Book of Common Prayer
Kuhusu Vyakula Vinavyotolewa kwa Sanamu
8 Sasa nitaandika kuhusu suala jingine mliloniandikia mkiuliza kuhusu nyama iliyotolewa sadaka[a] kwa sanamu. Ni kweli kuwa “Sote tuna ujuzi”, kama mnavyosema. Lakini ujuzi huu unawajaza watu majivuno. Upendo ndiyo unaolisaidia kanisa kuwa imara. 2 Wale wanaodhani kuwa wanajua jambo fulani bado hawajui chochote kwa namna inavyopaswa. 3 Lakini Mungu anamjua mtu anayempenda.
4 Hivyo sasa vipi kuhusu kula nyama iliyotolewa sadaka kwa sanamu? Tunajua kuwa “sanamu si lolote katika ulimwengu” huu na tunajua kuwa “kuna Mungu mmoja tu”. 5 Baadhi ya watu husema kuwa kuna miungu wanaoishi mbinguni na miungu wengine huishi duniani. Hata kama kuna “miungu” na “mabwana” wanaoaminiwa na watu, hilo si muhimu kwetu. 6 Tuna Mungu mmoja tu, na ambaye ndiye Baba yetu. Vitu vyote vilitoka kwake nasi tunaishi kwa ajili yake. Na kuna Bwana mmoja tu, Yesu Kristo. Vitu vyote viliumbwa kupitia yeye, nasi tunaishi kwa ajili yake.
7 Lakini si watu wote wanaojua hili. Baadhi ya watu walikuwa na tabia ya kuabudu sanamu huko nyuma. Hivyo wanapokula nyama, bado wanahisi kuhukumiwa kana kwamba wanakula nyama iliyotolewa kwa sanamu. Hawana uhakika ikiwa ni sahihi kula nyama. 8 Lakini chakula hakitatuweka karibu na Mungu. Kukataa kula hakutufanyi tumpendeze kidogo Mungu wala kula hakutuweki karibu na Mungu.
9 Lakini iweni makini na uhuru wenu. Uhuru wa kula kitu unaweza kuwafanya walio na mashaka wakaanguka katika dhambi kwa kula vyakula hivyo. 10 Mnaelewa kuwa inaruhusiwa kula kitu chochote, hivyo unaweza kula hata katika hekalu la sanamu. Lakini hilo linaweza kumfanya mtu mwenye mashaka akaona kuwa kula chakula kama hicho ni kitendo cha kuabudu sanamu. 11 Hivyo ndugu huyu aliye dhaifu, ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake, anaweza akaangamizwa kwa sababu ya uelewa wako ulio mzuri zaidi. 12 Unapomtenda dhambi kinyume cha ndugu zako walio katika Kristo kwa namna hii na unawaumiza kwa kuwafanya wafanye mambo wanayoyachukulia kuwa mabaya, nawe pia unamtenda dhambi Kristo. 13 Hivyo ikiwa chakula ninachokula kinamfanya mwamini mwingine kutenda dhambi, siwezi kula chakula hicho tena. Nitaacha kula chakula hicho ili nisimfanye ndugu yangu atende dhambi.
Wachache tu Ndiyo Huiona Njia ya Uzima
(Lk 13:24)
13 Unapaswa kuingia katika uzima wa kweli kupitia lango lililo jembamba. Kwa kuwa lango ni pana na njia inayoelekea katika uharibifu nayo ni pana na watu wengi wanaifuata njia hiyo. 14 Lakini lango la kuelekea katika uzima wa kweli ni jembamba. Na njia iendayo huko ni ngumu kuifuata. Na ni watu wachache wanaoiona.
Kile Wanachokifanya watu Kinadhihirisha jinsi gani Walivyo
(Lk 6:43-44; 13:25-27)
15 Mjihadhari na manabii wa uongo wanaokuja kwenu wakijifanya kondoo wasio na madhara ingawa ni watu hatari kama mbwa mwitu. 16 Mtawatambua watu hawa kwa matendo yao. Mambo mazuri hayatoki kwa watu wabaya, kama ambavyo zabibu haitokani na miiba, na tini hazitokani na mbigiri. 17 Vile vile, kila mti mzuri huzaa matunda mazuri na mti mbaya huzaa matunda mabaya. 18 Mti mzuri hauwezi kuzaa matunda mabaya, na wala mti mbaya hauwezi kuzaa matunda mazuri. 19 Kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa kwenye moto. 20 Mtawatambua manabii hawa wa uongo kwa matendo yao.
21 Si kila aniitaye Bwana ataingia katika ufalme wa Mungu. Watakaoingia ni wale tu wafanyao yale ambayo Baba yangu wa mbinguni anataka.
© 2017 Bible League International