Book of Common Prayer
32 Nataka msisumbuke. Mwanaume ambaye hajaoa hujishughulisha na kazi ya Bwana naye hujitahidi kumpendeza Bwana. 33 Lakini mwanaume aliyeoa hujishughulisha na mambo ya ulimwengu, ili ampendeze mke wake. 34 Ni lazima afikirie mambo mawili; kumpendeza mke wake na kumpendeza Bwana. Mwanamke ambaye hajaolewa au msichana ambaye hajawahi kuolewa hujishughulisha na kazi ya Bwana. Hutaka kuutoa mwili na roho yake kikamilifu kwa Bwana. Lakini mwanamke aliyeolewa hujishughulisha na mambo ya ulimwengu ili ampendeze mume wake. 35 Ninasema hili ili niwasaidie. Si kuwawekea vikwazo, lakini ninataka mwishi katika njia sahihi. Na ninataka mjitoe kikamilifu kwa Bwana pasipo kuchukuliwa katika mambo mengine.
36 Mwanaume anaweza kudhani kuwa hamtendei haki mchumba wake. Mchumba wake huyo anaweza kuwa ameshapita umri mzuri wa kuolewa.[a] Hivyo mwanaume anaweza kujisikia kuwa anapaswa kumwoa mchumba wake huyo. Basi na afanye anachotaka. Si dhambi kwao wakioana. 37 Lakini mwanaume mwingine anaweza kuwa na uhakika akilini mwake ya kuwa hakuna haja ya ndoa, hivyo yuko huru kufanya anachotaka. Ikiwa ameamua moyoni mwake kutomwoa mchumba wake, anafanya jambo sahihi. 38 Hivyo mwanaume anayemwoa mchumba wake anafanya jambo jema, na mwanaume asiyeoa anafanya vyema zaidi.
39 Mwanamke anapaswa kuishi na mume wake kipindi chote mumewe anapokuwa hai. Lakini mume akifa, mwanamke anakuwa huru kuolewa na mwanaume yeyote. Lakini mwanaume huyo lazima awe yule wa Bwana. 40 Ikiwa atabaki kuwa mjane, atakuwa na furaha sana. Haya ni maoni yangu, na ninaamini yanatoka kwa Roho wa Mungu.
Yesu Aenda Kwenye Mji wa Kwao
(Mt 13:53-58; Lk 4:16-30)
6 Yesu akaondoka pale, na kwenda katika mji wa kwao; na wanafunzi wake wakamfuata. 2 Sabato ilipofika, alianza kufundisha katika sinagogi. Watu wengi walishangazwa walipomsikiliza. Wakasema, “Mtu huyu alipata wapi mambo haya? Alipata wapi hekima hii? Na anaifanyaje miujiza hii inayofanyika kwa mikono yake? 3 Je, yeye si yule seremala? Je, yeye si mwana wa Maria? Je, yeye si kaka yake Yakobo, Yusufu, Yuda, na Simoni? Je, dada zake hawaishi hapa katika mji wetu?” Kulikuwa na vikwazo vilivyowazuia wasimkubali.
4 Yesu akawaambia, “kila mtu humheshimu nabii isipokuwa watu wa mji wa kwao mwenyewe, jamaa zake mwenyewe na wale wa nyumbani mwake mwenyewe.” 5 Yesu hakuweza kufanya miujiza ya aina yoyote pale, isipokuwa aliweka mikono juu ya wagonjwa wachache na kuwaponya. 6 Naye akashangazwa na jinsi watu wa mji wa kwao mwenyewe walivyokosa kuwa na imani. Kisha Yesu alizunguka vijijini akiwafundisha watu.
Yesu Awatuma Kazi Mitume Wake
(Mt 10:1,5-15; Lk 9:1-6)
7 Akawaita kwake wanafunzi wake kumi na wawili, na akaanza kuwatuma wawili wawili. Akawapa uwezo wa kuwaweka huru watu kutoka pepo wachafu. 8 Akawapa amri kuwa wasichukue kitu chochote kwa ajili ya safari yao isipokuwa fimbo; hawakupaswa kuchukua mkate, mfuko, hata kubeba fedha kwenye mikanda yao. 9 Aliwaruhusu kuvaa makobazi lakini wasichukue kanzu ya pili. 10 Naye akawambia, “ikiwa mtu atawapa mahali pa kuishi mkae katika nyumba hiyo kwa muda wote mtakapokuwa katika mji ule msihamehame kutoka nyumba moja hadi nyingine. 11 Ikiwa hamtakaribishwa ama kusikilizwa katika mji wowote au mahali popote, kwa kuwaonya kunguteni mavumbi toka miguuni mwenu.”
12 Kwa hiyo mitume wakatoka na kuhubiri ili watu watubu. 13 Mitume wakafukuza mashetani wengi na kuwapaka mafuta ya mizeituni[a] wagonjwa wengi na kuwaponya.
© 2017 Bible League International