Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Kazi ya Paulo Thesalonike
2 Ndugu zangu, mnafahamu kuwa safari yetu kuja kwenu ilikuwa yenye nguvu. 2 Lakini kabla ya kuja kwenu, watu wa Filipi walitutenda vibaya kwa kututukana matusi mengi na kutusababishia mateso. Mnafahamu yote kuhusu hilo. Na kisha tulipokuja kwenu, watu wengi huko walitupinga. Tuliwaeleza ninyi Habari Njema za Mungu lakini ni kwa sababu Mungu alitupa ujasiri tulio hitaji. 3 Hatukuwa na kitu cha kupata faida kwa kuwaomba ninyi muiamini Habari Njema. Hatukuwa tunataka kuwafanya wajinga wala kuwadanganya. 4 Hapana, tulifanya hivyo kwa sababu Mungu ndiye aliyetuagiza kazi hii. Na hii ilikuwa baada ya yeye kutupima na kuona ya kuwa tunaweza kuaminiwa kuifanya. Hivyo tunapoongea, tunajaribu tu kumpendeza Mungu, na sio wanadamu. Yeye tu ndiye awezaye kuona kilichomo ndani yetu.
5 Mnafahamu kuwa hatukujaribu kuwarubuni kwa kusema mambo mazuri juu yenu. Hatukuwa tunatafuta jinsi ya kuzichukua pesa zenu. Hatukutumia maneno ama matendo kuficha tamaa yetu. Mungu anajua ya kuwa huu ni ukweli. 6 Hatukuwa tukitafuta sifa toka kwa watu ama kutoka kwenu au kwa mtu yeyote.
7 Tulipokuwa pamoja nanyi, kama mitume wa Kristo tulikuwa na uwezo wa kutumia mamlaka yetu kuleta madai ya nguvu kwenu. Lakini tulikuwa wapole kwenu.[a] Tulikuwa kama vile mkunga anavyowahudumia watoto wake wadogo. 8 Ilikuwa ni upendo wetu mkuu sana kwenu uliotufanya tuwashirikishe Habari Njema za Mungu. Zaidi ya hayo yote tulifurahi kuwashirikisha ninyi nafsi zetu wenyewe. Hiyo inadhihirisha ni kwa kiwango gani tuliwapenda.
Amri ipi ni ya Muhimu Zaidi?
(Mk 12:28-34; Lk 10:25-28)
34 Mafarisayo waliposikia kuwa Yesu amewafanya Masadukayo waonekane wajinga nao wakaacha kumwuliza maswali. Kwa hiyo Mafarisayo wakafanya mkutano. 35 Ndipo mmoja wao, aliye mtaalamu wa Sheria ya Musa, akamwuliza Yesu swali ili kumjaribu. 36 Akasema, “Mwalimu, amri ipi katika sheria ni ya muhimu zaidi?”
37 Yesu akajibu, “‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote na akili yako yote.’(A) 38 Hii ndiyo amri ya kwanza na ya muhimu zaidi. 39 Na amri ya pili ni kama ya kwanza: ‘Mpende jirani yako[a] kama unavyojipenda wewe mwenyewe.’(B) 40 Sheria yote na maandiko ya manabii yamejengwa katika amri hizi mbili.”
Je, Masihi ni Mwana wa Daudi?
(Mk 12:35-37; Lk 20:41-44)
41 Hivyo Mafarisayo walipokuwa pamoja, Yesu aliwauliza swali. 42 Akasema, “Nini mawazo yenu juu ya Masihi? Je, ni mwana wa nani?” Mafarisayo wakajibu, “Masihi ni Mwana wa Daudi.”
43 Yesu akawaambia, “Sasa ni kwa nini Daudi anamwita ‘Bwana’? Daudi alikuwa anazungumza kwa nguvu ya Roho. Aliposema,
44 ‘Bwana Mungu alimwambia Bwana Mfalme wangu:
Keti karibu nami upande wangu wa kuume,
na nitawaweka adui zako chini ya udhibiti wako.’[b](C)
45 Ikiwa Daudi anamwita Masihi ‘Bwana’. Inakuwaje Masihi ni mwana wa Daudi?”
46 Hakuna Farisayo aliyeweza kumjibu Yesu. Na baada ya siku hiyo, hakuna aliyekuwa jasiri kumwuliza maswali zaidi.
© 2017 Bible League International