Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Yesu Amponya Mgonjwa
(Mk 1:40-45; Lk 5:12-16)
8 Yesu alipotelemka kutoka kwenye kilima, umati mkubwa wa watu ulimfuata. 2 Mtu mmoja mwenye ugonjwa mbaya sana wa ngozi akamwendea, akainama mbele yake mpaka chini na akasema, “Bwana ukitaka una uwezo wa kuniponya.”
3 Yesu aliunyoosha mkono wake akamshika mtu yule mwenye ugonjwa mbaya sana wa ngozi. Akasema, “Hakika, ninataka kukuponya. Upone!” Mtu huyo akapona ugonjwa mbaya sana wa ngozi saa hiyo hiyo. 4 Kisha Yesu akamwambia, “Usimwambie mtu yeyote kilichotokea, lakini nenda kwa kuhani akakuchunguze.[a] Na umtolee Mungu sadaka ambazo Musa aliamuru watu wanaoponywa watoe, ili iwe ushahidi kwa watu kwamba umepona.”
Yesu Amponya Mtumishi wa Afisa wa Jeshi
(Lk 7:1-10; Yh 4:43-54)
5 Yesu alikwenda Kapernaumu. Alipoingia mjini, afisa wa jeshi alimjia na kumwomba msaada. 6 Akasema, “Bwana, mtumishi wangu ni mgonjwa sana nyumbani na amelala kitandani. Hawezi hata kutingishika na ana maumivu makali sana.”
7 Yesu akamwambia yule afisa, “Nitakwenda nimponye.”
8 Yule afisa akajibu, “Bwana, mimi si mwema kiasi cha wewe kuingia katika nyumba yangu. Toa amri tu, na mtumishi wangu atapona. 9 Ninajua hii, kwa kuwa ninaelewa mamlaka. Kuna watu wenye mamlaka juu yangu, na nina askari walio chini ya mamlaka yangu. Nikimwambia askari mmoja ‘nenda’, huenda. Na nikimwambia mwingine ‘njoo’, huja. Pia nikimwambia mtumwa wangu ‘fanya hiki’, hunitii.”
10 Yesu aliposikia maneno hayo alishangaa. Akawaambia wale waliokuwa wakifuatana naye, “Ukweli ni kuwa, mtu huyu ana imani kuliko mtu yeyote niliyewahi kumwona katika Israeli. 11 Watu wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi na kula pamoja na Ibrahimu, Isaka, na Yakobo katika ufalme wa Mungu. 12 Na wale wanaopaswa kuwa katika ufalme watatupwa nje gizani. Na huko watalia na kusaga meno yao kwa sababu ya maumivu.”
13 Kisha Yesu akamwambia yule afisa, “Rudi nyumbani kwako. Mtumishi wako atapona kama unavyoamini.” Mtumishi wa afisa huyo akapona wakati ule ule.
© 2017 Bible League International