Book of Common Prayer
Baraka za Mungu Huja Kwa Imani
3 Ninyi watu wa Galatia, je mmepoteza fahamu zenu? Nilidhani mmeelewa kwa nini Yesu Kristo alisulubiwa msalabani! Niliwaeleza wazi kabisa jambo hilo, kama vile kuchora na kupaka rangi picha mbele ya macho yenu. Je, kuna mtu yeyote aliyewaloga mkasahau? 2 Niambieni jambo hili moja: Ni jinsi gani mlimpokea Roho? Je, mlimpokea Roho kwa kufuata sheria? Hapana, mlimpokea Roho kwa sababu ya ujumbe kuhusu Yesu unaoleta imani. 3 Mliyaanza maisha yenu mapya pamoja na Roho. Inakuwaje sasa mdhani kuwa mnaweza kukamilishwa na kitu kinyonge kama tohara kilichofanyika katika miili yenu?[a] Basi mmepoteza fahamu zenu! 4 Je, mlipata uzoefu huo mwingi pasipo manufaa yoyote? Sidhani kama hivyo ndivyo! 5 Je, Mungu anawapa ninyi Roho na kutenda miujiza miongoni mwenu kwa kuwa mnaifuata sheria? Hapana sivyo! Mungu anawapa ninyi baraka hizi kwa njia ya ujumbe unaoleta imani katika kumwamini Yesu.
6 Maandiko yanasema kitu hicho hicho kuhusu Ibrahimu. “Ibrahimu alimwamini Mungu, na Mungu akaikubali imani yake na akamhesabia haki.”(A) 7 Hivyo mnapaswa kuelewa kuwa watoto sahihi wa Ibrahimu ni wale walio na imani. 8 Maandiko yalieleza ambacho kingetokea katika siku zijazo. Maandiko haya yalisema kwamba Mungu angewafanya wasio Wayahudi kuwa wenye haki kwa njia ya imani. Mungu alizisema Habari Njema hizi kwa Ibrahimu kabla haijatokea. Mungu alimwambia Ibrahimu, “Kwa kukubariki wewe, nitawabariki watu wote duniani.”(B) 9 Kwa hiyo, wale wote wanaoweka imani yao kwa Mungu ndiyo wanaobarikiwa pamoja na Ibrahimu aliyekuwa mwaminifu.
10 Lakini watu wale wanaodhani kuwa kutii sheria ndicho kitu muhimu sana daima hukaa chini ya tishio la laana. Kama vile Maandiko yanavyosema, “Amelaaniwa mtu yeyote atakayeacha kuzishika na kuzitii sheria hizi zote.”(C) 11 Hivyo ni dhahiri kuwa hakuna anayeweza kuhesabiwa haki mbele za Mungu kwa kuifuata sheria. Maandiko yanasema, “Mwenye haki mbele za Mungu ataishi kwa imani.”(D)
12 Sheria haitegemei imani. Hapana, inasema kuwa njia pekee ambayo mtu anaweza kupata uzima kwa njia ya sheria ni kwa kutii amri zake.[b] 13 Sheria inasema kuwa sisi Wayahudi tuko chini ya laana kwa kutokuitii daima. Lakini Kristo alituweka huru kutoka katika laana hiyo. Alikubali kulaaniwa na sheria ili atuokoe. Maandiko yanasema, “Yeyote anayening'inizwa mtini[c] yuko chini ya laana.”(E) 14 Kwa sababu ya yale aliyoyafanya Kristo Yesu, baraka ambazo Mungu alimwahidi Ibrahimu zilitolewa pia kwa wasio Wayahudi. Kristo alikufa ili kwamba kwa kumwamini sisi sote, Wayahudi na wasio Wayahudi, tuweze kumpokea Roho ambaye Mungu aliahidi.
Yesu Awalisha Watu Zaidi ya 5,000
(Mk 6:30-44; Lk 9:10-17; Yh 6:1-14)
13 Yesu aliposikia kilichotokea kwa Yohana, aliondoka kwa kutumia mtumbwi. Alikwenda peke yake mpaka mahali ambapo hakuna aliyekuwa akiishi. Lakini watu walisikia kuwa Yesu alikuwa ameondoka. Hivyo waliondoka katika miji na kumfuata. Walikwenda mahali alikokwenda kupitia nchi kavu. 14 Yesu alipotoka katika mtumbwi, aliwaona watu wengi. Akawahurumia, na kuwaponya waliokuwa wagonjwa.
15 Baadaye mchana huo, wafuasi walimwendea Yesu na kusema, “Hakuna anayeishi katika eneo hili. Na tayari muda umepita, hivyo waage watu ili waende katika miji na kujinunulia chakula.”
16 Yesu akasema, “Watu hawahitaji kuondoka. Wapeni ninyi chakula wale.”
17 Wafuasi wakajibu, “Lakini tuna mikate mitano na samaki wawili tu.”
18 Yesu akasema, “Leteni kwangu mikate na samaki.” 19 Kisha akawaambia watu waketi chini kwenye nyasi. Akaichukua mikate mitano na samaki wawili. Akatazama mbinguni na akamshukuru Mungu kwa ajili ya chakula. Kisha akaivunja mikate katika vipande, akawapa wafuasi wake nao wakawapa watu chakula. 20 Kila mmoja alikula mpaka akashiba. Walipomaliza kula, wafuasi walijaza vikapu kumi na mbili vya vipande vilivyosalia. 21 Walikuwepo wanaume 5,000, pamoja na wanawake na watoto waliokula.
© 2017 Bible League International