Book of Common Prayer
Watu Saba Wachaguliwa kwa Kazi Maalumu
6 Watu wengi zaidi walipokuwa wafuasi wa Yesu. Wafuasi waliokuwa wakizungumza Kiyunani walianza kuwalalamikia wafuasi wenzao waliokuwa wanazungumza Kiebrania au Kiaramu. Walisema kuwa wajane wao walikuwa hawapewi mgao wao kutokana na kile wafuasi walikuwa wanapewa kila siku. 2 Mitume kumi na mbili wakaita kundi lote la wafuasi pamoja.
Mitume wakawaambia, “Haitakuwa sahihi sisi kuacha kazi yetu ya kuwafundisha watu neno la Mungu ili tuwe wasimamizi wa ugawaji wa chakula kwa watu. 3 Hivyo, kaka zetu na dada zetu, chagueni wanaume saba miongoni mwenu wenye ushuhuda mzuri, watu waliojaa hekima na Roho. Nasi tutawaweka kuwa wasimamizi wa kazi hii muhimu. 4 Na hivyo itatuwezesha sisi kutumia muda wetu wote katika kuomba na kufundisha neno la Mungu.”
5 Kundi lote la waamini likakubaliana na wazo hili. Hivyo wakawachagua wanaume saba: Stefano (aliyejaa imani na Roho Mtakatifu), Filipo,[a] Prokoro, Nikanori, Timoni, Parmena, na Nikolasi (mtu wa Antiokia aliyeongoka na kufuata dini ya Kiyahudi). 6 Kisha, wakawaweka watu hawa mbele ya mitume, nao mitume waliwaombea na kuweka mikono juu yao.
7 Neno la Mungu lilikuwa linawafikia watu wengi zaidi. Kundi la wafuasi katika Yerusalemu likawa kubwa sana. Hata idadi kubwa ya makuhani wa Kiyahudi waliamini na kutii.
59 Walipokuwa wanampiga kwa mawe, Stefano aliomba, akisema, “Bwana Yesu, pokea roho yangu.” 60 Alianguka kwa magoti yake na kupaza sauti, akasema, “Bwana usiwahesabie dhambi hii!” Haya yalikuwa maneno yake ya mwisho kabla ya kufa.
8 1-3 Sauli aliridhia kuwa kuuawa kwa Stefano lilikuwa jambo jema. Baadhi ya wacha Mungu walimzika Stefano, wakaomboleza na kumlilia kwa sauti kuu.
Matatizo Kwa waamini
Kuanzia siku hiyo Wayahudi walianza kulitesa sana kanisa na waamini katika mji wa Yerusalemu. Sauli pia alijaribu kuliharibu kanisa. Aliingia katika nyumba za waamini, akawaburuta wanaume na wanawake, na kuwafunga gerezani. Waamini wote walikimbia kutoka Yerusalemu, mitume peke yao ndiyo walibaki. Waamini walikwenda mahali tofauti tofauti katika Uyahudi na Samaria. 4 Walitawanyika kila mahali, na kila walikokwenda waliwahubiri watu Habari Njema.
Filipo Ahubiri Katika Samaria
5 Filipo[a] alikwenda katika mji mkuu wa jimbo la Samaria na kuwahubiri watu kuhusu Masihi. 6 Watu wa Samaria walimsikiliza Filipo na kuona miujiza aliyotenda. Wote walisikiliza kwa makini yale aliyosema. 7 Watu wengi miongoni mwao walikuwa na mapepo, lakini Filipo aliyakemea mapepo na yaliwatoka watu. Mapepo yalipiga kelele nyingi yalipokuwa yanawatoka watu. Walikuwepo pia watu wengi waliopooza na walemavu wa miguu pale. Filipo aliwaombea na wote walipona. 8 Kulikuwa furaha kubwa katika mji ule wa Samaria siku ile!
© 2017 Bible League International