Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
9 Tuna furaha tele mbele za Mungu wetu kwa ajili yenu! Lakini hatuwezi kumshukuru Mungu inavyopasa kwa furaha ile yote tuliyo nayo. 10 Usiku na mchana tuliendelea kuomba kwa mioyo yetu yote kwamba tuweze kuja huko na tuwaone tena. Tunataka kuwapa kila mnachohitaji ili imani yenu iwe timilifu.
11 Tunaomba kwamba Mungu wetu aliye Baba yetu, na Bwana Yesu wataiongoza njia yetu kuja kwenu. 12 Tunaomba kuwa Bwana ataufanya upendo wenu uendelee kukua. Tunaomba kuwa atawapa kupendana zaidi na zaidi miongoni mwenu na kwa watu wote. Tunaomba kuwa mtampenda kila mmoja kwa namna ile ile ambayo sisi tuliwapenda ninyi. 13 Hii itaongeza hamu yenu ya kutenda yaliyo haki, na mtakuwa watakatifu msio na kosa mbele za Mungu wetu na baba yetu wakati Bwana wetu Yesu atakapo kuja na watakatifu[a] wake wote.
Msiogope
(Mt 24:29-31; Mk 13:24-27)
25 Mambo ya kushangaza yatatokea kwenye jua, mwezi na nyota na watu katika dunia yote wataogopa na kuchanganyikiwa kutokana na kelele za bahari na mawimbi yake. 26 Watazimia kwa hofu na kuogopa watakapoona mambo yanayoupata ulimwengu. Kila kitu katika anga kitabadilishwa. 27 Kisha watu watamwona Mwana wa Adamu akija katika wingu mwenye nguvu na utukufu mwingi. 28 Mambo haya yakianza kutokea, simameni imara na msiogope. Jueni kuwa wakati wa Mungu kuwaweka huru umekaribia!”
Maneno Yangu Yataishi Milele
(Mt 24:32-35; Mk 13:28-31)
29 Kisha Yesu akawaambia mfano huu: “Tazameni miti yote. Mtini ni mfano mzuri. 30 Unapochipua majani mnatambua kwamba majira ya joto yamekaribia. 31 Kwa namna hiyo hiyo, mtakapoona mambo haya yote yanatokea, mtajua kwamba ufalme wa Mungu umekaribia kuja.
32 Ninawahakikishia kwamba, wakati mambo haya yote yatakapotokea, baadhi ya watu wanaoishi sasa watakuwa hai bado. 33 Ulimwengu wote, dunia yote na anga vitapita, lakini maneno yangu yataishi milele.
Kuweni Tayari Wakati Wote
34 Iweni waangalifu, msiutumie muda wenu katika sherehe za ulevi na kuhangaikia maisha haya. Mkifanya hivyo, hamtaweza kufikiri vyema na mwisho unaweza kuja mkiwa hamjajiandaa. 35 Mwisho utakuja kwa kushitukiza kwa kila mtu duniani. 36 Hivyo, iweni tayari kila wakati. Ombeni ili muepuke mambo haya yote yatakayotokea na mweze kusimama kwa ujasiri mbele za Mwana wa Adamu.”
© 2017 Bible League International