Add parallel Print Page Options

Yesu Aingia Yerusalemu Kama Mfalme

(Mt 21:1-11; Lk 19:28-40; Yh 12:12-19)

11 Walipokaribia Yerusalemu walifika eneo la Bethfage na Bethania lililo karibu na Mlima wa Mizeituni, Yesu aliwatuma wanafunzi wake wawili, na kuwaagiza, “Mwende katika kijiji kilichopo ngambo yenu kule, na mara tu mtakapoingia ndani yake mtakuta mwana punda amefungwa mahali na ambaye hajawahi kupandwa na mtu yeyote. Mfungueni na kisha mumlete hapa. Na mtu yeyote akiwauliza, ‘Kwa nini mnafanya hivi?’ ninyi mseme, ‘Bwana anamhitaji, na atamrudisha kwenu mara moja.’”

Hivyo wakaondoka, nao wakamkuta mwana punda huyo amefungwa katika mtaa wa wazi karibu na mlango. Wakamfungua. Baadhi ya watu waliokuwa wamesimama karibu na mahali pale wakawaambia, “Je, kwa nini mnamfungua mwana punda huyo?” Wanafunzi wake wakawaeleza yale walioambiwa na Yesu wayaeleze, nao wakawaacha waende zao.

Kisha wakamleta mwana punda yule kwa Yesu na wakaweka mavazi yao ya ziada juu ya mwana punda, naye akampanda na kukaa juu yake. Watu wengi wakatandika makoti yao barabarani, na wengine wakatandika matawi waliyoyakata kwenye mashamba yaliyo jirani. Wote wale waliotangulia mbele na wale waliofuata walipiga kelele kwa shangwe,

“‘Msifuni[a] Mungu!
Mungu ambariki yeye
    anayekuja katika Jina la Bwana!’(A)
10 Mungu aubariki ufalme unaokuja,
    ufalme wa Daudi baba yetu!
    Msifuni Mungu juu mbinguni!”

11 Ndipo Yesu aliingia Yerusalemu na kwenda hadi kwenye eneo la Hekalu akizunguka na kutazama kila kitu kilichokuwepo mahali hapo. Kwa kuwa muda ulikuwa umekwenda sana, aliondoka kwenda Bethania akiwa na wanafunzi wake kumi na wawili.

Yesu Aulaani Mtini

(Mt 21:18-19)

12 Siku iliyofuata, walipokuwa wakiondoka Bethania, Yesu akawa na njaa. 13 Na kutokea mbali akauona mti wa mtini umefunikwa kwa matawi yake mengi, hivyo akausogelea karibu ili kuona kama atakuta tunda lolote juu yake. Lakini alipoufikia hakukuta tunda lolote isipokuwa matawi tu kwani hayakuwa majira ya mitini kuwepo katika mti. 14 Akauambia mtini ule, “Mtu yeyote asile matunda kutoka kwako kamwe milele!” Na wanafunzi wake waliyasikia hayo maneno.

Yesu Asafisha Eneo la Hekalu

(Mt 21:12-17; Lk 19:45-48; Yh 2:13-22)

15 Walipofika Yerusalemu waliingia katika viwanja vya Hekalu. Yesu akaanza kuwafukuza nje wale waliokuwa wakifanya biashara ya kuuza na kununua katika eneo la Hekalu. Akapindua meza za wabadilishaji wa fedha na viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa. 16 Pia hakumruhusu mtu yeyote abebe kitu chochote kukatiza eneo la Hekalu. 17 Yesu akaanza kuwafundisha na kuwaeleza, “Je, haikuandikwa katika Maandiko kwamba: ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ambapo watu wa mataifa yote wataleta maombi yao kwangu’?(B) Lakini ninyi mmeifanya kuwa ‘mahali pa wezi kujificha.’(C)

18 Na viongozi wa makuhani na walimu wa Sheria waliyasikia haya, na hivyo wakaanza kutafuta njia ya kumuua. Kwani walimwogopa, kwa sababu watu wote walikuwa wamestaajabishwa na mafundisho yake. 19 Ilipofika jioni, Yesu na wanafunzi wake waliondoka Yerusalemu.

Mtini na Imani, Maombi na Msamaha

(Mt 21:20-22)

20 Ilipofika asubuhi Yesu na wanafunzi wake walikuwa wakitembea pamoja na wakauona ule mti wa mtini umekauka kuanzia kwenye mizizi yake. 21 Petro akakumbuka yale Yesu aliyosema kwa mti huo na kumwambia, “Mwalimu, tazama! Mti ule wa mtini ulioulaani umenyauka kabisa.”

22 Yesu akawajibu, “Mnapaswa kuweka imani yenu kwa Mungu. 23 Nawaambia kweli: Yeyote atakayeuambia mlima huu, ‘Ng'oka na ukajitupe katika bahari’; kama asipokuwa na mashaka moyoni mwake, Lakini akaamini kuwa kile anachokisema kitatokea, huyo atatendewa hayo. 24 Kwa sababu hiyo nawaambia chochote mtakachoomba katika sala, muamini kwamba mmekipokea na haja mliyoiomba nayo itakuwa yenu, 25 Na wakati wowote mnaposimama kuomba, mkiwa na neno lolote kinyume na mtu mwingine, mmsamehe mtu huyo. Na Baba yenu aliye mbinguni naye atawasamehe ninyi dhambi zenu.” 26 [b]

Viongozi Wawa na Mashaka Kuhusu Mamlaka ya Yesu

(Mt 21:23-27; Lk 20:1-8)

27 Yesu na wanafunzi wake walirudi Yerusalemu. Na walipokuwa wakitembea ndani ya viwanja vya Hekalu, viongozi wa makuhani, walimu wa Sheria na wazee walimjia Yesu 28 na kumwuliza, “Kwa mamlaka gani unafanya vitu hivi? Nani alikupa mamlaka ya kuvifanya?”

29 Yesu akawaambia, “Nitawauliza swali, na mkinijibu, ndipo nitawaeleza kwa mamlaka gani ninafanya vitu hivi. 30 Je, ubatizo wa Yohana ulitoka mbinguni ama ulitoka kwa watu? Sasa mnijibu basi.”

31 Walijadiliana wao kwa wao wakisema, “Tukisema ‘ulitoka mbinguni’, atasema, ‘Kwa nini basi hamumuamini?’ 32 Lakini kama tukisema kuwa ubatizo wa Yohana ulitoka kwa wanadamu, watu watatukasirikia.” Viongozi waliwaogopa watu, kwani watu wote waliamini kuwa Yohana kweli alikuwa nabii.

33 Kwa hiyo wakamjibu Yesu, “Hatufahamu.”

Hivyo Yesu akawaambia, “Hata mimi sitawaambia ni kwa mamlaka gani nafanya mambo haya.”

Yesu Atoa Simulizi Kuhusu Shamba la Mzabibu

(Mt 21:33-46; Lk 20:9-19)

12 Yesu alianza kuongea nao kwa simulizi zenye mafumbo: “Mtu mmoja alipanda mizabibu shambani. Akajenga ukuta kuizunguka, akachimba shimo kwa ajili ya kukamulia mizabibu na kisha alijenga mnara. Baadaye alilikodisha kwa baadhi ya wakulima na akaenda safari nchi ya mbali.

Yalipotimia majira ya kuvuna, alimtuma mtumishi wake kwa wakulima wale, ili kukusanya sehemu yake ya matunda ya mzabibu. Lakini wakulima wale walimkamata mtumishi yule, wakampiga, na kumfukuza pasipo kumpa chochote. Kisha akamtuma mtumishi mwingine kwao. Huyu naye wakampiga kichwani na kumtendea mambo ya aibu. Yule mmiliki wa shamba la mzabibu akamtuma mtumishi mwingine, na wakulima wale wakamuua na yule pia. Baada ya hapo alituma wengi wengine. Wakulima wale waliwapiga baadhi yao na kuua wengine.

Hata hivyo mwenye shamba yule bado alikuwa na mmoja wa kumtuma, mwanaye mpendwa. Alimtuma akiwa mtu wa mwisho. Akasema, ‘nina hakika watamheshimu mwanangu!’

Lakini wakulima wale walisemezana wao kwa wao, ‘Huyu ndiye yule mrithi. Njooni tukamuue, na urithi utakuwa wetu!’ Kwa hiyo wakamchukua na kumuua, kisha wakautupa mwili wake nje ya shamba la mizabibu.

Je! Mnadhani mwenye kumiliki lile shamba la mizabibu atafanya nini? Atakuja na kuwaua wakulima wale, na kukodisha shamba lile kwa watu wengine. 10 Je! Hamjayasoma maandiko haya:

‘Jiwe ambalo wajenzi wamelikataa
    limekuwa jiwe kuu la msingi.
11 Hii imefanywa na Bwana
    na ni ajabu kubwa kwetu kuona!’”(D)

12 Na viongozi wa kidini wakatafuta njia ya kumkamata Yesu, lakini waliogopa lile kundi la watu. Kwani walijua ya kwamba Yesu alikuwa ameisema simulizi ile yenye mafumbo ili kuwapinga. Kwa hiyo viongozi wa kidini wakamwacha na kuondoka.

Yesu Ajibu Swali Lenye Mtego

(Mt 22:15-22; Lk 20:20-26)

13 Viongozi wa Kidini wakamtumia baadhi ya Mafarisayo na Maherode ili kumkamata kama akisema chochote kimakosa. 14 Wale waliotumwa walifika na kumwambia, “Mwalimu tunajua, kwamba wewe ni mkweli, na tena hujali yale watu wanayoyafikiri kuhusu wewe, kwa sababu wewe hubabaishwi na wadhifa wa mtu. Lakini unafundisha ukweli wa njia ya Mungu. Tuambie ni haki kulipa kodi kwa Kaisari ama la? Je, tulipe au tusilipe?”

15 Lakini Yesu aliutambua unafiki wao na akawaambia, “Kwa nini mnanijaribu hivi? Mniletee moja ya sarafu ya fedha mnazotumia ili niweze kuiangalia.” 16 Hivyo wakamletea sarafu, naye akawauliza, “Je, sura hii na jina hili ni la nani?” Nao wakamwambia, “Ya Kaisari.”

17 Ndipo Yesu alipowaambia, “Mpeni Kaisari vilivyo vyake, na Mungu mpeni vilivyo vyake.” Wakastaajabu sana kwa hayo.

Baadhi ya Masadukayo Wajaribu Kumtega Yesu

(Mt 22:23-33; Lk 20:27-40)

18 Kisha Masadukayo wakamjia. (Hawa ni wale wanaosema hakuna ufufuo wa wafu.) Wakamwuliza, 19 “Mwalimu, Musa alituandikia kwamba ikiwa kaka wa mtu atafariki na kumwacha mke asiye na watoto, Basi yule kaka lazima aoe mke yule wa nduguye na kuzaa naye watoto kwa ajili ya kaka yake aliyefariki. 20 Palikuwepo na ndugu wa kiume saba. Wa kwanza alioa mke, naye alikufa bila kuacha mtoto yeyote. 21 Wa pili naye akamwoa yule mke wa nduguye wa kwanza aliyeachwa naye akafa bila kuacha watoto wowote. Ndugu wa tatu pia alifanya vivyo hivyo. 22 Ndugu wote wale saba walimwoa yule mwanamke na wote hawakupata watoto. Mwisho wa yote, yule mwanamke pia akafariki, 23 Katika ufufuo, pale wafu watakapofufuka toka katika kifo, Je, yeye atakuwa mke wa nani? Kwani wote saba walikuwa naye kama mke wao.”

24 Yesu akawaambia, “Hakika hii ndiyo sababu mmekosa sana: Hamyajui Maandiko wala uwezo wa Mungu. 25 Kwa kuwa wafu wanapofufuka toka katika wafu, hawaoi wala kuolewa. Badala yake wanakuwa kama malaika walioko Mbinguni. 26 Lakini kuhusu kufufuka kwa wafu, Je, hamjasoma katika kitabu cha Musa katika sura ile ya kichaka kinachoungua? Pale ndipo Mungu alipomwambia Musa, ‘Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo.’(E) 27 Yeye si Mungu wa waliokufa, bali wa wale wanaoishi. Hivyo ninyi mmekosa sana.”

Amri ipi ni ya Muhimu Zaidi?

(Mt 22:34-40; Lk 10:25-28)

28 Mwalimu wa Sheria alifika naye aliwasikia wakijadiliana. Alipoona jinsi Yesu alivyowajibu vizuri sana, alimwuliza, “Je, amri ipi ni muhimu sana kuliko zote?”

29 Yesu akajibu, “Muhimu sana ni hii: ‘Sikiliza, Israeli, Bwana Mungu wetu ni mmoja. 30 Nawe unapaswa kumpenda Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa nafsi yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote.’(F) 31 Amri ya pili ni hii: ‘mpende jirani yako[c] kama unavyojipenda mwenyewe.’(G) Hakuna amri nyingine kubwa kuliko hizi.”

32 Na mwalimu wa Sheria akamwambia, “Umejibu vema kabisa mwalimu. Upo sahihi kusema kuwa Mungu ni mmoja, na hakuna mwingine ila yeye. 33 Ni muhimu zaidi kumpenda Mungu kwa moyo wako wote, kwa ufahamu wako wote, na kwa nguvu zako zote, na kumpenda jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe kuliko sadaka zote za kuteketezwa na matoleo tunayompa Mungu.”

34 Yesu alipoona kwamba yule mtu amejibu kwa busara, alimwambia, “Wewe hauko mbali na Ufalme wa Mungu.” Baada ya hapo hakuwepo mtu mwingine aliyediriki kumwuliza maswali mengine zaidi.

Je, Masihi ni Mwana wa Daudi?

(Mt 22:41-46; Lk 20:41-44)

35 Yesu alipokuwa akifundisha katika mabaraza ya Hekalu, alisema, “Inawezekana vipi walimu wa Sheria kusema kwamba Kristo ni mwana wa Daudi? 36 Daudi mwenyewe kwa kupitia Roho Mtakatifu alisema,

‘Bwana Mungu alimwambia Bwana Mfalme wangu:
Keti karibu nami upande wangu wa kuume,
    nami nitawaweka adui zako chini ya udhibiti wako.’[d](H)

37 Daudi anamwita Masihi ‘Bwana’. Itakuwaje tena Kristo awe yote Bwana na pia mwana wa Daudi?”

Hapo lilikuwepo kundi kubwa la watu liliokuwa likimsikiliza kwa furaha.

Yesu Anawakosoa Walimu wa Sheria

(Mt 23:6-7; Lk 11:43; 20:45-47)

38 Katika mafundisho yake alisema, “Jihadharini na walimu wa Sheria.” Wao wanapenda kutembea huko na huko katika mavazi yanayopendeza huku wakipenda kusalimiwa masokoni, 39 Hao wanapenda kukaa viti vya mbele katika masinagogi na kupewa sehemu muhimu zaidi za kukaa katika karamu za chakula. 40 Hawa huwadanganya wajane ili wazichukue nyumba zao na wanasali sala ndefu ili kujionesha kwa watu. Watu hawa watapata hukumu iliyo kubwa zaidi.

Mjane Aonesha Jinsi Ulivyo Utoaji wa Kweli

(Lk 21:1-4)

41 Yesu aliketi mahali kuvuka pale palipokuwepo na sanduku la matoleo, alitazama jinsi ambavyo watu walikuwa wakiweka sadaka zao sandukuni. Matajiri wengi waliweka fedha nyingi. 42 Kisha mjane maskini alikuja na kuweka sarafu mbili ndogo za shaba, ambazo zilikuwa na thamani ndogo sana.

43 Yesu aliwaita wanafunzi wake pamoja na kuwaambia, “Nawaambieni ukweli mjane huyu maskini ameweka sarafu mbili tu. Lakini ukweli ni kwamba ametoa zaidi ya matajiri wote wale.” 44 Kwa kuwa wote walitoa kile cha ziada walichokuwa nacho. Lakini yeye katika umasikini wake, aliweka yote aliyokuwa nayo. Na hiyo ilikuwa fedha yote aliyokuwa nayo kutumia wa maisha yake.

Yesu Aonya Kuhusu Wakati Ujao

(Mt 24:1-25; Lk 21:5-24)

13 Yesu alikuwa akiondoka katika eneo la Hekalu na moja ya wanafunzi wake akamwambia, “Mwalimu, tazama mawe haya yanavyopendeza na jinsi majengo haya yanavyopendeza!”

Yesu akamjibu, “Je, mnayaona majengo haya makubwa? Yote yatabomolewa. Kila jiwe litaporomoshwa hata chini. Hakuna jiwe lolote kati ya haya litakaloachwa mahali pake.”

Naye alipokuwa ameketi juu ya Mlima wa Mizeituni upande wa pili kuvuka Hekalu, Petro, Yakobo, Yohana na Andrea walimwuliza wakiwa faragha, “Haya tuambie, ni lini mambo haya yatakapotokea? Ni ishara gani itakayoonesha ya kwamba yote yanakaribia kutimizwa?”

Yesu akaanza kuwaeleza, “Muwe waangalifu mtu asije akawadanganya. Wengi watakuja huku wakilitumia Jina langu na kusema, ‘Mimi ndiye Masihi,’[e] nao watawadanganya wengi. Mtasikia juu ya vita vinavyopiganiwa na mtasikia habari juu ya vita vingine vinavyoanza. Hata hivyo msishtushwe. Mambo hayo lazima yatokee, kabla ule mwisho wenyewe kufika. Kwani taifa moja litapigana dhidi ya taifa lingine na ufalme mmoja utapigana dhidi ya ufalme mwingine. Yatatokea matetemeko mengi mahali pengi na kutakuwepo na njaa kali sehemu nyingi. Mambo haya yatakuwa ni mwanzo tu wa uchungu wa mama mzazi kabla ya mtoto kuzaliwa.

Hivyo mjihadhari! Wapo watu watakaowakamata na kuwapeleka mkahukumiwe kwa kuwa ninyi ni wanafunzi wangu. Watawapiga katika masinagogi yao. Mtalazimishwa kusimama mbele ya wafalme na watawala. Nanyi mtawaeleza habari zangu. 10 Kabla ya mwisho kufika, ni lazima kwanza habari Njema itangazwe kwa mataifa yote. 11 Wakati wowote watakapowakamata na kuwashitaki, msiwe na wasiwasi kujiandaa kwa yale mtakayoyasema, lakini myaseme yale mtakayopewa saa ile ile, kwa kuwa si ninyi mnaozungumza; bali, ni Roho Mtakatifu anayezungumza.

12 Na ndugu atamsaliti nduguye hata kuuawa, na baba atamsaliti mwanawe. Watoto nao watawaasi wazazi wao na hata kuwatoa wauawe. 13 Nanyi mtachukiwa na wote kwa sababu yangu. Lakini yeyote atakayevumilia hadi mwisho ataokoka.

14 Wakati mtakapoliona chukizo la uharibifu[f] likisimama mahali pasipotakiwa lisimame.” (Msomaji aelewe hii ina maana gani?[g]) “Kisha wale waliopo katika Uyahudi wakimbilie milimani. 15 Ikiwa mtu yupo katika paa la nyumba yake, asishuke chini na kuingia nyumbani mwake kuchukua kitu chochote. 16 Ikiwa mtu yupo shambani asirudi kuchukua vazi lake.

17 Wakati huo itakuwa hatari kwa wanawake walio waja wazito na wale wenye watoto wachanga. 18 Ombeni kwamba haya yasitokee wakati wa majira ya baridi. 19 Kwa kuwa taabu itakayotokea katika siku hizo itakuwa ile ambayo haijawahi kutokea tangu mwanzo pale Mungu alipoumba dunia hadi sasa. Na hakitatokea tena kitu kama hicho. 20 Kama Bwana asingelifupisha muda huo, hakuna ambaye angenusurika. Lakini yeye amefupisha siku hizo kwa ajili ya watu wale aliowateuwa.

21 Ikiwa mtu atawaambia, ‘Tazama, Kristo ni huyu hapa!’ ama ‘Ni yule pale!’ Usiliamini hilo. 22 Kwani Makristo wa uongo na manabii wa uongo watatokea, nao watafanya ishara na miujiza kuwadanganya watu ikiwezekana hata wale ambao Mungu amewachagua. 23 Kwa hiyo mjihadhari nimewaonya juu ya mambo haya kabla hayajatokea.

Yesu Atakaporudi Tena

(Mt 24:29-51; Lk 21:25-36; 19:12-13,40)

24 Lakini katika siku hizo, baada ya kipindi cha dhiki,

‘Jua litatiwa giza,
    mwezi hautatoa mwanga,
25 nyota zitaanguka kutoka angani,
    na mbingu yote itatikisika.’[h]

26 Ndipo watu watakapomwona Mwana wa Adamu akija mawinguni pamoja na nguvu kubwa na utukufu. 27 Baada ya hapo Mwana wa Adamu atawatuma malaika, na atawakusanya wateule wake kutoka kila upande wa dunia.

28 Jifunzeni somo hili kutoka katika mti wa mtini: Matawi yake yanaponyauka na kubeba majani, unajua kwamba kiangazi kimekaribia. 29 Vivyo hivyo, unapoona mambo haya yanaanza kutokea unajua kwamba muda umekaribia na umeshafika mlangoni. 30 Ninawaambieni ukweli: Kizazi hiki hakitapita kabla ya mambo haya yote hayajatokea. 31 Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.

32 Hakuna anayejua wakiwemo malaika wa mbinguni ama Mwana bali baba peke yake lini siku au saa ile itakapowadia. 33 Mjihadhari; Kesheni! Kwani hamjui lini muda huo utafika.

34 Ni kama mtu anayeenda safarini na kabla ya kuondoka huiacha nyumba yake mikononi mwa watumishi wake. Kabla ya kuiacha nyumba yake anawaweka watumishi wake kusimamia kila mmoja akiwa na kazi yake maalumu. Kisha atamwamuru mlinzi mlangoni awe macho. 35 Vivyo hivyo ni lazima mjihadhari, kwa sababu hamjui ni muda gani mkuu wa nyumba atakuja; hamjui kama atakuja jioni, usiku wa manane, wakati jogoo anawika, au alfajiri. 36 Ikiwa atakuja ghafula, basi asiwakute mmelala. 37 Ninachowaambia, namwambia kila mmoja: ‘muwe tayari.’”

Mpango wa Kumwua Yesu

(Mt 26:1-5; Lk 22:1-2; Yh 11:45-53)

14 Ilikuwa yapata siku mbili kabla ya Sikukuu ya Pasaka na Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu. Wakuu wa makuhani na walimu wa Sheria walikuwa wakitafuta njia, kwa ujanja fulani, ya kumkamata na kumuua Yesu. Kwani walikuwa wakisema “tusifanye hivi wakati wa sherehe, ama sivyo watu watafanya fujo.”

Mwanamke Ampa Yesu Heshima

(Mt 26:6-13; Yh 12:1-8)

Yesu alikuwa Bethania, katika nyumba ya Simoni mwenye ugonjwa mbaya sana wa ngozi. Wakati ameketi mezani mwanamke mmoja alimwijia. Naye alikuwa na gudulia la mawe lililojaa manukato ya bei ghali yaliyotengenezwa kwa nardo safi. Mwanamke huyo alilifungua gudulia lile kwa kulivunja na kumwagia Yesu manukato kichwani mwake.

Baadhi ya watu waliokuwa pale walikasirika na kulalamika miongoni mwao, “Kwa nini kuwepo na ufujaji wa manukato namna hii? Gharama yake ni sawa na mshahara wa mwaka[i] mzima. Manukato haya yangeweza kuuzwa na fedha hiyo kupewa walio maskini.” Kisha wakamkosoa yule mwanamke kwa hasira kwa jambo alilolifanya.

“Lakini Yesu alisema mwacheni peke yake. Kwa nini mnamsumbua? Yeye amenifanyia kitendo chema. Kwani siku zote mnao maskini pamoja nanyi na mnaweza kuwasaidia wakati wowote mnaopenda. Lakini hamtakuwa pamoja nami siku zote. Yeye amefanya kile alichokiweza kufanya. Ameumwagia manukato mwili wangu kabla ya wakati kuuandaa kwa ajili ya maziko. Ninawaambia kweli: Popote injili itakapohubiriwa ulimwenguni, kile alichokifanya kitasimuliwa kwa kumkumbuka.”

Yuda Akubali Kuwasaidia Adui wa Yesu

(Mt 26:14-16; Lk 22:3-6)

10 Kisha Yuda Iskarioti, mmoja wa wale kumi na mbili, aliwaendea viongozi wa makuhani ili kumsaliti Yesu kwao. 11 Nao walifurahi kusikia hivyo, na wakaahidi kumpa fedha. Kwa hiyo Yuda akaanza kutafuta wakati unaofaa wa kumsaliti.

Karamu ya Pasaka

(Mt 26:17-25; Lk 22:7-14,21-23; Yh 13:21-30)

12 Siku ya kwanza ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, ambapo kila mara mwana kondoo alitolewa sadaka kwa ajili ya Pasaka. Wanafunzi wa Yesu wakamwendea na kumwuliza, “Ni wapi unapotaka tuende kukuandalia ili uweze kuila Karamu ya Pasaka?”

13 Hivyo Yesu aliwatuma wanafunzi wake wawili, naye akawaeleza, “ingieni mjini, na mtakutana na mtu mmoja aliyebeba gudulia la maji. Mfuateni, 14 popote pale atakapoingia, mwambieni mwenye nyumba ile, ‘mwalimu anasema, utuonyeshe chumba ambacho yeye na wanafunzi wake wanaweza kuila Karamu ya Pasaka.’ 15 Naye atawaonesha chumba kikubwa ghorofani, klichoandaliwa tayari kwa ajili yetu. Basi mtuandalie chakula pale.”

16 Wanafunzi wa Yesu waliondoka na kuelekea mjini. Huko walikuta kila kitu kama vile Yesu alivyowaeleza Hivyo, waliandaa mlo wa Pasaka.

17 Wakati wa jioni Yesu alienda pamoja na wanafunzi wake kumi na mbili katika nyumba ile. 18 Wote walipokuwa wameketi mezani wakila, Yesu akasema, “Mniamini ninapowambia kwamba mmoja wenu, yule anayekula nami sasa atanitoa kwa maadui zangu.”

19 Wanafunzi walihuzunika sana kusikia jambo hili. Kila mmoja akamwambia Yesu, “Hakika siyo mimi?”

20 Akawaambia, “Ni mmoja wa wale kumi na mbili; na ni yule atakayechovya mkate katika bakuli pamoja nami. 21 Mwana wa Adamu atakiendea kifo chake kama ilivyoandikwa juu yake. Lakini itakuwa ya kutisha namna gani kwa mtu yule ambaye kupitia yeye Mwana wa Adamu anasalitiwa. Itakuwa bora mtu huyu asingelikuwa amezaliwa.”

Chakula cha Bwana

(Mt 26:26-30; Lk 22:15-20; 1 Kor 11:23-25)

22 Na walipokuwa wakila Yesu aliuchukua mkate, akamshukuru Mungu kwa huo. Akamega vipande, akawapa wanafunzi wake, na kusema, “Chukueni na mle mkate huu. Ni mwili wangu.”

23 Kisha akakichukua kikombe chenye divai, akamshukuru Mungu kwa hicho, akawapa. Wote wakanywa toka kile kikombe. 24 Kisha akasema, “Kinywaji hiki ni damu yangu ambayo kwayo Mungu anafanya agano na watu wake. Damu yangu inamwagika kwa manufaa ya watu wengi. 25 Ninawaambia kweli sitakunywa diva tena mpaka siku ile nitakapokunywa divai mpya katika Ufalme wa Mungu.”

26 Na wao wakaimba mwimbo wa sifa na kutoka na kuelekea kwenye Mlima wa Miti ya Mizeituni.

Yesu Asema Wafuasi Wake Watamwacha

(Mt 26:31-35; Lk 22:31-34; Yh 13:36-38)

27 Yesu akawaambia, “Nyote mtaniacha, kwani imeandikwa,

‘Nitamuua mchungaji,
    na kondoo watatawanyika.’(I)

28 Lakini baada ya kuuawa, nitafufuka kutoka kwa wafu. Kisha nitaenda Galilaya. Nitakuwa pale kabla ninyi hamjafika.”

29 Lakini Petro akamwambia, “Hata kama wengine wote watapoteza imani yao, mimi sitapoteza imani yangu.”

30 Ndipo Yesu akamjibu kusema, “Ukweli ni kwamba, usiku wa leo utasema kuwa hunijui. Utasema hivyo mara tatu kabla ya jogoo kuwika mara mbili.”

31 Petro akasema kwa kusisitiza zaidi, “Hata kama itanipasa kufa nawe, sitasema kuwa sikujui.” Na wengine wakasema hivyo.

Yesu Aomba Akiwa Peke Yake

(Mt 26:36-46; Lk 22:39-46)

32 Kisha wakafika mahali palipoitwa Gethsemane. Hapo Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kaeni hapa wakati ninaomba.” 33 Naye Yesu akamchukua Petro, Yakobo, na Yohana pamoja naye, naye akaanza kusumbuka sana. 34 Akawaambia, “Nina huzuni sana na ninafikiri inaweza kuniua. Kaeni hapa, na mjihadhari.”

35 Akiendelea mbele kidogo, alianguka chini, na akaomba ikiwezekana angeiepuka saa ya mateso. 36 Akasema, “Aba,[j] yaani Baba, vyote vinawezekana kwako wewe. Hebu kiondoe kikombe[k] hiki kutoka kwangu, Lakini usifanye kama ninavyopenda mimi, lakini kama unavyopenda wewe.”

37 Kisha Yesu akaja na kuwakuta wamelala, na akamwuliza Petro, “Simoni, je umelala? Je, hukuweza kukaa macho kwa muda wa saa moja tu? 38 Kaeni macho na kuomba, ili msije mkaingia majaribuni. Roho inataka lakini mwili ni dhaifu.”

39 Yesu akaondoka kwenda kuomba tena, akilisema jambo lile lile. 40 Kisha akarudi tena na kuwakuta wamelala, kwani macho yao yalikuwa yamechoka. Wao hawakujua la kusema kwake.

41 Alirudi mara ya tatu na kuwaambia, “Je, bado mmelala na kupumzika? Imetosha! Saa imefika. Mwana wa Adamu atasalitiwa mikononi mwa watenda dhambi. 42 Amkeni! Twendeni! Tazama! Yule atakayenisaliti amekaribia.”

Yesu Akamatwa

(Mt 26:47-56; Lk 22:47-53; Yh 18:3-12)

43 Mara moja, wakati Yesu akali akizungumza, Yuda, mmoja wa wale kumi na mbili, alitokea. Pamoja naye walikuwa kundi kubwa la watu waliokuwa na majambia na marungu wakitoka kwa viongozi wa makuhani, walimu wa sheria na wazee.

44 Msaliti alikuwa tayari amewapa ishara: “Yule ambaye nitambusu ndiye mwenyewe. Mkamateni, mlindeni na muwe waangalifu mnapomwondoa.” 45 Mara tu Yuda alipowasili, alimwendea Yesu. Alipomkaribia alisema, “Mwalimu!” Kisha akambusu. 46 Ndipo walipomkamata na kumshikilia. 47 Mmoja wa wale waliosimama naye karibu akautoa upanga wake alani, akampiga nao mtumishi wa kuhani mkuu na kulikata sikio lake.

48 Kisha Yesu akawaambia, “Je, mlikuja kunikamata kwa upanga na marungu, kama vile mimi nimekuwa jambazi? 49 Kila siku nilikuwa nanyi, nikifundisha Hekaluni na hamkujaribu kunikamata wakati huo. Lakini Maandiko lazima yatimie.” 50 Wafuasi wake wote walimwacha na kumkimbia.

51 Miongoni mwa watu waliomfuata Yesu alikuwa kijana mmoja aliyevaa kipande cha nguo. Watu walipotaka kumkamata 52 alikiacha kile kipande cha nguo mikononi mwao na kukimbia akiwa uchi.

Yesu Akiwa Mbele ya Viongozi wa Kidini

(Mt 26:57-68; Lk 22:54-55,63-71; Yh 18:13-14,19-24)

53 Nao wakamwongoza Yesu kumpeleka kwa kuhani mkuu, na viongozi wote wa makuhani, wazee, na walimu wa Sheria walikutanika. 54 Petro akamfuata Yesu kwa mbali kidogo hadi ndani ya baraza la nyumba ya kuhani mkuu. Petro alikuwa ameketi na wale walinzi akijipasha joto na moto walioukoka.

55 Viongozi wa makuhani na Baraza lote la Wayahudi walikuwa wakitafuta ushahidi dhidi ya Yesu wa kuweza kumhukumu kifo, lakini hawakupata kitu chochote. 56 Watu wengi walikuja na kutoa ushahidi wa uongo dhidi yake, lakini wote walisema vitu tofauti. Ushahidi wao ulipingana.

57 Kisha wengine walisimama na kushuhudia kinyume chake kwa uongo, wakisema, 58 “Tulimsikia mtu huyu[l] akisema, ‘Nitaliharibu Hekalu hili lililotengenezwa kwa mikono ya wanadamu, na kwa siku tatu nitajenga lingine ambalo halikujengwa kwa mikono.’” 59 Lakini hata katika ushahidi wao huu hawakukubaliana.

60 Kisha kuhani mkuu akasimama mbele yao na akamwuliza Yesu, “Je, wewe hutajibu? Nini ushahidi huu ambao watu wanaleta dhidi yako?” 61 Lakini Yesu alinyamaza kimya na hakutoa jibu lolote.

Kwa mara nyingine kuhani mkuu akamwuliza, “Je, wewe ni Kristo, Mwana wa Mungu anayesifiwa?”

62 Yesu akasema, “Mimi ndiye. Nanyi mtamwona Mwana wa Adamu akiketi mkono wa kuume wa Mungu Mwenye uweza wote akija pamoja na mawingu ya mbinguni.”[m]

63 Kuhani mkuu alichana mavazi yake na kusema, “Tuna haja gani ya kuleta mashahidi zaidi? 64 Ninyi wote mmesikia akimtolea Mungu matusi.”

Wote walimhukumu na kumwona kwa anastahili kifo. 65 Na wengine walianza kutema mate, na kufunika uso wake, na kumpiga, na kumwambia, “Uwe nabii na utuambie nani aliyekupiga.” Kisha wale walinzi walimchukua na kuendelea kumpiga.

Petro Amkana Yesu

(Mt 26:69-75; Lk 22:56-62; Yh 18:15-18,25-27)

66 Wakati Petro alipokuwa bado barazani, mtumishi wa kike wa kuhani mkuu alifika pale. 67 Alipomwona Petro akijipasha moto, alimkazia macho na kumwambia, “Wewe pia ulikuwa pamoja na Yesu, Mnazareti.”

68 Lakini Petro alisema, “Hii si kweli, mie sifahamu wala kuelewa kile unachokisema.” Baada ya hapo Petro alitoka na kwenda barazani na hapo hapo jogoo akawika.

69 Yule mtumishi wa kike alipomwona alirudia tena kuwaeleza wale waliokuwa wamesimama pale, “Mtu huyu ni mmoja wao!” 70 Kwa mara nyingine tena Petro alikataa.

Baada ya muda mfupi wale waliokuwa wamesimama pale wakarudia tena kumwambia Petro, “Hakika wewe ni mmoja wao, kwa sababu wewe pia ni Mgalilaya.”

71 Petro akaanza kutoa maneno makali na kusema, “Naapa kwa Mungu, simjui mtu huyu mnayemzungumzia!”

72 Mara jogoo akawika kwa mara ya pili, na Petro akakumbuka lile neno la Yesu alilomwambia: “Kabla kogoo hajawika mara ya pili utanikana mara tatu.” Naye akavunjika moyo na kuanza kulia.

Gavana Pilato Amhoji Yesu

(Mt 27:1-2,11-14; Lk 23:1-5; Yh 18:28-38)

15 Asubuhi na mapema, Mara tu ilipofika asubuhi viongozi wa makuhani, viongozi wazee wa Kiyahudi, walimu wa sheria, na baraza kuu lote la Wayahudi liliamua jambo la kufanya kwa Yesu. Walimfunga Yesu, wakamwondoa pale, na wakamkabidhi kwa Pilato.

Na Pilato akamwuliza: “Je, wewe ni Mfalme wa Wayahudi?”

Yesu akajibu “Hayo ni maneno yako mwenyewe.”

Na viongozi wa makuhani wakamshitaki Yesu kwa mambo mengi. Kwa hiyo Pilato akamwuliza Yesu swali lingine. Akasema, “Wewe hata kujibu hujibu? Angalia una mashitaka mengi wanayokuletea!”

Lakini Yesu hakujibu kitu chochote, na Pilato akastaajabu.

Pilato Ajaribu Kumwachia Huru Yesu

(Mt 27:15-31; Lk 23:13-25; Yh 18:39-19:16)

Kila mwaka wakati wa Sherehe ya Pasaka Pilato atamweka huru mfungwa mmoja atakayechaguliwa na watu. Mtu mmoja aliyeitwa Baraba alikuwa gerezani amefungwa pamoja na waasi. Watu hawa walifanya mauaji wakati wa fujo.

Watu walikuja Kwa Pilato na kumwomba amweke huru mfungwa kama alivyofanya siku zote. Yeye akawauliza, “Je, mnataka nimwache huru mfalme wa Wayahudi?” 10 Pilato alilisema hili kwa sababu alijua kuwa viongozi wa makuhani walimleta kwake kwa ajili ya wivu tu. 11 Lakini wale viongozi wa makuhani walimchochea amwache Baraba badala ya Yesu.

12 Lakini Pilato akawauliza watu tena, “Kwa hiyo nifanye nini na mtu huyu mnayemwita Mfalme wa Wayahudi?”

13 Wakapiga kelele “Muue kwenye msalaba.”

14 Lakini Pilato akawauliza, “Kwa nini? Je, amefanya kosa gani?”

Lakini wote wakapiga kelele zaidi, “Muue kwenye msalaba!”

15 Pilato alitaka kuwaridhisha watu, kwa hiyo alimweka huru Baraba kwa ajili yao. Akaamuru maaskari wampige Yesu viboko na kisha akamtoa kwao ili akauawe kwenye msalaba.

16 Maaskari wakamwongoza Yesu hadi ndani ya baraza la jumba la gavana (lililojulikana kama Praitorio). Huko wakakiita pamoja kikosi cha maaskari. 17 Wakamvalisha Yesu joho la zambarau na wakafuma taji ya miiba na kumvisha kichwani. 18 Kisha wakaanza kumpigia saluti wakisema: “Heshima kwa Mfalme wa Wayahudi!” 19 Wakampiga tena na tena kichwani kwa fimbo na wakamtemea mate. Kisha wakapiga magoti mbele yake na kujifanya wanampa heshima kama mfalme. 20 Walipomaliza kumkejeli walimvua joho lile la kizambarau, na kumvisha mavazi yake mwenyewe. Baada ya hapo wakamtoa nje ili waweze kumsulubisha.

Yesu Awambwa Msalabani

(Mt 27:32-44; Lk 23:26-43; Yh 19:17-19)

21 Wakiwa njiani walikutana na mtu kutoka Kirenio aliyeitwa Simoni, akitoka vijijini kuja mjini. Yeye alikuwa baba yake Iskanda na Rufo. Wale wanajeshi wakamlazimisha kuubeba msalaba wa Yesu. 22 Wakamleta Yesu hadi mahali palipoitwa Golgotha (Yaani Mahali pa Fuvu la Kichwa) 23 Nao wakampa divai iliyochanganywa na siki, lakini yeye alikataa kuinywa. 24 Pale wakampigilia kwa misumari msalabani. Wakagawana mavazi yake miongoni mwao nao wakayapigia kura ili kuona kila mtu atapata nini.

25 Ilikuwa saa tatu asubuhi walipompigilia kwa misumari msalabani. 26 Ilani ya mashtaka dhidi yake ilikuwa na maandishi haya juu yake: “Mfalme wa Wayahudi.” 27 Hapo waliwapigilia msalabani wahalifu wawili pembeni mwa Yesu, mmoja kushoto kwake na mwingine kuume kwake. 28 [n]

29 Watu waliopita mahali pale walimtukana. Walitikisa vichwa vyao na kusema, “Haya! Wewe ndiye yule awezaye kuliharibu hekalu na kulijenga tena kwa siku tatu. 30 Hebu shuka msalabani na uyaokoe maisha yako.”

31 Kwa njia hiyo hiyo, viongozi wa makuhani na walimu wa Sheria walimfanyia dhihaka na wakasema wao kwa wao, “Aliwaokoa wengine lakini hawezi kujiokoa mwenyewe! 32 Ikiwa yeye kweli ni Masihi Mfalme wa Israeli, iinampasa ashuke sasa toka msalabani, tukiliona hilo nasi tutamwamini.” Wale wahalifu waliokuwa katika misalaba ile mingine pembeni waliosulubiwa pamoja naye nao walimtukana.

Yesu Afariki

(Mt 27:45-56; Lk 23:44-49; Yh 19:28-30)

33 Ilipofika saa sita mchana giza ilifunika nchi yote. Giza liliendelea hadi saa tisa. 34 Mnamo saa tisa Yesu alipiga kelele kwa sauti na kusema, “Eloi, Eloi, lema sabakthani?” maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”(J)

35 Na baadhi ya wale waliokuwa wamesimama karibu waliposikia hivi, walisema, “sikilizeni anamwita Eliya.”[o]

36 Mtu mmoja alikimbia na kujaza sifongo kwenye siki, akaliweka kwenye ufito, na akampa Yesu anywe akisema, “Subiri! Tuone ikiwa Eliya atashuka na kumshusha chini.”

37 Yesu akalia kwa sauti kubwa na kisha akafa.

38 Hapo pazia la Hekalu lilipasuka vipande viwili kutoka juu hadi chini. 39 Yule afisa wa jeshi aliyekuwa amesimama pale mbele na kuona jinsi Yesu alivyokufa. Afisa huyu alisema, “mtu huyu hakika alikuwa mwana wa Mungu!”

40 Baadhi ya wanawake walikuwa wakiangalia mambo haya toka mbali. Miongoni mwao alikuwapo Maria Magdalena, Salome, na Maria mama yake Yakobo na Yose. 41 Wanawake hawa ni wale waliomfuata Yesu huko Galilaya na kumhudumia. Wanawake wengi wengine waliofuatana naye kuja Yerusalemu walikuwapo pale pia.

Yesu Azikwa

(Mt 27:57-61; Lk 23:50-56; Yh 19:38-42)

42 Siku hii ilikuwa ni Siku ya Maandalizi ya Sabato. (Maana yake siku kabla ya Siku ya Sabato.) Jua lilikuwa bado halijazama. 43 Yusufu wa Arimathea alifika. Yeye alikuwa mjumbe wa Baraza la Kiyahudi aliyeheshimiwa, ambaye pia alikuwa anautazamia ufalme wa Mungu unaokuja. Kwa ujasiri mkubwa aliingia kwa Pilato na kuuomba mwili wa Yesu.

44 Pilato alishangaa Yesu angekuwa amekufa kwa haraka namna hii, hivyo alimwita yule akida na kumwuliza kama Yesu alikuwa tayari amekufa. 45 Aliposikia taarifa kutoka kwa yule afisa wa jeshi, ndipo alipoutoa mwili wa Yesu na kumpa Yusufu wa Arimathea.

46 Hivyo Yusufu alinunua mavazi kadhaa ya hariri, na akamshusha Yesu toka msalabani, akauzungushia mwili wake na hariri hiyo, na kumweka katika kaburi lililokuwa limechongwa katika mwamba. Kisha alivingirisha jiwe kubwa na kuliweka mlangoni mwa kaburi. 47 Mariamu Magdalena na Maria mama yake Yose aliona pale alipolazwa Yesu.

Yesu Amefufuka Kutoka Mauti

(Mt 28:1-8; Lk 24:1-12; Yh 20:1-10)

16 Sabato ilipomalizika, Mariamu Magdalena, Maria mama yake Yakobo, na Salome wakanunua manukato yenye harufu nzuri ili kuyapaka kwenye mwili wa Yesu. Alfajiri na mapema Jumapili, mara tu baada ya jua kuchomoza, walienda kwenye kaburi la Yesu. Nao walikuwa wakiambiana wao kwa wao, ni nani atakayelivingirisha jiwe litoke katika mlango wa kaburi kwa ajili yetu?

Kisha wakatazama juu na wakaona kuwa jiwe lile kubwa lilikuwa limevingirishwa tayari litoke mlangoni mwa kaburi la Yesu. Walipoingia kaburini, wakamwona kijana mmoja ameketi upande wa kulia naye alikuwa amevaa vazi jeupe, nao wakastaajabu.

Naye akamwambia, “Usistaajabu. Unamtafuta Yesu wa Nazareti, aliyesulubiwa? Tazama amefufuka! Hayupo hapa. Angalieni mahali walipokuwa wameweka mwili wake. Hata hivyo nendeni na kuwaeleza wafuasi wake pamoja na Petro kwamba: ‘Ametangulia mbele yenu kuelekea Galilaya. Mtamkuta kule, kama alivyowaambia.’”

Kwa hiyo wale wanawake walitoka na kukimbia kutoka kaburini, kwa sababu hofu na mshangao ulikuwa umewajia. Nao hawakusema chochote kwa mtu yeyote kwani waliogopa.[p]

Baadhi ya Wafuasi Wamwona Yesu

(Mt 28:9-10; Yh 20:11-18; Lk 24:13-35)

Baada ya Yesu kufufuka alfajiri na mapema siku ya Jumapili, alimtokea kwanza Maria Magdalena, ambaye awali alifukuza mashetani saba kutoka kwake. 10 Baada ya Mariamu kumwona Yesu, alienda na kuwaeleza wanafunzi wake. Walikuwa wamehuzunishwa sana na walikuwa wakilia. 11 Lakini Mariamu aliwaambia kwamba Yesu yu hai. Aliwaambia ya kwamba yeye amemwona, lakini wao hawakumwamini.

12 Baada ya hayo, Yesu kwa namna tofauti akawatokea wanafunzi wake wawili walipokuwa wakitembea kuelekea mashambani. 13 Hawa kisha walirudi na wakawasimulia wengine wote, lakini nao hawakuwaamini.

Yesu Awatokea Wafuasi Wake

(Mt 28:16-20; Lk 24:36-49; Yh 20:19-23; Mdo 1:6-8)

14 Baadaye, Yesu aliwatokea wale mitume kumi na mmoja walipokuwa wakila. Naye akawakaripia kwa kutokuwa na imani. Walikuwa wakaidi na walikataa kuwaamini wale waliomwona Yesu baada ya kufufuka kwake.

15 Naye akawaambia, “Nendeni ulimwenguni pote, na mkahubiri Habari Njema kwa uumbaji wote. 16 Yeyote atakayeamini na kubatizwa ataokolewa, lakini yeyote asiyeamini atahukumiwa. 17 Na wale waaminio wataweza kufanya ishara hizi kama uthibitisho: watafukuza mashetani kwa jina langu; watasema kwa lugha mpya wasizojifunza bado; 18 watakamata nyoka kwa mikono yao; na ikiwa watakunywa sumu yoyote, haitawadhuru; wataweka mikono yao kwa wagonjwa, nao watapona.”

Yesu Arudi Mbinguni

(Lk 24:50-53; Mdo 1:9-11)

19 Hivyo baada ya Bwana Yesu kuzungumza nao, alichukuliwa mbinguni, kuketi katika mkono wa kuume wa Mungu. 20 Na mitume wakatoka na kwenda kuhubiri kila mahali, na Bwana alifanya kazi pamoja nao akithibitisha kuwa ujumbe wao ni wa kweli kwa ishara zilizofuatana na mahubiri yao.

Footnotes

  1. 11:9 Msifuni Yaani, “Hosanna”, ambalo ni neno la Kiebrania lililotumika kumwomba msaada Mungu. Hapa, labda ilikuwa ni kelele ya shangwe iliyotumika kumsifu Mungu au Masihi wake. Pia katika mstari wa 10.
  2. 11:26 Nakala zingine za awali za Kiyunani zimeongeza mstari wa 26: “Lakini kama hamtawasamehe wengine, basi Baba yenu wa Mbinguni hatawasamehe ninyi dhambi zenu.”
  3. 12:31 jirani yako Mafundisho ya Yesu katika Lk 10:25-37 yanaonesha kwa uwazi kuwa hii ni pamoja na yeyote mwenye uhitaji.
  4. 12:36 chini ya udhibiti wako Mafundisho ya Yesu katika Lk 10:25-37 yanaonesha kwa uwazi kuwa hii ni pamoja na yeyote mwenye uhitaji.
  5. 13:6 Masihi Kwa maana ya kawaida, “Yule ambaye”, kwa maana ya Mfalme Mteule wa Mungu aliyetumwa na Mungu. Tazama Mt 24:5 na Masihi katika Orodha ya Maneno.
  6. 13:14 chukizo la uharibifu Ni maneno yanayoashiria kitu ambacho Mungu hapendezwi nacho. Tazama Dan 9:27; 11:31 na 12:11.
  7. 13:14 Msomaji aelewe hii ina maana gani Mwandishi anamtaka msomaji azingatie kwamba anazungumzia Jeshi la Rumi ambalo litaharibu Yerusalemu, ingawa hataki kulielezea hili kwa wazi. Tazama Lk 21:20-24.
  8. 13:24-25 Tazama Isa 13:10; 34:4.
  9. 14:5 mshahara wa mwaka Wa mwaka wa mtu kwa hali halisi “dinari 300” (sarafu za fedha). Sarafu moja, dinari ya Kirumi, ilikuwa ni wastani wa mshahara wa mtu wa siku moja.
  10. 14:36 Aba Ni neno la Kiaramu lililotumiwa na watoto wa Kiyahudi kama jina la kuwaita baba zao.
  11. 14:36 kikombe Kikombe ni ishara ya mateso. Yesu alitumia dhana ya kukinywea kikombe akimaanisha kuyakubali mateso ambayo angeyapata katika matukio ya kutisha ambayo yangetokea muda mfupi ujao.
  12. 14:58 mtu huyu Yaani, Yesu. Adui zake walikuwa wanakwepa kutamka jina lake.
  13. 14:62 Mwana wa Adamu … ya mbinguni Tazama Dan 7:13 na Zab 110:1.
  14. 15:28 Nakala zingine za Kiyunani zimeongeza mstari wa 28: “Na hili lilionyesha maana kamili ya Maandiko yaliyosema ‘walimweka pamoja wahalifu.’”
  15. 15:35 anamwita Eliya Neno hili “Mungu wangu” (ni Eli kwa Kiebrania ama Eloi kwa Kiaramu) ilisikika kwa watu kama jina la Eliya. Nabii maarufu aliyeishi mikaka kama 850 KK.
  16. 16:8 Kitabu kinaishia hapa katika nakala mbili za zamani za Kiyunani zilizopatikana. Nakala chache nyingine za baadaye zina mwisho huu mfupi: “Lakini mara wakampa maagizo yote Petro na wale waliokuwa pamoja naye. Kisha Yesu mwenyewe akawatuma watoke na kwenda mashariki na magharibi wakiwa na ujumbe mtakatifu ambao kamwe hautabadilika; kwamba watu wataokolewa milele.”