Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Mpango wa Kumwua Yesu
(Mt 26:1-5; Mk 14:1-2; Lk 22:1-2)
45 Walikuwepo Wayahudi wengi waliokuja kumtembelea Mariamu. Hawa walipoona aliyotenda Yesu, wengi wao wakamwamini. 46 Lakini baadhi yao wakaenda kwa Mafarisayo na kuwapa habari ya mambo aliyofanya Yesu. 47 Kisha viongozi wa makuhani na Mafarisayo wakaitisha kikao cha baraza kuu. Wakasema, “Tutafanyaje? Mtu huyu anafanya ishara nyingi sana. 48 Tukimwacha aendelee kufanya hivi, kila mtu atamwamini. Ndipo Warumi watakuja na kulichukua Hekalu na Taifa letu pia.”
49 Mmoja wa watu wale alikuwa ni Kayafa. Yeye alikuwa kuhani mkuu kwa mwaka ule. Akasema, “Ninyi hamjui lo lote! 50 Ni bora mtu mmoja akafa kwa ajili ya watu wengine badala ya taifa zima kuangamia. Ninyi bado hamjalitambua hili.”
51 Kayafa hakufikiri hivi peke yake. Hakika kama kuhani mkuu kwa mwaka ule, alikuwa akitabiri kwamba Yesu angekufa kwa ajili ya Wayahudi. 52 Kweli, angekufa kwa ajili ya Wayahudi. Lakini pia angekufa kwa ajili ya watoto wa Mungu waliotawanyika ulimwenguni pote. Angekufa ili awakusanye na kuwaweka katika kundi moja.
53 Siku ile viongozi wa Wayahudi wakaanza kupanga jinsi ya kumuua Yesu. 54 Hivyo Yesu akaacha kusafiri wazi wazi katikati ya Wayahudi. Akaelekea katika mji ulioitwa Efraimu uliokuwa kwenye eneo karibu na jangwa. Akakaa huko pamoja na wafuasi wake.
55 Wakati huo Sikukuu ya Pasaka ya Wayahudi ilikaribia. Watu wengi kutoka katika nchi yote ya Uyahudi wakaenda Yerusalemu siku chache kabla. Walienda kujitakasa tayari kwa ajili ya sikukuu hiyo. 56 Watu wakamtafuta Yesu. Nao walisimama katika maeneo ya Hekalu na kuulizana, “Je, naye atakuja kwenye sikukuu? Unafikirije wewe?” 57 Lakini viongozi wa makuhani na Mafarisayo walitoa agizo maalumu kuhusu Yesu. Walisema kuwa mtu yeyote anayejua mahali alipo Yesu awaambie ili waweze kumkamata.
© 2017 Bible League International