Book of Common Prayer
Barua ya Yesu kwa Kanisa la Smirna
8 Andika hivi kwa malaika wa kanisa lililoko Smirna:
“Huu ni ujumbe kutoka kwake aliye wa Kwanza na wa Mwisho, aliyekufa na akawa hai tena.
9 Ninayajua matatizo yako, na ninajua kwamba wewe ni maskini, lakini hakika wewe ni tajiri! Ninayajua matusi unayoteseka kutoka kwa watu wanaojiita Wateule wa Mungu.[a] Lakini si Wayahudi halisi. Watu hao ni wa kundi[b] la Shetani. 10 Usiogope mambo yatakayokupata hivi karibuni. Ninakwambia, Ibilisi atawafunga gerezani baadhi yenu ili kuipima imani yenu. Mtateseka kwa siku kumi, lakini iweni waaminifu, hata ikiwa mtatakiwa kufa. Mkiendelea kuwa waaminifu, nitawapa thawabu[c] ya uzima wa milele.
11 Kila anayesikia hili azingatie kile ambacho Roho anayaambia makanisa. Wale watakaoshinda hawatadhuriwa na mauti ya pili.
Barua ya Yesu kwa Kanisa la Pergamo
12 Andika hivi kwa malaika wa kanisa lililoko Pergamo:
Huu ni ujumbe kutoka kwake aliye na upanga wenye makali kuwili unaotoka katika kinywa chake.
13 Ninapafahamu mahali unapoishi. Unaishi mahali kilipo kiti cha enzi cha Shetani, lakini wewe ni mwaminifu kwangu. Hukukataa kueleza kuhusu imani yako kwangu hata wakati wa Antipa. Antipa alikuwa shahidi wangu mwaminifu[d] aliyeuawa katika mji wako, mji ambao shetani anaishi.
14 Lakini nina vitu vichache kinyume nawe. Una watu huko wanaofuata mafundisho ya Balaamu. Balaamu alimfundisha Balaki namna ya kuwafanya watu wa Israeli kutenda dhambi. Walitenda dhambi kwa kula vyakula vilivyotolewa kwa ajili ya sanamu na kwa kufanya uzinzi. 15 Ndivyo ilivyo hata kwa kundi lako. Una watu wanaofuata mafundisho ya Wanikolai. 16 Hivyo igeuzeni mioyo yenu! Msipobadilika, nitakuja kwenu haraka na kupigana kinyume na watu hawa kwa kutumia upanga unaotoka katika kinywa changu.
17 Kila anayesikia hili azingatie kile ambacho Roho anayaambia makanisa!
Kila atakayeshinda nitampa mana iliyofichwa. Pia nitampa kila mshindi jiwe jeupe lililoandikwa jina jipya juu yake. Na hakuna atakayejua jina hili isipokuwa yule atakayepata jiwe hili.
46 Naye Yesu akaenda tena kutembelea Kana huko Galilaya. Kana ni mahali alikoyabadili maji kuwa divai. Mmoja wa maafisa muhimu wa mfalme alikuwa anaishi katika mji wa Kapernaumu. Mwanawe afisa huyu alikuwa mgonjwa. 47 Afisa huyo akasikia kwamba Yesu alikuwa amekuja kutoka Uyahudi na sasa yuko Galilaya. Hivyo akamwendea Yesu na kumsihi aende Kapernaumu kumponya mwanawe, aliyekuwa mahututi sana. 48 Yesu akamwambia, “Ninyi watu ni lazima muone ishara zenye miujiza na maajabu kabla ya kuniamini.”
49 Afisa wa mfalme akasema, “Bwana, uje kabla mwanangu mdogo hajafa.”
50 Yesu akajibu, “Nenda, mwanao ataishi.”
Mtu huyo akayaamini maneno Yesu aliyomwambia na akaenda nyumbani. 51 Akiwa njiani kwenda nyumbani watumishi wake wakaja na kukutana naye. Wakasema, “Mwanao ni mzima.”
52 Mtu huyo akauliza, “Ni wakati gani mwanangu alipoanza kupata nafuu?”
Wakajibu, “Ilikuwa jana saa saba mchana homa ilipomwacha.”
53 Baba yake akatambua kuwa saa saba kamili ulikuwa ndiyo ule wakati aliposema, “Mwanao ataishi.” Hivyo afisa huyo na kila mmoja katika nyumba yake wakamwamini Yesu.
54 Huo ulikuwa muujiza wa pili ambao Yesu aliufanya baada ya kufika kutoka Uyahudi na Galilaya.
© 2017 Bible League International