Book of Common Prayer
Mwanamke Juu ya Mnyama Mwekundu
17 Mmoja wa malaika saba waliokuwa na bakuli sa akaja kuzungumza nami. Akasema, “Njoo, nami nitakuonesha adhabu itakayotolewa kwa kahaba maarufu. Ndiye yule aketiye juu ya maji mengi. 2 Watawala wa dunia walizini pamoja naye. Watu wa dunia walilewa kutokana na mvinyo wa dhambi yake ya uzinzi.”
3 Kisha malaika akanichukua mbali kwa Roho Mtakatifu mpaka jangwani. Huko nikamwona mwanamke amekaa juu ya mnyama mwekundu. Mnyama alikuwa ameandikwa majina ya kumkufuru Mungu katika mwili wake wote. Alikuwa na vichwa saba na pembe kumi. 4 Mwanamke aliyekuwa juu yake alikuwa amevaa nguo za zambarau na nyekundu. Alikuwa anang'aa kutokana na dhahabu, vito na lulu alizokuwa amevaa. Mkononi mwake alikuwa ameshika kikombe cha dhahabu. Kikombe hiki kilijaa maovu na machukizo ya dhambi yake ya uzinzi. 5 Alikuwa na jina kwenye kipaji cha uso wake. Jina hili lina maana iliyofichwa. Hiki ndicho kilichoandikwa:
babeli mkuu
mama wa makahaba
na machukizo ya dunia.
6 Nikatambua kuwa mwanamke alikuwa amelewa. Alikuwa amelewa kwa damu ya watakatifu wa Mungu. Alikuwa amelewa kwa damu ya wale walioshuhudia imani yao katika Yesu Kristo.
Nilipomwona mwanamke, nilishangaa sana. 7 Kisha malaika akaniambia, “Kwa nini unashangaa? Nitakuambia maana iliyofichwa kuhusu mwanamke huyu na mnyama mwenye vichwa saba na pembe kumi anayeendeshwa na mwanamke huyu. 8 Mnyama unayemwona alikuwa hai kwanza, lakini sasa si hai. Hata hivyo, atapanda kutoka kuzimu na kwenda kuangamizwa. Watu wanaoishi duniani watashangaa watakapomwona mnyama, kwa sababu aliwahi kuwa hai, hayuko hai, lakini atakuwa hai tena. Hawa ni watu ambao majina yao hayajawahi kuandikwa katika kitabu cha uzima tangu mwanzo wa ulimwengu.
9 Unahitaji hekima kulielewa hili. Vichwa saba juu ya mnyama ni milima saba ambako mwanamke amekaa. Pia ni watawala saba. 10 Watawala watano wamekwisha kufa tayari. Mmoja wa watawala anaishi sasa, na mtawala wa mwisho anakuja. Atakapokuja, atakaa kwa muda mfupi tu. 11 Mnyama ambaye hapo kwanza alikuwa hai, lakini haishi tena ni mtawala wa nane. Naye ni mmoja wa watawala saba wa kwanza. Naye ataangamizwa.
12 Pembe kumi ulizoziona ni watawala kumi. Watawala hawa kumi hawajapata falme zao, lakini watapata nguvu ya kutawala pamoja na mnyama kwa saa moja. 13 Lengo la watawala hawa wote kumi linafanana. Nao watampa mnyama nguvu na mamlaka yao. 14 Watafanya vita kinyume na Mwanakondoo. Lakini Mwanakondoo atawashinda, kwa sababu ni Bwana wa mabwana na Mfalme wa wafalme. Pamoja naye watakuwepo wateule wake na wafuasi waaminifu, watu aliowaita kuwa wake.”
Yesu Atembea Juu ya Maji
(Mk 6:45-52; Yh 6:16-21)
22 Mara baada ya hili Yesu akawaambia wafuasi wake wapande kwenye mtumbwi. Akawaambia waende upande mwingine wa ziwa. Aliwaambia angekuja baadaye, alikaa pale ili kuwaaga watu. 23 Baada ya Yesu kuwaaga watu, alikwenda kwenye vilima peke yake kuomba. Ikawa jioni na alikuwa pale peke yake. 24 Wakati huu mtumbwi ilikuwa mbali kutoka pwani. Kwa kuwa upepo ulikuwa unavuma kinyume na mtumbwi, mtumbwi ulikuwa unapata msukosuko kwa sababu ya mawimbi.
25 Kati ya saa tisa na saa kumi na mbili asubuhi, wafuasi wa Yesu walikuwa bado ndani ya mtumbwi. Yesu akaenda kwao akitembea juu ya maji. 26 Iliwatisha walipomwona anatembea juu ya maji. Wakapiga kelele kwa woga “Ni mzuka!”
27 Lakini haraka Yesu akawaambia, “Msihofu! Ni mimi! Msiogope.”
28 Petro akasema, “Bwana, ikiwa hakika ni wewe, niambie nije kwako juu ya maji.”
29 Yesu akasema, “Njoo, Petro.”
Kisha Petro akauacha mtumbwi na kutembea juu ya maji kumwelekea Yesu. 30 Lakini Petro alipokuwa anatembea juu ya maji, aliyaona mawimbi na upepo. Aliogopa na kuanza kuzama katika maji. Akapiga kelele, “Bwana, niokoe!”
31 Haraka Yesu akamshika Petro kwa mkono wake. Akasema, “Imani yako ni ndogo. Kwa nini ulisita?”
32 Baada ya Petro na Yesu kuingia kwenye mtumbwi, upepo ukakoma. 33 Kisha wafuasi wakamwabudu Yesu na kusema, “Hakika wewe ni Mwana wa Mungu.”
Yesu Awaponya Watu Wengi Wagonjwa
(Mk 6:53-56)
34 Baada ya kuvuka ziwa, wakafika pwani katika eneo la Genesareti. 35 Baadhi ya watu pale wakamwona Yesu na wakamtambua kuwa ni nani. Hivyo wakatuma ujumbe kwa watu wengine katika eneo lote kuwa Yesu amekuja. Watu wakawaleta wagonjwa wao wote kwake. 36 Walimsihi Yesu awaruhusu waguse tu upindo wa vazi lake ili waponywe. Na wagonjwa wote waliogusa vazi lake waliponywa.
© 2017 Bible League International