Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
16 Sijivuni kwa sababu ya kazi yangu ya kuhubiri Habari Njema kwa sababu ni wajibu wangu ambao ni lazima nifanye; ole wangu nisipowahubiri watu Habari Njema. 17 Ikiwa ningehubiri kwa sababu ya utashi kwangu, ningestahili kulipwa. Lakini sikuchagua kufanya kazi hii. Ni lazima nihubiri Habari Njema. Hivyo ninafanya kazi niliyokabidhiwa. 18 Sasa, kwa kufanya kazi hii ninapata nini? Thawabu yangu, ni kuwa ninapowahubiri watu Habari Njema, ninawapa bure na sizitumii haki zinazoambatana na kufanya kazi hii.
19 Niko huru. Similikiwi na mtu yeyote, lakini ninakuwa mtumwa ili watu wengi waokoke. 20 Kwa Wayahudi nilienenda kama Myahudi ili nisaidie Wayahudi wengi waokolewe. Sitawaliwi na sheria, lakini kwa wanaotawaliwa na sheria nilikuwa kama ninayetawaliwa na sheria. Nilifanya hivi kuwasaidia wanaotawaliwa na sheria, ili waokoke. 21 Kwa wasio na sheria nilikuwa kama nisiye na sheria, ili niwasaidie wasio na sheria kuokoka. Mimi si kama mtu asiye na Sheria ya Mungu, ninatawaliwa na sheria ya Kristo. 22 Kwa waliodhaifu, nilikuwa dhaifu ili niwasaidie kuokoka. Nilifanyika kila kitu kwa watu wote ili nifanye kila kinachowezekana niweze kuwasaidia watu waokolewe. 23 Ninafanya kila ninachoweza ili Habari Njema ijulikane na niweze kushiriki katika Habari zake.
Yesu Awaponya Watu Wengi
(Mt 8:14-17; Lk 4:38-41)
29 Wakaondoka kutoka katika sinagogi na mara hiyo hiyo wakaenda pamoja na Yakobo na Yohana hadi nyumbani kwa Simoni na Andrea. 30 Mara Yesu alipoingia ndani ya nyumba watu wakamweleza kuwa mama mkwe wake Simoni alikuwa mgonjwa sana na alikuwa amepumzika kitandani kwa sababu alikuwa na homa. 31 Yesu akasogea karibu na kitanda, akamshika mkono na kumsaidia kusimama juu. Ile homa ikamwacha, na yeye akaanza kuwahudumia.
32 Ilipofika jioni, baada ya jua kuzama waliwaleta kwake watu wote waliokuwa wagonjwa na waliokaliwa na mashetani. 33 Mji mzima ulikusanyika mlangoni pale. 34 Naye akawaponya watu waliokuwa na magonjwa ya kila aina, na kufukuza mashetani wengi. Lakini yeye hakuyaruhusu mashetani kusema, kwa sababu yalimjua.[a]
Yesu Aenda Katika Miji Mingine
(Lk 4:42-44)
35 Asubuhi na mapema, ilipokuwa giza na bado hakujapambazuka, Yesu aliamka na kutoka kwenye nyumba ile na kwenda mahali ili awe peke yake na kuomba. 36 Lakini Simoni na wale wote waliokuwa pamoja naye waliondoka kwenda kumtafuta Yesu 37 na walipompata, wakamwambia, “kila mmoja anakutafuta.”
38 Lakini Yesu akawaambia, “Lazima twende kwenye miji mingine iliyo karibu na hapa, ili niweze kuhubiri huko pia, kwa sababu hilo ndilo nililokuja kulifanya.” 39 Hivyo Yesu alienda katika wilaya yote iliyoko mashariki mwa ziwa la Galilaya akihubiri Habari Njema katika masinagogi na kuwafungua watu kutoka katika nguvu za mashetani.
© 2017 Bible League International