Book of Common Prayer
Paulo na Sila Wakiwa Thesalonike
17 Paulo na Sila walisafiri kupitia miji ya Amfipoli na Apolonia. Wakafika katika mji wa Thesalonike, ambako kulikuwa sinagogi la Kiyahudi. 2 Paulo aliingia katika sinagogi kuwaona Wayahudi kama alivyokuwa akifanya. Wiki tatu zilizofuatia, kila siku ya Sabato alijadiliana nao kuhusu Maandiko. 3 Alifafanua Maandiko kuwaonesha kuwa Masihi ilikuwa afe na kufufuka kutoka kwa wafu. Aliwaambia, “Huyu Yesu ninayewaambia habari zake ndiye Masihi.” 4 Baadhi ya Wayahudi pale waliwaamini Paulo na Sila na waliamua kujiunga nao. Idadi kubwa ya Wayunani waliokuwa wanamwabudu Mungu wa kweli na wanawake wengi maarufu walijiunga nao pia.
5 Lakini Wayahudi ambao hawakuamini wakaingiwa na wivu, hivyo wakawakusanya baadhi ya watu wabaya katikati ya mji ili kufanya vurugu. Wakaunda kundi na wakanzisha vurugu mjini. Walikwenda nyumbani kwa Yasoni kuwatafuta Paulo na Sila. Walitaka kuwaleta mbele ya watu. 6 Walipowakosa wakamkamata na kumburuta Yasoni na baadhi ya waamini wengine na kuwapeleka kwa viongozi wa mji. Watu wakapasa sauti na kusema, “Watu hawa Wamesababisha matatizo mengi kila mahali ulimwenguni, na sasa wamekuja hapa pia! 7 Yasoni amewaweka nyumbani mwake. Wanavunja sheria za Kaisari. Wanasema kuna mfalme mwingine anayeitwa Yesu.”
8 Viongozi wa mji na watu wengine waliposikia hili waliudhika sana. 9 Wakawalazimisha Yasoni na waamini wengine kuweka dhamana ya fedha kuthibitisha kuwa hakutakuwa vurugu tena. Kisha wakawaruhusu kuondoka.
Paulo na Sila Waenda Berea
10 Usiku ule ule waamini wakawapeleka Paulo na Sila katika mji mwingine ulioitwa Berea. Walipofika pale, walikwenda katika sinagogi la Kiyahudi. 11 Watu wa Berea walikuwa radhi kujifunza kuliko watu wa Thesalonike. Walifurahi waliposikia ujumbe aliowaambia Paulo. Waliyachunguza Maandiko kila siku ili kuhakikisha kuwa waliyoyasikia ni ya kweli. 12 Matokeo yake ni kuwa watu wengi miongoni mwao waliamini, wakiwemo wanawake maarufu Wayunani na wanaume.
13 Lakini Wayahudi wa Thesalonike walipojua kuwa Paulo alikuwa anawahubiri Ujumbe wa Mungu katika mji wa Berea, walikwenda huko pia. Waliwakasirisha watu na kufanya vurugu. 14 Hivyo waamini walimpeleka Paulo sehemu za pwani, lakini Sila na Timotheo walibaki Berea. 15 Wale waliokwenda na Paulo walimpeleka katika mji wa Athene. Waliporudi Berea, waliwapa ujumbe kutoka kwa Paulo Timotheo na Sila kuwa waende kuungana naye haraka kadiri watakavyoweza.
Yesu Amsaidia Mwanamke Asiye Myahudi
(Mt 15:21-28)
24 Yesu akaondoka mahali pale na kuenda katika eneo lililozunguka Tiro. Aliingia katika nyumba na hakutaka mu yeyote ajue hilo, lakini hakuweza kufanya siri kuwepo kwake. 25 Mwanamke mmoja ambaye binti yake alikuwa na pepo mchafu mara moja akasikia juu ya Yesu hivyo alimwijia na kuanguka chini yake. 26 Mwanamke huyo alikuwa ni Mgiriki na siyo Myahudi, na alikuwa amezaliwa Foeniki ya Shamu. Yeye alimsihi amfukuze pepo yule kutoka kwa binti yake.
27 Yesu akamwambia, “Kwanza waache watoto watosheke, kwani sio haki kuwanyanganya watoto mkate wao na kuwapa mbwa.”
28 Lakini yeye akajibu, “Bwana hata mbwa walio chini ya meza wanakula mabaki ya chakula cha watoto.”
29 Kisha Yesu akamwambia, “kwa majibu haya unaweza kwenda nyumbani kwa amani: pepo mbaya amekwisha mtoka binti yako.”
30 Kwa hiyo akaenda nyumbani na akamkuta amelala akipumzika kitandani, na yule pepo tayari amekwisha mtoka.
Yesu Amponya Asiyesikia
31 Yesu akarudi kutoka katika eneo kuzunguka jiji la Tiro na akapita katika jiji la Sidoni hadi Ziwa Galilaya akipita katika jimbo la Dekapoli. 32 Pale watu wengine wakamletea mtu asiyeweza kusikia na tena aliyesema kwa shida. Nao wakamwomba Yesu amwekee mikono yake na kumponya.
33 Yesu akamchukua pembeni, kutoka katika kundi, na akaweka vidole vyake ndani ya masikio yake. Kisha Yesu akatema mate na kuugusa ulimi wa yule mtu. 34 Akaangalia juu mbinguni, akapumua na kumwambia “Efatha” yaani, “Funguka!” 35 Mara masikio ya mtu yule yakafunguka, na ulimi wake ukawa huru, na akaanza kuzungumza, vizuri.
36 Lakini kadiri jinsi alivyowaamuru wasimwambie mtu ndivyo walivyozidi kueneza habari hiyo. 37 Na watu wakashangazwa kabisa na kusema, “Yesu amefanya kila kitu vyema. Kwani amewafanya wale wasiosikia kusikia na wasiosema kusema.”
© 2017 Bible League International