmoja aliyekuwa akitoka damu (kama ilivyo desturi ya wanawake kila mwezi) kila siku kwa miaka kumi na miwili. 26 Huyu alikuwa ameteseka sana akiwa chini ya uangalizi wa madaktari wengi. Yeye alikuwa ametumia vyote alivyokuwa navyo. Hata hivyo hali yake iliendelea kuwa mbaya zaidi.
27 Wakati aliposikia juu ya Yesu, alimwendea kwa nyuma akiwa katika kundi lile na kuligusa joho lake. 28 Kwani alikuwa akijisemea mwenyewe, “Ikiwa nitagusa tu vazi lake, nitapona.” 29 Mara moja chanzo cha kutoka kwake damu kikakauka, na akajisikia mwilini mwake kwamba amepona matatizo yake. 30 Naye Yesu akatambua mara moja kwamba nguvu zilimtoka. Aligeuka nyuma na kuuliza “Nani aliyegusa mavazi yangu?”
31 Wanafunzi wake wakamwambia, “Uliliona kundi likisukumana kukuzunguka, nawe unauliza, Nani aliyenigusa?”
32 Lakini Yesu aliendelea kuangalia kumzunguka kuona ni nani aliyeyafanya haya. 33 Yule Mwanamke akiwa anatetemeka kwa hofu akijua nini kilichotokea kwake, alikuja na kuanguka mbele yake, akamweleza ukweli wote. 34 Kisha Yesu akamwambia, “Binti yangu imani yako imekuponya. Nenda kwa amani, na uendelee kupona matatizo yako.”
35 Wakati alipokuwa akizungumza haya watumishi walikuja kutoka nyumbani kwa afisa wa sinagogi. Nao wakamwambia yule afisa, “Binti yako amefariki kwa nini uendelee kumsumbua huyo mwalimu?”
36 Lakini Yesu aliyasikia yale waliyokuwa wakisema, na akamwaambia yule afisa wa sinagogi, “Usiogope. Amini tu.”
37 Naye hakumruhusu mtu yeyote kumfuata isipokuwa Petro, Yakobo na Yohana ndugu yake Yakobo, 38 nao wakaenda katika nyumba ya yule afisa wa sinagogi, na Yesu akaona vurugu na watu wakilia kwa sauti. 39 Yesu aliingia ndani na kuwaambia, “Za nini vurugu zote hizi na vilio hivi? Mtoto hajafa; amelala tu.” 40 Nao wakamcheka.
Yeye aliwatoa nje watu wote, akamchukua baba na mama wa mtoto na wale waliokuwa pamoja naye, akaenda hadi pale alipokuwepo mtoto, 41 akaushika mkono wa mtoto yule na kumwambia “Talitha koum!” (maana yake, “Msichana mdogo, ninakuambia amka usimame!”) 42 Yule msichana aliinuka mara moja na kuanza kutembea mahali pale. Naye alikuwa na miaka kumi na miwili. Nao mara moja wakaelemewa na mshangao mkubwa. 43 Yeye akawapa amri kuwa mtu yeyote asijue juu ya jambo hili. Kisha akawaambia wampatie msichana yule chakula ale.
© 2017 Bible League International