Book of Common Prayer
28 Watu hawa waliona kuwa haikuwa muhimu kwao kumkubali Mungu katika fikra zao. Hivyo Mungu akawaacha wayafuate mawazo yao mabaya. Hivyo hufanya mambo ambayo mtu yeyote hapaswi kufanya. 29 Maisha yao yamejaa kila aina ya matendo mabaya, uovu, tamaa na chuki. Wamejaa wivu, uuaji, ugomvi, uongo na hamu ya kuwadhuru wengine. Wanasengenya 30 na kusemana maovu wao wenyewe. Wanamchukia Mungu. Ni wakorofi, wana kiburi na hujivuna. Hubuni njia za kufanya maovu. Hawawatii wazazi wao. 31 Ni wapumbavu, hawatimizi ahadi zao. Hawawaoneshi wema wala huruma wengine. 32 Wanajua amri ya Mungu kuwa yeyote anayeishi kwa namna hiyo lazima afe. Lakini si tu kwamba wanaendelea kufanya mambo haya wenyewe, bali wanakubaliana na wengine wanaofanya mambo hayo.
Huwezi Kuwahukumu Wengine
2 Je, unadhani unaweza kuwahukumu watu wengine? Unakosea. Wewe pia una hatia ya dhambi. Unawahukumu kwa kuwa wanatenda mabaya, lakini wewe unatenda yale wanayotenda. Hivyo unapowahukumu, unajihukumu wewe mwenyewe. 2 Lakini tunajua kwamba Mungu yuko sahihi kwa kuwahukumu wote wanaotenda mambo ya jinsi hiyo! 3 Lakini kwa kuwa unatenda mambo sawa na wale unaowahukumu, hakika unaelewa kuwa Mungu atakuadhibu nawe pia. Unawezaje kufikiri kuwa utaiepuka hukumu yake? 4 Mungu amekuwa mwema kwako. Na amekuwa mvumilivu sana, akisubiri ubadilike. Lakini haufikirii jambo lolote kuhusu wema wake mkuu. Pengine huelewi kwamba Mungu ni mwema kwako ili ubadili moyo na maisha yako.
5 Lakini wewe ni mkaidi sana! Unakataa kubadilika. Hivyo unaikuza hukumu yako wewe mwenyewe zaidi na zaidi. Utahukumiwa siku ile ambapo Mungu ataonesha hasira yake. Siku ambayo kila mtu ataona Mungu anavyowahukumu watu kwa haki.[a] 6 Kama anavyosema, “Atamlipa au kumwadhibu kila mtu kutokana na matendo yale.”(A) 7 Watu wengine hawachoki kutenda mema. Wanaishi kwa ajili ya utukufu na heshima kutoka kwa Mungu na kwa ajili ya maisha yasiyoweza kuharibiwa. Mungu atawapa watu hao uzima wa milele. 8 Lakini wengine hutenda mambo yanayowafurahisha wao wenyewe. Hivyo hukataa yaliyo haki na huchagua kutenda mabaya. Watateseka kwa hukumu ya Mungu yenye hasira. 9 Matatizo na mateso yatampata kila mmoja anayetenda uovu; kuanzia Wayahudi kwanza kisha wale wasio Wayahudi. 10 Lakini atampa utukufu, heshima na amani kila atendaye mema; wale wote wanaotenda mema; kuanzia Wayahudi kwanza kisha wale wasio Wayahudi. 11 Ndiyo, Mungu humhukumu kila mtu pasipo upendeleo, bila kujali yeye ni nani.
Nani ni Mkuu Zaidi?
(Mk 9:33-37; Lk 9:46-48)
18 Wakati huo huo wanafunzi wake wakamjia Yesu na kuuliza, “Nani ni mkuu zaidi katika ufalme wa Mungu?”
2 Yesu akamwita mtoto mdogo, akamsimamisha mbele yao. 3 Kisha akasema, “Ukweli ni huu, ni lazima mbadilike katika namna mnavyofikiri na muwe kama mtoto mdogo. Msipofanya hivi hamtaingia katika ufalme wa Mungu. 4 Aliye mkuu zaidi katika ufalme wa Mungu ni yule anayejinyenyekeza kama mtoto huyu.
5 Unapomkubali mtoto mdogo kama huyu kama aliye wangu, unanikubali mimi.
Yesu Aonya Kuhusu Chanzo cha Dhambi
(Mk 9:42-48; Lk 17:1-2)
6 Ikiwa mmoja wa watoto hawa wadogo ananiamini, na mtu yeyote akasababisha mtoto huyo kutenda dhambi, ole wake mtu huyo. Ingekuwa bora mtu huyo kufungiwa jiwe la kusagia shingoni mwake na kuzamishwa katika kina kirefu baharini. 7 Nawasikitikia watu wa ulimwengu kwa sababu ya mambo yanayofanya watu watende dhambi. Mambo haya lazima yatokee, lakini ole wake mtu yeyote anayeyafanya yatokee.
8 Mkono au mguu wako ukikufanya utende dhambi, ukate na uutupe. Ni bora ukapoteza kiungo kimoja cha mwili wako na ukaupata uzima wa milele kuliko kuwa na mikono au miguu miwili na ukatupwa katika moto wa milele. 9 Jicho lako likikufanya utende dhambi, ling'oe na ulitupe. Ni bora kwako kuwa na jicho moja tu na ukaupata uzima wa milele kuliko kuwa na macho mawili na ukatupwa katika moto wa Jehanamu.
© 2017 Bible League International