Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
11 Mimi ni mchungaji mwema. Mchungaji mwema huyatoa maisha yake kwa ajili ya kondoo. 12 Mtumishi anayelipwa ili kuwachunga kondoo yuko tofauti na mchungaji. Mtumishi wa mshahara, kondoo siyo mali yake. Hivyo anapomwona mbwa mwitu anakuja, hukimbia na kuwaacha kondoo peke yao. Mbwa mwitu huwashambulia na kuwatawanya kondoo. 13 Mtu huyu huwakimbia kondoo kwa sababu yeye ni mfanyakazi wa mshahara tu. Hawajali kabisa kondoo.
14-15 Mimi ni mchungaji ninayewajali kondoo. Nawafahamu kondoo wangu kama ambavyo Baba ananijua mimi. Na kondoo wananijua kama nami ninavyomjua Baba. Nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo hawa. 16 Nina kondoo wengine ambao hawamo kwenye kundi hili hapa. Hao nao napaswa kuwaongoza. Kwani wataisikia sauti yangu. Baadaye kutakuwa na kundi moja na mchungaji mmoja.[a] 17 Baba ananipenda kwa sababu nautoa uhai wangu. Nautoa uhai wangu ili niweze kuuchukua tena. 18 Hakuna anayeweza kuuchukua uhai wangu kutoka kwangu. Nautoa uhai wangu kwa hiari yangu. Ninayo haki ya kuutoa, na ninayo haki ya kuuchukua tena. Haya ndiyo aliyoniambia Baba yangu.”
19 Kwa mara nyingine tena Wayahudi wakagawanyika juu ya yale aliyoyasema Yesu. 20 Wengi wao wakasema, “Pepo mchafu amemwingia na kumfanya awe mwendawazimu. Kwa nini sisi tumsikilize?”
21 Lakini wengine wakasema, “Haya siyo maneno ya mtu anayeendeshwa na pepo mchafu. Pepo mchafu hawezi kuponya macho ya mtu asiyeona.”
© 2017 Bible League International