Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
36 Katika mji wa Yafa kulikuwa na mfuasi wa Yesu aliyeitwa Tabitha, Jina lake kwa Kiyunani lilikuwa Dorkasi.[a] Daima aliwatendea watu mambo mema na kuwapa pesa wale wenye mahitaji. 37 Petro alipokuwa Lida, Tabitha aliugua na kufa. Waliusafisha mwili wake na kuuweka chumbani ghorofani. 38 Wafuasi waliokuwa Yafa wakasikia kuwa Petro yuko Lida, mji ambao haukuwa mbali na Yafa. Hivyo waliwatuma watu wawili, waliomsihi Petro wakisema, “Tafadhali njoo kwetu haraka!”
39 Petro alijiandaa na kwenda pamoja nao. Alipofika, walimchukua na kumpeleka kwenye chumba ghorofani. Wajane wote walisimama wakamzunguka huku wakilia na wakamwonesha mavazi ambayo Tabitha alitengeneza alipokuwa hai. 40 Petro akawatoa watu wote chumbani. Akapiga magoti na kuomba. Kisha akaugeukia mwili wa Tabitha na kusema, “Tabitha! Simama.” Akafumbua macho yake. Alipomwona Petro akaketi. 41 Petro akamshika mkono na akamsaidia kusimama. Ndipo akawaita waamini na wajane chumbani. Akawaonyesha Tabitha; akiwa hai!
42 Watu kila mahali katika mji wa Yafa wakatambua kuhusu hili, na wengi wakamwamini Bwana. 43 Petro alikaa Yafa siku nyingi nyumbani kwa mtu mmoja aitwaye Simoni, aliyekuwa mtengenezaji wa ngozi.
Umati Mkubwa
9 Kisha nikatazama, nikaona umati mkubwa wa watu. Walikuwa wengi hakuna mtu angeweza kuwahesabu wote. Walikuwa wametoka katika kila taifa, kabila, rangi za watu na lugha za dunia. Walikuwa wamesimama mbele ya kiti cha enzi na mbele ya Mwanakondoo. Wote walikuwa wamevaa majoho meupe na wameshika matawi ya mitende mikononi mwao. 10 Walipaza sauti kwa nguvu, wakasema “Ushindi ni wa Mungu wetu, anayeketi kwenye kiti cha enzi, na kwa Mwanakondoo.”
11 Wazee na wenye uhai wanne walikuwa pale. Malaika wote walikuwa wamesimama kuwazunguka na kukizunguka kiti cha enzi. Malaika wakainamisha nyuso zao, wakasujudu mpaka chini mbele ya kiti cha enzi, wakamwabudu Mungu. 12 Walisema, “Amina! Sifa, utukufu, hekima, shukrani, heshima, nguvu na uweza ni vyake Mungu wetu milele na milele. Amina!”
13 Kisha mmoja wa wazee akaniuliza, “Watu hawa waliovaa kanzu nyeupe ni akina nani? Wametoka wapi?”
14 Nikajibu, “Wewe unajua ni akina nani, bwana.”
Mzee akasema, “Hawa ni wale waliokuja kutokana na mateso makuu. Wamefua kanzu zao[a] kwa kutumia damu ya Mwanakondoo, wako safi na ni weupe. 15 Hivyo sasa watu hawa wako mbele ya kiti cha enzi cha Mungu. Wanamwabudu Mungu mchana na usiku hekaluni mwake. Naye aketiye kwenye kiti cha enzi atawalinda. 16 Hawatasikia njaa tena. Hawatasikia kiu tena. Jua halitawadhuru. Hakuna joto litakalowachoma. 17 Mwanakondoo mbele ya kiti cha enzi atakuwa mchungaji wao. Atawaongoza kwenda kwenye chemichemi za maji ya uzima. Na Mungu atafuta kila chozi kutoka kwenye macho yao.”
Viongozi wa Kiyahudi Wasimama Kinyume na Yesu
22 Ulikuwa ni wakati wa baridi, na wakati wa Sikukuu ya Kuweka Wakfu[a] kule Yerusalemu. 23 Yesu alikuwa katika eneo la Hekalu katika Ukumbi wa Sulemani. 24 Viongozi wa Kiyahudi wakakusanyika kumzunguka. Wakasema, “Ni mpaka lini utatuacha na mashaka juu yako? Kama wewe ndiwe Masihi, basi tuambie wazi wazi.”
25 Yesu akajibu, “Nilikwisha kuwaambia tayari, lakini hamkuamini. Nafanya miujiza katika jina la Baba yangu. Miujiza hii inaonesha mimi ni nani. 26 Lakini hamuamini, kwa sababu ninyi siyo kondoo wangu. 27 Kondoo wangu huisikia sauti yangu. Nami nawajua, nao hunifuata. 28 Mimi nawapa kondoo wangu uzima wa milele. Nao hawatakufa kamwe, na tena hakuna atakayemchukua yeyote kutoka mkononi mwangu. 29 Baba yangu ndiye aliyenipa hao, naye ni mkuu kuliko wote.[b] Hakuna anayeweza kuwaiba kondoo wangu kutoka mkononi mwangu. 30 Mimi na Baba tu umoja.”
© 2017 Bible League International