Book of Common Prayer
Barua ya Yesu kwa Kanisa la Laodikia
14 Andika hivi kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia:
Huu ni ujumbe kutoka kwa yeye aliye Amina,[a] shahidi mwaminifu na wa kweli, aliye chanzo cha uumbaji wa Mungu.
15 Ninayajua matendo yako. Wewe si moto wala baridi. Ninatamani kama ungekuwa moto au baridi! 16 Lakini wewe ni vuguvugu tu, si moto, wala baridi. Hivyo niko tayari kukutema utoke mdomoni mwangu. 17 Unasema wewe ni tajiri. Unadhani ya kuwa umekuwa tajiri na huhitaji kitu chochote. Lakini hujui kuwa wewe ni mnyonge, mwenye masikitiko, maskini, asiyeona na uko uchi. 18 Ninakushauri ununue dhahabu kutoka kwangu, dhahabu iliyosafishwa katika moto. Kisha utakuwa tajiri. Nakuambia hili: Nunua kwangu mavazi meupe. Ndipo utaweza kuifunika aibu ya uchi wako. Ninakuagiza pia ununue kwangu dawa ya kuweka kwenye macho yako, nawe utaweza kuona.
19 Mimi huwasahihisha na kuwaadhibu wale niwapendao. Hivyo onesha kuwa kuishi kwa haki ni muhimu kwako kuliko kitu kingine. Geuzeni mioyo na maisha yenu. 20 Niko hapa! Nimesimama mlangoni nabisha hodi. Ikiwa utaisikia sauti yangu na ukaufungua mlango, nitaingia kwako na kula pamoja nawe. Nawe utakula pamoja nami.
21 Nitamruhusu kila atakayeshinda kuketi pamoja nami kwenye kiti changu cha enzi. Ilikuwa vivyo hivyo hata kwangu. Nilishinda na kuketi pamoja na Baba yangu kwenye kiti chake cha enzi. 22 Kila anayesikia hili azingatie kile ambacho Roho anayaambia makanisa.”
32 Jifunze kwa mtini: Matawi yake yanapokuwa ya kijani na laini na kuanza kutoa majani mapya, ndipo mnatambua kuwa majira ya joto yamekaribia. 33 Katika namna hiyo hiyo, mtakapoona mambo haya yote yakitokea, mtajua kuwa wakati[a] umekaribia wa kile kitakachotokea. 34 Ninawahakikishia kuwa mambo haya yote yatatokea wakati ambao baadhi ya watu wa nyakati hizi wakiwa bado hai. 35 Ulimwengu wote, dunia na anga vitaangamizwa, lakini maneno yangu yatadumu milele.
Mungu Peke Yake Ndiye Ajuaye Siku ya Kurudi kwa Mwana wa Adamu
(Mk 13:32,35; Lk 17:26-30,34-36)
36 Hakuna anayeijua siku wala wakati. Malaika wa mbinguni hawaijui hata Mwana hajui itakuwa lini. Baba peke yake ndiye anayejua.
37 Mwana wa Adamu atakapokuja, itakuwa kama ilivyokuwa nyakati za Nuhu. 38 Siku zile kabla ya gharika, watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuwatoa binti zao kuolewa mpaka siku ambayo Nuhu aliingia kwenye safina. 39 Hawakujua juu ya kilichokuwa kinaendelea mpaka mafuriko yalipowajia na kuwaangamiza wote.
Ndiyo itakavyokuwa Mwana wa Adamu atakapokuja. 40 Wanaume wawili watakuwa wakifanya kazi shambani, mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa. 41 Wanawake wawili watakuwa wanasaga nafaka pamoja, mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.
42 Hivyo iweni tayari daima. Hamjui siku ambayo Bwana wenu atarudi. 43 Mwenye nyumba angefanya nini ikiwa angejua wakati ambao mwizi atakuja? Mnajua angelikesha ili mwizi asivunje na kuingia. 44 Hivyo, ninyi nanyi iweni tayari. Mwana wa Adamu atakuja katika wakati msiomtarajia.
© 2017 Bible League International