Add parallel Print Page Options

Nani ni Mkuu Zaidi?

(Mk 9:33-37; Lk 9:46-48)

18 Wakati huo huo wanafunzi wake wakamjia Yesu na kuuliza, “Nani ni mkuu zaidi katika ufalme wa Mungu?”

Yesu akamwita mtoto mdogo, akamsimamisha mbele yao. Kisha akasema, “Ukweli ni huu, ni lazima mbadilike katika namna mnavyofikiri na muwe kama mtoto mdogo. Msipofanya hivi hamtaingia katika ufalme wa Mungu. Aliye mkuu zaidi katika ufalme wa Mungu ni yule anayejinyenyekeza kama mtoto huyu.

Unapomkubali mtoto mdogo kama huyu kama aliye wangu, unanikubali mimi.

Yesu Aonya Kuhusu Chanzo cha Dhambi

(Mk 9:42-48; Lk 17:1-2)

Ikiwa mmoja wa watoto hawa wadogo ananiamini, na mtu yeyote akasababisha mtoto huyo kutenda dhambi, ole wake mtu huyo. Ingekuwa bora mtu huyo kufungiwa jiwe la kusagia shingoni mwake na kuzamishwa katika kina kirefu baharini. Nawasikitikia watu wa ulimwengu kwa sababu ya mambo yanayofanya watu watende dhambi. Mambo haya lazima yatokee, lakini ole wake mtu yeyote anayeyafanya yatokee.

Mkono au mguu wako ukikufanya utende dhambi, ukate na uutupe. Ni bora ukapoteza kiungo kimoja cha mwili wako na ukaupata uzima wa milele kuliko kuwa na mikono au miguu miwili na ukatupwa katika moto wa milele. Jicho lako likikufanya utende dhambi, ling'oe na ulitupe. Ni bora kwako kuwa na jicho moja tu na ukaupata uzima wa milele kuliko kuwa na macho mawili na ukatupwa katika moto wa Jehanamu.

Yesu Atumia Simulizi ya Kondoo Aliyepotea

(Lk 15:3-7)

10 Iweni waangalifu, msidhani kuwa watoto hawa wadogo si wa muhimu. Ninawaambia kuwa watoto hawa wana malaika mbinguni. Na hao malaika daima wako pamoja na Baba yangu mbinguni. 11 [a]

12 Mtu akiwa na kondoo 100, lakini mmoja wa kondoo akapotea, atafanya nini? Atawaacha kondoo wengine 99 kwenye kilima na kwenda kumtafuta mmoja aliyepotea. Sawa? 13 Na akimpata kondoo aliyepotea, atafurahi kwa sababu ya kondoo huyo mmoja kuliko kondoo wengine 99 ambao hawakupotea. Ninaweza kuwathibitishia, 14 Kwa namna hiyo hiyo, Baba yenu wa mbinguni hapendi mmoja wa watoto hawa wadogo apotee.

Mrekebishe Kila Anayekosea

(Lk 17:3)

15 Ikiwa mmoja wa ndugu au dada yako katika familia ya Mungu akifanya kosa kwako,[b] umwendee na umwambie kile alichokukosea. Ufanye hivi mnapokuwa ninyi wawili tu. Ikiwa mtu huyo atakusikiliza, basi umemsaidia na umfanye kuwa kaka ama dada yako tena. 16 Lakini ikiwa mtu huyo atakataa kukusikiliza, mrudie ukiwa pamoja na ndugu wengine wawili waaminio. Ndipo watakuwepo watu wawili au watatu watakaoweza kueleza kile kilichotokea.[c] 17 Ikiwa mtu aliyetenda dhambi atakataa kuwasikiliza, ndipo uliambie kanisa. Na akikataa kulisikiliza kanisa, mchukulie kama ambavyo ungemchukulia mtu asiyemfahamu Mungu au mtoza ushuru.

18 Ninawahakikishia kuwa mnapotoa hukumu hapa duniani, hukumu hiyo itakuwa hukumu ya Mungu. Na mnapotoa msamaha, nao utakuwa msamaha wa Mungu.[d] 19 Kwa namna nyingine, ikiwa watu wawili waliopo duniani watakubaliana kwa kila wanachokiombea, Baba yangu wa mbinguni atatenda kile wanachokiomba. 20 Ndiyo, ikiwa watu wawili au watatu wanaoniamini watakusanyika pamoja, mimi nitakuwa pamoja nao.”

Simulizi Kuhusu Msamaha

21 Kisha Petro akamwendea Yesu na kumwuliza, “Bwana, ndugu yangu akiendelea kunikosea, ninapaswa kumsamehe anaponikosea mara ngapi? Mara saba?”

22 Yesu akamjibu, “Ninakwambia, ni lazima umsamehe zaidi ya mara saba. Ni lazima uendelee kumsamehe hata kama atakukosea saba mara sabini.[e]

23 Ninawaambia kwa sababu ufalme wa Mungu unafanana na mfalme aliyetaka kupata taarifa kutoka kwa watumishi wake. 24 Mtumishi aliyekuwa anadaiwa na mfalme tani 300[f] za fedha aliletwa kwake. 25 Hakuwa na fedha za kutosha kulipa deni lake. Hivyo mfalme aliamuru kila kitu anachomiliki mtumishi yule kiuzwe ikiwa ni pamoja na mke na watoto wake.

26 Lakini mtumishi alipiga magoti na kumsihi mfalme akisema, ‘Nivumilie. Nitakulipa kila kitu unachonidai.’ 27 Mfalme alimhurumia. Hivyo akamsamehe yule mtumishi deni lote na akamwacha aende akiwa huru.

28 Lakini mtumishi huyo alipoondoka, alimwona mtumishi mwingine aliyekuwa anamdai sarafu mia za fedha. Akamkaba shingo yake na akasema, ‘Nilipe pesa ninayokudai!’

29 Mtumishi anayedaiwa akapiga magoti na kumsihi akisema, ‘Nivumilie. Nitakulipa kila kitu unachonidai.’

30 Lakini mtumishi wa kwanza alikataa kumvumilia. Alimwambia hakimu kuwa alikuwa anamdai pesa, na mtumishi yule alitupwa gerezani mpaka atakapoweza kulipa deni lake. 31 Watumishi wengine walipoona hili, walimhurumia mtumishi aliyefungwa gerezani. Hivyo walienda na kumwambia mfalme kila kitu kilichotokea.

32 Ndipo mfalme alimwita msimamizi wa kwanza na kumwambia, ‘Wewe ni mbaya sana! Ulinisihi nikusamehe deni lako, na nilikuacha ukaondoka bila kulipa kitu chochote! 33 Hivyo ulipaswa kumpa mtu yule mwingine anayetumika pamoja nawe rehema ile ile niliyokupa mimi.’ 34 Mfalme alikasirika sana. Hivyo alifungwa gerezani mpaka atakapoweza kulipa kila kitu anachodaiwa.

35 Mfalme huyu alifanya kama ambavyo Baba yangu wa mbinguni atawafanyia ninyi. Ni lazima umsamehe ndugu au dada yako kwa moyo wako wote, usipofanya hivyo, Baba yangu wa mbinguni hatakusamehe wewe.”

Yesu Afundisha Kuhusu Talaka

(Mk 10:1-12)

19 Yesu alipomaliza kuzungumza haya yote, aliondoka Galilaya. Alikwenda maeneo ya Yuda ng'ambo ya Mto Yordani. Watu wengi walimfuata na akaponya wagonjwa wengi huko.

Baadhi ya Mafarisayo wakamjia Yesu. Walitaka aseme jambo fulani lisilo sahihi. Wakamwuliza, “Je, ni sahihi kwa mume kumtaliki mke wake kutokana na sababu yoyote ile kama anavyotaka?”

Yesu akajibu, “Hakika mmesoma hili katika Maandiko: Mungu alipoumba ulimwengu, ‘aliumba watu wa jinsi ya kiume na wa jinsi ya kike.’(A) Na Mungu alisema, ‘Hii ndiyo sababu mwanaume atawaacha baba na mama yake na kuungana na mke wake. Na hao watu wawili watakuwa mmoja.’(B) Hivyo wao si wawili tena, bali mmoja. Ni Mungu aliowaunganisha pamoja, hivyo mtu yeyote asiwatenganishe.”

Mafarisayo wakauliza, “Sasa kwa nini Musa alitoa amri ya kumruhusu mwanaume kumtaliki mke wake kwa kuandika hati ya talaka?”[g]

Yesu akajibu, “Musa aliwaruhusu kuwataliki wake zenu kwa sababu mlikataa kupokea mafundisho ya Mungu. Lakini talaka haikuruhusiwa hapo mwanzo. Ninawaambia kuwa, kila anayemtaliki mke wake, isipokuwa kutokana na uzinzi, na akamwoa mwanamke mwingine, anazini.”

10 Wafuasi wakamwambia Yesu, “Ikiwa hiyo ndiyo sababu pekee ambayo mtu anaruhusiwa kumtaliki mke wake, ni bora kutooa.”

11 Akajibu, “Tamko hili ni la kweli kwa baadhi ya watu, lakini si kwa kila mtu. Bali ni kwa wale tu waliopewa karama hii. 12 Kuna sababu tofauti kwa nini baadhi ya wanaume hawaoi.[h] Wengine wamezaliwa wakiwa hawana uwezo wa kuzaa watoto, wengine walifanywa hivyo katika maisha yao ya baadaye. Na wengine walichagua kutokuoa kwa ajili ya ufalme wa Mungu. Hili liko hivyo kwa kila anayeweza kulikubali.”

Yesu Awakaribisha Watoto

(Mk 10:13-16; Lk 18:15-17)

13 Ndipo watu wakawaleta watoto wao wadogo kwa Yesu ili awabariki na kuwaombea. Wafuasi wake walipoliona hili, waliwakataza watu wasiwalete watoto kwa Yesu. 14 Lakini Yesu akasema, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie, kwa sababu ufalme wa Mungu ni wa watu walio kama watoto hawa wadogo.” 15 Baada ya Yesu kuwabariki watoto, aliondoka huko.

Mtu Tajiri Akataa Kumfuata Yesu

(Mk 10:17-31; Lk 18:18-30)

16 Mtu mmoja alimwendea Yesu na kumwuliza, “Mwalimu, nifanye jambo gani lililo jema ili niweze kuupata uzima wa milele?”

17 Yesu akajibu, “Kwa nini unaniuliza kuhusu jambo gani lililo jema? Mungu pekee yake ndiye mwema. Lakini ikiwa unataka kuupata uzima wa milele, zitii amri.”

18 Yule mtu akauliza, “Amri zipi?”

Yesu akajibu, “‘Usiue, usizini, usiibe, usiseme uongo, 19 mheshimu baba na mama yako,’(C) na ‘mpende jirani yako[i] kama unavyojipenda wewe mwenyewe.’”(D)

20 Yule kijana akasema, “Ninazitii amri hizi zote. Nifanye nini zaidi?”

21 Yesu akajibu, “Ikiwa unataka kuwa mkamilifu, nenda ukauze kila kitu unachomiliki. Uwape pesa maskini na utakuwa na utajiri mbinguni. Kisha njoo unifuate!”

22 Lakini kijana aliposikia Yesu anamwambia kuhusu kugawa pesa yake, alihuzunika. Hakutaka kufanya hivi kwa kuwa alikuwa tajiri sana. Hivyo aliondoka.

23 Ndipo Yesu aliwaambia wafuasi wake, “Ukweli ni huu, itakuwa vigumu sana kwa tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu. 24 Ndiyo, ninawaambia, ni rahisi kwa ngamia kupita katika tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.”

25 Wafuasi waliposikia hili walishangaa. Wakauliza, “Sasa ni nani ataweza kuokolewa?”

26 Yesu akawatazama na kuwaambia, “Hili haliwezekani kwa wanadamu, Lakini yote yanawezekana kwa Mungu.”

27 Petro akamwambia, “Tuliacha kila kitu tulichonacho na kukufuata wewe. Tutapata nini?”

28 Yesu akawaambia, “Wakati wa ulimwengu mpya utakapofika, Mwana wa Adamu ataketi kwenye kiti chake cha enzi, kikuu na chenye utukufu mwingi. Na ninaweza kuwaahidi kuwa ninyi mnaonifuata mtaketi kwenye viti kumi na viwili vya enzi, na mtayahukumu makabila kumi na mawili ya Israeli. 29 Kila aliyeacha nyumba, ndugu, dada, baba, mama, watoto au shamba na akanifuata atapata zaidi ya yale aliyoacha. Na atapata uzima wa milele. 30 Watu wengi walio wa kwanza sasa watakuwa wa mwisho siku zijazo. Na walio wa mwisho sasa watakuwa wa kwanza siku zijazo.

Yesu Atumia Mfano wa Wakulima Katika Shamba la Mizabibu

20 Ufalme wa Mungu umefanana na mtu aliyemiliki shamba la mizabibu. Asubuhi mmoja akatoka kwenda kuajiri watu ili walime katika shamba lake la mizabibu. Alikubaliana nao kuwa atawalipa sarafu moja ya fedha ikiwa watafanya kazi siku ile. Kisha akawapeleka kwenye shamba la mizabibu kulima.

Ilipofika saa tatu asubuhi mtu huyo alitoka na kwenda sokoni ambako aliwaona baadhi ya watu wamesimama na hawafanyi kazi yo yote. Akawaambia, ‘Ikiwa mtakwenda kufanya kazi shambani kwangu, nitawalipa kutokana na kazi yenu.’ Hivyo walikwenda kufanya kazi kwenye shamba lake la mizabibu.

Ilipofika saa sita mchana na saa tisa alasiri alitoka tena. Na nyakati zote mbili aliwaajiri watu wengine waende kufanya kazi shambani mwake. Ilipofika saa kumi na moja alikwenda sokoni tena. Akawaona watu wengine wamesimama pale. Akawauliza, ‘Kwa nini mmesimama hapa siku nzima na hamfanyi kazi?’

Wakasema, ‘Hakuna aliyetupa kazi.’

Mwenye shamba akawaambia, ‘Basi mnaweza kwenda kufanya kazi katika shamba langu la mizabibu.’

Mwishoni mwa siku, mwenye shamba akamwambia msimamizi wa wafanyakazi wote, ‘Waite wafanyakazi na uwalipe wote. Anza kwa kulipa watu niliowaajiri mwishoni, na malizia kwa wale niliowaajiri mwanzoni.’

Wafanyakazi walioajiriwa saa kumi na moja jioni walipata malipo yao. Kila mfanyakazi alipata sarafu moja ya fedha. 10 Ndipo wafanyakazi walioajiriwa kwanza wakaja kupokea malipo yao. Walidhani wangelipwa zaidi ya wengine. Lakini kila mmoja wao alipokea sarafu moja ya fedha. 11 Walipopata sarafu ya fedha, walimlalamikia mmiliki wa shamba. 12 Walisema, ‘Watu hao walioajiriwa mwishoni wamefanya kazi saa moja tu. Lakini umewalipa sawa na sisi. Na tumefanya kazi siku nzima kwenye jua kali.’

13 Lakini mmiliki wa shamba akamwambia mmoja wao, ‘Rafiki, nimekulipa kama tulivyopatana, ulikubali kufanya kazi kwa malipo ya sarafu moja ya fedha. Sawa? 14 Hivyo chukua malipo yako na uende. Ninataka kumlipa mtu niliyemwajiri mwishoni sawa na kiasi nilichokulipa. 15 Ninaweza kufanya chochote ninachotaka na pesa yangu. Wewe unao wivu[j] na unataka kuwadhuru wengine kwa kuwa mimi ni mkarimu?’

16 Hivyo walio wa mwisho sasa watakuwa wa kwanza siku zijazo. Na walio wa kwanza sasa watakuwa wa mwisho siku zijazo.”

Yesu Azungumza Tena Kuhusu Kifo Chake

(Mk 10:32-34; Lk 18:31-34)

17 Yesu alikuwa anakwenda Yerusalemu akiwa na wafuasi wake kumi na wawili. Walipokuwa wakitembea, aliwakusanya pamoja wafuasi hao na kuzungumza nao kwa faragha. Akawaambia, 18 “Tunakwenda Yerusalemu. Mwana wa Adamu atatolewa kwa viongozi wa makuhani na walimu wa sheria, nao watasema ni lazima auawe. 19 Watamkabidhi wa wageni, watakaomcheka na kumpiga kwa mijeledi, kisha watamwua kwenye msalaba. Lakini siku ya tatu baada ya kifo chake, atafufuliwa kutoka kwa wafu.”

Mama Ataka Upendeleo Maalum kwa Wanaye

(Mk 10:35-45)

20 Ndipo mke wa Zebedayo akamjia Yesu akiwa na wanaye. Akainama mbele ya Yesu na akamwomba amtendee kitu.

21 Yesu akasema, “Unataka nini?”

Akasema, “Niahidi kuwa mmoja wa wanangu atakaa upande wa kuume na mwingine wa kushoto katika ufalme wako.”

22 Hivyo Yesu akawaambia wana wa Zebedayo, “Hamwelewi mnachokiomba. Mnaweza kukinywea kikombe[k] ambacho ni lazima nikinywee?”

Wana wa Zebedayo wakajibu, “Ndiyo tunaweza!”

23 Yesu akawaambia, “Ni kweli kuwa mtakinywea kikombe nitakachokinywea. Lakini si mimi wa kuwaambia ni nani ataketi mkono wangu wa kuume au wa kushoto. Baba yangu amekwisha amua ni nani ataketi kuume au kushoto kwangu. Amekwisha andaa nafasi hizo kwa ajili yao.”

24 Wafuasi wengine kumi waliposikia hili walikasirika kwa ajili ya wale ndugu wawili. 25 Hivyo Yesu akawaita pamoja, akawaambia, “Mnajua kuwa watawala wa watu wasio Wayahudi[l] wanapenda kuonesha nguvu yao kwa watu. Na viongozi wao muhimu wanapenda kutumia mamlaka yao yote juu ya watu. 26 Lakini isiwe hivyo miongoni mwenu. Kila anayetaka kuwa kiongozi wenu lazima awe mtumishi wenu. 27 Kila anayetaka kuwa wa kwanza ni lazima awatumikie ninyi nyote kama mtumwa. 28 Fanyeni kama nilivyofanya: Mwana wa Adamu hakuja ili atumikiwe na watu. Alikuja ili awatumikie wengine na kutoa maisha yake ili kuwaokoa watu wengi.”

Yesu Awaponya Watu Wawili Wasiyeona

(Mk 10:46-52; Lk 18:35-43)

29 Yesu na wanafunzi wake walipokuwa wanaondoka Yeriko, umati mkubwa wa watu ulimfuata. 30 Walikuwepo wasiyeona wawili wamekaa kando ya njia. Waliposikia kuwa Yesu anapita pale walipaza sauti wakasema, “Bwana, Mwana wa Daudi, tafadhali tusaidie!”

31 Watu waliwakemea wale wasiyeona, wakawaambia wanyamaze. Lakini waliendelea kupaza sauti zao zaidi na zaidi, “Bwana, Mwana wa Daudi, tafadhali tusaidie!”

32 Yesu alisimama na kuwaambia, “Mnataka niwafanyie nini?”

33 Wakajibu, “Bwana, tunataka tuweze kuona.”

34 Yesu aliwahurumia wale wasiyeona. Akayagusa macho yao, na mara hiyo hiyo wakaanza kuona. Wakawa wafuasi wa Yesu.

Yesu Aingia Yerusalemu Kama Mfalme

(Mk 11:1-11; Lk 19:28-38; Yh 12:12-19)

21 Yesu na wafuasi wake walipokaribia Yerusalemu, walisimama Bethfage kwenye kilima kinachoitwa Mlima wa Mizeituni. Wakiwa hapo Yesu aliwatuma wafuasi wake wawili mjini. Aliwaambia, “Nendeni kwenye mji mtakaoweza kuuona huko. Mtakapoingia katika mji huo, mtamwona punda na mwanapunda wake.[m] Wafungueni wote wawili, kisha waleteni kwangu. Mtu yeyote akiwauliza kwa nini mnawachukua punda, mwambieni, ‘Bwana anawahitaji. Atawarudisha mapema.’”

Hili lilitimiza maneno yaliyosemwa na nabii:

“Waambie watu wa Sayuni,[n]
    ‘Mfalme wako anakuja sasa.
Ni mnyenyekevu na amempanda punda.
    Na amempanda mwana punda dume tena safi.’”(E)

Wafuasi walikwenda na kufanya yale walioambiwa na Yesu. Waliwaleta kwake punda jike na mwanapunda. Waliwafunika punda kwa nguo zao na Yesu akaketi juu yao. Akiwa njiani kuelekea Yerusalemu, watu wengi walitandaza mavazi yao barabarani kwa ajili Yake. Wengine walikata matawi ya miti na kuyatandaza barabarani ili kumkaribisha. Wengine walimtangulia Yesu, na wengine walikuwa nyuma yake. Wote walipaza sauti wakisema:

“Msifuni[o] Mwana wa Daudi!
‘Karibu! Mungu ambariki yeye
    ajaye katika jina la Bwana!’(F)
Msifuni Mungu wa mbinguni!”

10 Kisha Yesu aliingia Yerusalemu. Watu wote mjini wakataharuki. Wakauliza, “Mtu huyu ni nani?”

11 Kundi la watu waliomfuata Yesu wakajibu, “Huyu ni Yesu. Ni nabii kutoka katika mji wa Nazareti ulio Galilaya.”

Yesu Asafisha Eneo la Hekalu

(Mk 11:15-19; Lk 19:45-48; Yh 2:13-22)

12 Yesu alipoingia katika eneo la Hekalu, aliwatoa nje wote waliokuwa wanauza na kununua vitu humo. Alizipindua meza za watu waliokuwa wanabadilishana pesa. Na alipindua viti vya watu waliokuwa wanauza njiwa. 13 Yesu aliwaambia, “Maandiko yanasema, ‘Hekalu langu litaitwa nyumba ya sala.’(G) Lakini mmelibadilisha na kuwa ‘maficho ya wezi’.(H)

14 Baadhi ya watu waliokuwa wasiyeona na walemavu wa miguu walimjia Yesu alipokuwa eneo la Hekalu, naye aliwaponya. 15 Viongozi wa makuhani na walimu wa sheria waliona mambo ya ajabu aliyokuwa anatenda. Na waliona watoto walivyokuwa wanamsifu wakisema, “Sifa kwa Mwana wa Daudi.” Mambo haya yote yaliwakasirisha makuhani na walimu wa sheria.

16 Wakamwuliza Yesu, “Unasikia wanayosema watoto hawa?”

Akajibu, “Ndiyo. Maandiko yanasema,

‘Umewafundisha watoto wadogo na watoto
    wanyonyao kusifu.’(I)

Hamjasoma Maandiko haya?”

17 Kisha Yesu akawaacha na akaenda katika mji wa Bethania akalala huko.

Yesu Aulaani Mtini

(Mk 11:12-14,20-24)

18 Mapema asubuhi iliyofuata, Yesu alikuwa anarudi mjini Yerusalemu naye alikuwa na njaa. 19 Aliuona mtini karibu na njia na akaenda kuchuma tini kwenye mti huo. Yalikuwepo maua tu. Hivyo Yesu akauambia mti ule, “Hautazaa matunda tena!” Mtini ukakauka na kufa hapo hapo.

20 Wafuasi wake walipoona hili, walishangaa sana. Wakauliza, “Imekuwaje mtini ukakauka na kufa haraka hivyo?”

21 Yesu akajibu, “Ukweli ni kuwa, mkiwa na imani na msiwe na mashaka, mtaweza kufanya kama nilivyofanya kwa mti huu. Na mtaweza kufanya zaidi ya haya. Mtaweza kuuambia mlima huu, ‘Ng'oka na ujitupe baharini.’ Na ikiwa una imani, litafanyika. 22 Mkiamini, mtapokea kila mnachoomba.”

Viongozi Wawa na Mashaka Kuhusu Mamlaka ya Yesu

(Mk 11:27-33; Lk 20:1-8)

23 Yesu aliingia katika eneo la Hekalu na akaanza kufundisha humo. Viongozi wa makuhani na viongozi wa wazee wakamjia. Wakasema, “Tuambie! Una mamlaka gani ya kufanya mambo haya unayofanya? Na nani amekupa mamlaka hii?”

24 Yesu akajibu, “Nitawauliza swali pia. Mkinijibu, ndipo nitawaambia nina mamlaka gani ya kufanya mambo haya. 25 Niambieni: Yohana alipowabatiza watu, mamlaka yake ilitoka kwa Mungu au kwa wanadamu?”

Makuhani na viongozi wa Kiyahudi wakajadiliana kuhusu swali la Yesu, wakasemezana, “Tukisema, ‘Ubatizo wa Yohana ulitoka kwa Mungu,’ atasema, ‘Sasa kwa nini hamkumwamini Yohana?’ 26 Lakini hatuwezi kusema ubatizo wa Yohana ulitoka kwa watu wengine. Tunawaogopa watu, kwa sababu wote wanaamini kuwa Yohana alikuwa nabii.”

27 Hivyo wakamwambia Yesu, “Hatujui jibu.”

Yesu akasema, “Basi hata mimi siwaambii aliyenipa mamlaka ya kufanya mambo haya.”

Yesu Atumia Simulizi Kuhusu Wana Wawili

28 “Niambieni mnafikiri nini kuhusu hili: Alikuwepo mtu mwenye wana wawili. Alimwendea mwanaye wa kwanza na kumwambia, ‘Mwanangu, nenda ukafanye kazi kwenye shamba la mizabibu leo.’

29 Mwanaye akasema, ‘Siendi.’ Lakini baadaye akabadili uamuzi wake na akaenda.

30 Kisha baba akamwendea mwanaye mwingine na kumwambia, ‘Mwanangu, nenda ukafanye kazi kwenye shamba la mizabibu leo.’ Akajibu, ‘Sawa baba, nitakwenda kufanya kazi.’ Lakini hakwenda.

31 Ni yupi kati ya wana hawa wawili alimtii baba yake?”

Viongozi wa Kiyahudi wakajibu, “Ni mwana wa kwanza.”

Yesu akawaambia, “Ukweli ni huu, ninyi ni wabaya kuliko watoza ushuru na makahaba. Ukweli ni kuwa hao wataingia katika ufalme wa Mungu kabla yenu. 32 Yohana alikuja akiwaonesha njia sahihi ya kuishi, na hamkumwamini. Lakini watoza ushuru na makahaba walimwamini Yohana. Mliona yaliyotokea, lakini hamkubadilika na mlikataa kumwamini.

Yesu Atoa Simulizi Kuhusu Shamba la Mzabibu

(Mk 12:1-12; Lk 20:9-19)

33 Sikilizeni simulizi hii: Alikuwepo mtu aliyemiliki shamba la mizabibu. Alijenga uzio kuzunguka shamba lile la mizabibu na akachimba shimo kwa ajili ya kukamulia zabibu.[p] Kisha akajenga mnara wa lindo. Akalikodisha shamba kwa wakulima kisha akasafiri. 34 Wakati wa kuvuna zabibu ulipofika, akawatuma watumishi wake waende kwa wakulima ili apate gawio lake la zabibu.

35 Lakini wakulima waliwakamata wale watumishi na kumpiga mmoja wao. Wakamwua mwingine na wa tatu wakampiga kwa mawe mpaka akafa. 36 Hivyo mwenye shamba akawatuma baadhi ya watumishi wengine wengi zaidi ya aliowatuma hapo kwanza. Lakini wakulima wakawatendea kama walivyowatendea watumishi wa kwanza. 37 Hivyo mwenye shamba akaamua kumtuma mwanaye kwa wakulima. Alisema, ‘Wakulima watamheshimu mwanangu.’

38 Lakini wakulima walipomwona mwanaye, wakaambizana, ‘Huyu ni mwana wa mwenye shamba. Shamba hili litakuwa lake. Tukimwua, shamba la mizabibu litakuwa letu.’ 39 Hivyo wakulima wakamchukua mwana wa mwenye shamba, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu na kumwua.

40 Hivyo mmiliki wa shamba la mizabibu atawafanya nini wakulima hawa atakaporudi?”

41 Makuhani wa Kiyahudi na viongozi wakasema, “Kwa hakika atawaua watu hao waovu. Kisha atawakodishia wakulima wengine shamba hilo, watakaompa gawio la mazao yake wakati wa mavuno.”

42 Yesu akawaambia, “Hakika mmesoma hili katika Maandiko:

‘Jiwe walilolikataa waashi
    limekuwa jiwe kuu la pembeni.
Bwana amefanya hivi,
    na ni ajabu kubwa kwetu kuliona.’(J)

43 Hivyo ninawaambia kuwa, ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu na watapewa watu wanaofanya mambo anayoyataka Mungu katika ufalme wake. 44 Kila aangukaye kwenye jiwe hili atavunjika na litamsaga kila linayemwangukia.”[q]

45 Viongozi wa makuhani na Mafarisayo waliposikia simulizi hizi, wakajua kuwa Yesu alikuwa anawasema wao. 46 Walitaka kumkamata Yesu. Lakini waliogopa kwani watu waliamini kuwa Yesu ni nabii.

Simulizi Kuhusu Watu Walioalikwa Kwenye Sherehe

(Lk 14:15-24)

22 Yesu aliendelea kuwajibu viongozi wa Kiyahudi kwa mifano zaidi. Akasema, “Ufalme wa Mungu unafanana na jambo lililotokea mfalme alipoandaa sherehe ya harusi kwa ajili ya mwanaye. Aliwaalika baadhi ya watu. Wakati ulipofika mfalme aliwatuma watumwa wake kuwaambia watu waende kwenye sherehe. Lakini walikataa kwenda kwenye sherehe ya mfalme.

Ndipo mfalme aliwaita baadhi ya watumishi wengine zaidi na akawaambia namna ya kuwaambia wale aliowaalika: ‘Njooni sasa! Sherehe imeandaliwa. Nimechinja ng'ombe wangu madume na ndama wanono waliolishwa nafaka, na kila kitu kiko tayari kuliwa. Njooni kwenye sherehe ya harusi.’

Lakini watu walioalikwa hawakujali yale waliyoambiwa na watumwa wa mfalme. Wengine waliondoka wakaenda kufanya mambo mengine. Mmoja alikwenda shambani na mwingine alikwenda kwenye shughuli zake. Wengine waliwakamata watumwa wa mfalme, wakawapiga na kuwaua. Mfalme alikasirika sana na akatuma jeshi lake kuwaua wale waliowaua watumwa wake. Na jeshi likauchoma moto mji wao.

Kisha mfalme akawaambia watumishi wake, ‘Sherehe ya harusi iko tayari. Niliwaalika wale watu lakini hawakustahili. Hivyo nendeni kwenye pembe za mitaa na mwalikeni kila mtu mtakayemwona, waambieni waje kwenye sherehe yangu.’ 10 Hivyo watumwa wake waliingia mitaani, wakawakusanya watu wote waliowaona, wabaya na wema na kuwaleta kwenye sherehe. Na jumba la sherehe likawa na wageni wengi.

11 Mfalme alipoingia ili kuwasalimu wageni, alimwona mtu ambaye hakuwa amevaa vazi rasmi la harusi. 12 Mfalme akamwuliza, ‘Rafiki ilikuwaje ukaruhusiwa kuingia humo? Hujavaa vazi nadhifu kwa arusi!’ Lakini mtu yule hakuwa na neno la kusema. 13 Hivyo mfalme akawaambia baadhi ya wale waliokuwa wanawahudumia watu kwa chakula, ‘Mfungeni mtu huyu mikono na miguu yake na mtupeni gizani, ambako watu wanalia na kusaga meno yao kwa maumivu.’

14 Ndiyo, watu wengi wamealikwa, lakini wachache tu ndiyo waliochaguliwa.”

Yesu Ajibu Swali Lenye Mtego

(Mk 12:13-17; Lk 20:20-26)

15 Kisha Mafarisayo wakaondoka mahali ambapo Yesu alikuwa anafundisha. Wakapanga mpango wa kumfanya aseme kitu ambacho wangekitumia dhidi yake. 16 Wakawatuma kwake baadhi ya wafuasi wao na baadhi ya watu kutoka katika kundi la Maherode. Watu hawa walipofika kwa Yesu wakasema, “Mwalimu, tunajua kuwa wewe ni mtu mwema na kwamba daima unafundisha ukweli kuhusu njia ya Mungu, bila kujali ni nani anakusikiliza. Huna wasiwasi namna ambavyo wengine wanaweza wakasema. 17 Sasa tuambie, unadhani ni sahihi kulipa kodi kwa Kaisari au la?”

18 Lakini Yesu alijua kuwa watu hawa walikuwa wanamtega. Hivyo akasema, “Enyi wanafiki! Kwa nini mnajaribu kunitega ili niseme jambo lililo kinyume? 19 Nionesheni sarafu inayotumika kulipa kodi.” Wakamwonesha Yesu sarafu iliyotengenezwa kwa fedha. 20 Kisha Yesu akauliza, “Picha iliyo kwenye sarafu hii ni ya nani? Na jina lililo kwenye sarafu hii ni la nani?”

21 Wakajibu, “Ni picha ya Kaisari na ni jina la Kaisari.”

Ndipo Yesu akawajibu, “Mpeni Kaisari vilivyo vyake na mpeni Mungu vilivyo vyake.”

22 Waliposikia yale Yesu aliyosema, wakashangaa na kuondoka.

Baadhi ya Masadukayo Wajaribu Kumtega Yesu

(Mk 12:18-27; Lk 20:27-40)

23 Siku hiyo hiyo baadhi ya Masadukayo walimjia Yesu. (Masadukayo hawaamini kuwepo kwa ufufuo wa wafu.) Masadukayo walimwuliza Yesu swali. 24 Wakasema, “Mwalimu, Musa alituambia kuwa ikiwa mwanaume aliyeoa atakufa na hana watoto, ndugu yake lazima amwoe mkewe ili aweze kuzaa watoto kwa ajili ya nduguye aliyekufa.[r] 25 Walikuwepo ndugu saba miongoni mwetu. Ndugu wa kwanza alioa lakini akafa bila ya kupata watoto. Hivyo ndugu yake akamwoa mkewe. 26 Na ndugu wa pili akafa pia, jambo hili hilo likatokea kwa ndugu wa tatu na ndugu wengine wote. 27 Mwanamke akawa wa mwisho kufa. 28 Lakini wanaume wote saba walikuwa wamemwoa. Sasa watu watakapofufuliwa kutoka kwa wafu, mwanamke huyu atakuwa mke wa yupi?”

29 Yesu akajibu, “Mnakosea sana! Hamjui kile ambacho Maandiko yanasema. Na hamjui lolote kuhusu nguvu ya Mungu. 30 Watu watakapofufuliwa kutoka kwa wafu, wanaume hawataoa wake na wanawake hawataozwa kwa wanaume. Kila mtu atakuwa kama malaika walio mbinguni. 31 Someni kile ambacho Mungu alikisema kuhusu watu kufufuliwa kutoka kwa wafu. 32 Mungu alisema, ‘Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo.’(K) Ni Mungu wa walio hai tu, hivyo hakika watu hawa hawakuwa wafu.”

33 Watu waliposikia hili, waliyashangaa mafundisho ya Yesu.

Amri ipi ni ya Muhimu Zaidi?

(Mk 12:28-34; Lk 10:25-28)

34 Mafarisayo waliposikia kuwa Yesu amewafanya Masadukayo waonekane wajinga nao wakaacha kumwuliza maswali. Kwa hiyo Mafarisayo wakafanya mkutano. 35 Ndipo mmoja wao, aliye mtaalamu wa Sheria ya Musa, akamwuliza Yesu swali ili kumjaribu. 36 Akasema, “Mwalimu, amri ipi katika sheria ni ya muhimu zaidi?”

37 Yesu akajibu, “‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote na akili yako yote.’(L) 38 Hii ndiyo amri ya kwanza na ya muhimu zaidi. 39 Na amri ya pili ni kama ya kwanza: ‘Mpende jirani yako[s] kama unavyojipenda wewe mwenyewe.’(M) 40 Sheria yote na maandiko ya manabii yamejengwa katika amri hizi mbili.”

Je, Masihi ni Mwana wa Daudi?

(Mk 12:35-37; Lk 20:41-44)

41 Hivyo Mafarisayo walipokuwa pamoja, Yesu aliwauliza swali. 42 Akasema, “Nini mawazo yenu juu ya Masihi? Je, ni mwana wa nani?” Mafarisayo wakajibu, “Masihi ni Mwana wa Daudi.”

43 Yesu akawaambia, “Sasa ni kwa nini Daudi anamwita ‘Bwana’? Daudi alikuwa anazungumza kwa nguvu ya Roho. Aliposema,

44 ‘Bwana Mungu alimwambia Bwana Mfalme wangu:
Keti karibu nami upande wangu wa kuume,
    na nitawaweka adui zako chini ya udhibiti wako.’[t](N)

45 Ikiwa Daudi anamwita Masihi ‘Bwana’. Inakuwaje Masihi ni mwana wa Daudi?”

46 Hakuna Farisayo aliyeweza kumjibu Yesu. Na baada ya siku hiyo, hakuna aliyekuwa jasiri kumwuliza maswali zaidi.

Yesu Awakosoa Viongozi wa Kidini

(Mk 12:38-40; Lk 11:37-52; 20:45-47)

23 Kisha Yesu akazungumza na watu pamoja na wafuasi wake, akasema, “Walimu wa sheria na Mafarisayo wana mamlaka ya kuwaambia Sheria ya Musa inasema nini. Hivyo mnapaswa kuwatii. Fanyeni kila wanachowaambia. Lakini maisha yao sio mfano mzuri wa kuufuata. Hawatendi wale wanayofundisha. Hutengeneza orodha ndefu ya kanuni na kujaribu kuwalazimisha watu kuzifuata. Lakini sheria hizi ni kama mizigo mizito ambayo watu hawawezi kuibeba, na viongozi hawa hawatazirahisisha kupunguza mzigo kwa watu.

Wao wanatenda mambo mema tu ili waonwe na watu wengine. Hufanya visanduku vidogo vya Maandiko[u] wanavyovaa kuwa vikubwa zaidi. Hufanya mashada ya urembo[v] kwenye mavazi yao ya nje kuwa marefu zaidi ili waonwe na watu. Watu hawa wanapenda kukaa sehemu za heshima kwenye sherehe na kwenye viti muhimu zaidi katika masinagogi. Wanapenda kuitwa ‘Mwalimu’ Na kusalimiwa kwa heshima na watu kwenye masoko.

Ninyi nyote ni ndugu, dada na kaka kwa sababu mnaye mwalimu mmoja tu. Hivyo msikubali kuitwa ‘Mwalimu’. Nanyi msimwite mtu yeyote duniani ‘Baba’, maana mnaye Baba mmoja tu, naye yuko mbinguni. 10 Msikubali kuitwa ‘Mwalimu’, kwa sababu mnaye Mwalimu mmoja tu, naye ni Masihi. 11 Kila atakayetumika kama mtumishi ndiyo mkuu zaidi kati yenu. 12 Wanaojifanya kuwa bora kuliko wengine watanyenyekezwa kwa lazima. Lakini watu wanaojinyenyekeza wenyewe watafanywa kuwa wakuu.

13 Ole wenu[w] walimu wa sheria nanyi Mafarisayo! Ninyi ni wanafiki! Mnawafungia watu njia ya kuingia katika ufalme wa Mungu, kwa kuwa ninyi wenyewe hamwingii na mnawazuia wale wanaojaribu kuingia. 14 [x]

15 Ole wenu walimu wa sheria nanyi Mafarisayo! Ninyi ni wanafiki. Mnasafiri kuvuka bahari na nchi nyingine ili kumtafuta mtu mmoja atakayefuata njia zenu. Mnapompata mtu huyo, mnamfanya astahili maradufu kwenda Jehanamu kama ninyi mlivyo!

16 Ole wenu walimu wa sheria nanyi Mafarisayo! Mnawaongoza watu lakini ninyi wenyewe ni wasiyeona. Mnasema, ‘Mtu yeyote akiweka kiapo au nadhiri kwa jina la Hekalu, haimaanishi kitu. Lakini yeyote atakayeweka kiapo kwa kutumia dhahabu iliyo Hekaluni lazima atimize nadhiri au kiapo hicho.’ 17 Ninyi ni wasiyeona mlio wajinga! Hamwoni kuwa Hekalu ni kuu kuliko dhahabu iliyo ndani yake? Hekalu ndilo huifanya dhahabu kuwa takatifu!

18 Na mnasema, ‘Mtu yeyote akitumia madhabahu kuweka nadhiri au kiapo, haina maana yeyote. Lakini kila anayetumia sadaka iliyo kwenye madhabahu na kuapa au kuweka nadhiri, lazima atimize nadhiri au kiapo hicho.’ 19 Ninyi ni wasiyeona! Hamwoni kuwa madhabahu ni kuu kuliko sadaka yo yote iliyo juu yake? Madhabahu ndiyo inaifanya sadaka kuwa takatifu! 20 Kila anayeitumia madhabahu kuapa au kuweka nadhiri ni dhahiri anatumia madhabahu na kila kitu kilicho juu yake. 21 Na kila anayetumia Hekalu kuapa au kuweka nadhiri kwa hakika analitumia Hekalu na Mungu, anayeishi ndani humo. 22 Kila anayetumia mbingu kuapa au kuweka nadhiri anakitumia kiti cha enzi cha Mungu na yule aketiye juu yake.

23 Ole wenu walimu wa sheria nanyi Mafarisayo! Ninyi ni wanafiki! Mnampa Mungu sehemu ya kumi ya chakula mnachopata,[y] hata mnanaa, binzari na jira.[z] Lakini hamtii mambo ya muhimu katika mafundisho ya sheria; kuishi kwa haki, kuwa wenye huruma, na kuwa waaminifu. Haya ndiyo mambo mnayopaswa kufanya. Na mwendelee pia kufanya mambo hayo mengine. 24 Mnawaongoza watu lakini ninyi wenyewe ni wasiyeona![aa] Ninyi ni kama mtu anayemtoa nzi katika kinywa chake na kisha anammeza ngamia!

25 Ole wenu walimu wa sheria nanyi Mafarisayo! Ninyi ni wanafiki! Mnaosha vikombe na sahani zenu kwa nje. Lakini ndani yake vimejaa vitu mlivyopata kwa kuwadang'anya wengine na kujifurahisha ninyi wenyewe. 26 Mafarisayo, ninyi ni wasiyeona! Safisheni kwanza vikombe kwa ndani ili viwe safi. Ndipo vikombe hivyo vitakuwa safi hata kwa nje.

27 Ole wenu walimu wa sheria na ninyi Mafarisayo! Ninyi ni wanafiki! Ninyi ni kama makaburi yaliyopakwa rangi nyeupe, lakini ndani yake yamejaa mifupa ya wafu na kila aina ya uchafu. 28 Ndivyo ilivyo hata kwenu. Watu wanawatazama na kudhani kuwa ninyi ni wenye haki, lakini mmejaa unafiki na uovu ndani yenu.

29 Ole wenu walimu wa sheria na Mafarisayo! Ninyi ni wanafiki! Mnajenga makaburi ya manabii, na kuyaheshimu makaburi ya wenye haki waliouawa. 30 Na mnasema, ‘Ikiwa tungeishi nyakati za mababu zetu, tusingewasaidia kuwaua manabii hawa.’ 31 Hivyo mnathibitisha kuwa ninyi ni uzao wa wale waliowaua manabii. 32 Na mtaimalizia dhambi waliyoianza mababu zenu!

33 Enyi nyoka! Ninyi mlio wa uzao wa nyoka wenye sumu kali! Hamtaikwepa adhabu. Mtahukumiwa na kutupwa Jehanamu! 34 Hivyo ninawaambia: Ninawatuma manabii na walimu wenye hekima na wanaojua Maandiko. Lakini mtawaua, mtawatundika baadhi yao kwenye misalaba na kuwapiga wengine katika masinagogi yenu. Mtawafukuza kutoka katika mji mmoja hadi mwingine.

35 Hivyo mtakuwa na hatia kutokana vifo vyote vya watu wema wote waliouawa duniani. Mtakuwa na hatia kwa kumwua mtu wa haki Habili, na mtakuwa na hatia kwa kuuawa kwa Zakaria[ab] mwana wa Barakia mliyemwua kati ya Hekalu na madhabahu. Mtakuwa na hatia ya kuwaua watu wote wema walioishi kati ya wakati wa Habili mpaka wakati wa Zakaria. 36 Niaminini ninapowaambia kuwa mambo haya yote yatawapata ninyi watu mnaoishi sasa.

Yesu Awaonya Watu wa Yerusalemu

(Lk 13:34-35)

37 Ee Yerusalemu, Yerusalemu! Unayewaua manabii. Unawapiga kwa mawe wale ambao Mungu amewatuma kwako. Mara nyingi nimetaka kuwasaidia watu wako. Nimetaka kuwakusanya watu wako kama kuku anavyowakusanya vifaranga wake chini ya mbawa zake. Lakini hukuniruhusu kufanya hivyo. 38 Sasa Hekalu lako litaachwa ukiwa kabisa. 39 Ninakwambia, hautaniona tena mpaka wakati utakaposema, ‘Karibu! Mungu ambariki yeye ajaye katika jina la Bwana.’”(O)

Yesu Aonya Kuhusu Wakati Ujao

(Mk 13:1-31; Lk 21:5-33)

24 Yesu alipokuwa anaondoka eneo la Hekalu, wanafunzi wake walimwendea na kumwonyesha majengo ya Hekalu. Akawauliza, “Mnayaona majengo haya? Ukweli ni kuwa, yataharibiwa. Kila jiwe litadondoshwa chini, hakuna jiwe litakaloachwa juu ya jiwe jingine.”

Baadaye, Yesu alipokuwa ameketi mahali fulani katika Mlima wa Mizeituni, Wafuasi wake walimwendea faraghani. Wakasema, “Twambie mambo haya yatatokea lini. Na nini kitatokea ili kutuandaa kwa ajili ya ujio wako na mwisho wa nyakati?”

Yesu akajibu, “Mjihadhari! Msimruhusu mtu yeyote awadanganye. Watu wengi watakuja na watatumia jina langu. Watasema, ‘Mimi ndiye Masihi.’ Na watawadanganya watu wengi. Mtasikia kuhusu vita vinanavyopiganwa na pia matetesi ya kuwapo vita vingine. Lakini msiogope. Mambo haya lazima yatokee na mwisho wenyewe hautafuata palepale. Mataifa yatapigana na mataifa mengine. Falme zitapigana na falme zingine. Utakuwepo wakati wa njaa ambapo watu watakosa chakula. Na kutakuwa matetemeko ya ardhi sehemu mbalimbali. Mambo haya ni mwanzo wa matatizo, kama uchungu wa kwanza mwanamke anapozaa.

Kisha mtakamatwa na kupelekwa kwa wenye mamlaka ili mhukumiwe na kuuawa. Watu wote katika ulimwengu watawachukia kwa sababu mnaniamini mimi. 10 Nyakati hizo watu wengi wataacha kuwa wafuasi wangu. Watasalitiana na kuchukiana. 11 Manabii wengi watatokea na kusababisha watu wengi kuamini mambo yasiyo ya kweli. 12 Kutakuwepo na uovu mwingi sana duniani kiasi kwamba upendo wa waaminio wengi utapoa. 13 Lakini yeyote yule atakayekuwa mwaminifu mpaka mwisho ataokolewa. 14 Na Habari Njema niliyoihubiri kuhusu Ufalme wa Mungu itahubiriwa ulimwenguni kote. Itatawanywa katika kila taifa. Kisha mwisho utakuja.

15 Nabii Danieli alizungumza kuhusu ‘jambo la kutisha litakalosababisha uharibifu.’[ac] Mtakapoliona jambo hili la kutisha limesimama patakatifu.” (Asomaye hili anapaswa kuelewa jambo hili linamaanisha nini.) 16 “Watu walio Uyahudi wakimbilie milimani. 17 Wakimbie pasipo kupoteza muda ili kuchukua kitu chochote. Wakiwa darini wasiteremke ili kuchukua kitu na kukitoa nje ya nyumba. 18 Wakiwa shambani wasirudi nyumbani kuchukua koti.

19 Itakuwa hali ngumu kwa wanawake wenye mimba na wenye watoto wachanga! 20 Ombeni isiwe majira ya baridi au isiwe siku ya Sabato mambo haya yatakapotokea na mkalazimika kukimbia, 21 kwa sababu utakuwa wakati wa dhiki kuu. Kutakuwepo na usumbufu mwingi sana kuliko ule uliowahi kutokea tangu mwanzo wa ulimwengu. Na hakuna jambo baya kama hilo litakalotokea tena.

22 Lakini Mungu amekwisha amua kuufupisha wakati huo. Ikiwa usingefupishwa, hakuna ambaye angeendelea kuishi. Lakini Mungu ataufupisha ili kuwasaidia watu aliowachagua.

23 Wakati huo watu wataweza kuwaambia, ‘Tazama, Masihi yuko kule!’ Au wakasema, ‘Ni yule!’ Msiwaamini. 24 Manabii wa uongo na masihi wa uongo watatokea na kufanya miujiza na maajabu[ad] makuu, ili ikiwezekana wawadanganye wateule. 25 Na sasa nimewatahadharisha kuhusu hili kabla halijatokea.

Yesu Atakaporudi Tena

(Mk 13:24-31; Lk 17:23-24,37; 21:25-32)

26 Inawezekana mtaambiwa, ‘Masihi yuko jangwani!’ Msiende jangwani kumtafuta. Mtu mwingine anaweza akasema, ‘Masihi yuko katika chumba kile!’ Msiamini. 27 Mwana wa Adamu atakapokuja, kila mtu atamwona. Itakuwa kama radi inavyowaka angani na kuonekana kila mahali. 28 Ni kama kutafuta mzoga: Mzoga hupatikana mahali ambapo tai wengi wamekusanyika.

29 Mara baada ya mateso ya siku hizo, mambo haya yatatokea:

‘Jua litakuwa jeusi,
    na mwezi hautatoa mwanga.
Nyota zitaanguka kutoka angani,
    na kila kitu kilicho angani
    kitatikiswa kutoka mahali pake.’[ae]

30 Kisha kutatokea ishara angani kuwa Mwana wa Adamu anakuja. Watu wote wa ulimwengu watajipiga kifuani wakiomboleza. Kila mtu atamwona Mwana wa Adamu akija katika mawingu ya angani akiwa na nguvu na utukufu mkuu. 31 Naye atatumia parapanda kuu kuwatuma malaika zake kila mahali duniani. Nao watawakusanya wateule wake kutoka mwisho mmoja wa mbingu hadi mwingine.

32 Jifunze kwa mtini: Matawi yake yanapokuwa ya kijani na laini na kuanza kutoa majani mapya, ndipo mnatambua kuwa majira ya joto yamekaribia. 33 Katika namna hiyo hiyo, mtakapoona mambo haya yote yakitokea, mtajua kuwa wakati[af] umekaribia wa kile kitakachotokea. 34 Ninawahakikishia kuwa mambo haya yote yatatokea wakati ambao baadhi ya watu wa nyakati hizi wakiwa bado hai. 35 Ulimwengu wote, dunia na anga vitaangamizwa, lakini maneno yangu yatadumu milele.

Mungu Peke Yake Ndiye Ajuaye Siku ya Kurudi kwa Mwana wa Adamu

(Mk 13:32,35; Lk 17:26-30,34-36)

36 Hakuna anayeijua siku wala wakati. Malaika wa mbinguni hawaijui hata Mwana hajui itakuwa lini. Baba peke yake ndiye anayejua.

37 Mwana wa Adamu atakapokuja, itakuwa kama ilivyokuwa nyakati za Nuhu. 38 Siku zile kabla ya gharika, watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuwatoa binti zao kuolewa mpaka siku ambayo Nuhu aliingia kwenye safina. 39 Hawakujua juu ya kilichokuwa kinaendelea mpaka mafuriko yalipowajia na kuwaangamiza wote.

Ndiyo itakavyokuwa Mwana wa Adamu atakapokuja. 40 Wanaume wawili watakuwa wakifanya kazi shambani, mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa. 41 Wanawake wawili watakuwa wanasaga nafaka pamoja, mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.

42 Hivyo iweni tayari daima. Hamjui siku ambayo Bwana wenu atarudi. 43 Mwenye nyumba angefanya nini ikiwa angejua wakati ambao mwizi atakuja? Mnajua angelikesha ili mwizi asivunje na kuingia. 44 Hivyo, ninyi nanyi iweni tayari. Mwana wa Adamu atakuja katika wakati msiomtarajia.

Watumishi Wema na Wabaya

(Mk 13:33-37; Lk 12:41-48)

45 Fikiria mtumishi aliyewekwa na bwana wake kuwapa chakula watumishi wake wengine katika muda uliopangwa. Ni kwa namna gani mtumishi huyo atajionyesha kuwa ni mwangalifu na mwaminifu? 46 Bwana wake atakaporudi na kumkuta anafanya kazi aliyompa, siku hiyo itakuwa siku ya furaha kwa mtumishi huyo. 47 Ninawaambia bila mashaka yoyote kuwa, bwana wake atamchagua mtumishi huyo awe msimamizi wa kila kitu anachomiliki yule Bwana.

48 Lakini nini kitatokea ikiwa mtumishi huyo ni mbaya na akadhani kuwa bwana wake hatarudi karibuni? 49 Ataanza kuwapiga watumishi wengine na kuanza kunywa na kula na walevi. 50 Ndipo bwana wake atakuja wakati asioutarajia, ambapo mtumishi hakujiandaa. 51 Bwana atamwadhibu mtumishi huyo na kumpeleka anakostahili kuwapo pamoja na watumishi wengine waliojifanya kuwa wema. Huko watalia na kusaga meno kwa maumivu.

Footnotes

  1. 18:11 Nakala zingine za Kiyunani zimeongeza mstari wa 11: “Mwana wa Adamu amekuja kuokoa waliopotea.” Tazama Lk 19:10.
  2. 18:15 kwako Nakala bora za kale za Kiyunani hazina neno “kwako”.
  3. 18:16 Ndipo watakuwepo … kile kilichotokea Tazama Kum 19:15.
  4. 18:18 mnapotoa msamaha … wa Mungu Kwa maana ya kawaida, “chochote mtakachokifunga hapa duniani kitakuwa kimefungwa mbinguni, na chochote mtakachokifungua kitakuwa kimefunguliwa mbinguni”.
  5. 18:22 saba mara sabini Ni idadi kubwa sana ya makosa, ikiwa na maana kuwa msamaha haupaswi kuwekewa kiwango.
  6. 18:24 tani 300 Kwa maana ya kawaida, “talanta 10,000”. Talanta 1 ilikuwa kama kilo 27 hadi 36 za sarafu za dhahabu, fedha, ama za shaba.
  7. 19:7 amri ya … ya talaka Tazama Kum 24:1.
  8. 19:12 wanaume hawaoi Kwa maana ya kawaida, “Maana wapo walio matowashi”.
  9. 19:19 jirani yako Mafundisho ya Yesu katika Lk 10:25-37 yanaonesha kwa uwazi kuwa hii ni pamoja na yeyote mwenye uhitaji.
  10. 20:15 wivu Kwa maana ya kawaida, “Jicho lako lina uovu.” Kwa maana ya akasema mtu aliye na wivu anaweza kuleta madhara kwa mtu kwa kumkodolea macho tu. Imani hii ipo katika ukanda wa Bahari ya Kati hapo kale na hata leo.
  11. 20:22 kikombe Kikombe ni ishara ya mateso. Yesu alitumia dhana ya kukinywea kikombe akimaanisha kuyakubali mateso ambayo angeyapata katika matukio ya kutisha ambayo yangetokea muda mfupi ujao. Pia katika mstari wa 23.
  12. 20:25 Watu Wasio Wayahudi Au “Mataifa”.
  13. 21:2 mwanapunda wake Kifungu katika Agano la Kale ambacho Mathayo ananukuu mstari wa 5 kinasema wazi kwamba punda wa pili ni mwanapunda.
  14. 21:5 watu wa Sayuni Kwa maana ya kawaida, “binti Sayuni”, ina maana mji wa Yerusalemu. Tazama Sayuni katika Orodha ya Maneno.
  15. 21:9 Msifuni Yaani, “Hosanna”, ambalo ni neno la Kiebrania lililotumika kumwomba msaada Mungu. Hapa, labda ilikuwa ni kelele ya shangwe iliyotumika kumsifu Mungu au Masihi wake. Pia mwishoni mwa mstari huu na pia katika mstari wa 15.
  16. 21:33 shimo kwa ajili ya kukamulia zabibu Au “shinikizo”.
  17. 21:44 Nakala zingine za Kiyunani hazina mstari wa 44.
  18. 22:24 nduguye aliyekufa Tazama Kum 25:5,6.
  19. 22:39 jirani yako Mafundisho ya Yesu katika Lk 10:25-37 yanaonesha kwa uwazi kuwa hii ni pamoja na yeyote mwenye uhitaji.
  20. 22:44 chini ya udhibiti wako Kwa maana ya kawaida, “kuweka chini ya miguu”.
  21. 23:5 visanduku vidogo vya Maandiko Visanduku vidogo vya ngozi vyenye Maandiko manne muhimu. Baadhi ya Wayahudi walivifunga visanduku hivi kwenye vipaji vya nyuso zao na mkono wa kushoto kuonesha kumpenda au uaminifu wao kwa Mungu na Neno lake. Mafarisayo wengi walitengeneza visanduku hivi vikubwa kuliko vya wengine kuonesha kuwa wao ni watu wa dini kuliko watu wengine.
  22. 23:5 mashada ya urembo Urembo uliotengenezwa kwa nyuzi za sufu au manyoya ya kondoo zinazotambaa mpaka chini kutoka pembe nne za vazi la kusalia au vazi la maombi lililovaliwa na Wayahudi. Urembo huu ulipaswa kuwa ukumbusho wa amri za Mungu (tazama Hes 15:38-41).
  23. 23:13 Ole wenu Ama Itakuwa vibaya kwenu enyi walimu wa sheria na Mafarisayo.
  24. 23:14 Nakala zingine za Kiyunani zimeongeza mstari wa 14: “Ole wenu walimu wa sheria nanyi Mafarisayo. Ninyi ni wanafiki. Mnawadanganya wajane na kuchukua nyumba zao. Kisha mnafanya maombi marefu ili watu wawaone. Mtapata adhabu mbaya zaidi.” Tazama Mk 12:40; Lk 20:47.
  25. 23:23 Mnampa Mungu … mnachopata Sheria ya Musa iliwataka Waisraeli kumtolea Mungu sehemu ya kumi ya mazao yao (tazama Law 27:30-32; Kum 26:12).
  26. 23:23 mnanaa, binzari na jira Haya ni mazao yaliyotolewa malipo ya fungu la kumi. Lakini sheria ya Musa halikujumuisha mazao madogo kama haya yaliyotajwa hapa. Bali Mafarisayo walikuwa wanatoa zaidi ili kuwa na uhakika kuwa hawavunji Sheria.
  27. 23:24 lakini ninyi wenyewe ni wasiyeona Hii ina maana kuwa “Mnajishughulisha kwa mambo madogo sana lakini mnatenda dhambi kubwa.”
  28. 23:35 Habili, Zakaria Katika Agano la Kale la Kiebrania, hawa ni watu wa kwanza na wa mwisho kuuawa. Tazama Mwa 4:8-11 na 2 Nya 24:20-25.
  29. 24:15 jambo … uharibifu Tazama Dan 9:27; 12:11 (pia Dan 11:31).
  30. 24:24 miujiza na maajabu Hapa ina maana ya kazi za ajabu zinazofanywa kwa kutumia nguvu za Shetani.
  31. 24:29 Tazama Isa 13:10; 34:4.
  32. 24:33 wakati Wakati ambao Yesu aliuzungumzia ni ule ambapo kitu muhimu kitatokea. Tazama Lk 21:31, pale ambapo Yesu anasema huu ni wakati wa Ufalme wa Mungu kutufikia.